Miongoni mwa wananchi wa Zanzibar walioshiriki kwenye mkutano wa kutoa maoni juu ya muswada wa kuunda kamisheni ya kukushana maoni ya kuandika katiba mpya ya jamhuri ya muungano Tanzania. (Picha na Zanzibar Yetu Bolog)

Mkutano wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mswaada wa uundwaji wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umevunjika kufuatia washiriki kuuchana mswaada huo katika mkutano uliokuwa aukiendelea kukusanya maoni visiwani Zanzibar.

Mkutano huo kujadili katiba kwa wadau mbali mbali umevunjika kufuatia sheikh Farid Hadi Ahmed kuchana rasimu ya katiba iliyowasilishwa kwa wadau mbali hapo katika ukumbi wa skuli ya Haile Sellasie ambapo awali mkutano huo ulipangwa kumalizika saa 8 mchana lakini ulilazimika kukatishwa baada ya kuchanwa na watu wote kutawanyika katika ukumbi huo.

Akichangia kwa ufupi mswaada huo Farid amesema lazima maamuzi ya wananchi yachukuliwe na suala la kuheshimu mawazo yao ni suala la lazima hivyo hakuna sababu ya kuwalazimisha kitu wasichokitaka.

Awali akichangia mswada huu Mwanasheria Ibrahim Mzee Ibrahim ambae pia ni katibu wa Baraza la wawakilishi amesema katiba ya jamhuri ya muuungao wa Tanzania ina mapungufu mengi na pia mswada huo uliowasilishwa una mapungufu yake.

Amesema kinachojadiliwa hivi sasa ni rasimu ya mswaada hivyo ni vyema kuweka wazi vifungu vya mswaada huo ambavyo vyengine amesema kuwa vinaleta utata.

Amesema katika kujadili mswaada huo ni lazima kuangalia kilichoandikwa ndani ya mswada na sio kusikiliza mawazo ya mtu binafsi ambayo anayatoa kichwani mwake.

Akiyataja mapungufu mengine yaliokuwemo katika mswada huo ni pamoja na kifungu cha nane za mswada huo kinachogusia kutengenezwa kwa hadidu rejea haijaanishwa wazi kwa kutajwa nafasi ya Zanzibar katika utengenezaji huo na kuongeza kuwa ni vyema kwa Zanzibar kupewa nafasi ipasavyo na kushirikishwa na kukubaliana katika kutengenezwaji hadidu rejea.

Awali akisoma mswaada huo kwa niaba ya waziri wa katiba na sheria wa Tanzania waziri wa afrika mashariki Samuel Sitta amesema wamewataka washirki wa mdahalo huo kuchangia kwa mujibu wa mahitaji ya mswaada huo.

Hapo jana Wananchi, viongozi wa siasa, serikali na wanasheria wameukataa muswada wakidai upande wa Zanziar haukishikishwa.

Wakitoa maoni yao katika mkutano uliofanyika hoteli ya Bwawani wamesema muswada huo umezingatia zaidi upande wa Tanzania bara na una kasoro za kisheria na kikatiba, hivyo unahitaji kurejeshwa tena ili kufanyiwa marekebisho

Nae mkurugenzi wa mashtaka Zanzibar Othman Masoud akitaja baadhi ya kasoro amesema bunge la Jamhuri ya muungano haliwezi kutunga sheria ya kuunda ya katiba mpya.

Amesema mamlaka iliyonayo bunge ni kurekebisha katiba na sio vyenginevyo

Nao wajumbe wengine wamemuomba rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kuitisha kikao cha dharura cha baraza la Mapinduzi ili kutoa kauli ya serikali juu ya muswada huo.

Muswada huo wa kuunda tume ya kukusanya maoni ya wanchi juu ya kuundwa katiba mpya unaendelewa kujadiliwa katika maeneo mbali mbali mbali nchini Tanzania.

Advertisements