0
JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA UCHUMI
MHESHIMIWA MUSTAFA HAIDI MKULO (MB)
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA
YA FEDHA NA UCHUMI
KWA MWAKA 2010/11
Dodoma
JULAI, 2010
1
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato, Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha 2010/11.
2. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Kamati za Bunge, kwa kuendesha majadiliano ya bajeti ya mwaka 2010/11 kwa umakini tangu yalipoanza hadi sasa. Aidha, nawashukuru Wajumbe wa Kamati mbalimbali za Bunge kwa michango na ushauri waliotoa wakati wa kupitia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara, Idara na Mikoa. Michango na ushauri wao utaendelea kuboresha utendaji wa serikali katika kutoa huduma kwa umma.
3. Mheshimiwa Spika, vile vile, nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa namna ya pekee Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Abdallah Omar
2
Kigoda Mbunge wa Jimbo la Handeni kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa. Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati katika kuandaa hotuba hii, pia napenda kueleza kuwa maoni hayo pamoja na yale yatakayotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili hoja hii yataendelea kuzingatiwa wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2010/11.
4. Mheshimiwa Spika, naomba pia niwashukuru Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Mheshimiwa Omari Y. Mzee (Mb.) na Mheshimiwa Jeremiah S. Sumari (Mb.) kwa ushirikiano mkubwa walionipa katika kutekeleza majukumu yangu na pia maandalizi ya bajeti hii. Aidha, ninawashukuru wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi zake, chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Bw. Ramadhani M. Khijjah, na Naibu Makatibu Wakuu Bw. John M. Haule, Bw. Laston T. Msongole na Dkt. Servacius B. Likwelile, Makamishna na Wakurugenzi kwa kazi nzuri wanayoifanya bila kuchoka. Vile vile, nawashukuru wafanyakazi wa Benki Kuu chini ya uongozi wa Gavana Prof. Benno Ndulu na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania chini ya uongozi wa Kamishna Mkuu Bw. Harry Kitilya kwa kazi nzuri na ushirikiano wao
3
mkubwa. Ninaomba ushirikiano walionipa uendelee ili Wizara iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
UTEKELEZAJI WA MAELEKEZO YA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2005
5. Mheshimiwa Spika, katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005, Wizara ya Fedha na Uchumi imeelekezwa kujikita katika kufanya mambo makuu yafuatayo: kusimamia Uchumi Jumla; kusimamia Bajeti ya serikali; Kuhakikisha sekta za kipaumbele zinapatiwa rasilimali fedha; kuboresha sekta ya fedha; kuboresha huduma kwa wastaafu; na kusimamia Mashirika ya Umma. Katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi mafanikio mengi yamepatikana.
6. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitano (2005 – 2009) uchumi umeendelea kuimarika na Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 7.2 kwa mwaka katika kipindi hicho. Ukuaji huu wa uchumi ulichangiwa zaidi na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika sekta za: viwanda; ujenzi; fedha; na mawasiliano na uchukuzi. Aidha, kutokana na idadi ya watu Tanzania Bara kukadiriwa kuwa milioni 39.3
4
katika mwaka 2009, pato la wastani la kila Mtanzania lilikadiriwa kuwa shilingi 682,737.70 mwaka huo sawa na Dola za Kimarekani 517.6 ikilinganishwa na shilingi 441,030.20 mwaka 2005, sawa na Dola za Kimarekani 392.8.
7. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Wizara ya Fedha na Uchumi, kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imechukua hatua mbalimbali za marekebisho ya sera za kodi na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa lengo la kupanua wigo wa kodi. Hatua hizi ni pamoja na kuhimiza ulipaji kodi kwa hiari na kusimamia Sheria za kodi ambazo zimesaidia kuweka mazingira mazuri zaidi ya uzalishaji na kurahisisha ukusanyaji wa kodi na kuongeza mapato ya ndani. Kufuatia maboresho katika mfumo mzima wa ukusanyaji kodi, mapato ya ndani ya Serikali yameongezeka kwa asilimia 121 kutoka shilingi bilioni 2,124.8 mwaka 2005/06 hadi shilingi bilioni 4,688.3 mwaka 2009/10. Wastani wa makusanyo ya Kodi kwa mwezi yamefikia shilingi bilioni 390 ikilinganishwa na shilingi bilioni 177 kwa mwezi mwaka 2005/06.
8. Mheshimiwa Spika, kuanzishwa kwa Mfuko wa Dhamana wa Mikopo kwa
5
Wafanyabiashara Wadogo na Kati (SME Credit Guarantee Scheme) ambao unaratibiwa na Benki Kuu kumeboresha mazingira ya kupata mikopo kwa wahitaji wa mitaji midogo na ya kati kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha. Tangu Mfuko huu uanzishwe, jumla ya SMEs 48 zimepata udhamini wa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 6.393. Aidha, mikopo hiyo ilielekezwa katika maeneo ya kiuchumi yafuatayo: uzalishaji wa chakula, ujenzi, shughuli za hoteli na utalii, maeneo ya elimu, afya na maji, ufugaji wa kuku, uvuvi, mawasiliano na usafirishaji.
9. Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuboresha huduma kwa wastaafu mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuhamishia huduma ya malipo ya wastaafu kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Wastaafu 53,600 ambao wapo kwenye daftari la pensheni la Hazina, wamehamishiwa katika Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) na wameanza kulipwa Pensheni zao kupitia Mfuko huo kuanzia Julai, 2008. Wastaafu ambao ni askari Polisi na Magereza, wamehamishiwa kwenye Mfuko wa GEPF tangu Januari, 2009. Aidha, viongozi wengine wa Kitaifa wanaendelea kulipwa mafao yao kupitia Hazina. Hadi kufikia
6
Julai, 2009, idadi ya wastaafu waliokuwa kwenye orodha ya kulipwa pensheni na Wizara ya Fedha na Uchumi kupitia Mfuko wa PPF, ilifikia 55,051 ikiwa ni ongezeko la wastaafu 1,451. Ongezeko hili limetokana na wastaafu wapya kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Usalama wa Taifa ambao bado hawajajiunga na utaratibu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na wastaafu wanaorejeshwa kwenye daftari la pensheni la Hazina baada ya kulipwa kwa mkupuo.
10. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni Wastaafu walioko kwenye daftari la Hazina kulipwa pensheni zao kupitia akaunti binafsi badala ya utaratibu wa kulipiwa kwenye kaunta za benki. Utaratibu huo umewawezesha wastaafu kuchukua fedha zao wakati wowote kwa kutumia kadi ya ATM. Aidha, Wizara imeendelea kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za wastaafu walioko kwenye daftari la Hazina kwa kutumia mfumo wa kompyuta. Vile vile, Wizara iliendesha Semina za kikanda, zilizowahusisha waajiri na maafisa wanaoshughulikia mafao na mirathi katika Wizara na Mikoa kuhusu wajibu wao wa kushughulikia mafao ya kustaafu na mirathi.
7
11. Mheshimiwa Spika, katika kubinafsisha Mashirika ya Umma mafanikio mbalimbali yamepatikana. Mashirika yaliyobinafsishwa na kuanza kufanya kazi sasa yanalipa kodi Serikalini badala ya kutegemea ruzuku kutoka Serikalini; Wawekezaji kutoka nje wameongezeka kwa kuwekeza katika mashirika yaliyobinafsishwa; Teknolojia katika mashirika mengi imeboreshwa kwa kuweka mifumo mipya na hivyo kuwezesha kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora zaidi. Watanzania wameendelea kuelimishwa na kupewa fursa ya kununua hisa na kumiliki mashirika yaliyobinafsishwa.
12. Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kutoka dola za kimarekani milioni 2,048.4 sawa na uwezo wa uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.8 kwa mwaka 2005 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 3,551.3 mwaka 2009. Kiasi hiki ni sawa na uwezo wa uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 5.6.
13. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP), Wizara imepata mafanikio makubwa yakiwemo yafuatayo: kuboresha uwezo wa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi
8
Mkuu ikiwa ni pamoja na kusomesha wakaguzi ili waweze kumudu kazi zao ipasavyo; kuhamasisha utayarishaji wa hesabu za serikali kwa kutumia viwango vya kimataifa (IPSAs) hatua ambayo imewezesha utoaji wa taarifa za hesabu za Serikali kwa wakati. Aidha, Kamati za Bunge za usimamizi wa fedha nazo zimewezeshwa kutathimini uwezo wa usimamizi wa fedha katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma. Wizara imeendelea kutoa mafunzo kwa wizara nyingine, Mikoa na Serikali za Mitaa katika kuboresha uandaaji wa Mipango, Bajeti na utoaji wa taarifa za utekelezaji.
14. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne (2006 -2009) ya utekelezaji wa MKUKUTA awamu ya kwanza, uchumi wa Tanzania uliendelea kuimarika. Uchumi ulikua kwa wastani wa kiwango cha asilimia 6.9 ukilinganisha na shabaha ya MKUKUTA ya ukuaji wa kati ya asilimia 6 na 8. Kiwango cha jumla cha umaskini kilipungua kwa asilimia 2.2. Aidha, kwa upande wa viashiria vya kuboresha Maisha na Ustawi wa Jamii, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka watoto 112 kati ya 1000 mwaka 2004/05 hadi kufikia watoto 91 mwaka 2008/09. Lengo lilikuwa kupunguza
9
vifo kufikia 79 kati ya watoto 1000. Vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 68 kati ya watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2004/05 na kufikia 58 kati ya watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2008/09. Kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi kimeongezeka kutoka asilimia 96.1 mwaka 2006 hadi asilimia 97.2 mwaka 2008, dhidi ya lengo la asilimia 99 mwaka 2010. Vile vile, kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI imepungua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2005 hadi asilimia 5.7 mwaka 2008 ikilinganishwa na lengo lililowekwa la asilimia 5.0 mwaka 2010.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2009/10 NA MALENGO YA MWAKA 2010/11
15. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia na kutekeleza majukumu yake, Wizara inaongozwa na Mpango Mkakati ulioandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Malengo ya Milenia 2015, MKUKUTA na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, sambamba na kutekeleza Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) 2008/09 – 2010/11.
10
16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Wizara ya Fedha na Uchumi imeendelea kutekeleza majukumu yake ya: Kubuni na kusimamia utekelezaji wa Sera na Mikakati ya Uchumi Jumla; Kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na ya nje, na matumizi ya Serikali; Utekelezaji wa MKUKUTA, Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kupanga mipango ya maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uhasibu, ukaguzi wa ndani Serikalini, ununuzi wa umma na usimamizi wa mali ya Serikali.
17. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha majukumu haya yanatekelezwa kwa ufanisi, Wizara imegawanywa katika mafungu manne ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 – Wizara ya Fedha na Uchumi; Fungu 21 – Hazina; Fungu 22 – Deni la Taifa; na Fungu 23 – Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali. Vile vile, Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo inajitegemea, linaombewa fedha Bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi kwa mujibu wa Sheria.
Mwenendo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani Mwaka 2009/10
11
18. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2009/10 Wizara ililenga kupata mapato ya ndani ya jumla ya Shilingi bilioni 5,096.016. Hadi kufikia Aprili, 2010 matokeo ya kuridhisha yamepatikana kufuatia utekelezaji wa sera za kodi. Katika kipindi cha Julai, 2009 hadi Aprili, 2010 Serikali ilikusanya mapato ya ndani ya jumla ya Shilingi bilioni 3,821.162 sawa na asilimia 90.7 ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 4,211.764 kwa kipindi hicho. Katika kipindi hiki, Wizara iliendelea kuboresha ukusanyaji wa Mapato ya ndani na nje kwa kutekeleza yafuatayo: kuendelea kupanua wigo wa kodi, kupunguza misamaha ya kodi na kuendelea kuimarisha uchumi tulivu; kusimamia kwa karibu mageuzi yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato (TRA) chini ya Mpango wa Tatu wa Maboresho wa Miaka Mitano; kuendelea kurekebisha mfumo wa kodi na kuimarisha Idara ya Walipa kodi Wakubwa kwa kuboresha mifumo ya utendaji; kurekebisha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani SURA 148; na Kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa SURA 147. Mafanikio yaliyopatikana kufuatia utekelezaji wa hatua hizi pamoja na malengo ya utekelezaji kwa mwaka 2010/11 ni kama yalivyoainishwa katika
12
hotuba ya bajeti ya Serikali niliyowasilisha hapa Bungeni tarehe 10 Juni, 2010.
Misaada na Mikopo
Mapato kutokana na misaada na mikopo kutoka nje
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/10, Wizara ilipanga kukusanya mapato kutokana na misaada na mikopo kutoka nje yenye thamani ya Shilingi bilioni 3,182. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2010, misaada na mikopo iliyokuwa imepokelewa ilikuwa Shilingi bilioni 2,375, sawa na asilimia 75 ya makadirio ya Shilingi bilioni 3,182. Kati ya fedha hizo zilizopokelewa, Shilingi bilioni 1,214.0 au asilimia 102 ya makadirio ya Shilingi bilioni 1,193.91 ni misaada na mikopo ya kibajeti na Shilingi bilioni 1,161 au asilimia 63.0 ya makadirio ya Shilingi bilioni 1,857.4 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo na mifuko ya pamoja (Basket Funds).
20. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara imepanga kukusanya mapato ya Shilingi bilioni 3,274.553 kutokana na misaada na mikopo kutoka nje. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 821.645 ni misaada na
13
mikopo ya kibajeti na Shilingi bilioni 2,452.908 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania
21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Serikali iliendelea kutekeleza Mkakati wa Pamoja wa Misaada (Tanzania Joint Assistance Strategy – JAST) kwa nia ya kuongeza ufanisi wa misaada inayotolewa kwa nchi yetu. Aidha, kwa kutumia Mkakati huu Serikali iliendelea kujenga uwezo wa kusimamia na kutunza kumbukumbu sahihi za misaada na mikopo inayopokelewa pamoja na kukuza ushirikiano kati ya serikali na wadau wengine katika mchakato wa maendeleo ya nchi yetu. Vile vile, Serikali imeendelea kuandaa Sera ya Misaada ya Kiufundi, kukamilisha Mfumo wa Mawasiliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, kukamilisha mgawanyo wa majukumu miongoni mwa Washirika wa Maendeleo na kuendelea kuboresha Mfumo wa Kumbukumbu na Takwimu za Misaada na Mikopo kwa Tanzania (Aid Management Platform).
14
22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/11, Wizara inatarajia kukamilisha kazi ya kuandaa Mkakati wa Misaada ya Kiufundi, kuendeleza juhudi za kuboresha Mfumo wa Kumbukumbu na Takwimu za Misaada na Mikopo kwa kutoa mafunzo na vitendea kazi kwa wataalamu pamoja na kuunganisha mtandao huo na mitandao mingine katika Wizara na wadau wengine wa maendeleo.
Kukuza Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo
23. Mheshimiwa Spika, jukumu jingine muhimu la Wizara ni kukuza na kuboresha mahusiano kati ya Serikali na Washirika wetu wa maendeleo kupitia mikutano na mashauriano ya mara kwa mara. Katika mwaka 2009/10, Wizara iliandaa na kuendesha mkutano wa mwaka wa mapitio ya utekelezaji wa malengo ya MKUKUTA na vigezo vya kupima ufanisi wa misaada ya kibajeti (MKUKUTA and Perfomance Assesment Framework Reviews). Mkutano huo ulifanyika mjini Dar es Salaam mwezi Novemba, 2009 kwa mafanikio makubwa.
15
Mwenendo wa Matumizi kwa mwaka 2009/10
Fungu 50- Wizara ya Fedha na Uchumi
24. Mheshimiwa Spika, bajeti kwa ajili ya matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2009/10 ilikuwa Shilingi bilioni 113.64. Kati ya hizo mishahara ni Shilingi bilioni 2.81, matumizi mengineyo ni Shilingi bilioni 110.83 na Shilingi bilioni 188.2 ilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Mei, 2010 Fungu hili limepokea na kutumia Shilingi bilioni 92.71 kwa matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia 81.58 ya makadirio ya mwaka 2009/10. Shilingi bilioni 40.67 kwa matumizi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 21.6 ya makadirio ya mwaka.
Fungu 21-Hazina
25. Mheshimiwa Spika, bajeti kwa ajili ya matumizi ya kawaida ilikuwa Shilingi bilioni 597.61. Kati ya hizo mishahara ni Shilingi bilioni 1.14 na Shilingi bilioni 68.52 ni kwa ajili ya marekebisho ya mishahara ya Kitaifa. Shilingi bilioni 365.79 ilikuwa ni kwa ajili ya matumizi maalum ikiwa ni pamoja na dharura. Shilingi bilioni 126.38 ilikuwa ni kwa ajili ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na Shilingi bilioni 35.78 ilikuwa
16
kwa ajili ya taasisi zilizo chini ya Wizara, michango ya kimataifa na matumizi ya idara zilizo chini ya fungu hili. Shilingi bilioni 73.99 ilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ambapo kati ya hizo Shilingi bilioni 63.9 ni fedha za nje. Hadi tarehe 30 Aprili, 2010 matumizi ya kawaida yalifikia Shilingi bilioni 457.85 sawa na asilimia 76.64 wakati matumizi ya maendeleo yalifikia Shilingi bilioni 44.8 sawa na asilimia 60.6 ya makadirio.
Fungu 22 – Deni la Taifa
26. Mheshimiwa Spika, bajeti ya Fungu 22 ilikuwa Shilingi bilioni 1,517.05. Hadi kufikia mwisho wa mwezi Aprili 2010 matumizi yote yalifikia Shilingi bilioni 1,327.69 ambayo ni sawa na asilimia 87.5 ya bajeti.
Fungu 23-Mhasibu Mkuu wa Serikali
27. Mheshimiwa Spika, bajeti ya matumizi ya kawaida ilikuwa Shillingi bilioni 97.62. Hadi mwezi Aprili 2010 matumizi ya kawaida yalifikia Shilingi bilioni 75.357 ambayo ni sawa na asilimia 77.2 ya makadirio. Bajeti ya maendeleo ilikuwa Shilingi bilioni 12.05. Kati ya hizo, Shilingi bilioni 6.0 zikiwa fedha za ndani na Shilingi bilioni 6.05
17
fedha za nje. Matumizi ya fedha za maendeleo hadi Aprili, 2010 yalifikia Shilingi bilioni 1.192. Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi milioni 703. 8 na Shilingi milioni 488.2 ni fedha za nje.
Fungu 45: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
28. Mheshimiwa Spika, bajeti ya Fungu 45 kwa matumizi ya kawaida ilikuwa Shilingi bilioni 19.2. Bajeti ya maendeleo kwa Fungu hili ilikuwa Shilingi bilioni 5.8 ambapo kati ya hizo fedha za ndani ni Shilingi bilioni 2.8 na fedha za nje zikiwa ni Shilingi bilioni 3.0. Hadi mwezi Aprili, 2010 matumizi ya kawaida yalifikia Shilingi bilioni 14.12 sawa na asilimia 73.7 ya makisio. Matumizi ya maendeleo yalifikia Shilingi bilioni 1.37 fedha za nje na Shilingi bilioni 1.6 fedha za ndani.
Utekelezaji wa Majukumu kwa mwaka 2009/10 na Malengo ya 2010/11
Kusimamia na kuendeleza uchumi
29. Mheshimiwa Spika, kuhusu jukumu la kusimamia na kuendeleza uchumi, Wizara ilifanya tathmini ya maoteo ya takwimu za kiuchumi na matokeo yake kutumika katika kuandaa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2009 na
18
maoteo ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2010/11. Aidha, Wizara ilifanya tathmini ya athari za msukosuko wa uchumi na kuandaa mapendekezo ya kunusuru uchumi, kufanya tathmini ya udhamini wa Serikali katika bajeti ya Serikali, kufanya tathmini ya uanzishwaji wa Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP), na kutayarisha Sera ya Fedha itakayojumuisha makundi yote yanayohusika na masuala ya fedha.
30. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2010/11, Wizara itaendelea kuchambua na kubuni sera, kuratibu na kusimamia shughuli za kiuchumi; kuandaa sera na mikakati inayolenga kuongeza mapato ya ndani hadi kufikia lengo la shilingi bilioni 6,003.59 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,688.3 mwaka 2009/10.
Usimamizi wa Deni la Taifa
31. Mheshimiwa spika, katika mwaka wa fedha wa 2009/10 Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Madeni (NDMC) iliendelea na kazi zake za kusimamia Deni la Taifa na kuwezesha deni hilo kuwa stahimilivu (sustainable). Uchambuzi wa
19
Deni la Taifa uliofanyika mwaka 2008 unaonyesha kuwa viashiria vya Deni la Taifa vinakubaliana na vile vinavyokubalika Kimataifa. Kazi ambazo NDMC ilifanya ni pamoja na kuchambua mikopo kutoka nje ya nchi na ile ya ndani hususan maombi ya dhamana za Serikali kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufadhili miradi katika Taasisi za Umma na kumshauri Waziri wa Fedha na Uchumi kuchukua mikopo yenye masharti nafuu.
32. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za Serikali za kudhibiti deni la nje, Wizara ya Fedha na Uchumi ilifanya majadiliano na nchi ya Brazili ambayo ndiyo iliyokuwa haijatupatia unafuu wa deni katika Kundi la Paris ili watupatie unafuu wa deni makubaliano ya awali yameshaafikiwa. Katika mwaka wa fedha 2010/11, Serikali itaendelea kujadiliana na nchi zilizobaki za Non Paris Club ambazo hazijatupatia unafuu wa madeni ili kuendelea kupunguza Deni la Taifa.
Uandaaji, Usimamizi na Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali
33. Mheshimiwa Spika, katika uandaaji, usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja
20
na: kukamilisha rasimu ya vipaumbele vya Taifa kwa ajili ya maandalizi ya Mwongozo na Mpango wa Bajeti 2010/11- 2012/13 na mwongozo huu ndio uliotumika katika kuandaa Mpango na Bajeti ya 2010/11 – 2012/13; kuratibu na kusimamia kazi ya bajeti classification of functions of Government (CoFoG) ambayo inatarajiwa kutumika katika kutoa taarifa za kibajeti kuanzia mwaka wa fedha 2010/11. Aidha, Wizara ilitoa mafunzo ya uandaaji wa mipango na bajeti kwa watumishi 42 kutoka Mikoani, na watumishi 798 kutoka Halmashauri zote za Tanzania bara; na mafunzo ya uandaaji wa MTEF yaliendelea kutolewa. Vile vile, viwango vya bajeti ya matumizi ya kawaida na maendeleo viliandaliwa na kutumika katika uandaaji wa bajeti ya mwaka 2010/11.
34. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2010, Wizara chini ya kitengo chake cha Ufuatiliaji Matumizi ya Serikali na Ukaguzi wa Miradi ilifanya kaguzi nne ambazo zilihusisha fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo katika mikoa sita, fedha za chakula cha njaa katika Mikoa minne, barabara zilizoharibiwa na mvua katika Halmashauri nane na mradi wa TBC Mkoani Singida. Kaguzi hizi zilibaini dosari
21
kadhaa, ambazo ziliwasilishwa kwa wahusika ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuondosha dosari hizo. Aidha, Wizara ilifanya uhakiki wa madeni ya watumishi wa Serikali katika Mikoa kumi na Halmashauri 51, pamoja na ulipaji wa madeni ya walimu katika Halmashauri 132 Tanzania Bara. Madeni ya watumishi wa Serikali yatalipwa baada ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi wa madai hayo.
35. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2010/11 Wizara itaendelea kupitia utaratibu wa uwasilishaji wa bajeti za Wizara, Idara za Serikali, Mikoa na Halmashauri; kuhakikisha sera na mipango ya kitaifa na ya kisekta inaingizwa kwenye Bajeti ya Serikali na kufanya tathmini ya Bajeti ya Serikali ili kuhakikisha kuwa inatenga mahitaji ya makundi yote ya jamii kwa kuzingatia uwezo wa kifedha. Aidha, Wizara itafanya marekebisho ya mpangilio wa bajeti ya Serikali kwa kuzingatia programu mbali mbali; kujenga uwezo wa Wizara, Idara za Serikali, Mikoa na Halmashauri katika uandaaji wa Bajeti ya Muda wa Kati, usimamizi wake na utoaji taarifa za utekelezaji kwa wakati na kufuatilia pamoja na kutathmini matumizi ya fedha za umma. Vile vile,
22
Wizara itaendelea na ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Serikali na ile ya ubia na Sekta Binafsi.
Kuondoa Umaskini na Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
36. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuratibu mchakato wa maandalizi ya awamu ya pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA). Maandalizi haya yalitanguliwa na tathmini ya utekelezaji wa MKUKUTA awamu ya kwanza. Aidha, tafiti na chambuzi mbalimbali zilifanyika kwa lengo la kubaini changamoto na fursa zilizopo katika kuendeleza juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Tafiti hizo zimesaidia kuainisha maeneo ya vipaumbele katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa MKUKUTA I na kupata matokeo mazuri katika maeneo yaliyoonyesha fursa za kuleta maendeleo zaidi. Matokeo ya tafiti na chambuzi hizo, pamoja na mashauriano ya wadau yamechangia katika maandalizi ya MKUKUTA awamu ya pili.
23
37. Mheshimiwa Spika, MKUKUTA awamu ya pili ni mwendelezo wa awamu ya kwanza kimuundo. Hivyo, MKUKUTA II umezingatia matokeo katika nguzo zake tatu, yaani Ukuzaji wa Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato, Kuboresha Maisha na Ustawi wa Jamii na Utawala Bora na Uwajibikaji. Maeneo yanayopewa kipaumbele katika kuleta ukuaji wa haraka wa uchumi yanajumuisha: kilimo, miundombinu, utalii, uzalishaji viwandani, na uchimbaji madini. Maeneo haya yana mchango mkubwa katika kuongeza kipato kwa haraka, ukuzaji wa ajira, uwezo wa kuchangia katika kuongeza mapato ya Serikali, uwezo wa kuongeza ukuaji wa uchumi hasa maeneo ya vijijini, kuongeza mauzo ya bidhaa nje, na kuleta maendeleo katika viwanda. Kilimo kinaendelea kupewa kipaumbele ikizingatiwa kuwa wengi kati ya watu maskini wanaoishi vijijini wanategemea sekta hii. Katika kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanaleta matokeo tarajiwa, maeneo ya Elimu (hasa upanuzi wa elimu ya ufundi na ile ya juu), Afya (hasa kwa makundi hatarishi) na Maji pia yatapewa kipaumbele.
38. Mheshimiwa Spika, utawala bora na uwajibikaji ni muhimu katika kujenga mazingira
24
mazuri ya ukuaji uchumi na kupunguza umaskini nchini. Katika eneo hili, MKUKUTA II utalenga zaidi katika kusisitiza uwepo wa mazingira mazuri ya kisera ikijumuisha kulinda na kutetea haki miliki; haki za binadamu; kuhakikisha kuwepo kwa ufanisi katika mfumo wa usimamizi wa rasilimali; kutokomeza rushwa; kuhakikisha kuwepo kwa mfumo imara wa kitaasisi ambao utasaidia katika kuleta maisha bora kwa watu.
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/10, Wizara iliendelea kusimamia Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi. Katika kusimamia utekelezaji wa Sera hii, Serikali iliendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu na elimu ya ujasiriamali. Aidha, miradi ya SELF na NIGP iliratibiwa. Hadi kufikia Aprili 2010, mfuko wa SELF ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 5.012 kati ya Shilingi bilioni 5.416 zilizotengwa kukopeshwa katika kipindi hicho, mfuko ulikusanya Shilingi bilioni 4.07 kati ya Shilingi bilioni 4.17 ziliokusudiwa kukusanywa kama marejesho ya mikopo. Vile vile, tangu mfuko uzinduliwe mwaka 2000, jumla ya asasi 270 zimepatiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 26.923 ambayo imewanufaisha
25
wajasiriamali wadogo 71, 065 kati yao wanawake ni asilimia 58.3
40. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2010, Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira (J.K Fund) ulitoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 45.4 kwa wajasiriamali 72,113 wakiwemo wanawake 26,261 na wanaume 45,852. Aidha, jumla ya fedha zilizorejeshwa ni Shilingi bilioni 35.6 ambazo ni sawa na asilimia 78.5 ya mikopo iliyoiva. Mikopo iliyotolewa na Mifuko ya uwezeshaji imeleta mafanikio makubwa kwa wajasiriamali wadogo kwa kuboresha mitaji yao. Vile vile, Mfuko wa Uwezeshaji (Mwananchi Empowement Fund), hadi Aprili 2010, ulitoa dhamana kwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.2 kwa wajasiriamali 4,437 wakiwemo wanawake 1,341 na wanaume 3,096. Pia, Wizara iliendelea kuhamasisha uanzishwaji wa SACCOS kama njia muafaka ya kupata mikopo yenye masharti nafuu. Kutokana na juhudi zilizofanyika, idadi ya SACCOS imeongezeka nchini kutoka 4,780 mwaka 2008 hadi kufikia 6,000 mwaka 2009.
41. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iliendelea
26
kutoa elimu ya ujasiriamali; ilifanya tafiti juu ya wakulima na wajasiriamali kwa lengo la kuwaunganisha na taasisi za utafiti ili wanufaike na matokeo ya tafiti mbalimbali; ilifanya tafiti ya jinsi ya kuboresha sekta ya useremala ili kubaini namna ya kuinua viwango vya ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kuishauri Serikali na wadau wengine kununua samani za ndani badala ya zile zinazotoka nje. Aidha , zoezi la kuainisha aina za biashara zinazostahili kuendeshwa na Watanzania pekee na zile zinazoweza kuendeshwa kwa ubia na wageni lilifanyika
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara itatekeleza yafuatayo:- kuandaa mwongozo wa utekelezaji wa MKUKUTA II; kuandaa makadirio ya gharama kwa sekta kuu tano za MKUKUTA II; kukamilisha Mwongozo wa ufuatiliaji na Tathmini kuhusu Mkakati wa Utekelezaji wa Masuala ya Uwezeshaji Kiuchumi; kuandaa na kuratibu utekelezaji wa mfumo wa ufuatiliaji wa MKUKUTA II; kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mradi wa NIGP. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kuangalia maeneo yatakayoinua hali ya wananchi kiuchumi kwa muda mfupi kwa kushirikiana na wadau
27
mbalimbali; na kuifanyia marekebisho Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Namba 16 ya mwaka 2004 ili kulipa Baraza nguvu ya kubuni, kupanga, kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya uwezeshaji.
Kuimarisha Nidhamu ya Matumizi ya Fedha za Umma
43. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia matumizi ya bajeti kwa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara iliandaa na kutoa mgao wa fedha za matumizi ya kawaida na maendeleo kama hali ya kifedha ilivyo ruhusu. Hadi kufikia Aprili, 2010 mgao wa fedha za matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Serikali za Mitaa zilikuwa Shilingi bilioni 5,111.34 ikiwa ni asilimia 76.2 ya bajeti ya matumizi ya kawaida ya Shilingi bilioni 6,707.254. Fedha za maendeleo zilizotolewa ni Shilingi bilioni 2,471.15 ikiwa ni asilimia 87.5 ya bajeti ya matumizi ya maendeleo ya Shilingi bilioni 2,825.431. Fedha za ndani zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo ni Shilingi bilioni 645.881 sawa na asilimia 66.7 ya bajeti wakati fedha za nje zilizotolewa ni Shilingi bilioni 1,825.269 sawa na asilimia 98.3 ya bajeti.
28
44. Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuimarisha nidhamu ya matumizi ya bajeti, hadi Aprili, 2010 Wizara ilichambua nyaraka za waajiriwa wapya 26,649 ambao waliingizwa kwenye orodha ya malipo ya mishahara. Aidha, uchambuzi wa marekebisho ya mishahara ya watumishi wa Serikali Kuu na mamlaka za Serikali za Mitaa waliopandishwa vyeo pamoja na uchambuzi wa mishahara na madai ya malimbikizo ya watumishi wa Taasisi za Umma 72 ulifanyika.
45. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2010/11, Wizara itaendelea na utaratibu wa kuandaa na kutoa mgao wa fedha za matumizi ya kawaida na maendeleo kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu. Aidha, Wizara itaandaa na kukamilisha Mwongozo wa Mpango na Bajeti 2011/12- 2013/14 kwa mujibu ratiba ya kitaifa itakavyoelekeza na mwongozo huu ndio utakaotumika katika kuandaa Mpango na Bajeti kwa kipindi hicho.
29
Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Serikali.
46. Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha majaribio ya kutumia mtandao wa Benki Kuu wa malipo ya Elektroniki wa Tanzania Inter-bank Settlement System (TISS). Wizara imeandaa na kutoa miongozo ya matumizi ya mfumo huo ikiwa ni pamoja na kufanya semina elekezi kwa baadhi ya maafisa watakaotumia mfumo huo. Mfumo huu mpya utatekelezwa kwa awamu mbili kama ifuatavyo: awamu ya kwanza imehusisha Wizara na Idara za Serikali zilizopo Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam ambao malipo yake yalikuwa yanalipwa kupitia Ofisi Kuu ya Malipo iliyopo Hazina makao makuu; awamu ya pili itahusisha Wizara, Idara za Serikali na Mikoa yote ambayo malipo yake yalikuwa hayalipwi kupitia Ofisi Kuu ya Malipo. Mfumo huu umeanza kutumika Julai, 2010 katika awamu ya kwanza.
47. Mheshimiwa Spika, hesabu za mwaka za Serikali ziliendelea kuandaliwa kwa mara ya pili mfululizo kwa kutumia viwango vya kimataifa vya uandishi wa Hesabu (IPSAs). Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Juni 2009, zilitolewa moja kwa
30
moja kutoka kwenye Mtandao wa Malipo wa Serikali (IFMS) na hivyo kuongeza ubora wa taarifa hizo. Ubora wa hesabu za mwaka unaendelea kuongezeka. Kwa mwaka wa fedha 2008/09, Wizara na Idara 46, Mikoa 18 na balozi 28, sawa na asilimia 86, zilipata hati safi za ukaguzi kulinganisha na hali ilivyokuwa mwaka 2004/05 ambapo Wizara na Idara 15, na Mikoa 8 tu sawa na asilimia 34 ndiyo zilipata hati safi.
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Mpango na Bajeti unalenga kuendelea kusimamia udhibiti wa matumizi ya fedha katika Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Mikoa na Halmashauri kupitia Mtandao wa Malipo wa Serikali; kusimamia, kuimarisha na kuboresha uendeshaji na uunganishaji wa IFMS; kuimarisha mtandao kwa kuanza kushughulikia kasoro zilizoainishwa kwenye ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali; kuendelea kuimarisha Kituo cha Kuhifadhia Kumbukumbu (Disaster Recovery Site); kuanzisha Idara ya Ukaguzi wa Ndani itakayowajibika kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali; kuimarisha Kamati za Ukaguzi (Audit Committees) katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Halmashauri;
31
kuboresha Kitengo cha Usimamizi wa Fedha (Cash Management Unit); kutayarisha majumuisho ya hesabu za Wizara, Mikoa na Idara zote za Serikali kwa viwango vya kimataifa (IPSAs); kusimamia na kudhibiti mapato ya ndani na nje; na kuendeleza kada za uhasibu, ukaguzi, maafisa mipango na wataalam wa kompyuta katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Usimamizi wa malipo ya mishahara ya watumishi wa Umma
49. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuandaa na kutoa mishahara kwa watumishi wa Serikali kabla ya tarehe 23 ya kila mwezi ikiwa na lengo la kuwapunguzia usumbufu wa kufuatilia mishahara hiyo. Aidha, kumbukumbu za malipo ziliendelea kupelekwa hadi ofisi za Hazina Ndogo Mikoani kila mwezi kwa lengo la kuzipunguzia Halmashauri, Idara na Taasisi za Serikali gharama za kufuatilia mishahara ya watumishi makao makuu. Vile vile, Wizara ilifanya uhakiki wa mishahara ya watumishi wa Serikali katika Mikoa 10 na Halmashauri 51. Matokeo ya uhakiki huo yameshafanyiwa kazi.
32
50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, wizara itaendelea kusimamia usambazaji wa nyaraka za kulipia mishahara, ulipaji wa mishahara kwa kupeleka fedha kwa wakati. Aidha, Wizara itakamilisha zoezi la uhakiki wa mishahara kwa Mikoa na Halmashauri zilizosalia pamoja na kufanya uhakiki wa watumishi kwa kufanya malipo ya mishahara kwa mwezi mmoja dirishani.
Huduma kwa Wastaafu na Warithi
51. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuboresha utoaji wa huduma kwa wastaafu, Serikali imeendelea na kazi ya kuweka kwenye mfumo wa kompyuta kumbukumbu za wastaafu kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wastaafu. Kumbukumbu za majalada ya wastaafu 24,446 kati ya 45,000 yaliyokusudiwa kuwekwa kwenye mfumo wa kompyuta zimewekwa kwenye kompyuta na kazi ya kuweka kumbukumbu za majalada yaliyobaki inaendelea. Vile vile, katika juhudi za kuimarisha na kudhibiti malipo ya pensheni na kuboresha huduma kwa wastaafu, Serikali imeamua kutumia mfumo wa malipo unaoitwa Government Pension Payment System (GPPS) unaotumiwa na Mfuko wa Pensheni ya
33
Mashirika ya Umma (PPF). Mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huo kwa watumishi wa kitengo cha pensheni yametolewa.
52. Mheshimiwa Spika, ili kuwapunguzia usumbufu wajane na watoto wa marehemu katika kufuatilia malipo ya mirathi, Wizara ya Fedha na Uchumi imeendelea kutoa elimu kwa umma ili kuwawezesha wajane na watoto wa marehemu wawe na uelewa wa utaratibu unaopaswa kufuatwa ili malipo ya mirathi yalipwe kwa wakati. Aidha, vikao vya kazi vilivyohusisha watumishi kutoka Hazina makao makuu na Ofisi za Hazina Ndogo Mikoani wanaoshughulikia mafao ya kustaafu na Mirathi vimefanyika, kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuwapunguzia wajane na watoto wa marehemu usumbufu.
53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11 Wizara imepanga kukamilisha shughuli ya kuweka kumbukumbu za mafaili ya wastaafu kwenye mfumo wa kompyuta; kuendesha mafunzo kwa watumishi wanaotoa huduma ya pensheni namna ya kutumia Mfumo wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF); na kuendelea kutoa mafunzo juu ya masuala ya pensheni kwa wadau mbalimbali wanaotoa
34
huduma kwa wastaafu hasa watumishi kutoka ofisi za RAS, Hazina Ndogo pamoja na Mahakama ambako malipo ya mirathi hupitia.
Usimamizi wa Mali ya Serikali
54. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10 , Wizara iliendelea kusimamia mali ya Serikali kulingana na taratibu na kanuni zilizopo kama ifuatavyo: ushauri ulitolewa kuhusu upokeaji, utunzaji na uondoshaji wa mali zisizohitajika katika Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na wakala wa Serikali, uthamini wa mali za Serikali katika Wizara na Idara zinazojitegemea 20 ulikamilishwa. Aidha, Wizara ilifanya ukarabati mkubwa kwa ofisi za usimamizi wa mali za Serikali katika Mikoa ya Kagera, Iringa, Lindi na Kilimanjaro na kuboresha vitendea kazi katika ofisi zote za Mikoa.
55. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11 Wizara itaendelea kutekeleza yafuatayo: kuhakiki bohari, kufuta na kuondosha vifaa chakavu zikiwemo samani, magari, mitambo, madawa na vifaa vingine visivyohitajika katika Wizara, Mikoa, Idara za Serikali zinazojitegemea na Wakala za Serikali; kufanya uthamini wa Mali
35
za Serikali, kuhuisha daftari la mali za Serikali lenye kuonyesha idadi na thamani yake kwa ajili ya kufanya usuluhishi kwa njia ya mtandao; na uchambuzi wa madai mbalimbali ya fidia na kutekeleza amri za Mahakama kwa kulipa fidia na kifuta machozi. Aidha, Wizara itashughulikia taarifa za ajali na potevu za mali kwa mujibu wa Kanuni za Fedha.
Usimamizi, Ushauri na Uratibu wa utekelezaji wa shughuli za Wizara
56. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, jukumu la ushauri, uratibu na usimamizi wa shughuli za Wizara liliendelea kutekelezwa. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: watumishi wapya 574 waliajiriwa kwenye kada za Uhasibu na Ukaguzi wa ndani, kati ya hao watumishi wapya 394 walipelekwa Serikali za Mitaa na 180 walipelekwa Serikali Kuu. Wizara ilitoa udhamini kwa wanafunzi 200 wanaosoma katika Chuo cha Uhasibu Arusha, Chuo cha Usimamizi wa Fedha na Taasisi ya Uhasibu Tanzania. Kwa kutambua umuhimu wa kuwaongezea uwezo watumishi, Wizara iliendelea kuboresha utendaji kazi wa watumishi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi watumishi
36
200 na watumishi 26 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu.
57. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza dhana ya uongozi shirikishi Wizara iliendesha mikutano miwili ya Baraza la Wafanyakazi ambapo hoja mbali mbali za Wafanyakazi zilijadiliwa na maazimio kufikiwa. Aidha, katika kujenga afya za watumishi na kudumisha mahusiano mazuri, watumishi 150 walishiriki kwenye michezo ya Shirikisho la Michezo ya Mawizara (SHIMIWI) iliyofanyika mkoani Morogoro. Vile vile, Wizara iliendelea kuwahudumia watumishi wake wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa lengo la kuimarisha afya zao na hivyo kuendelea kulitumikia taifa.
58. Mheshimiwa Spika, Wizara ilikusanya maoni ya wadau wake toka mikoa tisa ya Tanzania Bara kwa lengo la kuhuisha Mkataba wa Huduma kwa Mteja na Mpango Mkakati wa Wizara. Mchakato wa uhuishaji wa Mkataba huo unaendelea; Wizara iliendelea kuratibu maandalizi ya taarifa mbali mbali za utekelezaji wa bajeti ya Wizara kwa kila robo mwaka ikiwa ni pamoja na kusimamia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP); kuratibu na
37
kushiriki katika mikutano ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; taarifa mbali mbali za utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ziliandaliwa na kusambazwa; uhakiki na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara na Taasisi zake ulifanyika na kuwezesha kuidhinishwa kwa fedha za matumizi ya maendeleo.
59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11 Wizara itaendelea na utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma ikiwa ni pamoja na kuandaa Programu ya Maboresho Awamu ya nne. Awamu hii itajikita katika kuendelea kusimamia maeneo muhimu ya kipaumbele katika kuboresha sekta ya fedha hapa nchini ili iweze kutoa mchango wake kikamilifu katika kutekeleza MKUKUTA awamu ya pili. Aidha, Wizara itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi, kushiriki katika michezo, kuwahudumia watumishi wanaoishi na virus vya ukimwi na itakamilisha uhuishwaji wa Mpango Mkakati na Mkataba wa Huduma kwa Mteja.
38
Ushauri wa kisheria kwa Wizara, Idara na Taasisi
60. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, majukumu mbalimbali ya kisheria yanayohusu Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na Taasisi zake yametekelezwa ikiwa ni pamoja na: kuandaa na kukamilisha Kanuni za kuwezesha matumizi ya mfumo mpya wa ukusanyaji kodi ya mapato unaotumia Electronic Fiscal Devices badala ya mfumo wa sasa unaotumia cash registers; kuandaa na kukamilisha Kanuni zinazoanzisha chombo cha ukusanyaji wa taarifa za wakopaji (Credit Reference Bureau); kuandaa na kukamilisha Azimio la Kuongeza Mtaji wa Mfuko wa kutoa Mikopo (Advances Fund) kwa Waheshimiwa Wabunge na Watumishi wa Serikali; na kukamilisha marekebisho ya Sheria ya Msajili wa Hazina, SURA 370 ambayo yaliwasilishwa katika mkutano wa Bunge wa mwezi Aprili, 2010.
61. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa yanajumuisha: kuandaa na kukamilisha marekebisho ya Sheria ya Soko la Mitaji na Dhamana SURA 79 ambayo yaliwasilishwa katika mkutano wa Bunge wa
39
mwezi Aprili, 2010; na kuandaa Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2010 ambao unatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti unaoendelea. Aidha, Wizara katika mwaka wa fedha 2010/11 itaendelea kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria nyingine zinazosimamiwa na Wizara ili ziweze kwenda na wakati.
UNUNUZI WA UMMA
62. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Wizara iliendelea na zoezi la kuwatambua na kuwaorodhesha watumishi wa Kada ya Ununuzi wa Umma hapa nchini. Zoezi hili linahusisha Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa na Wakala wa Serikali. Lengo ni kuyatumia matokeo ya zoezi hilo katika kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha Kada ya Ununuzi wa Umma hapa nchini. Katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara itaendelea na maandalizi ya Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha ununuzi wa umma.
40
63. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kusimamia na kuhakikisha huduma na vifaa mbalimbali vinapatikana kwa Idara na vitengo vyake. Ili kutimiza azma hii, Wizara iliandaa Mpango wa Ununuzi wa Mwaka na kutangaza zabuni 37 kwa ajili ya kupata huduma na vifaa mbali mbali. Katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara itaendelea kutekeleza Mpango wa Ununuzi wa 2010/11 ulioandaliwa.
Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, ilitekeleza yafuatayo: kuendesha mafunzo kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Kuzuia Rushwa kwenye Ununuzi wa Umma kwa taasisi za umma 200; iliendelea na mchakato wa utafiti wa kuanzisha Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia mtandao (e-procurement system). Upembuzi yakinifu juu ya uanzishwaji wa mfumo huo umekamilishwa na masuala yaliyobainishwa katika utafiti huo yatashughulikiwa katika mwaka wa fedha 2010/11; mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake yalitolewa katika kanda nne za Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya.
41
Watumishi 1,901 pamoja na Wakaguzi wa Ndani 100 wamefaidika na mafunzo hayo; pia ukaguzi wa ununuzi katika taasisi za umma zipatazo 99 umefanyika.
65. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara kwa kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma pamoja na kuendelea kutekeleza majukumu ya msingi yaliyomo kwenye Sheria ya Ununuzi, itafanya yafuatayo: kuimarisha uhusiano kati ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma na malengo ya MKUKUTA; kuendeleza harakati za kupambana na rushwa katika michakato ya ununuzi; kuongeza kiwango cha utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi kwenye Taasisi za Umma kutoka asilimia 55 kufikia asilimia 80 na; kuimarisha uwezo wa Mamlaka ili kuwafikia wadau wake kwa kupanua ofisi ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi za kanda, na kuongeza watumishi.
Rufaa za Zabuni
66. Mheshimiwa Spika, Mamlaka iliyapitia na kutolea uamuzi mashauri 21 kati ya mashauri 23 yaliyopokelewa. Mashauri mawili yaliyobaki yanaendelea kushughulikiwa. Aidha, Mamlaka
42
ilifanya uelimishaji umma katika mikoa ya Tanga, Tabora, na Kigoma na pia katika wilaya za Sengerema, Tarime na Korogwe ili kuwawezesha wadau kufahamu haki na wajibu wao pale wanapoona taratibu za ununuzi hazikuzingatiwa au haki haikutendeka katika utoaji wa zabuni. Pia, Mamlaka ilishiriki katika semina ya uelimishaji kwa wabunge kuhusu utekelezaji wa sheria ya ununuzi wa umma.
67. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11 Mamlaka itaendelea kutekeleza majukumu yafuatayo: kusikiliza na kusuluhisha migogoro katika Ununuzi wa Umma; kuelimisha umma na wadau kwa ujumla kwa kukamilisha uelimishaji katika mikoa ambayo haijaweza kufikiwa; kukamilisha uandaaji wa taratibu za uwasilishaji wa malalamiko katika lugha ya Kiswahili na kuzisambaza kama njia ya kuelimisha umma.
Huduma ya Ununuzi Serikalini
68. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2009/10 Wizara kupitia Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA) ilianza utekelezaji wa utaratibu unaoziwezesha Wizara, Idara za Serikali
43
zinazojitegemea, Taasisi za Serikali na Halmashauri kuanza kununua vifaa na huduma zitumikazo mara kwa mara (Common use items and services) kwa pamoja. Wakala uliitisha zabuni 13 za ununuzi wa vifaa na vyakula pamoja na zabuni 9 za utoaji huduma. Aidha, Wakala umeingia makubaliano na wazabuni 3,016 kwa niaba ya Serikali.
69. Mheshimiwa Spika, Wakala umemwajiri Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini iwapo ununuzi wa mafuta ya magari ya Serikali unaweza kufanywa kwa kutumia Smart Card ambapo kila gari la Serikali litapewa kadi kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kwenye vituo vya mafuta vya Wakala. Aidha, wakala umemwajiri mkandarasi kwa ajili ya kufanya kazi ya ukarabati na upanuzi wa kituo cha mafuta cha Dodoma. Zabuni ya ukarabati na upanuzi wa kituo cha mafuta Kurasini (Dar es Salaam) imeitishwa upya baada ya kukosa mzabuni mwenye sifa kwenye mchakato wa awali.
70. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2010/11 Wizara imepanga kuimarisha Wakala katika maeneo ya rasilimali watu, fedha, vitendea kazi pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia
44
kazi ili uweze kuchukua dhamana ya usimamizi wa ununuzi wa magari ya Serikali. Aidha, Wakala umepanga kuimarisha mfumo wa ununuzi wa vifaa na huduma kwa pamoja kwa kujenga uwezo wa watumishi na wazabuni; kutekeleza matokeo ya upembuzi yakinifu (feasibility study) kuhusu matumizi ya Smart Card; na kukamilisha kazi ya kukarabati na kupanua uwezo wa visima vya mafuta Kurasini (DSM) na Dodoma.
Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na
Ugavi – PSPTB
71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10 Bodi iliendesha warsha 11 zinazohusu majukumu ya Bodi. Warsha hizo ziliendeshwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Mbeya, Mtwara na Arusha. Aidha, Bodi iliandaa mtaala mpya wa mafunzo ulioanza kutumika rasmi mwezi Januari, 2010. Mtaala huu umezingatia mahitaji ya wadau na mabadiliko ya taaluma kimataifa. Vile vile, Bodi iliendelea kutoa ushauri wa kitaalamu na kuandaa operations manuals zilizolenga kuratibu na kusimamia shughuli za ununuzi na ugavi kwenye Taasisi mbalimbali.
45
72. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2010/11, Bodi itaendelea kuongeza idadi ya watahiniwa, kupanua maktaba kwa kuongeza vitabu na nyenzo za kusomea ili kuongeza kiwango cha ufaulu wa watahiniwa toka kiwango cha sasa cha asilimia 46.2 hadi kufikia asilimia 51.
Habari, Elimu na Mawasiliano kwa Umma
73. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia mawasiliano ya habari kwa kutekeleza yafuatayo: kutoa elimu kwa Umma kwa kutumia vyombo vya habari kuelezea mafanikio ya Wizara katika Serikali ya Awamu ya Nne pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Desemba 2005 – Desemba 2009; kuandaa documentary ya utekelezaji wa MKUKUTA I; kusanifu machapisho mbalimbali ya Wizara ili yasambazwe kwa wananchi wakati wa Maonesho ya kitaifa. Aidha, Tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz) imeendelea kuhuishwa kwa kuwekewa taarifa mbalimbali za Wizara ikiwa ni pamoja na maelezo ya mgao wa fedha za matumizi ya kawaida.
46
Ukaguzi wa Ndani
74. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Wizara iliendelea kusimamia kada ya Ukaguzi wa Ndani, kwa kuajiri na kutoa mafunzo ili kuimarisha ukaguzi wa ndani. Wizara iliendesha mafunzo yaliyohusu ukaguzi wa ununuzi na mikataba na mafunzo yaliyohusu mbinu za kubaini pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha katika ununuzi na kandarasi; kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 kupitia Sheria ya Fedha 2010 (The Finance Act, 2010) ambapo inawezesha kuanzishwa kwa Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor General Department); na Wizara inaendelea kukamilisha muundo wake ili kuwezesha uwepo wa Idara kamili ya ukaguzi wa ndani ambayo itaimarisha usimamizi wa kada na kazi za ukaguzi.
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara itatekeleza yafuatayo; kuijengea uwezo Idara mpya ya Ukaguzi wa Ndani kwa maana ya kuajiri watumishi ili kujaza nafasi kulingana na muundo wa Idara; na kutoa mafunzo kwa watumishi wa Idara mpya ili kuendana na majukumu yake.
47
Mamlaka ya Mapato Tanzania –TRA
76. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Mamlaka ya mapato Tanzania iliendelea na jukumu lake la ukusanyaji wa mapato ya Serikali chini ya Mpango wake wa Tatu wa Maboresho wa Miaka Mitano (Third Corporate Plan) ambao malengo yake ni pamoja na: kuziba mianya ya ukwepaji kodi; kudhibiti uvujaji wa mapato ya Serikali; kuendelea kutoa elimu ya biashara; na kuimarisha namna ya ukokotoaji kodi kwa wafanyabiashara; kuboresha mifumo ya utendaji ya Idara ya Walipakodi Wakubwa; kuendelea kuboresha usimamizi na utendaji katika Idara ya Forodha kwa kuongeza uwajibikaji, matumizi ya teknolojia, na kupunguza kero kwa walipa kodi; kuendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti katika kupeleka mizigo kwenye bandari za nchi kavu (Inland Container Depot – ICD) ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa; na kuimarisha udhibiti wa bidhaa za mafuta ya petroli, ikiwemo kuhakikisha kuwa, mita za kupitishia bidhaa hizo (flow metres) zinafanya kazi kwa ufanisi wakati wote.
48
77. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Mamlaka ya Mapato Tanzania, imejipanga kuongeza juhudi zaidi katika ukusanyaji wa mapato kwa kuendelea kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya; kuendelea kusimamia kwa karibu mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania chini ya Mpango wake wa Tatu wa Maboresho wa Miaka Mitano (Third Corporate Plan) ambayo yamekuwa msingi wa kuongezeka kwa mapato ya ndani mwaka hadi mwaka kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali; kuendelea kuchukua hatua za kuziba mianya ya uvujaji wa mapato ya Serikali; na kuboresha ukaguzi wa kodi (field and desk audits) na usimamizi wa ukusanyaji wa malimbikizo ya kodi.
Rufaa za Kodi
78. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Bodi ya Rufani za Kodi ilipokea rufani 96 na maombi 23. Bodi ilisikiliza na kutolea maamuzi rufani 79. Kati ya hizo, rufani 12 zilikuwa ni zile zilizopokelewa mwaka 2008/09. Aidha, kati ya maombi 23 iliyopokea, Bodi ya Rufani ilisikiliza na kutolea maamuzi maombi 22. Kati ya hayo, maombi sita yalikuwa ni yale
49
yaliyopokelewa mwaka wa fedha 2008/09. Vile vile, Wizara kupitia Baraza la Rufani za Kodi ilipokea na kutolea maamuzi rufani 23. Kati ya hizo, rufani tatu zilikuwa ni zile zilizopokelewa mwaka wa fedha 2008/09.
79. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Bodi ya Rufani itaendelea kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi ya rufani za kodi kwa wakati pamoja na kutoa elimu kuhusu taratibu za kukata rufaa katika maeneo ambayo elimu hiyo haijatolewa. Aidha, Bodi na Baraza la Rufani za Kodi, kwa pamoja zitakamilisha uchapishaji wa ripoti za kesi zote zilizoamuliwa tangu mwaka 2005 hadi 2008.
Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma.
80. Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2009/10, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikusudia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 38.4 kama maduhuli. Hadi kufikia Juni 2010 Ofisi iliweza kukusanya maduhuli ya Shilingi bilioni 40.5 sawa na asilimia 105.5 ya makadirio. Katika kipindi hicho, Ofisi iliendelea kuchambua Miundo na Kanuni za Utumishi kwa mashirika 46, Kanuni za Fedha na Mifumo ya Mishahara ya Mashirika na
50
Taasisi 32; kuchambua na kuidhinisha makadirio ya Ikama kwa Taasisi za Serikali 110 kwa ajili ya malipo ya mishahara na ajira mpya. Aidha, uchambuzi wa mikataba sita ya hiari kwa mashirika ulikamilishwa na uchambuzi wa mikataba miwili ya Taasisi unaendelea.
81. Mheshimiwa Spika, kufuatia kupitishwa na Bunge kwa marekebisho ya Sheria ya Mashirika ya Umma SURA 257 na Sheria ya Msajili wa Hazina SURA 370, katika mwaka 2010/11 Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia mashirika na Taasisi za Umma kwa kurekebisha muundo wake ili iwe na mamlaka zaidi katika kusimamia kwa karibu Mashirika na Taasisi za Umma.
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
82. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imetekeleza yafuatayo: kukagua hesabu za mafungu yote ya Wizara na Idara za Serikali, Mikoa yote 21 ya Tanzania Bara, na Serikali za Mitaa 133;
51
Mashirika ya Umma 95, Balozi zote 32 nje ya nchi na Wakala za Serikali 33. Taarifa za ukaguzi wa hesabu za Mashirika 51 zilikamilika na kuwasilishwa Bungeni. Ukaguzi wa hesabu za Mashirika 105 unaendelea katika hatua mbalimbali ambapo Mashirika 10 yalikuwa hayajawasilisha hesabu zake kwa ajili ya ukaguzi; Aidha, Ofisi imeendelea na ujenzi wa ofisi za mikoa ya Lindi na Morogoro.
83. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2010/11 Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imepanga kutekeleza yafuatayo: kukagua mafungu ya Wizara na Idara za Serikali, hesabu za mikoa yote ya Tanzania Bara, hesabu za Halmashauri 133 za miji, Wilaya, Manispaa na Majiji pamoja na hesabu za mashirika ya Umma 170, Balozi zote 32 nje ya nchi na Wakala 33 za Serikali; kuendelea kuimarisha utendaji wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; kuendelea na ujenzi wa ofisi za mikoa ya Kilimanjaro na Shinyanga pamoja na kuanza ujenzi wa ofisi za mikoa ya Dodoma na Rukwa.
52
Udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu
84. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Wizara kupitia Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya Udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu, iliratibu maandalizi ya mkutano wa kumi na tisa (19) wa maafisa waandamizi (Makatibu Wakuu) wa Wizara za Fedha, Sheria na Mambo ya Ndani wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG) kuhusu udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi. Tanzania iliandaa na kuwasilisha katika mkutano huo, rasimu ya Mpango wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Taarifa ya Tathmini (Mutual evaluation) kuhusu Mfumo wa Udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi kwa Tanzania.
85. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara itaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa Serikali inakuwa na mfumo madhubuti unaokubalika kimataifa wa kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi. Tanzania itashiriki katika mkutano wa mwaka wa Baraza la Mawaziri wa ESAAMLG (Council of Ministers) utakaofanyika mjini Lilongwe-Malawi mwezi Agosti, 2010 ambapo itawasilisha Mpango
53
wa Utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa ya tathmini (Mutual Evaluation Implementation Plan) kuhusu mfumo wa udhibiti wa biashara ya fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi. Katika mkutano huo Tanzania itawasilisha pia mkakati wake wa kitaifa (National Strategy) wa kudhibiti biashara ya fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na nchi wanachama kupitia hati ya makubaliano (MoU).
Tume ya Pamoja ya Fedha
86. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2009/10 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimeendelea na uchambuzi wa Taarifa mbalimbali za Tume kwa ajili ya kufanya maamuzi ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume kuhusu vigezo vya kugawana mapato na kuchangia gharama za Muungano. Aidha, Tume imekamilisha mapendekezo ya Mwongozo wa Uendeshaji wa Akaunti ya Fedha ya Pamoja na Mfumo wa Bajeti utakaohusisha pande mbili za Muungano. Vile vile, Tume inaendelea na uchambuzi wa Deni la Taifa linalohusu Serikali mbili (SMT na SMZ). Hata hivyo, kuhusu kufanya
54
utafiti wa Mfumo wa Kodi utakaokubalika kwa pande mbili za Muungano, kazi hii inaendelea kutekelezwa.
87. Mheshimiwa spika, katika mwaka wa fedha 2010/11 Tume inakusudia kufanya yafuatayo: kukamilisha uchambuzi wa Deni la Taifa linalohusu serikali mbili (SMT na SMZ); kufanya uchambuzi na kubainisha gharama za mambo ya Muungano; kujenga uwezo wa wataalamu wa Tume kufanya utafiti wa kufuatilia maendeleo ya kiuchumi kwa mambo ya Muungano; kufanya mapitio na kutekeleza kazi ya utafiti wa mfumo wa kodi utakaokubalika kwa pande mbili; na kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu uhusiano wa kifedha baina ya SMT na SMZ.
MIFUKO YA PENSHENI
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma –PSPF
88. Mheshimiwa Spika, Mfuko uliendelea kulipa mafao, kusajili wanachama, kukusanya michango na kuhifadhi kumbukumbu za wanachama. Katika mwaka wa fedha 2009/10
55
Mfuko ulipanga kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 291.83, kati ya hizo Shilingi bilioni 234.99 ni michango ya wanachama na Shilingi bilioni 56.84 ni mapato yatokanayo na vitega uchumi. Aidha, katika kipindi hicho, Mfuko ulipanga kulipa kiasi cha Shilingi bilioni 223.87 kwa ajili ya mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi, ambapo jumla ya wanachama wapatao 7,572 walitarajiwa kustaafu kwa mujibu wa sheria.
89. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Mfuko utaendelea kusajili wanachama, kukusanya michango na kuhifadhi kumbukumbu za wanachama. Aidha, Mfuko utaendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wanachama ili waweze kuwasilisha nyaraka na kumbukumbu zilizokamilika na kwa wakati na hivyo kuondoa kero ya kucheleweshwa kwa malipo ya wastaafu.
Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini –GEPF
90. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF) uliendelea kutekeleza
56
majukumu ya kuboresha huduma kwa wanachama, kukusanya michango kutoka kwa wanachama, kuwekeza fedha za wanachama katika vitega uchumi vilivyo salama na kulipa mafao kwa wastaafu. Katika kipindi hicho mfuko umeendelea kulipa mafao kwa wanachama wake kwa wakati. Vile vile, Mfuko umeanzisha utaratibu wa Uchangiaji wa Hiari (Voluntary Saving Retirement Scheme – VSRS). Kufikia Juni, 2010, jumla ya Shilingi milioni 60,268.15 zilikuwa zimekusanywa kutoka kwenye michango ya wanachama na mapato ya vitega uchumi. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 103.88 ya malengo ya mwaka.
91. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11 Mfuko unategemea kukusanya jumla ya Shilingi milioni 66,199.13 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ikijumuisha michango ya wanachama, mapato yanayotoka kwenye vitega uchumi na vitega uchumi vitakavyoiva. Katika kipindi hicho, Mfuko utaweka msukumo mkubwa katika kutoa elimu kwa wananchi ili wajiunge na utaratibu wa hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni ambao unawalenga wote wasiochangia katika Mifuko ya Hifadhi ya
57
Jamii iliyopo kutokana na ajira zao kutotegemea mishahara.
Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma -PPF
92. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009, Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma ulikusanya jumla ya Shilingi bilioni 136.6 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi bilioni 109.8 kilichokusanywa katika mwaka 2008. Mapato yatokanayo na uwekezaji baada ya kodi (Net Investments Income) yaliongezeka kutoka Shilingi bilioni 52.4 mwaka 2008 hadi kufikia Shilingi bilioni 54.6 kwa mwaka 2009. Thamani ya Mfuko hadi Desemba 2009, ilikuwa Shilingi bilioni 624.85 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 499.33 ilivyokuwa Desemba, 2008 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25. Kwa upande wa mafao, mfuko ulilipa jumla ya Shilingi bilioni 47.2 kwa mwaka 2009 kutoka Shilingi bilioni 36.9 zilizolipwa katika mwaka 2008.
93. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2010, Mfuko unatarajia kuandikisha jumla ya wanachama 40,000 kutoka katika sekta ya umma na binafsi. Thamani ya Mfuko inategemea kukua
58
hadi kufikia Shilingi bilioni 730.87 kutoka Shilingi bilioni 624.85 kwa mwaka 2009. Ukuaji huo utatokana na kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa katika kukusanya michango kutoka kwa wanachama kiasi cha Shilingi bilioni 149.80 na mapato yatokanayo na uwekezaji ambayo yanatarajiwa kufikia Shilingi bilioni 60.93. Aidha, Mfuko utaendelea na ujenzi wa Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dodoma na ukamilishaji wa ujenzi wa hoteli ya kisasa katika Jiji la Mwanza.
HUDUMA ZA KIBENKI
Benki Kuu ya Tanzania
94. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Wizara ya Fedha na Uchumi kwa kushirikiana na Benki Kuu imeendelea kufanya mageuzi katika sekta ya fedha kwa lengo la kurekebisha sera na sheria mbalimbali za fedha ili kuongeza uwazi na ushindani katika utoaji wa huduma za kibenki na hivyo kurahisisha upatikanaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na kupunguza riba kwa wakopaji. Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kutekeleza Programu ya Awamu ya Pili ya Kurekebisha Sheria ya Fedha
59
(Second Generation Financial Sector Reform Program 2006 -2010) ambapo mambo kadhaa yamefanyika yakiwemo: kutungwa kwa Sheria inayoweka mazingira ya kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa njia ya ukodishaji vifaa, mitambo na rasilimali nyingine (Lease Financing); kutungwa kwa sheria ya mikopo ya nyumba ambayo inafanya marekebisho ya vipengele kadhaa vya Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na nyinginezo ili kuweka mazingira ya upatikanaji wa mikopo ya nyumba. Aidha, Benki Kuu imeandaa Mkakati wa Kuboresha Huduma za Kifedha Maeneo ya Vijijini. Vile vile, Benki Kuu inaandaa Mkakati wa Elimu ya Fedha kwa Umma na utaratibu wa kisheria wa kuanzisha soko la dhamana za Halmashauri za Manispaa.
95. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Benki Kuu itaendelea kuimarisha sekta ya fedha ili iweze kukabili ipasavyo changamoto ya huduma na kupanuka kwa uchumi wa taifa. Ili kufanikisha azma hii, Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kufanya mageuzi katika sekta ya fedha ambayo yanalenga kurekebisha sera mbali mbali za fedha kwa kuongeza uwazi na ushindani katika utoaji wa huduma za kibenki na hivyo kurahisisha
60
upatikanaji wa mikopo. Hii ni pamoja na kupunguza riba kwa wakopaji. Hatua hizi zitaenda sambamba na utekelezaji wa program ya Awamu ya Pili ya Kurekebisha Sekta ya Fedha. Kadhalika, Serikali kupitia Benki Kuu itaanzisha utaratibu wa kukusanya na kusambaza taarifa za wakopaji (Credit Information Sharing System) ili kuwezesha wananchi kupata mikopo toka mabenki kwa urahisi. Benki Kuu imeandaa Mkakati wa Kuboresha Huduma za Kifedha Maeneo ya Vijijini (Rural Financial Services Strategy) ili kuongeza ushiriki wa wananchi vijijini katika kupata huduma za vyombo vya fedha. Benki Kuu inaandaa pia Mkakati wa Elimu ya Fedha kwa Umma (Financial Literacy Strategy) ili kuwahamasisha wananchi katika utumiaji wa huduma zitolewazo na taasisi za fedha na hivyo kuboresha maisha yao. Utaratibu wa kisheria unaandaliwa ili kuwezesha kuanzishwa kwa Soko la Dhamana za Halmashauri za Manispaa. Uanzishwaji wa soko hili utawezesha Halmashauri za Manispaa kupata fedha za miradi ya maendeleo kwa kukopa kutoka soko hili.
61
Benki ya Rasilimali Tanzania –TIB
96. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Benki ya Rasilimali Tanzania iliendelea kutoa mikopo ya maendeleo ya muda wa kati na mrefu, ambayo iliongezeka kutoka Shilingi bilioni 71.6 mwaka 2008 hadi kufikia Shilingi bilioni 81.8 mwaka 2009 ikiwa ni ongezeko la asilimia 14. Aidha, benki imeidhinisha mikopo ya Shilingi bilioni 5 kupitia Dirisha la Kilimo, kati ya maombi ya Shilingi bilioni 31.8 yaliyopokelewa. Maombi ya mikopo mingine ipatayo Shilingi bilioni 14.3 yanaendelea kuchambuliwa. Vile vile, katika kipindi hicho amana za wateja ziliongezeka kwa Shilingi bilioni 16.3 kutoka Shilingi bilioni 88.1 hadi Shilingi bilioni 104.4 sawa na asilimia 18.5.
97. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Serikali itaendelea kuimarisha mtaji wa TIB kwa kuwapatia fedha zaidi kwa shughuli za mikopo ya maendeleo na kwa ajili ya dirisha la Kilimo. Aidha, TIB inaendelea na mkakati wa kujirekebisha kwa kuunda kampuni mama (TIB Limited) kwa ajili ya mikopo ya maendeleo (DFI) na TIB Corporate itakayokuwa Benki ya Biashara kwa ajili ya wateja wake
62
watakaochukua mikopo kwa muda wa kati na mrefu.
Benki ya Posta Tanzania –TPB
98. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Benki ya Posta Tanzania iliendelea kutoa huduma za kibenki katika matawi 26 na kupitia ofisi 115 za Shirika la Posta (TPC) pale ambapo Benki hii haijafungua matawi. Amana za wateja ziliongezeka kutoka Shilingi bilioni 79.637 mwaka 2008 hadi kufikia Shilingi bilioni 88.479 mwaka 2009 likiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 8.842 sawa na asilimia 11. Katika kipindi hicho, Benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shillingi bilioni 38.179, ikilinganishwa na mikopo ya Shilingi bilioni 45.644 mwaka 2008. Benki ilipata faida ya Shilingi milioni 365, ikilinganishwa na faida ya Shilingi milioni 313 iliyopatikana mwaka 2008.
99. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Benki imelenga kukuza biashara yake kwa kuimarisha huduma kwa wateja kwa kuongeza ukusanyaji wa amana za wateja; kukuza mikopo; kukuza mtaji wa benki; na kuimarisha huduma ya utumaji wa fedha. Aidha,
63
Benki inatarajia kuongeza mapato yake kwa kuwekeza katika dhamana za Serikali, kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato, kuwaomba wanahisa hasa Serikali kuchangia zaidi mtaji wa benki hii na kuirekebisha sheria iliyoanzisha Benki na kuwa chini ya sheria ya Makampuni ili kuiwezesha kupanua wigo wa michango ya wanahisa na kuhimili ushindani.
Twiga Bancorp Limited
100. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009 Taasisi ya Twiga Bancorp Limited ilikusanya mapato ya Shilingi bilioni 7.9, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 6.2 kwa mwaka uliotangulia ikiwa ni ongezeko la asilimia 27.4. Taasisi iliweza kupata faida kabla ya kodi ya Shilingi milioni 182.4 kwa mwaka ulioishia Desemba 2009 ikilinganishwa na faida kabla ya kodi ya Shilingi milioni 286.6 ya mwaka 2008 sawa na upungufu wa asilimia 36.4. Hadi kufikia Desemba, 2009, Taasisi iliweza kuongeza amana za wateja kufikia Shilingi bilioni 46.4 kutoka Shilingi bilioni 32.5 kama ilivyokuwa tarehe 31 Desemba 2008 sawa na ongezeko la asilimia 42.8. Aidha, katika kipindi hicho, mikopo iliyotolewa kwa wateja mbalimbali ilifikia Shilingi bilioni 29.4,
64
ikilinganishwa na Shilingi bilioni 24.2 kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba 2008, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.5. Hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2009 Taasisi ilikuwa imewekeza Shilingi bilioni 8.5 kwenye Dhamana za Serikali na Amana katika benki zingine ikilinganishwa na Shilingi bilioni 5.0 kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba 2008 sawa na ongezeko la asilimia 70.
101. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11 Twiga Bancorp Limited itaendelea kuimarisha shughuli zake ili iweze kumudu ushindani wa kibiashara unaoendelea kukua katika sekta ya fedha hapa nchini. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na: kuboresha na kuongeza huduma ya mashine za kuchukulia fedha ‘ATMs’; kufungua matawi zaidi; kuimarisha huduma za mikopo kwa sekta ya viwanda na Biashara ndogondogo na kati, na mikopo ya kulipia bima za wateja; kupanua wigo wa huduma za kibenki zikiwemo huduma za VICOBA; pamoja na kubadilisha muundo wa taasisi kuwa benki kamili.
65
Consolidated Holdings Corporation -CHC
102. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009 CHC ilitekeleza kazi zifuatazo: kukusanya madeni chechefu ya iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara ambapo katika kipindi hicho makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 1.62; madeni yatokanayo na ubinafsishaji kiasi cha Shilingi bilioni 1.71 yalikusanywa; kiasi cha Shilingi bilioni 8.59 zilikusanywa kutokana na ufilisi wa mashirika ya Umma; na kushughulikia kesi 541 ambapo kesi 85 zilimalizika. Hadi Juni, 2010, jumla ya vitengo na mashirika 105 yametathminiwa kati ya 312 yaliyobinafsishwa. Tathmini na ufuatiliaji wa vitengo na mashirika 207 yaliyobaki unaendelea. Aidha, Shirika limeendelea na jukumu la kusimamia hisa za Serikali katika NBC Ltd na kupata gawio la Shilingi bilioni 3.98.
103. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Shirika limepanga kukusanya mapato kiasi cha Shilingi milioni 7,230. Majukumu yatakayotekelezwa ni pamoja na: kukamilisha ukusanyaji wa madeni yote chechefu; uuzaji wa mali mbalimbali; ufilisi wa mashirika ya umma; na ukusanyaji wa mapato kutokana na riba itakayotolewa na mabenki kwa amana zake.
66
HUDUMA ZA BIMA
Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima – TIRA
104. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa 2009/2010, Mamlaka iliendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima Na. 10 ya mwaka 2009. Utekelezaji wa sheria hiyo umeliwezesha soko la bima kuwa na mazingira bora zaidi ya ushindani wa kibiashara na kumlinda mteja. Katika kipindi hicho, idadi ya Makampuni ya Bima iliongezeka kutoka 18 mwaka 2008 hadi 25 mwaka 2009.
105. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2010/11, Wizara imepanga kufungua ofisi za mikoa za Mamlaka kuanzia na miji ya Arusha na Mwanza ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Aidha, maandalizi ya kuanzishwa kwa Baraza la Usuluhishi la Bima (Insurance Ombudsman) yatafanyika ikiwa ni pamoja na kukamilisha Sera ya Taifa ya Bima. Vile vile, mpango wa Miaka Mitano wa Kutoa Elimu ya Bima kwa Umma utaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2010/11.
67
Shirika la Bima la Taifa- NIC
106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Wizara iliendelea na mchakato wa kurekebisha Shirika la Bima la Taifa ili liweze kuongeza tija na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na: kutengeneza muundo mpya wa Shirika; kuandaa Ikama ya menejimenti na wafanyakazi wengine; imeajiri watumishi wapya katika ngazi zote; kuandaa Mpango wa Biashara na kuandaa Mfumo mpya wa TEKNOHAMA unaofaa kwa shughuli za bima. Aidha, katika mwaka wa fedha 2010/11, Wizara itaendelea na zoezi la urekebishaji wa shirika hili pamoja na kusimamia uuzaji wa mali za shirika zilizoainishwa kuuzwa ili fedha zitakazopatikana zitumike katika kulipia malimbikizo ya madai ya bima na kuweka Mfumo mpya wa TEKNOHAMA utakaosaidia katika kuendesha shughuli za bima kwa ufanisi zaidi.
68
MASOKO YA MITAJI NA DHAMANA
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana – CMSA
107. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana iliendelea na majukumu yake kwa kufanya yafuatayo: kukamilisha kazi ya kupitia Sheria ya Masoko ya Mitaji kwa kuzingatia Kanuni za Masoko ya Mitaji Duniani (IOSCO Principles) kwa lengo la kuiwezesha kushirikiana na wasimamizi wengine duniani. Marekebisho ya Sheria hiyo yamepitishwa na Bunge mwezi Aprili 2010. Marekebisho ya Sheria hiyo yanaruhusu kuanzishwa kwa soko la kukuza kampuni na ujasiriamali ndani ya Soko la Hisa la Dar es Salaam. Aidha, Wizara imeandaa rasimu ya Kanuni mbalimbali kuhusu utoaji wa leseni kwa washiriki wa soko la mitaji na kushughulikia maombi ya kampuni zinazotaka kuingia sokoni.
108. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, CMSA itaendelea kutekeleza mpango wake wa miaka mitano wa 2007/2008 – 2011/12 kwa kufanya maandalizi ya kuanzishwa kwa Soko la Kukuza Kampuni za Ujasiriamali;
69
kuendelea kuboresha Soko la Pili la Hatifungani za Serikali kwa kuzingatia matokeo ya utafiti uliofanyika kuhusu suala hili; kusimamia uanzishwaji wa Soko la Hatifungani za Serikali za Mitaa; kuboresha Mfumo wa Sheria ili kukidhi viwango vya Kimataifa; kuunganisha na Masoko ya Mitaji ya Afrika Mashariki pamoja na kuendelea na utoaji wa elimu kwa umma.
Soko la Hisa la Dar es Salaam – DSE
109. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10 shughuli za uuzaji na ununuzi wa hisa na hatifungani katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ziliendelea, ambapo kufikia Juni 2010 hisa zenye thamani ya shilingi bilioni 52.98 ziliuzwa na kununuliwa ikilinganishwa na hisa za shilingi bilioni 33.81 zilizouzwa na kununuliwa katika mwaka ulioishia Juni 2009. Aidha, mauzo ya hatifungani za Serikali yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 5.83 kwa mwaka 2008/09 hadi shillingi bilioni 256.81 mwaka 2009/2010, sawa na ongezeko la asilimia 4,305. Hadi kufikia Juni 2010, Serikali ilikuwa imeorodhesha hatifungani za muda mbalimbali zenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 1,414.2. Vile vile, Soko la Hisa
70
liliendelea kuuelimisha umma kuhusu uendeshaji wake na jinsi ya kutumia fursa zilizopo.
110. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Soko la hisa la Dar es Salaam litaendelea kuelimisha umma na kushawishi makampuni binafsi na ya umma kuorodhesha hisa zao. DSE pia itashirikiana na wadau wengine kusukuma mbele shughuli za uwezeshaji biashara za dhamana katika Jumuiya za Afrika Mashariki na nchi za kusini mwa Afrika. Aidha, mifumo ya TEKNOHAMA itaboreshwa ili kuwaunganisha madalali na soko kwa lengo la kuwafikia watanzania wengi.
Dhamana ya Uwekezaji Tanzania – UTT
111. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/10, UTT iliingia kwenye makubaliano na Shirika la Posta Tanzania na Benki ya CRDB. Katika makubaliano hayo, UTT ilitumia miundombinu ya Shirika la Posta kuanzisha ofisi sita za Kanda na kuwapa wenye akaunti za mfumo wa Tanzanite unaoendeshwa na Benki ya CRDB fursa ya kuwekeza kwenye mfuko wa Umoja. Aidha, UTT ilipata fursa ya kuuza vipande kwa Watanzania waishio nje ya nchi wenye nia ya
71
kuwekeza nchini kupitia mfumo huo. Mwitikio umekuwa ni wa kuridhisha.
112. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, UTT inatarajia kuboresha ofisi za Kanda katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Zanzibar, Mbeya, Dodoma na Dar es Salaam ili kuongeza idadi ya wananchi wanaojiunga na mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Aidha, itaanzisha mifuko ya Real Estate Investement Trust na Vision Tanzania Fund (VTF). Katika kutekeleza kaulimbiu ya KILIMO KWANZA, mfuko huu utachangia katika kutoa mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati katika sekta ya kilimo, madini, teknolojia ya mawasiliano na nishati asilia.
TAASISI ZA KITAALAM NA HUDUMA NYINGINEZO
Ofisi ya Taifa ya Takwimu –NBS
113. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2009/10, Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliendelea kutekeleza majukumu yake ya kukusanya, kuchambua, kutunza na kuwasilisha takwimu zilizohitajika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Takwimu za Pato la Taifa kwa kila nusu mwaka zilitolewa na kwa mara ya
72
kwanza takwimu hizo zilitolewa kwa robo mwaka. Aidha, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeendelea kutayarisha takwimu za mfumuko wa bei kila mwezi. Kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaendelea na imekamilika katika mikoa minane. Mikoa hiyo ni Pwani, Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Morogoro na Dodoma kwa Tanzania Bara. Kwa upande wa Visiwani ni Unguja kaskazini na Unguja Kusini. Vile vile, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imefanya majaribio ya utafiti wa Hali ya Rasilimali Watu nchini 2010 na utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto 2009/10.
114. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuboresha takwimu nchini, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeendelea na maandalizi ya Mpango Kabambe wa kitaifa wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu nchini (Tanzania Statistical Master Plan) ambao umeidhinishwa na Serikali mwezi Juni 2010. Katika mwaka wa fedha 2010/11 Taasisi itaendelea na: maandalizi ya Sensa ya watu ya majaribio itakayofanyika Agosti 2011; kufanya tafiti zilizoainishwa katika MKUKUTA II kwa ajili ya kutoa viashiria vilivyobainishwa; kufanya uchambuzi wa Sensa ya Kilimo na Mifugo na
73
kusambaza matokeo yake; kutoa takwimu za mfumuko wa bei kila mwezi; kutoa takwimu za Pato la Taifa kila robo mwaka na kutekeleza Mpango Kabambe wa kitaifa wa kuboresha na kuimarisha takwimu nchini.
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi –NBAA
115. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, NBAA kwa kushirikiana na wadau wengine, iliendesha semina na kongamano 58 ili kuelimisha Wahasibu pamoja na Walimu wa Vyuo vya Uhasibu kuhusu matumizi ya miongozo ya kimataifa ya utayarishaji wa hesabu na ukaguzi katika shughuli za kifedha serikalini, sekta binafsi pamoja na mashirika yanayojitegemea. Bodi pia ilipitia upya Mpango wa maendeleo 2005/06-2009/10, ili uiwezeshe NBAA pamoja na wadau wake kuendesha shughuli zao kulingana na matarajio.
116. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, NBAA itaendelea na sera ya kuhariri silabi ya mitihani yake ikiwa ni sehemu ya baadhi ya malengo yaliyopangwa kutekelezwa katika Mpango wa Maendeleo wa Bodi. Aidha, Bodi itaendelea na jukumu la usimamizi wa ubora
74
wa kazi ya ukaguzi wa hesabu nchini na itaendelea na ujenzi wa awamu zilizobaki kukamilisha Kituo cha utaalamu wa uhasibu, eneo la Bunju wilayani Kinondoni.
Bodi ya Michezo ya Kubahatisha – GBT
117. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha iliendelea kusimamia sekta ya michezo ya kubahatisha nchini. Bodi ilianzisha aina mpya ya leseni ya uendeshaji wa mashine za slots yenye maudhui ya kasino ndogo ambayo inaitwa 40-machine sites ambapo kanuni za uendeshaji wake zipo tayari na zimechapishwa katika Gazeti la Serikali- GN 278 la tarehe 14 Agosti, 2009. Aidha, Bodi imekwishatoa leseni kwa mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa kupitia mchakato wa ushindani. Bodi inakusudia kufanya mchakato ambao utawezesha mashine zote za slots kuunganishwa kwa mfumo wa kompyuta (Central Electronic Monitoring System). Nia ya zoezi hili ni kurahisisha usimamizi wa mashine hizi na kuwezesha kutoa kodi kutokana na mapato ya kila mashine badala ya utaratibu wa sasa ambapo kodi hutozwa kwa idadi ya mashine. Katika mwaka wa fedha 2009/10, Bodi ilikusanya kodi
75
iliyofikia Shilingi bilioni 4.6 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 4.2 iliyokusanywa mwaka 2008/09.
118. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/11, Bodi itaendelea kusimamia michezo ya kubahatisha nchini, na inatarajia kukusanya kodi inayofikia Shilingi bilioni 5.8 kutokana na kuendelea kukua kwa shughuli zilizopo ikiwa ni pamoja na kuanza kwa Michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa ifikapo Januari, 2011.
Mpango wa Millenium Challenge Account- Tanzania
119. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, MCA-T ilitekeleza kazi zifuatazo: kukamilisha makabrasha ya usanifu na mipango ya fidia kwa barabara za Tanga –Horohoro, Namtumbo – Songea, Peramiho – Mbinga na Tunduma – Sumbawanga; kukamilisha zoezi la uteuzi wa Wahandisi Wasimamizi na Makandarasi; kuanza ujenzi wa barabara ya Tanga- Horohoro; kufanya upya usanifu wa barabara za Vijijini Pemba na kuandaa michoro ya kihandisi na ripoti ya athari za mazingira. Kazi zote hizi zilikamilika kama zilivyopangwa.
76
120. Mheshimiwa Spika, kwa miradi ya umeme kazi zifuatazo zilifanyika: usanifu, michoro ya kiuhandisi, ripoti ya mazingira na mipango ya fidia katika maeneo ya mradi wa kupeleka umeme Zanzibar kupitia chini ya bahari, kusaini mkataba kati ya MCA-T na kampuni ya VISCAS ya Japan kwa kazi ya kuweka nyaya za umeme kupitia chini ya bahari kwenda Zanzibar; kukamilisha zoezi la uchujaji wa makampuni kwa kazi ya ukarabati ya vituo vya umeme (sub-stations); na kutangaza zabuni na kuanza uchambuzi wa makampuni kwa kazi ya ukarabati wa mtandao wa umeme katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya na Mwanza. Kwa miradi ya maji, kazi zilizofanyika ni kukamilisha michoro ya kiuhandisi na makabrasha ya zabuni za miradi ya ujenzi wa chujio la maji Ruvu Chini kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani na mfumo wa maji kwa mkoa wa Morogoro. Kwa mwaka 2010/11 kazi ya ujenzi kwa miradi mingi chini ya MCA-T itaanza kutekelezwa kwani mikataba yote mikubwa itakuwa imesainiwa na wakandarasi kuanza kazi ifikapo Septemba 2010.
77
ASASI ZA MAFUNZO
Taasisi ya Uhasibu Arusha – IAA
121. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Chuo kiliendelea na utoaji wa mafunzo katika fani za Uhasibu, Ugavi, Usimamizi wa Kodi, Benki, Utawala wa Biashara, Teknolojia ya Habari na Sayansi ya Kompyuta katika ngazi ya Stashahada ya juu. Aidha, Chuo kiliendelea kutoa mafunzo ya uhasibu na usimamizi wa fedha katika ngazi ya Stashahada ya uzamili. Tangu mwezi Septemba 2009, Chuo kimeanza kutoa mafunzo ya Shahada ya Uzamili katika fani ya Teknolojia ya Habari na Logistics kwa kushirikiana na Chuo cha Coventry cha Uingereza, hii imepelekea kuongezeka kwa udahili kutoka wanafunzi 2,860 mwaka wa masomo 2008/09 hadi wanafunzi 3,008 kwa mwaka wa masomo 2009/10.
Taasisi ya Uhasibu Tanzania – TIA
122. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Taasisi iliendelea kujenga na kukarabati majengo ili kuongeza uwezo katika matawi yake yaliyopo Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara na Singida. Katika mwaka wa fedha
78
2010/11, Taasisi itaendelea kuboresha elimu inayotolewa kwa kuongeza wahadhiri, kuimarisha kitengo cha utafiti na ushauri wa kibiashara, kuendelea kufundisha kozi zinazotolewa na Taasisi pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi. Aidha, Chuo kitaendelea kuboresha mfumo wa usimamizi wa fedha na rasilimali watu.
Chuo cha Usimamizi wa Fedha – IFM
123. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Chuo cha Usimamizi wa Fedha-IFM kiliandaa mitaala ya shahada katika fani ya Uhasibu, Benki na Fedha, Bima na Hifadhi ya Jamii, Kodi, Teknolojia ya Habari na Sayansi ya Kompyuta na kuanza kutumika katika mwaka huo wa masomo. Lengo ni kuhakikisha kuwa mitaala ya elimu ya chuo inakidhi mahitaji ya soko la ajira pamoja na kujiajiri.
124. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Chuo kimeendelea kutoa mafunzo ya uzamili kwa kushirikiana na Taasisi ya Biashara za Kimataifa ya India, Chuo Kikuu cha Strathclyde (Scotland), pamoja na Chuo Kikuu cha Avinashilingam kilichopo India. Mafunzo hayo ni ya Shahada ya Uzamili ya Biashara za Kimataifa,
79
Shahada ya Uzamili ya Teknolojia ya Habari na Uongozi na Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Fedha. Idadi ya wanafunzi waliodahiliwa katika kipindi hicho ni 6,132. Chuo pia kimeanzisha ushirikiano wa Kitaaluma na taasisi ya Teknolojia ya Habari ya Dublin nchini Ireland katika mafunzo ya Shahada ya Sayansi ya Kompyuta. Aidha, ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji, utafiti na ushauri, Chuo kimeendelea kuajiri wafanyakazi katika fani mbalimbali wakiwemo walimu.
125. Mheshimiwa Spika, Chuo kiliboresha majengo yaliyopo ili kuongeza nafasi kwa ajili ya kukidhi ongezeko la wanafunzi. Baadhi ya majengo yalipanuliwa kwa kuongeza ghorofa na baadhi yaliyokuwa ofisi yalibadilishwa kuwa madarasa na maabara za kompyuta. Katika mwaka wa fedha 2010/11, Chuo kitaendelea kuandaa mitaala ya Shahada ya Uzamili katika fani za Uhasibu, Usimamizi wa Fedha, Kodi, Uendeshaji Biashara, Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bima na Usimamizi wa Uzuiaji Majanga.
80
Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini – IRDP
126. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Chuo kimefanya yafuatayo: kimeendesha mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa wanafunzi wapatao 1910; kimefanya utafiti na kutoa ushauri na uelekezi kwa wadau mbalimbali wa maendeleo nchini; kimekamilisha ujenzi wa ukumbi utakaotumika kwa shughuli mbalimbali za kitaaluma na kijamii. Aidha, Chuo kilikamilisha uandaaji wa michoro na kuanza ujenzi wa jengo la pili la taaluma ambalo kwa kiasi kikubwa litaondoa tatizo la upungufu wa madarasa, kumbi za mihadhara na ofisi za walimu.
127. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2010/11, Chuo kitaendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi za Cheti, Stashahada, Shahada na Stashahada za Uzamili. Aidha, Chuo kitaanzisha mafunzo ya Shahada za Uzamili katika fani za Uchumi, na Mipango ya Mazingira. Programu hizo zote zitakuwa na jumla ya wanafunzi 2500. Vile vile, Chuo kitaendelea kujenga jengo la pili la taaluma, kujenga uwezo wa watumishi wake na kuajiri watumishi wapya ili
81
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC
128. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2009/10, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, kiliendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu ya Stashahada na Cheti cha Takwimu. Idadi ya wanafunzi waliosajiliwa walikuwa 108 kutoka nchi za Tanzania, Namibia, Uganda, Jamhuri ya Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Shelisheli. Kati ya wanafunzi hao, wanawake walikuwa 30 sawa na asilimia 27.8 ya wanafunzi waliosajiliwa. Pia Chuo kiliendesha mafunzo ya muda mfupi ya ukusanyaji na matumizi ya Takwimu kwa Taasisi mbalimbali. Jumla ya washiriki 104 walinufaika na mafunzo hayo. Aidha, Chuo kiliendelea na maandalizi ya kuanzisha Shahada ya kwanza ya Takwimu. Vile vile, Chuo kilifanya uzinduzi wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja mnamo tarehe 28 Mei, 2010.
129. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2010/11, Chuo kitaendelea kufanya yafuatayo: kutoa mafunzo ya muda mrefu ya Cheti na Stashahada; kukamilisha na kuanza kutoa
82
mafunzo ya shahada ya kwanza ya Takwimu; kutoa mafunzo ya muda mfupi na ushauri wa kitakwimu kwa Asasi mbalimbali na watu binafsi; kuanza ujenzi wa jengo la Utawala; kuajiri wafanyakazi wenye sifa na kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo wafanyakazi. Aidha, Chuo kupitia Mpango Mkakati wake, kitaendelea kukamilisha ujenzi wa njia za mawasiliano ya barabara na mfumo wa mawasiliano ya teknolojia kwenye jengo jipya la madarasa na kuanza mchakato wa kuongeza vyanzo vya maji safi, pamoja na kufanya maandalizi ya kupata michoro ya jengo la mhadhara na viwanja vya michezo.
CHANGAMOTO NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA
130. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni kama ifuatavyo:
i) Makusanyo ya mapato ya ndani kuwa chini ya malengo ya kila mwezi na hivyo kusababisha ugawaji wa rasilimali fedha kuwa chini ya malengo;
ii) Ucheleweshaji wa uwasilishaji wa hati za madai wizarani;
83
iii) Ucheleweshaji wa Majalada ya watumishi wanaotakiwa kustaafu na kufikishwa Hazina yakiwa na nyaraka pungufu;
iv) Upungufu katika Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria zilizoanzisha Asasi na Mashirika mbalimbali;
v) Upungufu katika kusimamia ununuzi wa Umma na udhibiti wa fedha za Umma;
vi) Upungufu wa Ofisi kwa watumishi wa Wizara.
vii) Kuwasilishwa kwa maombi mengi nje ya Bajeti mara baada ya Bajeti kuidhinishwa na Bunge
131. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, hatua zifuatazo zilichukuliwa:
i) Wizara kwa kupitia TRA inaendelea na mikakati mbalimbali ya kupunguza mianya ya ukwepaji kodi na kurekebisha upungufu katika ukusanyaji wa mapato;
84
ii) Wizara imewashauri wadai kuwasilisha hati zao za madai kwa wakati;
iii) Wizara imewaelimisha Maafisa Utumishi kuhusu kuandaa na kuwasilisha mapema nyaraka za watumishi wao wanaotarajia kustaafu;
iv) Marekebisho ya Sheria ya Msajili wa Hazina (SURA 370) yamefanyika na Sheria imeshapitishwa katika Bunge la mwezi Aprili mwaka 2010 na Sheria zilizoanzisha Asasi na Mashirika mbalimbali zinaendelea kupitiwa;
v) Sheria ya Fedha za Umma na ya Ununuzi wa Umma zimepitiwa na kufanyiwa marekebisho; na
vi) Wizara katika mpango wa muda mfupi, imeendelea kutafuta ofisi na katika mpango wa muda mrefu Wizara imepanga kujenga jengo la ofisi.
vii) Wizara imeendelea kuwakumbusha Maafisa Masuuli kusimamia upangaji wa vipaumbele vya maeneo yao na kuhakikisha fedha za kutosha zinatengwa
85
kwa maeneo hayo pamoja na kufuata taratibu za Kibajeti kama zinavyofafanuliwa kwenye Mwongozo wa Mpango na Bajeti.
MAKADIRIO YA MATUMIZI KWA MWAKA 2010/11
Maombi ya Fedha:
132. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza majukumu ya Wizara na kufikia malengo yaliyokusudiwa katika mwaka wa fedha 2010/11, ninaomba Bunge lako liidhinishe kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
Fungu 50:
(a) Matumizi ya kawaida ni Shilingi 94,271,677,000 (Bilioni 94.27) Kati ya hizo, Mishahara ni Shilingi 2,957,023,000 (Bilioni 2.96) na matumizi mengineyo Shilingi 91,314,654,000 (Bilioni 91.31).
(b) Miradi ya Maendeleo Shilingi 278,921,290,000 (Bilioni 278.92). Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi 7,309,135,000 (Bilioni 7.31) na fedha za nje ni Shilingi 271,612,155,000 (Bilioni 271.61).
86
Fungu 21:
(a) Fedha za matumizi ya kawaida ni Shilingi 962,062,861,500 (Bilioni 962.10). Kati ya hizo Shilingi 1,238,047,000 (Bilioni 1.24) ni mishahara na Shilingi 960,824,814,500 (Bilioni 960.82) ni kwa ajili ya matumizi ya idara na taasisi zilizo chini ya Wizara marekebisho ya mishahara ya watumishi wa Serikali, pamoja na matumizi maalum ikiwemo dharura na michango ya kimataifa.
(b) Fedha za miradi ya maendeleo ni Shilingi 100,023,194,000 (Bilioni 100.02). Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi 50,832,264,000 (Bilioni 50.83) na fedha za nje ni Shilingi 49,190,930,000 (Bilioni 49.20)
Fungu 22:
Deni la Taifa Shilingi 1,747,233,792,000 (Bilioni 1,747.23)
Fungu 23:
(a) Fedha za matumizi ya kawaida ni Shilingi 82,344,269,000 (Bilioni 82.34). Kati ya
87
hizo, mishahara Shilingi 2,794,013,000 (Bilioni 2.80) na matumizi mengineyo ni Shilingi 79,550,256,000 (Bilioni 79.55).
(b) Fedha za miradi ya maendeleo ni Shilingi 10,264,794,000 (Bilioni 10.26) Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi 4,185,752,000 (Bilioni 4.20) na fedha za nje ni Shilingi 6,079,042,000 (Bilioni 6.10).
Fungu 45: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
(a) Fedha za matumizi ya kawaida ni Shilingi 26,574,258,500 (Bilioni 26.57). Kati ya hizo, mishahara ni Shilingi 3,216,577,000 (Bilioni 3.22) na matumizi mengineyo ni Shilingi 23,357,681,500 (Bilioni 23.36).
(b) Fedha za miradi ya maendeleo ni Shilingi 10,581,010,000 (Bilioni 10.58) kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi 4,812,494,000 (Bilioni 4.81) na fedha za nje ni Shilingi 5,768,516,000 (Bilioni 5.77).
HITIMISHO
133. Mheshimiwa Spika, hotuba hii ya Wizara ya Fedha na Uchumi inahitimisha uwasilishaji wa mapendekezo ya Serikali ya Bajeti ya mwaka 2010/11 kwa Wizara, Idara za Serikali
88
zinazojitegemea, Mikoa na Serikali za Mitaa. Aidha, tunatarajia leo hii Bunge lako Tukufu litapata fursa ya kupitisha Muswada wa kuidhinisha matumizi ya Serikali kwa mwaka huu. Kama nilivyoeleza katika hotuba ya Bajeti ya Serikali, Mkutano huu wa Bunge ni wa mwisho katika muhula huu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne. Katika kipindi chote cha Bunge hili la Bajeti, Serikali imefarijika na maoni na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wa kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali yakijumuisha kilimo, ufugaji, uvuvi, miundombinu ya barabara, reli, bandari, nishati, sekta za maendeleo ya jamii (Elimu, Afya, Maji), viwanda, mawasiliano na sekta ya fedha. Vile vile, Serikali imefaidika na maoni na ushauri wa Bunge hili katika kuboresha Utawala Bora na Uwajibikaji, Mazingira, Usawa wa kijinsia na Demokrasia.
134. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuonyesha imani yake kubwa kwangu ya kuniteua kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadhifa ambao naamini nimeutumikia
89
kwa uadilifu mkubwa. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Makamu wa Rais kwa kusimamia kwa uhodari mkubwa vikao vya mashauriano kuhusu kero za Muungano baina ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na masuala ya mazingira. Aidha, napenda kumshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb) kwa kusimamia shughuli za Serikali Bungeni kwa umahiri mkubwa ulionisaidia sana katika utekelezaji wa kazi zangu.
135. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano wao mkubwa. Napenda pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano wao wakati wa kujadili nyaraka mbalimbali za Serikali nilizowasilisha Bungeni. Kipekee, napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kilosa kwa kunipa fursa ya kuwawakilisha katika awamu hii. Ni matumaini yangu kwamba sikuwaangusha na hivyo natarajia watanipa fursa nyingine ya kuendelea kuwatumikia ili kukamilisha kazi niliyoianza.
136. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Advertisements