Wakulima wa mpunga wa mabonde ya Mkoa wa Kaskazini Unguja yaliokumbwa na ukame wameiomba Serikali kuwapatia mbegu ndogo wakati wa mvua za Masika ili wazipande tena katika konde zao zilizoharibika kwa jua kali.

 

Ombi hilo la Wakulima liliwasilishwa kwenye ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika mabonde ya Mpunga ya Kilombero, Kibokwa, Machekechuni na Kibonongwa alipofika kuwapa pole kufuati mpunga wao kuunguliwa na jua kali.

 

Akitoa maelezo kuhusu kadhia hiyo mkulima Bw. Ame Haji na wenzake walimpongeza Mhe Balozi Seif kwa uwamuzi wake wa kuwatembelea na kuwafariji, jambo ambalo limeonesha anavyojali shida za wananchi.

 

Halikadhalika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Ndg Afani Othman Maalim alitoa ufafanuzi juu ya maharibiko hayo ya konde za mpunga na pia alieleza maandalizi yaliokwishafanywa na Wizara yake kukabiliana na tatizo hilo.

 

Kwa upande wake Mhe Makamu wa Pili wa Rais alieleza kusikitishwa kwake na kadhia hiyo na kusema kuwa ni mambo ya Mungu hayakutarajiwa bali mabadiliko ya hali ya hewa yamebadilisha miongo na mvua. Pia alikubali ombi la wakulima la kuwapatia mbegu na pembejeo.

 

Kuhusu umuhimu wa kilimo Mhe Balozi Seif aliwaambia wakulima kuwa kazi yao ya kilimo ni muhimu sana kwa taifa kwakuwa wanaisaidia Serikali kupunguza matumizi ya uwagiziaji na pia kutotegemea sana vyakula kutoka nje.

 

Aidha. baadhi ya wakulima walieleza tatizo la maji safi linalowakabili wakati huu wa kiangazi. lakini walisifu matayarisho mazuri ya mwaka huu kwa kulimiwa na matrekta mapema.

Advertisements