Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi ameeleza haja ya Serikali mbili baina ya Iran na Zanzibar kuangalia upya makubaliano yao ya awali kwa lengo la kuyatafutia njia bora za utekelezaji wake.

Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyaeleza hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mhe. Dk. Mahmoud AhmediNejad katika Ikulu ya mjini Tehran.

Mhe. Balozi Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na kuwa na makubaliano kadhaa yanayohitaji kutekelezwa ambayo mengi hayajafanyiwa kazi.

Hivyo alishauri kuundwa kwa Tume ya watu wachache ya kufanyia mapitio ya makubaliano yote na kukaa pamoja na wajumbe wa Serikali ya Iran kwa ajili ya kuyatafutia njia za kuyatekeleza.

Aidha, alieleza kufurahishwa kwake na nia ya Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuimarisha ushirikiano wao kwa kuanzisha Ubalozi Mdogo wa nchi hiyo hapa Zanzibar.

Halikadhalika aliwasilisha salaam za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein za kumtakia kheri katika sherehe za mwaka za jadi.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mhe. Dk. Mahmoud AhmediNejad alieleza kupendezewa kwake na salaam za viongozi hao wa Tanzania na kwa ujumbe wa Zanzibar kushiriki Tamasha hilo.

Alisema Iran na Zanzibar ni ndugu marafiki wa muda mrefu kutokana na historia ya utamaduni wao mambo ambayo yamezidi kuimarisha uhusiano baina yao na kuishauri Zanzibar kufanya maadhimisho kama haya.

Aidha, alikubaliana na mapendekezo na ushauri wa Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ya kutafuta mbinu za kuanza utekelezaji wa makubaliano yao kwa haraka.

Kuhusu maadhimisho ya Jadi ya Mwaka wa Nowruz, Mhe. Dk. AhmediNejad amesema sherehe hizo zina madhumuni ya kuimarisha imani miongoni mwa jamii na kujenga mapenzi na umoja miongoni wao.

Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi tayari yuko Iran akimuwakilisha Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika maadhimisho ya Sherehe za mwaka za Iran.

Advertisements