RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, amewataka watendaji wakuu wa serikali kuzianika mchana taarifa za serikali kwa vyombo vya habari na haitavumilia kuona maafisa wake wanaendeleza tabia ya kuficha ama kuwakimbia waandishi wa habari.

 

Dk .Shein, alitoa kauli hiyo jana katika kikao cha majumuisho ya ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa Mjini Magharibi, mapema wiki hii, kwa kukagua shughuli za maendeleo za Mkoa huo katika Sekta ya Afya, Elimu, Kilimo na shughuli za kijamii.

 

Kikao hicho kiliwashirikisha watendaji wakuu wa serikali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Masheha, na baadi ya watendaji katika taasisi mbali mbali za serikali na Vyama.

 

Alisema ni lazima kwa watendaji wa serikali kubadilika kuona wanashirikina na vyombo vya habari kwa kuwaeleza maendeleo ya serikali badala ya kujenga tabia ya kuwakimbia kwani serikali inajiandaa kutoa habari kwa wananchi bila ya kuficha.

 

Alisema anashangaa kuona baadhi ya watendaji wamekuwa wanashindwa kutumia vyombo vya habari kuelezea mafanikio yaliofikiwa na serikali wakati wakijua serikali ina mambo mengi ambayo wananchi wanahitaji kuyaelewa.

 

Alisema tabia ya kukimbia kuzungumza na vyombo vya habari kwa mambo ya serikali inaweza kabisa kusababisha jamii kukosa taarifa za nchi yao na kuwepo mambo ya uongo wanayopewa jamii.

 

“Habari za uongo zipo nyingi iko siku nitasema wanatia chumvi maana haukujasikika kujibu wanapokuwa hawana uhakika waje watuulize wakati wa propaganda za siasa umekwisha vyombo vya habari ni marafiki wa serikali lazima wajenge uzalendo kwa wananchi wetu” alisema Dk. Shein.

 

Akiendelea alisema kuwa kazi ya kutoa habari ni lazima ifanyike kwani ndio njia pekee itayoweza kusaidia kuifanya jamii kufahamu nini serikali yao inawafanyia katika kuwapatia maendeleo yao.

 

Dk Shein katika kulifanyia kazi suala hilo alisema kuanzia sasa serikali inamtaka kila Mkuu wa Wilaya, Mkoa na Masheha na Watendaji wa serikali kuona wanalitekeleza hilo wakati wowote.

 

“Sasa serikali inaamua kusema mambo yake tutaunda utaratibu wa kutoa habari yoyote ya serikali hatuna haja ya kuficha mchna wala asubuhi tunajipanga kwani habari ni muhimu kwa maendeleo ya jamii” Alisema Dk Shein.

 

Alieleza kuwa analazimika kulisisitiza hilo ikiwa ni moja ya jambo la msingi kwani hawawezi kwenda na mfumo wa sasa wa kuficha mambo kutokana na ulimwengu wa sasa unataka kuwapo kwamfumo wa teknohama kwa kupeleka  mawasiliano katika jamii na sio kubakisha katika serikali pekee.

 

Alisema kwa kuzingatia hilo serikali inajiandaa kuona inawatumia maafisa uhusiano waliopo katika maidara ya serikali kutoa taarifa kwa kila kipindi na ikiwezekana kwa kila mwezi.

 

Hata hivyo Dk. Shein, aliwataka watendaji hao kuacha woga wakijiona wameandikwa sivyo wanavyotaka na badala yake watumie fursa hizo kwa kuelezea ukweli.

 

“Matumaini yangu tunawatumikia Wazanzibari mengine yanayosemwa yaachane ya magezeti ukweli nitakwambieni mimi mwenyewe nitasema na nyinyi mtasema jipangeni kwa hilo” alisema Dk. Shein.

 

Dk Shein alisema wasilione suala hilo zito kwani hata pale serikali inapokosea basi wakubali kusemwa kwani hivyo ndivyo dunia inavyoenda na wanahitaji kuona wanabadilika kwa kuwafanya waandishi wa habari kuwa ni marafiki zao badala ya kuwakimbia.

 

 

Dk. Shein alikamisha zira hiyo baada ya kukitembelea kituo cha Afya cha Mpendae, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani, Skuli ya Chekechea ya Meya, Uwanja wa Mnazi mmoja, Bwawa la Hoteli ya Bwawani, Bonde la Mpunga Mtwango na Bumbwisudi, Hospitali ya Mbuzini, Kukagua uwanja wa Timu ya Bweleo na Skuli ya Maandalizi ya Bweleo

Advertisements