Switzerland Flag

SWITZERLAND imeeleza  kuwa kufanikiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa kunatokana na juhudi zilizochukuliwa na serikali kwa  kuwaelimisha mapema wananchi wake juu ya hatua hiyo.

Balozi wa Switzerland  nchini Tanzania Mhe. Adrian Schlapfer alisema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

 

Katika maelezo yake Balozi Schlapfer alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kufanikisha uchaguzi kwa amani na utulivu na hatimae kuundwa kwa Serikali ambayo imepata mafanikio kwa kuanza kazi vizuri.

 

Alisema kuwa hatua iliyofikiwa na Zanzibar katika kufanikisha Serikali hiyo na kuanza kuleta maendeleo inatokana na elimu ya kutosha iliyotolewa kwa wananchi juu ya serikali yao hiyo kabla na baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

 

Balozi huyo alieleza  kuwa Zanzibar imejijengea heshima na sifa kubwa kitaifa na kimataifa kutokana na kufanya uchaguzi uliokuwa huru na haki ambao umefanyika kwa amani na utulivu mkubwa.

 

Akieleza miongoni mwa mambo yaliopelekea kufanikiwa kwa serikali ni pamoja na kuwepo kwa suala zima la Utawala Bora wenye kufuata sheria na taratibu za nchi ambapo Balozi Schlapfer aliipongeza hatua hiyo.

 

Katika maelezo yake hayo, Balozi Schlapfer alisema kuwa Switzerland inathamini uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo kati ya nchi hiyo na Zanzibar na kuahidi kuimarisha zaidi uhusiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.

 

Alisema kuwa Switzerland itaendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo hapa Zanzibar na kueleza lengo  la serikali yake la  kuanzisha mradi maalum wa afya. Balozi huyo alisema kuwa azma ya kuanzisha mradi huo ni kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.

 

Akieleza juu ya sifa na haiba ya Zanzibar katika sekta ya Utalii, Balozi huyo alieleza kuwa visiwa vya Zanzibar vimejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii sanjari na ukarimu wa wananchi wake kwa wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar.

 

Alisema kuwa kutambulika na kukua kwa sekta ya utalii hapa Zanzibar kumeweza kupanua soko la ajira ambapo baadhi ya wataalamu wa huduma za utalii kutoka nchini mwake wapo hapa Zanzibar wanafanya kazi katika hoteli za kitalii.

 

Kwa misingi hiyo alieleza kuwa nchi yake ina nafasi nzuri ya kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo na kuahidi kuitangaza Zanzibar kiutalii na kiuwekezaji nchini mwake.  Sanjari na kuimarisha ushirikiano wa kiutamaduni

 

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alimueleza Balozi huyo kuwa ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Switzerland umeweza kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo nchini.

 

Dk. Shein alimueleza Balozi Schlapfer kuwa Switzerland imekuwa mdau mzuri wa maendeleo ya Zanzibar kwa kuweza kuunga mkono sekta mbali mbali zikiwemo elimu, kwa kutoa nafasi za masomo pamoja na sekta nyenginezo.

 

Alisema kuwa azma ya Switzerland ya kuanzisha mradi maalum wa sekta ya afya hapa Zanzibar utaweza kusaidia juhudi za serikali katika kuimarisha sekta hiyo ambayo ni muhimu katika maendeleo ya wananachi katika kufikia malengo ya Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi  Zanzibar (MKUZA).

 

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara  ya Afya itahakikisha inatoa mashirikiano ya karibu zaidi kwa lengo la kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

 

Akizungumza juu ya mafanikio  ya kisiasa yaliopatikana hapa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa amani, utulivu na mshikamano sanjari na umoja wa Wazanzibari ndio uliopelekea kufanyika uchaguzi uliokuwa huru na haki.

 

Alieleza kuwa kikubwa kinachohitajiwa na Wazanzibari hivi sasa ni maendeleo, hivyo juhudi za pamoja zitaendelea kuchukuliwa kwa kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo zaidi.

 

Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi kwa mashirikiano yake  pamoja na misaada inayotoa kwa Zanzibar pamoja na kutoa shukurani zake kwa nchi hiyo kwa kushiriki vyema katika uangalizi wa uchaguzi mkuu uliopita.

 

Alisema kuwa hatua hiyo imeitia moyo mkubwa Zanzibar na kuweza kujitambua kuwa inanafasi kubwa katika kujiletea maedneleo endelevu na kuendeleza amani na utulivu uliopo.

 

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar ni sehemu moja wapo ya uwekezaji hivyo inawakaribisha waekezaji kutoka nchini humo kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo  sekta ya utalii, uvuvi na sekta nyenginezo.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuimarisha uhusiano wa kielimu kwa vyuo vikuu vya nchini humo na vile vya  Zanzibar  kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA)

Advertisements