KAMPUNI ya Uwekezaji ya TAWASOOL yenye makao makuu yake Dubai imeeleza nia yake ya kuekeza katika sekta mbali mbali za maendeleo Unguja na Pemba zikiwemo sekta za uvuvi, ufugaji, viwanda, kilimo, Benki, ujenzi, usafiri na usafirishaji.

 

Akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dk. Ali Mohamed Shein  kiongozi wa ujumbe maalum uliofika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo hayo Dk. Ehsan Ravari alieleza kuwa Kampuni yake imevutiwa kuja kuekeza Zanzibar.

 

Dk Ravari alisema kuwa kampuni yake tayari imeshaangalia maeneo ya kuekeza ikiwa ni pamoja na maeneo ya uvuvi na ufugaji ambapo alisema kuwa Kampuni hiyo ina uzofu mkubwa katika sekta hizo.

 

Akieleza juu ya sekta hizo mbili muhimu Dk. Ravari alisema kuwa kampuni ya TAWASOOL ina uzofu mkubwa juu ya masuala ya uvuvi na ufugaji sanjari na usafiri na usafirishaji kwa njia za anga, bahari na hata nchi kavu.

 

Walieleza kuwa tayari wameshatembelea na kuangalia maeneo katika kisiwa cha Pemba pamoja na Unguja na kilichobaki hivi sasa ni kuangalia namna ya utekelezaji kwa kupitia taratibu zinazohusika.

 

Akieleza juu ya sekta ya ujenzi alisema kuwa kampuni ya TAWASOOL tayari ina uzoefu mkubwa katika masuala ya uekezaji kwenye sekta ya ujenzi ambapo hivi sasa ina matawi yake makubwa ya uuzaji wa vifa vya ujenzi nchini Iran, Abudhabi  na sehemu nyengine duniani.

 

Alisema kuwa  katika kuhakikisha kampuni yake inaekeza hapa Zanzibar hatua mbali mbali atazichukua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anatoa mafunzo kwa wafanyakazi wake pamoja na kujenga hospitali ambazo zitatoa huduma za afya kwa wafanyakazi wake na jamii kwa jumla.

 

Dk. Ravari alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Kampuni yake pia, ina uzoefu mkubwa katika  masuala ya uekezaji katika Mabenki na Bima na kueleza kuwa katika sekta ya viwanda kampuni hiyo imeona haja ya kuekeza viwanda vya matunda na vyakula.

 

Aidha, kiongozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa wanamatarajio makubwa ya kuendelea kupata mashirikiano ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa zaidi na kusifu mashirikiano ambayo kwa hivi sasa wanayapata hasa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

 

Sambamba na hayo, Dk. Ravari alimuhakikishia Dk. Shein kuwa kampuni yake itashirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.

 

Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa shukurani zake kwa ujio huo wa uongozi wa Kampuni ya TAWASOOL pamoja na kueleza nia yao ya kuekeza hapa Zanzibar.

 

Katika maelezo yake  Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  kupitia Mamlaka ya Maeneo Huru na Vitega Uchumi  Zanzibar (ZIPA), imeweka mazingira mazuri ya kuhakikisha inawapa maelekezo na miongozo wawekaji.

 

Alieleza kuwa kwa upande wa uwekezaji kwenye sekta za uvuvi na ufugaji Zanzibar ina maeneo mazuri ambayo yanaweza kuwavutia wawekezaji.

 

Dk. Shein alieleza kuwa uvuvi pia, una nafasi nzuri ya uwekezaji hapa Zanzibar kwani bado sekta hiyo haijapata mafanikio makubwa hasa katika uvuvi wa bahari kuu ambao unahitajia utaalamu na vifaa vya kisasa.

 

Kwa upande wa kilimo, alisisitiza haja ya kuekeza hasa katika kilimo cha matunda na viungo ambapo  kuna matumaini kuwa mafanikio makubwa yatapatikana.

 

Alisema kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake na wawekezaji kutoka maeneo mbali mbali duniani na kueleza kuwa azma ya kambuni ya TAWASOOL ya kuja kuekeza katika visiwa vya Unguja na Pemba itapewa ushirikiano mzuri na serikali anayoiongoza.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa serikali itaendelea kuhakikisha kuwa mali za wawekezaji zinalindwa na kupewa haki zote za msingi kwa mujibu wa sheria na taratibu za uwekezaji zilizowekwa hapa Zanzibar.

 

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imedhamiria kuifanyia ukarabati mkubwa hospitali ya Wete ili iendelee kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo ya jirani na kurudi hali yake ya zamani katika utoaji wa huduma hiyo ya afya.

 

Kutokana na hatua hiyo Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa azma ya kampuni hiyo kuekeza katika sekta ya uwekazaji itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kufikia lengo hilo.

Advertisements