Balozi Seif Ali Iddi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi amekemea vikali juu ya tabia mbaya ya baadhi ya watendaji wa Serikali ya kukiuka sheria na taratibu za nchi kwa makusudi ili kuwanufaisha baadhi ya wakubwa.

Makamu huyo wa Pili wa Rais aliyasema hayo alipokutana na Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, hapo Ofisini kwake Vuga.

Alisema kuwa ni jambo la aibu linalofanywa na baadhi ya wanaowania uongozi wakati wa uchaguzi na kuwaomba kura wananchi na baadaye kuwanyanganya haki zao.

“Inasikitisha sana na ni jambo la aibu tunavyofanya baadhi yetu ya kuomba kura wakati wa uchaguzi na baada ya kuchaguliwa kuwanyanganya watu haki zao,” alisema Balozi Iddi.

Alieleza kuwa amegundua sehemu za wazi nyingi wanazopewa wakubwa zinatolewa na vibali halali za mamlaka husika wakati watoa vibali hao na wanaopewa wote wanafahamu kuwa ni kinyume cha sheria.

Hivyo amesema Serikali haitavumilia suala hilo, na alitoa mfano wa viwanja vya kwa Mchina ambako alishauri kama patahitajika kujengwa basi bora Serikali yenyewe ijenge Taasisi itayowahudumia jamiii kwa ujumla.

Kabla ya hapo Mwenyeketi wa Kamati hio Mhe. Makame Mshimba Mbarouk pamoja na Naibu wake Mhe. Rashid Seif walieleza kero zao ikiwa ni pamoja na masuala ya ujenzi wa sehemu za wazi na kupuuzwa kwa ripoti zao za kamati na Wizara husika.

Aidha, kuhusu ripoti za Kamati za Baraza kutoshughulikiwa na Wizara husika Mhe. Balozi Iddi alieleza kusikitishwa kwake na jambo hilo na kusema kuwa Kamati ni muhimu sana kwa kusaidia Serikali na kupunguza makero ya wananchi.

Kwa hivyo aliahidi kulifuatilia suala hilo na kuhakikisha ripoti za Kamati za Baraza zinazingatiwa ipasavyo na kufanyiwa kazi.

Advertisements