Raiswa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali MohamedShein,akishiriki katika uzinduzi wa Uvunaji wa Mpunga wa mbegu,aina yaNERICA,huko katika shamba la kilimo la Mbegu hiyo Bambi Mkoa wa Kusini Unguja. ( Picha na Othman Mapara)

MRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kufanya Mapinduzi ya kilimo tayari limeanza kutekelezwa na mbegu ya aina ya NERICA ndio mkombozi wa kufikia lengo hilo.

 

Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti  mara baada ya kushiriki kikamilifu katika uvunaji wa mbegu ya mpunga wa kilimo cha juu aina ya  (NERICA) huko Bambi  na uzinduzi za uvunaji mpunga Kitaifa, huko katika bonde la Kisimamchanga Kiboje Mkwajuni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

 

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa mbegu ya aina ya NERICA ni mkombozi mkubwa katika kufikia malengo yaliokusudiwa katika Mapinduzi ya Kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula.

 

Alisema kuwa Serikali kwa upande wake tayari imeshaanza kutekeleza Mapinduzi ya Kilimo kwa kuamini kuwa hatua hiyo ni moja ya kupambana na mfumko wa bei ya vyakula hasa mchele ambao ndio chakula kikibwa hapa Zanzibar.

 

Dk. Shein alisema kuwa ongezeko la idadi ya watu hapa Zanzibar tokea Mapinduzi Matukufu ya Januari mwaka 1964 ambapo idadi ya watu ilikuwa ni laki 3 na mnamo mwaka 1974 ilikuwa ni laki 640 elfu na sensa ya mwaka 2002 idadi ikafikia milioni 1.2 hatua ambayo nayo imepelekea maongezeko ya mahitaji yakiwemo chakula.

 

Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuongeza uzalishaji wa chakula kwani kwa mujibu wa takwemi inaoneshakuwa mchele unaotumiwa kwa chakula hapa Zanzibar ni tani 80 elfu lakini unazozalishwa na wakulima hapa nyumbani ni tani 16 elfu tu na kiasi chote kilichobaki hununuliwa nje ya nchi, ‘Hii ni mbegu na yule atakae piga goti ale basi ataharibu”alisisitiza Dk. Shein.

 

Aidha, Dk. Shein aliwataka wakulima nao kubadilika na kushirikiana vizuri na wataalamu wa sekta ya kilimo katika kuhakikisha mbegu hiyo ya aina ya NERICA inaleta tija kwa wakulima na wananchi kwa jumla na kusisitiza nia ya serikali ya kubadilisha mfumo mzima wa kilimo kwa kutumia vifaa na nyenzo za kisasa za kilimo ili kuondokana na kilimo cha kilichopitwa na wakati.

 

Alisema kuwa serikali kwa mara ya kwanza italeta mashine za kuvunia mpunga ili wakulima wapate kuvuna kwa tija kwani ni njia moja wapo ya kuimarisha sekta ya kilimo.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa mikakakti madhubuti iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara yake ya Kilimo ni kuhakikisha wakulima wanapatiwa mbegu bora, mbolea, pembejeo,Mabwana Shamba,huduma ya umeme na maji ya kutosha.

 

Dk. Shein alisema kuwa tayari washirika wa maendeleo nao wanaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta hiyo wakimo Japan, Korea ya Kusini, Marekani hasa katika mradi wao wa ‘Feed the future’ na wengineo.

 

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa serikali imedhamiria kukiimarisha kilimo cha aina zote likiwemo zao la karafu, pilipili na nyenginezo pamoja na kuimarisha mbegu mpya ya muhogo ambayo ipo na kuwaahidi wakulima kuwa watapewa.

 

Akiwa katika bonde wa Kisimamchanga akizungumza na wakulima wa bonde hilo, alitoa pongezi kwa wakulima hao kwa jitihada zao za  kuendeleza kilimo cha mpunga kwa kuongeza mara nne uzalishaji wa mpunga katika bonde lao kutoka na mradi wa PADEP.

 

Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana pamoja na wakulima hao katika kufikia lengo hilo “Ili tule ni lazima tulime”,alisema Dk. Shein.

 

Alisema kuwa tayari serikali imeshapitisha Sheria ya Usalama wa Chakula hivi karibuni kwa kuzingatia umuhimu wa uhifadhi  wa chakula  ambapo serikali itajenga mahala ya chakula kwa lengo la kuweza kusaidia pale patakapotokezea uhaba wa chakula.

 

Pia, Dk. Shein akiwa katika bonde hilo aliwaahidi wakulima hao kuwajengea njia yao inayotoka barabara kuu hadi bondeni kwa kiwango cha kifusi, umeme, kuchimbiwa kisimatela la kubebea mizigo, mashine za kuvunia na iwapo wataalamu watahsuri kujengwa hala la kuhifadhi mpunga, pia, serikali itajenga.

 

Nae, Waziri wa Kilimo na Maliasili Mhe. Mansour Yussuf Himid aliwaeleza Wakulima kuwa katika Bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2011-2012 itakuwa na matumaini makubwa na kuleta faraja kwa wakulima wote wa Zanzibar.

 

Alisema kuwa miongoni mwa malengo na matarajio ni kuhakikisha bei ya mboleo, mbegu, huduma za matrekta, dawa za kuulia wadudu bei zake zitakuwa ndogo sana kwani serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein ameshakisikia vilio vya wakulima juu ya bei za mahitaji hao.

 

Alisema kuwa dhamira ya Wizara ya Kilimo ndani ya miaka mitano ni kulima hekta 6000 za umwagiliaji maji ndani ya hekta 8521 ambapo kati ya hizo ni hekta 700 tu ndizo inzolimwa hivi sasa na kueleza kuwa tayari Korea ya Kusini katika mradi wake italima hekta 2000 na Marekani hekta 2000.

 

Aidha, alisema kuwa mashamba darasa yataongezwa na kufikia 1200, ambapo pia mashaba darasa nne za mikarafuu zikiwemo mbili za Unguja na mbili za Pemba zitaanzishwa ikiwa ni pamoja na kuazishwa kwa mradi mpya utaoweza kuwakopesha wakulima fedha sanjari na kuliimarisha bonde la Kibonde Mzungu ili kuweza kuzalisha mbegu za mpunga.

 

Pia, Mkuu wa Mkoa aliwatoa hofu na kuwataka wakulima wa Bonde la Kisimamchanga kuendelea kulitumia bonde hilo ambapo tayari limeshapimwa na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuanza kilimo cha umwagiliaji maji.

 

Nao wakulima wa bonde la Kisimachanga walieleza kuwa mara baada ya kuingia katika mradi wa PADEP ambao umetumia zaid ya Shilingi milioni 32 mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa mpunga ambapo hivi sasa wanazalisha polo 4 kwa robo hekta ambazo hapo zamani ndizo walizokuwa wakizalisha kwa hekta nzima.

 

Katika hafla hiyo ya kitaifa baadhi ya wakulima na viongozi kutoka mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba walihudhuria pamoja na Mawaziri, Wawakilishi,Mkuu wa Mkoa wa Kusini ambaye n mwenyeji pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Mgharibi na Kusini Pemba walihudhuria, viongozi wa serikali na kisiasa, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali walihudhuria.

 

Jumla ya heka tano za mbegu ya mpunga wa aina ya NERICA zimevunwa pia mbegu hizo zinatarajiwa kupandwa kwa wingi katika mvua za vuli zinazokuja kwa lengo la la kuja kupandwa wakati wa Masika ambapo zaidi ya tani 3700 za ziada zinatarajiwa kupatikana katika msimu wa masika ujao lengo ni kufikia asilimia 50 ya uzalishaji ndani ya miaka mitano

 

Advertisements