Chama cha Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar
(WAHAMAZA)

25 Mei, 2011

Kuh: Kukamatwa Haji Bwegege, TBC

Chama cha Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA) kimesikitishwa
na tukio la kukamatwa Mwandishi Haji Bwegege wa Shirika la Utangazji
Tanzania (TBC)  jana Mei 24 wakati akiwa kazini.

Kitendo cha kukamatwa Haji Bwegege kimetokea katika eneo la Makontena
Darajani wakati akifanya kazi yake halali na katika eneo ambalo
halilindwi kisheria.

Mwandishi huyo alikuwa akifuatilia kadhia ya Makontena ambayo kwa
hakika Mahakama Kuu ya Zanzibar tayari imeshatoa amri kuwa Makontena
hayo yaliokuwa yamefungiwa na Manispaa ya Zanzibar yafunguliwe wakati
shauri la kesi iliyo Mahakmani iliyofunguliwa na Wafanyabiashara hao
likisubiri kusiki8lizwa.

Mwandishi alikuwa akifanya wajibu wake kuona kuwa amri ya Mahakama
inatekelzwa katika hali ambayo ni wajibu wa taasisi za Serikali kuwa
mfano wa Utawala Bora, ambapo amri ya Mahakama iliyotolewa Alkhamis
iliypita hadi jana ilikuwa bado haijatekelezwa.

Wana vikosi wanaofanya lindo katika eneo hili hii ni mara ya pili
kunyanyasa waandishi wa habari wanapofika katika eneo hilo , mara ya
kwanza ikiwa ni dhidi ya Mwandishi Munir Zakaria wa Channel Ten.

Jambo hili halikubalika hata kidogo tukijua kuwa Rais wa Zanzibar Dk
Ali Muhammed Shein katika hotuba yake ya kuingia Serikali alisema kuwa
utawala wake utakuwa karibu na vyombo vya habari na utaheshimu uhuru
wa vyombo vya habari.

Haya yakitokea waandishi wa habari wa Zanzibar kwa ujumla hawaridhiki
na namna wanavyowekwa kando na mfumo mzima wa Serikali ya zanzibar na
kwa ujumla ikiwawia vigumu kupata habari, kama alivyotanbahisha Dk
Shein alipozungumza na watendaji wa Serikali baada ya semina elekezi
lakini pia kurudia baada ya ziara yake ya Mkoa Mjini Magharibi.

WAHAMAZA inatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua ya kutoa maelekezo
kwa vyombo vya ulinzi vikiwemo Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na kuwawacha waandishi
wa habari wafanya kazi yao kama mhimili wa nne wa dola.

Pia WAHAMAZA inapenda kutoa wito wa Serikali kujivua gamba katika
suala zima la kutoa habari na kufungua milango kwa wananchi, ambao
hivi sasa miezi sita tokea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,
hawajui mengi kuhusu Serikali yao na kwa hivyo si waelewa wa
kilichofanyika na kisichoweza kufanyika hadi sasa, lakini zaidi kwa
sababu gani na huku hali yao ya maisha ikiwa ngumu zaidi.

WAHAMAZA inapenda kutoa ahadi kuwa iko tayari kufanya kazi na Serikali
kwa karibu zaidi kwa kuelewa kuwa vyombo vya habari ni kiungo muhimu
baina ya Serikali na wananchi na tunajua kuwa Serikali iliyochaguliwa
na watu haitaki kujitenga na wapiga kura na wananchi.

Katibu wa WAHAMAZA

………………..

Salma Said

Advertisements