Rais wa Zanzibar Dr. Shein

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein amesema serikali imeanza kufanya mazungumzo na wawekezaji nje ya nchi ili kuja kuwekeza Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kisiwani Pemba amesema baadhi ya mawaziri wake wameanza kusafiri nje nchi za Ngambo kwenda kufanya mazungumzo na wawekezaji hao.

Dr. Shein amesema katika hatua za awali wawekezaji hao wameonesha nia ya kutaka kuwekeza Zanzibar miradi mbali mbali ya kiuchumi.

Amesema Zanzibar imefikia pahali pazuri na kutaka amani na utulivu uliopo nchini unahitaji kuenziwa kwa vile ndio msingi wa kukuza uchumi wa taifa na wananchi mmoja mmoja

Aidha Dr. Shein amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia uzalendo wa nchi yao.

Amesema kwa sasa Zanzibar inakoelekea vyama vya siasa vitabaki kama njia za kuwapata viongozi watakaoingia madarakani.

Katika mkutano huo Dr. Shein amesema mawaziri wote wanafanya kazi kwa bidii na ushirikiano bila ya kujali vyama vya siasa wanavyotoka.

Dr. Shein ambae pia ni mjumbe wa kamati kuu ya CCM amewataka viongozi wa chama hicho kushirikiana na kujiepusha kuwagawa wananchama kwa njia za makundi.

Mkutano wa Dr. Shein wa mikoa miwili ya Pemba ulikuwa na lengo la kuwapongeza wana CCM kwa kukiunga mkono chama hicho kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba mwaka jana.

Advertisements