Mpiga duri Zanzibar

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, amesema Serikali imeweka kipaumbele uanzishaji wa Bandari mpya, ili kuondokana na changamoto kadhaa zinazoikabili bandari ya Malindi hivi sasa.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwa na Bandari kubwa ya kisasa itakayoweza kutoa huduma kwa ufanisi, kulingana na Teknolojia ya Dunia ilivyo.

Maalim Seif amesema hayo leo Bandarini Malindi, alipokuwa na mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi pamoja na watendaji wakuu wa Shirika hilo, kufuatia ziara yake kuangalia shughuli zinazoendeshwa na Shirika pamoja na changamoto mbali mbali zinazokabili.

Amesema suluhisho pekee la kuondokana na changamoto kadhaa zinazoikabili Bandari hiyo, ikiwemo ufinyu wa nafasi na miundo mbinu chakavu ni kupata Bandari mpya itayojengwa kulingana na mahitaji ya nchi na kwa wakati uliiopo.

Alisema Serikali inaendelea na mazungumzo na washirika wa Maendeleo Duniani, kusaidia mpango huo ili kuimarisha biashara na kukuza uchumi wa Taifa.

Alitaka Menejment ya Shirika hilo kuendelea na juhudi za kuliimarisha Shirika hilo na kukabiliana na changamoto zilizo ndani ya uwezo wake ili kuongeza mapato, kujiendesha kibiashara na kuleta ushindani kwa Bandari nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki za Mombasa, Tanga na Dar es Salaam.

Alisema pale Shirika litakapokuwa na vifaa vya kisasa kutasaidia kuondosha mlundikano wa Meli na mizigo hivyo kuvutia zaidi wafanyabiashara kutumia bandari hiyo.

Akigusia uimarishaji wa Bandari ndogo ndogo zilizo chini ya Shirika hilo, hususan ile ya Mkokotoni,Malim Seif alishauri utafiti wa kutosha ufanyike ili kuangalia faida itakayopatikana katika ujenzi wa Bandari hiyo, baada ya kuibuka kwa mawazo mapya ya kujengwa katika eneo la Fukuchani badala ya Mkokotoni.

Alitaka kutumiwa vyema fedha kidogo zilizopo kwa kuwekeza katika maeneo yenye faida kwa siku zijazo kulingana na mabadiliko ya dunia na kuondokana na dhana ya mazoea.

Katika hatua nyingine Maalim Seif alisistiza umuhimu wa Menejment hiyo kuzingatia suala la usalama wa Bandari kwa kuweka udhibiti wa kutosha kukabiliana na uingiaji holela wa watu banadarini.

Alisema katika utekelezaji wa jambo hilo, elimu ya kutosha inapaswa kutolewa ili wananchi waelewe umuhimu na ‘unyeti’ wa eneo hilo na kuondokana na dhana ya kuwa wanasumbuliwa pale wanapofanyiwa ukaguzi wa mizigo yao.

Aliwataka wafanyakazi wa mizigo (wapekuzi) kufanya shughuli zao kwa uangalifu mkubwa na kuipekua mizigo yote inayoingia na kutoka Bandarini, ikiwemo vifaa vilivyokwisha kutumika (used) kwa kutumia mashine za kisasa pamoja na mbwa, ikiwa ni juhudi za kukabiliana na uingizaji wa madawa ya kulevya.

Mapema Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Hamad Masoud alisema Bandari hiyo ilikuwa katika hatari ya kukimbiwa na meli kutoka nje kwa kukosa usalama wa kutosha,kulingana na masharti ya I.M.O.

Hata hivyo alisema juhudi kubwa zimechukuliwa kuzipatia ufumbuzi baadhi ya kasoro zilizokuwepo, na kuainisha kuibuka kwa manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wananchi, wakihisi kusumbuliwa kufuatia utaratibu wa kuwekwa vitambulisho.

Aidha alisema kufuatia ujio wa Wawakilishi wa Meli, mchakato unaendelea utakaowezesha kupata meli za mizigo kutoka Dubai na kuja moja kwa moja hadi Pemba, na kuainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuondosha tofauti za bei za bidhaa kati ya Unguja na Pemba.

Alisema pale mambo yatakapoiva wafanyabaishara wote watajuilishwa juu ya jambo hilo sambamba na azma ya Serikali ya ubadilishaji wa Tishali hivi karibuni.

Mapema Mkurugenzi wa Shirika hilo, Mustapha Aboud Jumbe, alimweleza Makamu wa Rais juu ya changamoto kadhaa zinazolikabili shirika hilo, ikiwemo ufinyu wa eneo la bandari na uchakavu wa miundo mbinu,mlundikano wa makontena matupu, ongezeko la uzito wa meli,usalama wa meli hususan zile za kitalii, ukosefu wa taa katika minara na maboya , kutoka nyufa kwa Jet katika gati ya Wete, pamoja na kudidimia kwa gati ya Mkoani.

Aidha alieleza malengo ya Shirika lake la kuwa na mradi wa kutumia nishati ya Jua (solar power) katika minara yake Unguja na Pemba, badala ya gesi na kuweka kando matumizi ya umeme ambao una gharama kubwa.

Katika ziara hiyo, Maalim Seif alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali, ikiwemo eneo la Abiria na tishali la vyombo, sehemu ya kuhudumia vyombo vya ufukweni (landing Craft), kuangalia ukuta wa Forodhani ulioathirika na mawimbi ya Bahari, eneo la majahazi, karakana ya Shirika, eneo la kupitishia mashine za usalama (screen area) pamoja na eneo la Bwawani lililofukiwa na kutumika kwa ajili ya kuhifadhia Makontena.

 

Advertisements