Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema licha ya ufinyu wa bajeti uliopo serikali itaendelea kuwahudumia wananchi kwa kutumia raslimali kwa umakini.

Akifungua semina ya Uongozi kwa watendaji wa serikali ya mapinduzi Zanzibar huko hoteli ya Zanzibar Beach Resort amesema dawa ya ufinyu huo unahitaji kubana matumizi na kuongeza vyanzo vya mapato.

Dr. Shein amesema serikali kupitia wizara zake imepitisha sera za maendeleo ikiwemo kilimo na kuwasisitiza viongozi hao kuzieleza na kuzitekeleza sera hizo kwa wananchi ili ziwe chachu ya maendeleo.

        Aidha, Dk. Shein amewaeleza watendaji hao kuwa amewateua kwa lengo la kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Amesema mahitaji makubwa ya wananchi ni huduma bora za afya, elimu, maji, barabara, kilimo na huduma nyenginezo ambazo ni msingi mkubwa wa kukuza uchumi.

Katika semina hiyo Dk. Shein pia aliwasisitiza viongozi hao kufuata maadili, nidhamu na utiifu katika kuwahudumia wananchi na kuwatekelezea mahitaji yao katika sehemu zao za kazi.

Nae Mshauri wa Masuala ya Utawala, anaehusika na nchi za Afrika Mashariki kutoka jumuiya Madola, mjini London Dustan Maina amesema watendaji wa serikali wanajukumu la kuwatumikia wananchi.

Miongoni mwa mada zitakazotolewa katika semina hiyo ya siku tatu ni Hali ya uchumi wa Zanzibar, Sheria ya Utumishi wa Umma, Mpango wamaendeleo wa Zanzibar na Mfumo wa sheria wa Usimamizi wa Fedha.

 

Advertisements