CHINA imeahidi kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kueleza azma yake ya kuekeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo. Balozi mdogo mpya wa China Bi Chen Yiman aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar. Balozi Yiman alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa kuongeza idadi ya madaktari ambao watawahusisha madaktari waliopata mafunzo ya lugha ya kiswahili ili iwe rahisi kuwasiliana na jamii wakati wanapotoa huduma za afya. Katika uungwaji mkono huko Balozi huyo pia, alieleza mpango wa nchi hiyo wa kupanua na kuweka vifaa vipya na vya kisasa katika hospitali ya Abdalla Mzee, Mkoa Pemba. Aidha, alisema kuwa nchi yake itasaidia kuanzisha Idara ya majeruhi na matibabu ya dharura katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja na Hospitali ya Abdala Mzee iliyopo Pemba. Balozi Yiman alisema kuwa China imefurahishwa na uhusiano uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa katika hatua za kuzidisha uhusiano huo nchi hiyo inatarajia kuleta jopo la wawekezaji kwa madhumuni ya kuzungumza na Mamlaka ya Vitega Uchumi na Maeneo Huru Zanzibar (ZIPA) juu ya maeneo ya uwekezaji na masharti yake. Alieleza kuwa miongoni mwa shughuli kubwa watakazofanya wawekezaji hao wakati watakaofika Zanzibar ni pamoja na kuangalia bidhaa za viwanda kwani nchi hiyo imeshaonesha utayari wa kununua mazao ya viungo yanayopatikana Zanzibar. Kwa vile China tayari imeshapiga hatua katika sekta ya Utalii pia, nchi hiyo imekubali kuwahamasisha watalii na wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuitembelea na kuekeza katika sekta hiyo hapa Zanzibar. Balozi huyo alieleza kuwa China ina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na Zanzibar hasa katika uimarishaji wa sekta za maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo sekta ya afya, elimu, habari, maji na nyenginezo ambazo China iliahidi kuendela kuzisaidia kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana hapa nchini. Kwa upande wa sekta ya elimu alisisitiza azma ya kuongeza nafasi za masomo pamoja na kujenga skuli nyengine ya kisasa kama ile iliyojengwa kwa msaada wa nchi hiyo huko Kijichi nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Kutokana na ushirikiano mwema uliopo kati ya nchi mbili hizo ikiwemo sekta ya habari China imeahidi kuendelea kuisaidia sekta hiyo. Pamoja na hayo, Balozi huyo alisisitiza kuwa nchi yake itasaidia kuwajengea uwezo wataalamu wazalendo kwenda kujifunza nchini humo pamoja na kuahidi kuendelea kutoa misaada yake kwa Zanzibar ikiwemo kusaidia miradi ya usambazaji maji vijijini. Nae Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara yake ya Afya ina lengo la kuanzisha kitengo cha kushughulikia maradhi ya figo, moyo na saratani hivyo ahadi hiyo ya china ya kuiunga mkono sekta hiyo kutasaidia kufikia lengo lililokusudiwa. Aidha, Dk. Shein alitoa shukurani na pongezi kwa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa kuweza kutoa misaada yake mbali mbali ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na ahadi yake ya kuisaidia sekta ya afya pamoja na vifaa katika hospitali za MnaziMmoja na hospitali ya Abdalla Mzee. Alisema kuwa kwa upande wa hospitali ya MnaziMmoja serikali inaendelea na mikakati ya lengo lake la kuifanya hospitali hiyo kuwa ya hospitali ya rufaa na ile ya Abdalla Mzee kuwa hospitali ya Mkoa Dk. Shein alisema kuwa hatua ya China kuleta ujumbe wa wawekezaji na wafanyabiashara itasaidia kuimarisha sekta hizo za maendeleo ambapo kwa kupitia (ZIPA), wawekezaji hao watapata kujua kanuni na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya uwekezaji hapa Zanzibar. Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii hivyo ni fursa nzuri kwa watalii wa China kuja kuitembelea Zanzibar. Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itampa mashirikiano makubwa Balozi huyo ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi. Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano mkubwa wa kihistoria uliopo kati yake na China ambao aliahidi kuendelezwa.

Advertisements