UONGOZI wa Mtandao wa Hospitali za Apollo kutoka India umeahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya nchini ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za mafunzo ya udaktari kwa madaktari wa Zanzibar.

 

 

Afisa Mkuu Kanda ya Kati Dr. Hari Prasad kutoka Mtandao wa Hospitali za Apollo nchini India akiwa amefuatana na Meneja Mkuu Ustawi wa Biashara wa Kimataifa  kutoka Apolo, Bwana Radhey Mohan, alieleza hayo wakati walipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

 

Katika maelezo yake Dk. Prasad alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Hospitali za Apollo ziko tayari kusaidia kutoa nafasi za mafunzo ya udaktari kwa madaktari wa Zanzibar hadi kufikia hatua za kuwa mabingwa kwa mujibu wa mahitaji yanayotakikana.

 

Dk. Prasad alieleza kuwa tayari umoja huo wa Hospitali za Apollo umeshatenga fedha maalum kwa ajili ya mafunzo hayo ya udaktari ikiwa ni pamoja na kuwafunza madaktari bingwa katika mafunzo ya awali.

 

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa tayari Mtandao huo wa Hospitali za Apollo utakamilisha hospitali yake ya kisasa inayojegwa mjini Dar-es-Salaam ambayo alisema kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma kwa Watanzania wote wakiwemo wagonjwa kutoka Zanzibar.

 

Alieleza kuwa wanamatarajio makubwa kuwa hospitali hiyo itakamilika na kuanza kazi baada ya miaka miwili.

 

Pamoja na hayo, Dk. Prasad alieleza kuwa Mtandao wa Hospitali za Apolo unajumla ya hospitali 55 na kusisitiza kuwa katika nchi za Asia, Apollo ni mtandao mkubwa wa hospitali kutokana na kuwa na hospitali nyingi.

 

Alisema kuwa hivi sasa mtandao huo umekuwa na kuweza kutoa huduma bora zaidi na kusisitiza kuwa kutokana na mashirikiano na uhusiano mwema uliopo kati ya Apollo na Wizara ya Afya ya Zanzibar mafanikio zaidi yatapatikana.

 

Uongozi huo ulieleza kuwa  kumekuwa na uhusiano na mashirikiano mazuri kati ya Wizara ya Afya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala zima la kuimarisha huduma za afya sanjari na kutoa huduma za tiba kwa wananchi mbali mbali kutoka Tanzania.

 

Sambamba na hayo, uongozi huo ulimueleza Dk. Shein kuwa miongoni mwa malengo ya safari yao ya kuja Zanzibar ni pamoja na kukaa na uongozi wa Wizara ya Afya ya Zanzibar kuangalia na kujadiliana juu ya mchakato mzima wa kuimarisha mahusiano katika kuimarisha sekta afya kati ya Zanzibar na Mtandao wa Hospitali za Apollo.

 

Kwa upande wake Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa uongozi huo wa Hospitali za Apollo kwa ujio wao huo hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na mashirikiano makubwa inayotoa katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini.

 

Alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakifaidika kwa kiasi kikubwa na huduma za afya inayotolewa na Mtandao wa hospitali hizo ambazo makao makuu yake yapo nchini India na kueleza kuwa azma yao ya kuanzisha kutoa huduma za afya hapa Tanzania kwa kujenga hospitali ambayo itakuwa tayari baada ya miaka miwili ni jambo la busara na la kuungwa mkono.

 

Dk. Shein alisema kuwa kwa kipindi kirefu Zanzibar imekuwa na uhusiano na mashirikiano mazuri na Hospitali za Apollo nchini India kiasi ambacho wagonjwa wengi kutoka Zanzibar wamekuwa wakipelekwa katika hospitali za Apollo na kuridhishwa na tiba wanazopata.

 

Aidha, Dk. Shein alimueleza uongozi huo kuwa mashirikiano na mahusiano hayo yatasaidia zaidi juhudi za Serikali ya Mapinduzi za kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuimarisha chuo chake cha mafunzo ya Udaktari kinachoendeshwa kwa mashirikiano ya Serikali ya Cuba.

 

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mikakati thabiti ya kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo cha kutoa huduma za utibabu wa maradhi ya saratani, huduma za utibabu wa maradhi ya figo na maradhi ya moyo.

 

Katika maelezo yake pia, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mafunzo kwa madaktari wake yanapatikana ambapo kwa hivi sasa imekuwa ikikiimarisha chuo chake cha Sayansi ya Afya kilichopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

 

Alisistiza kuwa mbali ya hatua hiyo pia, serikali imo katika mikakati ya kukipanua chuo hicho kwa kuongeza idadi ya wanafunzi, kuwaongeza walimu wa kufundisha masomo ya fani mbali mbali kwa kiwango cha Shahada

Advertisements