Malim Seif Sharif Hamad

Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Serikali itazingatia upya viwango vya kodi vinavyotozwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kutoka nje.

Amesema viwango vikubwa vya kodi wanavyotozwa wafanyabiashara, vinawaumiza wananchi  na kuwanufaisha baadhi ya watu wachache kutoka taasisi zinazosimamia makusanyo hayo.

Maalim Seif amesema hayo ofisini kwake Migombani, alipokuwa na mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara,wenye viwanda na Wakulima Zanzibar, waliofika kujitambulisha na kubadilishana mawazo.

Amesema iko haja kwa serikali kuangalia upya viwango vya kodi kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini ili Zanzibar irudie hadhi yake ya kuwa kituo cha kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Malim Seif amesema iwapo viwango vya kodi vitapungua, bidhaa nyingi na zilizo bora zitaingia nchini na kuuzwa kwa bei nafuu, hivyo kufungua milango kwa wafanyabiashara wa ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika kuja Zanzibar, badala ya kwenda Ughaibuni.

Akizungumzia hoja ya kubinafsishwa kwa zao la Karafuu ili kumnufaisha zaidi mkulima, Maalim Seif amesema Serikali inaifanyia kazi hoja hiyo, ikitilia maanani uepukaji wa matatizo yanayoweza kujitokeza.

Amesema moja ya mifano inayoangaliwa kwa karibu na Serikali ni zao la mwani, ambalo limeonekana kuwanufaisha zaidi mawakala na wafanyabiashara wakubwa wakulima wakiendelea kusumbuka.

Malim Seif amesema utafiti uliofanywa unaonyesha matajiri wamekuwa wakiwakandamiza wakulima wa mwani kutokana na bei ndogo wanayowalipa ikilinganishwa na faida wanayoipata.

Nae Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wenye viwanda  na Wakulima Zanzibar, Mbarouk Omar Mohamed, alishauri serikali kupunguza viwango vya kodi, za bidhaa zinazoingizwa kutoka nje.

Amesema Dubai imefikia maendeleo mazuri  ya kibiashara kutokana na mfumo wa ulipaji kodi nafuu, unaowawezesha wafanyabiashara kutoka nchi mbali mbali Duniani, ikiwemo Zanzibar kukimbilia huko.

Aidha Rais huyo aliitaka Serikali, kuitumia kiamilifu fursa ya uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarisha biashara ili kuinua uchumi na kukuza maendeleo ya Zanzibar.

Advertisements