MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad,amewataka wawekezaji kutoka China kuja Zanzibar kuwekeza katika nyanja mbali mbali za kiuchumi.

Maalim Seif ametoa changamoto hiyo leo,ofisini kwake Migombani wakati alipozungumza na Balozi mdogo wa China aliopo Zanzibar, Chen Qiman, aliefika kujitambulisha.

Amesema visiwa vya Zanzibar vyenye hali ya hewa nzuri na ya kupendeza, vimebarikiwa kuwa na amani pamoja na vivutio vingi vya uwekezaji, hususan katika sekta ya Utalii,hivyo ni fursa nzuri kwao kuja kuwekeza.

Alisema China inaweza kuimarisha uhusiano wake wa muda mrefu na Zanzibar, kwa kuanzisha kituo cha uwekezaji na kuwashajiisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuwekeza na kupata faida.

Alisema uvuvi wa bahari kuu ni moja kati ya eneo linalohitaji uwekezaji, kwa kuzingatia hazina kubwa ya samaki iliopo ambayo imekuwepo bila kutumika kwa kipindi kirefu.

Alimuomba Balozi huyo kukutana na viongozi wa mamlaka ya Vitega Uchumi na Maeneo Huru (ZIPA) ili kupata taarifa za kutosha juu ya maeneo ya kuwekeza na kanuni zilizopo.

Maalim Seif aliishukuru Serikali ya China kwa misaada yake ya kiuchumi na kijamii kwa Zanzibar katika nyanja za elimu, afya,kilimo cha umwagiliaji maji na zana za kilimo,Teknoojia ya habari pamoja na michezo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi itatoa kila ya mashirikiano kuona miradi na misaada yote iliolengwa kutolewa inafanikishwa kama ilivyopangwa.

Katika kukuza ushirikiano wake na Zanzibar, aliiomba nchi hiyo kutanua wigo na kuelekeza misaada yake katika nyanja nyengine mpya.

Mapema Balozi Chen, alimweleza Makamo wa Rais kuwa hatua ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi mbili hizo ni moja kati ya malengo makuu ya nchi yake.

Alisema China itaendelea na juhudi za kuisaidia Zanzibar katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii, ikiwemo uimarishaji wa huduma za Afya.

Alisema inalenga kuongeza Madaktari kwa kuwahusisha wale waliopata mafunzo ya lugha ya Kiswahili, iwe rahisi kwao kuwasiliana moja kwa moja na wagonjwa wakati wa utoaji huduma za afya.

Aidha alisema nchi yake inakusudia kuanzisha idara ya majeruhi na matibabu ya dharura katika Hospitali ya Mnazi mmoja na kuiimarisha Hospitali ya Abdalla Mzee ilioko Pemba pamoja na kusaidia vifaa mbali mbali na madawa.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Balozi huyo ameahidi nchi yake kuipa msukumo Zanzibar kwa kujenga skuli nyingine ya kisasa kama iliokwisha kujenga kabla katika eneo la Kijichi.

Katika hatua nyingine inayoonekana hatua ya kupanua wigo zaidi ya ushirikiano kati ya nchi mbili hizo katika miradi mipya, China imeahidi kusaidia uwekaji wa taa (street light) katika maeneo ya mitaani katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar, kwa kutumia nishati ya nguvu za jua.

Balozi huyo alimweleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa mazungumzo rasmi juu ya utekelezaji wa mradi huyo yameshafanyika kati yake na mstahiki Meya wa Jiji wa Zanzibar.

 

 

Advertisements