Eneo la hospitali ya Chakechake Pemba

Wafanyakazi 21 waliopelekwa hospitali ya Chakechake Pemba wakitokea Unguja wamekosa makazi ya kudumu baada ya kuwasili kisiwani humo kufanya kazi.

Wakizungumza na wandishi wa habari wafanyakazi hao wamesema tangu kuwasili kisiwani humo wamekuwa na tatizo la makazi jambo ambalo ni kinyume walivyoahidiwa.

Walifahamisha kabla ya kuwasili katika kituo hicho cha kazi waliahidiwa kupatiwa makazi pamoja na huduma muhimu wanazopaswa kupewa.

Kutokana na hali hiyo wafanyakazi hao wamesema wanalazimika kukaa chumba kimoja watu watano huku wakikabiliwa na tatizo la maji na umeme.

Wamesema tangu wafike Pemba wameshahama nyumba mara nne ndani ya wiki moja hali inayowasababishia kuongezeka kwa gharama za matumizi ya chakula na usafiri.

Nae daktarai dhamana wa hospitali hiyo Sauda Kassim amesema suala la makaazi kwa wahudumu hao wanalifanyia kazi na tayari wameshakutana na kamati ya wilaya kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi.

Hata hivyo amesema suala la kuwasili kwa wafanyakazi hao katika hospitali ya Chakechake ni faraja kutokana na uhaba wa wahudumu uliopo kwa muda mrefu.

Hivyo amewataka wafanyakazi hao pamoja na matatizo walionayo wawe na moyo wa subira huku viongozi wao wakiendelea kuyatafutia ufumbuzi.

Advertisements