Mtangazaji mkongwe Zanzibar, Joseph Caitan Asama(79) amefariki dunia jana mchana huko nyumbani kwake Mbweni Zanzibar.

Marehemu Asama alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu na alizidiwa jana mchana wakati akiwa katika matayarisho ya kwenda Hospitali Mnazi Mmoja kwa matibabu na hatimaye kufariki dunia.

Misa ya marehemu Joseph Caitan Asama itafanyika kesho mchana  katika Kanisa la Anglikana  Mbweni nje kidogo ya Manispaa ya Zanzibar na kutarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Mwanakwerekwe Unguja saa 9:00 Alasiri.

 

Viongozi mbalimbali wa juu wa Serikali pamoja na wananchi wanatarajiwa kuhudhuria katika mazishi ya mtangazaji huyo mkongwe wa Sauti ya Tanzania Zanzibar, marehemu Joseph Asama.

Joseph Asama, alizaliwa tarehe 12/07/1932 Kisima Majongoo Unguja na   ni miongoni mwa  wa watangazaji wa mwanzo katika Tasnia ya Utangazaji  kwa wakati huo Visiwani Zanzibar. Alianza kazi katika miaka ya mwishoni mwa hamsini katika Idara ya Habari na Utangazaji akiwa katika sehemu ya Utangazaji ya Sauti ya Unguja kabla ya kuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar.

Ukiacha uzoefu katika utangazaji, marehemu Joseph Asama alikuwa  Mkuu wa vipindi wa STZ, Mwandishi wa Habari  wa Rais wa Zanzibar na Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi,Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Utangazaji pamoja na kuwa Afisa Uhusiano wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar.

Marehemu Joseph Asama, ameacha kizuka mmoja na watoto wawili.

Advertisements