UINGEREZA imeahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake  uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi kuendelea kuunga mkono uimarishaji  miradi ya maendeleo ukiwemo mpango wa kusomesha lugha ya kiengereza kwa skuli za Zanzibar.

 

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Dianne Conner, aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

 

Katika  mazungumzo yake, Balozi Corner alisema kuwa  Uingereza inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar ambao ni wa kihistoria na kuahidi kuuimarisha zaidi hasa katika kuunga mkono miradi ya maendeleo.

 

Alisema kuwa nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano na misaada yake kwa skuli za Zanzibar kwa lengo la kuimarisha lugha ya kiengereza.

 

Balozi Corner alisema kuwa Uingereza itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania ikiwemo Zanzibar kutokana na nchi hiyo kuwa mdau mkubwa wa Tanzania.

 

Alisema kuwa katika juhudi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano ulipo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar nchi yake  pia, imeahidi kuendelea kuiunga mkono bajeti ya  Tanzania.

 

Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii, Balozi Corner alipongeza na hatua zinazochukuliwa na serikali  katika kuimarisha sekta hiyo na kuahidi kuitangaza Zanzibar  nchini mwake ili watalii wengi kutoka nchi hiyo waweze kuitembelea Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

 

Katika mazungumzo hayo pia,  Balaozi Corner aliendelea kutoa pongezi kwa mara nyengine tena kwa Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi uliokuwa wa amani na utulivu mkubwa.

 

Pamoja na hayo, Balozi Corner alifurahishwa na mipango ya maendeleo ya Mji Mkongwe iliyowekwa na serikali pamoja na historia ya mji huo na kuahidi kuunga mkono juhudi zote za kuimarisha mji huo.

 

Balozi huyo pia, alieleza haja ya kuendelea kutunzwa na kutangazwa zaidi kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar  kutokana na historia na haiba yake sanjari na mambo mengine  yaliomo ndani yake.

 

Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa salamu zake za shukurani kwa Balozi huyo pamoja na uongozi wa nchi hiyo kwa juhudi zake za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake wa kihistoria na Zanzibar.

 

Alieleza kuwa Zanzibar inatambua kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Uingereza ni wa kihistoria na ndio maana inaona haja  ya kuendelea kuuimarisha zaidi.

 

Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi ya Uingereza kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo sanjari na hatua yake ya kuendelea kuisaidia bajeti ya Tanzania.

 

Dk. Shein alimueleza Balozi Corner kuwa juhudi kubwa zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo ambapo hatua ya nchi hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kutasukuma na kuendeleza mbele juhudi hizo.

 

Alisema kuwa  serikali anayoingoza imekuwa ikifanya kazi kwa pamoja na mashirikiano makubwa kwa kutambua kuwa mafanikio yanayopatikana ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.

 

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliendelea kusisitiza kuwa amani na utulivu iliyopo Zanzibar ni njia moja wapo ya kuzidisha na kuimarisha maendeleo yaliofikiwa.

 

Kwa upande wa Mji Mkongwe wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuuhifadhi na kuulinda mji huo kutokana na umuhimu wake mkubwa.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni kuendeleza juhudi za makusudi katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na uhifadhi wake na ndio maana serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha sekta ya kilimo na sekta nyenginezo hapa nchini.

 

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisistiza kuwa serikali imeweka vipaumbele  katika sekta zote za maendeleo hapa Zanzibar kwa kutambua umuhimu wake mkubwa katika maendeleo ya nchi na wananchi wake.

Advertisements