Kisiwa cha Unguja kimetajwa kuwa na wakaazi wengi wanaougua ugonjwa wa kifua kikuu kutokana na ongezeko la idadi ya watu na wahamiaji.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani wataalamu wa kifua kikuu Zanzibar wamesema kati ya wagonjwa 449 waliobainika kuwa na ugonjwa huo mwaka 2010 aslimia 82 wamegunduliwa katika maeneo ya Unguja.

Wamesema maeneo yaliogunduliwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu ni Wilaya ya magharibi ambayo ina idadi kubwa ya wakaazi na wahamiaji.

Wataalamu hao wamesema ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa unambukizwa kupitia njia ya hewa kutoka kwa mtu mwenye kifua kikuu hivyo wamewataka wananchi kufika katika vituo vya afya kupatiwa tiba.

Wamesema dadili za ugonjwa huo ni kikohozi cha wiki mbili au zaidi,  maumivu ya kifua na kushindwa kupumua, homa za jioni, kutokwa na jasho jingi usiku na kukonda.

Nae waziri wa afya Juma Duni Haji amesema huduma za matibabu ya kifua kikuu zimeimarishwa kwenye vituo vya afya vya vijijini na mijini, hospitali za umma na binafsi ambazo hutolewa bila ya malipo.

Hivyo ametoa wito kwa wananchi wenye dadili za ugonjwa huo kufika katika vituo vya afya na hospitali kupatiwa matibabu ili kuepusha kuwambukiza watu wengine.

Takwimu zinaonesha zaidi ya watu bilioni 1.7 wameugua kifua kikuu duniani, wagonjwa milioni 7.5 wako katika nchi zinazoendelea ambapo Tanzania ni nchi ya 22 zenye wagonjwa wengi ulimwenguni.

Kwa mwaka Tanzania inapata wastani wa wagonjwa elfu 66 kati yao wagonjwa 450 wanagunduliwa Zanzbiar.

Advertisements