Wananchi waliovunjiwa nyumba zao katika maeneo ya Mtoni Kidatu wametishia kuishtaki serikali ya Mapinduzi Zanzibar endapo hawatalipwa fidia baada ya kubainika nyumba zao zilivunjwa kimakosa.

Mwenyekiti wa kamati ya waathirika hao Ali Shamte Nahodha amesema tokea nyumba zao walipovunjiwa mwaka 1996 hadi sasa hajalipwa fidia licha ya kuahidiwa na serikali kulipwa.

Amesema kamati hiyo ilimuandikia barua katibu wa baraza la mapinduzi na katibu mkuu kiongozi, na kutakiwa wasubiri katika kipindi kifupi, lakini hadi sasa bado hawajalipwa.

Mwenyekiti huyo amesema kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 wamekuwa wakifuatilia malipo yao, huku wengine wakiwa wameshafariki dunia na waliobaki wanaendelea kuhangaika kutokana na kukosa makazi.

Kwa mujibu wa Nahodha ripoti iliyotolewa na tume iliyokuwa ikishughulikia muafaka mwaka 1998 ilitaka wathirika hao walipwe fidia ya thamani ya nyumba zao kufuatia kufanywa tathmini.

Jumla ya nyumba mia saba na 72 zilivunjwa katika eneo la Kidatu Mtoni tokea mwaka 1996 wakati wa utawala wa Dr. Salim Amour Juma kwa madai sehemu hiyo  haikuruhusiwa kujengwa nyumba za kuishi watu

Advertisements