Umeme wa upepo

Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali imevutiwa na azma ya Jumuiya ya Ulaya EU, kusaidia sekta ya umeme nchini, kupitia vyanzo mbali mbali. Amesema hatua hiyo italisaidia taifa kuondokana na upungufu wa nishati hiyo inayokatika mara kwa mara na kusababisha kushuka kwa shughuli za uzalishaji. Maalim Seif amesema hayo katika ukumbi wa hoteli ya kitalii ya Movenpik jijini Dar es Salaam, alipozungumza na ujumbe wa Jumuiya ya EU, ulioongozwa na Balozi Tim Cleark. Ujumbe huo wa EU pia umeahidi kuisaidia Zanzibar katika uimarishaji wa nishati ya umeme kupitia teknolojia ya kisasa, ikiwemo upepo, maji ya bahari na jua. Malim Seif amesema Zanzibar inahitaji umeme wa uhakika ili kufikia lengo lake la kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kijamii nchini. …2….DAR ES SALAAM… DAR ES SALAAM….2 Amesema Zanzibar inategemea umeme wa nguvu za maji kupitia waya wa chini ya bahari, ambapo kutokana na uchakavu uwezo wake wa kusambaza umeme ni megawati 40 ambapo mahitaji ni megawati 50. Malim Seif amefahamisha mbali na mpango wa Shirika la MCC kusambaza umeme kupitia waya wa chini ya bahari mwaka 2013, bado ipo haja ya kuanzisha vyanzo vyengine vya uzalishaji umeme. Katika hatua nyingine Maalim Seif alimweleza Balozi huyo azma ya Serikali ya ujenzi wa bandari mpya ya mizigo katika eneo la Mpigaduri. Nae Balozi Clearck ameishauri serikali kukaa pamoja na wadau wa sekta ya umeme na kutaka kufanywa utafiti ili kufahamu athari na gharama za uzalishaji wa umeme huo kupitia vyanzo hivyo. Amesema Jumuiya ya Ulaya iko tayari kugharamia uendeshaji wa miradi hiyo kupitia teknolojia ya kisasa ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini. Aidha alimhakikishia Makamu wa kwanza wa Rais kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kutoa misaada yake ya kifedha kwa ajili ya maendeleo na ukuzaji wa uchumi wa Zanzibar.

Advertisements