Mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe imemuhukumu Ramadhan Handa Tuma mwenye umri wa miaka 28 kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miezi 24 kwa kupatikana na  kosa la kuchoma moto Msahafu na Juzuu za dini ya Kiisilamu.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu Khamis Ali Simai  mara baada ya kumtia hatiani mshitakiwa huyo dhidi ya mashitaka ya kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani pamoja na kukashifu dini.

Akitoa hukumu hiyo, hakimu Khamis amesema shitaka la kwanza la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani atalipa faini ya shilingi 200,000 na endapo atashindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.

Kosa la pili lililomkabili mshitakiwa huyo ni kukashifu dini, mahakama hiyo imempa adhabu ya kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi 18, na kufahamisha kuwa adhabu zote hizo zitakwenda sambamba.

Upande wa mashitaka ulioongozwa na Raya Issa Mselem, amesema haukuridhishwa na Hukumu hiyo na kusema kwamba anakusudia kukata rufaa dhidi ya adhabu iliyotolewa kwa shitaka la pili la kukashifu dini.

Hata hivyo Mwendesha mashitaka Raya Mselem ameomba itolewe adhabu kali dhidi ya mshitakiwa huyo  kutokana na kitendo alichokifanya ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo.

Kwa upande wake mshitakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa madai ana familia inayomtegea akiwemo mke na mtoto, pamoja kusumbuliwa na maradhi ya tumbo.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, Ramadhan Handa Tuma alifanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani Novemba 16 mwaka jana Mombasa zanzibar ambapo kwa makusudi na bila ya halali alichoma moto msahafu pamoja na juzuu za dini ya Kiisilamu .

Advertisements