MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar,amesema azma ya Marekani kuisaidia Zanzibar katika sekta ya kilimo cha uwagiliaji maji na uhifadhi wa chakula, itasaidia sana wakati huu, ambapo Zanzibar imo katika jitihada za kujitosheleza kwa chakula.

Maalim Seif amesema hayo leo ofisini kwake Migombani, wakati alipokutana na ujumbe kutoka Shirika la misaada la Kimataifa la Marekeni (USAID).

Ameueleza ujumbe huo kuwa uamuzi wa Shirika hilo kusaidia katika mradi wa kilimo cha umwagiliaji, hususan katika zao la mpunga ni muhimu kwa vile Serikali tayari imetenga kiasi cha hekta nane kwa ajili ya kuendeleza kilimo hicho, ili kupunguza kasi ya uagiziaji wa mchele kutoka nje.

Alisema wakati huu nchi inakabiliwa na mfumko mkubwa wa kupanda kwa bei za bidhaa ikiwemo mchele, kutokana na uzalishaji duni wa chakula hicho tofauti na mahitaji yaliopo.

Alisema baadhi ya maeneo ya nchi kama vile Micheweni,Mkoa wa Kaskazini Pemba, hali ni mbaya kukiwa na ongezeko kubwa la utapia mlo kwa watoto.

Akizungumzia uzalishaji wa mboga mboga uliomo katika mradhi huo, Maalim Seif alisema ni muhimu sana kwa vile baadhi ya Mahoteli ya kitalii yaliopo, hutegemea zaidi bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Hata hivyo Makamu wa Kwanza wa Rais, aliuomba ujumbe huo kuzingatia suala la kuipatia Zanzibar kasma yake,kama hatua ya kuepuka “kusahauliwa” wakati  wa utekelezaji wa mradi huo unaohusisha sehemu ya pili ya Muungano.

Alisema suala la Kilimo sio la Muungano, hivyo ni vyema Zanzibar ikatengewa kasma yake kama nchi, ili kuepuka sintofahamu wakati wa utekelezaji.

“Kuna masuala ya Muungano na yasio ya Muungao, Kilimo sio suala la Muuungano, Zanzibar ina mambo yake , ni vyema ikapewa kasma yake kuepusha kusahauliwa wakati wa utekelezaji”, alisema.

Akizungumzia mradi wa elimu utakaohusisha matumizi ya Teknolojia ya Komputa maskulini (education for 25 th Century),alisema ni muhimu katika karne hii ya 21wakati Dunia ikiwa imejikita katika matumizi ya teknoljia ya Habari na Mawasiliano.

Alisema hatua hiyo italeta mustakbali mzuri na faida kubwa kwa kizazi kijacho.

Kuhusiana na mradi wa Afya,Maalim Seif alipongeza Shirika hilo kutokana na msaada mkubwa katika udhibiti wa ugonjwa wa Malaria, kushuka hadi kufikia asilimia moja.

Alishauri mradi huo kuendelezwa kwa kuzingatia kuwa hivi sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa la mazalia ya mbu, wakiwemo wale wanaosababisha Malaria.

Katika hatua nyingine Maalim Seif, aliliomba shirika hilo kutupia macho changamoto mbali mbali zinazoikabili Zanzibar zikiwemo za uharibifu wa kimazingira, zinazotokana na binaadamu.

Akitolea mfano, Maalim Seif alisema kumekuwepo wimbi kubwa la ukataji wa mikoko kisiwani Pemba, hatua inayopelekea maji ya bahari kupanda na kumega maeneo ya ardhi.

Alisema Serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua juhudi za kuwashajiisha wananchi kupanda miti kwa wingi ili kuepusha uwepo wa jangwa au mmong’onyoko wa ardhi.

Mapema Kiongozi wa ujumbe huo kutoka Shirika la misaada la Kimataifa la Marekani (USAID) Robbert Cunnane, alisema Shirika hilo linalenga kusaidia Zanzibar katika miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji, uzalishaji wa mboga mboga pamoja na huduma za Afya.

Alisema mradi wa elimu,utatoa fursa kwa walimu wa Zanzibar kupata mafunzo na hatimae kuweza kufundisha wanafunzi kupitia mtandao.

Alisema matumizi ya vyandarua vyevye dawa yataendelezwa kwa kuzingatia kuwa mbali na kuwa kinga lakini pia vinaua mbu na hivyo kupunguza hatari ya kuongezeka kwa ugonjwa wa Malaria.

Alifafanua kuwa katika mradi wa kilimo cha  umwagiliaji maji pia utahusisha na kilimo cha zao la Mahindi.

 

 

 

 

 

 

Advertisements