Archive for August, 2011

WAFANYABIASHARA WA REJA REJA WAKAIDI AGIZO LA SMZ

Baadhi ya wafanyabiashara katika manispaa ya mji wa Zanzibar wamekaidi agizo la serikali ya Mapinduzi Zanzibar la kuwataka kuuza bei za bidhaa za vyakula kama ilivyotangazwa jana na wizara ya biashara.

Uchunguzi ulifanywa na mwandishi wa habari hizi katika maduka ya vyakula ya Darajani, Mwembeladu na maeneo mengine ya Ngambo umegundua bei ya mchele wa kawaida unauzwa kati ya shilingi 1,100 hadi 1,200 kwa kilo.

Bei mpya iliyotangazwa na serikali kilo moja ya mchele wa kawaida kwa maeneo ya mjini ni shilingi elfu moja na 60 na maeneo ya mashamba ni shilingi elfu moja na 70.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mfanyabiashara wa reje reja kutoka maeneo ya Kinuni wilaya ya magharibi ambae hakutaka kutajwa jina lake ameiomba serikali kufuatilia bei za mchele wanazouza wafanyabiashara wakubwa.

Amesema wafanyabiashara wadogo wananunua kipolo cha kilo 50 kwa shilingi elfu 50 na kutumia elfu moja gharama za usafiri hivyo haiwezekani kuuza bei ya mchele huo kama ilivyotangazwa na serikali.

 

‘’ Kama serikali imekutuma unichunguze mimi shilingi 20 haitumiki, hivyo hiyo bei ya shilingi 1,070 iliyotangazwa na serikali haiji, na siwezi kununua mchele shilingi 50, 000 nikauza kwa bei ile ile……wakati natumia shilingi 1,000 gharama za usafiri kutoka ghalani hadi dukani kwangu’’. Alisema mfanyabiashara huyo.

Hata hivyo bei ya sukari na unga wa ngano katika baadhi ya maeneo ya manispaa ya mji wa Zanzibar inauzwa kama ilivyotangazwa na serikali kati ya shilingi 1,620 na shilingi 1,670 kwa kilo.

Aidha bei ya unga wa ngano kwa jana (juzi) imeongezeka kwa shilingi 100 na kuuzwa shilingi 1,100 kutoka kutoka shilingi 1,000 kwa kilo kablaya kutangazwa bei mpya na serikali ya shilingi kati shilingi 1,050 na 1,060.

Bei ya sukari nayo pia imeongezeka katika baadhi ya maduka ya reja reja na kuuzwa hadi shilingi 1,700, wakati bei iliyotangazwa na serikali ni kati ya shilingi 1,060 kwa kilo.

Akitangaza bei hizo mpya kwa wandishi wa habari huko hoteli ya Bwawani Jumapili iliyopita waziri wa biashara, viwanda na masoko Nassor Ahmmed Mazuri amesema mfanya biashara yoyote atakaekwenda kinyume na bei hizo mpya atachukuliwa hatua za kisheria.

Amesema bei hizo zilizotangazwa zinafuatia makubaliano kati ya serikali na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa za vyakula nchini

ZANZIBAR HASHUDIA TENA IDDEL- FITR MBILI

Kamati ya kuandama kwa mwezi Zanzibar imewataka waislamu nchini kukamilisha siku 30 za mwezi mtukufu wa Ramadhan kutokana na juhudi za kamati hiyo kushindwa kuona na kupata taarifa za kuandama kwa mwezi hapo jana. Hata hivyo baadhi ya waislamu wa Zanzibar wanaofuata muandamo wa mwezi popote duniani leo watasherehekea siku kuu ya Edil-fitri baada ya kuwepo madai ya kuonekana kwa mwezi katika nchi za Dubai, Saud Arabia, Malasia na nchi za Amerika ya Kusini. Katibu wa afisi ya Musfti Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga amewatahadharisha waislamu wanaweza kula mchana wa mwezi mtukufu wa Ramadhan endapo watafuata mataifa mengine…

Aidha Soraga amewataka waislamu kufuata kauli za viongozi wa dini waliokuwepo nchini kupitia kamati ya kitaifa ya kuandama kwa mwezi ambayo iliwasiliana na waislamu wa Mombasa, Tanga na maeneo mengine na mwezi haukonekana.

SMZ KUTANGAZA BEI ELEKEZI YA MCHELE, SUKARI, UNGA WA NGANO

Nassor Ahmmed Mazurui

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza bei mpya ya bidhaa muhimu za vyakula za mchele, sukari na Unga wa ngano kwa wafanya biashara wakubwa na wa reja reja.

Akitangaza bei hizo mbele ya waandishi wa habari huko hoteli ya Bwawani waziri wa Biashara  Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui amesema bei hizo zimefikiwa kufuatia makubaliano kati ya serikali na wafanyabiashara.

Amesema bei ya mchele wa kawaida aina ya Red Rose, Supetr Rice, Super Falcon na mwengine unaofanana na huo, bei ya jumla ni shilingi elfu 50, 350 kwa polo la kilo 50 na bei ya reje reja ni shilingi 1,060 maeneo ya mjini na mashamba atauza elfu moja na 70 kwa kilo moja.

Kisiwani Pemba bei ya jumla ni shilingi 52,650 bei ya reja reja utauza kati ya shilingi 1,100 na 1,120.

 

Bei ya sukari Unguja muingizaji atauza  elfu 77,400, bei ya jumla elfu 78,400  kwa polo la kilo 50 na bei ya reja reja itauza shilingi 1,620 kwa maeneo ya mjini na bei ya mashamba ni shilingi 1,640 .

Kisiwani Pemba bei ya sukari muingizaji atauza shilingi 80, 680, bei ya  jumla ni shingili elfu 84,180 kwa polo la kilo 50 na  bei ya reja reja ni shilingi elfu 1, 680 kwa kilo moja.

Unga wa ngano Unguja muingizaji atauza kwa shilingi elfu 48, 560 bei ya jumla shilingi elfu   49, 560 kwa polo la kilo 50 na bei ya reja reja ni kati ya shilingi elfu 1, 050 na shilingi elfu 1, 060 kwa kilo moja.

Pemba unga wa ngano muingizaji atauza shilingi elfu 51, 855, bei ya jumla shilingi elfu 55, 355 kwa polo la kilo 50 na bei ya reja reja kati ya shilingi elfu 1, 90 na shilingi eflu 1, 110 kwa kilo moja .

Hata hivyo Mazrui alisema wafanya biahshara wanaweza kupunguza bei hiyo lakini hawataruhusiwa kuongeza bei zaidi iliyotangazwa na serikali

Kuhusu bei ya bidhaa zinazozalishwa na wananchi kama vile mchele wa Zanzibar naTanzania bara utauzwa kutokana na makubaliano kati ya wateja na wauzaji.

Aidha Waziri Mazrui ameawataka wafanya biahsra  kuweka bei hizo ambazo wanunuzi wataziona kwa  urahisi zaidi.

Bei hizo mpya zilizotangazwa na serikali ni makubaliano yaliofikiwa kati ya  serikali na wafanyibiashara  ambazo zitaanza kutumika rasmi kuanzia leo.

HIZBU UT-TAHARIRI AFRIKA MASHARIKI YALAANI UKANDAMIZAJI WA WAISLAMU PAKISTAN

Jumuiya ya Hizb ut-tahariri Afrika Mashariki imelaani vitendo vya dhulma na uonevu wanaofanyiwa wanachama na baadhi ya viongozi wandamizi wa Jumuiya hiyo nchini Pakistan.

Taarifa ya jumuiya hiyo iliyotumwa kwa ubalozi wa Pakistan mjini Dar es Salaam imesema ukamataji wa siri dhidi ya wanaharakati wa kislamu wanaolingania dini yao nchini humo unaofanywa na vyombo vya dola ni vitendo vya uonevu.

Taarifa ya jumuiya hiyo ambayo Zanzibar Islamic News  imepata nakala yake imetaja baadhi ya majina ya viongozi wandamizi wanaondelea kushikiliwa mafichoni ni Hayan Khan, Ousama Haif na Dr. Abdul Qayuum.

Hivyo Jumuiya hiyo imetoa wito kwa serikali ya Pakistan kuwacha vitendo vya dhuluma dhidi ya waislamu wanaolingania dini yao na kuwachia huru viongozi hao waliokamatwa bila ya hatia.

Taarifa hiyo ya Hizb ut Taharii Afrika mashariki ilitolewa na naibu mwakilishi wa jumuiya hiyo kwa vyombo vya habari aliepo Zanzibar Masoud Msellem.

UGONJWA WA SURUA WARIPUKA ZANZIBAR

Ugonjwa wa surua umeripuka kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika wilaya ya magharibi.

Mkurugenzi mkuu wa wizara ya afya Zanzibar Dr. Malik Abdalla Juma amesema watoto 14 wanaougua ugonjwa huo wamelazwa katika hospitali ya Mnazi mmoja na watoto wengine 62 wamepatiwa matibabu tangu kuripuka kwa ugonjwa huo mwanzoni mwa mwezi huu.

Ameyataja maeneo yaliokumbwa na ugonjwa huo ni Magogoni, Nyarugusu, Kinuni, Kimara, Chunga na Mwera wilaya ya magharibi.

Aidha amesema matukio machache ya maradhi hayo pia yamejitokeza katika maeneo ya Kiembesamaki, Chumbuni na Daraja bovu.

Juma amesema sababu za kuzuka kwa ugonjwa surua ni wazazi kutowapeleka watoto wao kupatiwa chanjo ya surua wanapofikia umri wa miezi sita, mwamko mdogo na kukosa taaluma ya maradhai hayo.

Dr. Malik amesema wizara ya afya imeanza kuchukua hatua ikiwemo kutoa taaluma, kuwapatia chanjo watoto wenye umri wa miezi sita hadi miaka mitano kuanzia tarehe 27 mwezi huu katika maeneo hayo

MAGENDO YA PEMBE ZA NDOVU YAPATIKANA ZANZIBAR

VIKOSI vya ulinzi katika bandari ya Zanzibar vimefanikiwa kukamata shehena ya pembe za ndovu zenye uzito ambao hadi sasa haujajulikana tayari zikisafirishwa kuelekea Malaysia.Vipande vya pembe 1041 viligundulika vikiwa katikati ya magunia yaliofungwa vizuri na kushindiliwa dagaa kavu kutoka mkoani Mwanza Tanzania bara, tayari likisafirishwa kuelekea Malaysia.

Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Ahmada Abdulla Khamis alisema vipande hivyo havijapimwa kujulikana uzito wake ambapo utaratibu unaandaliwa kuwapa wataalamu kufanyakazi hiyo.

Alisema upimaji unahitaji gharama wa kuzisafirisha kwenda Dar es Salaam, huku pia kukiwa na kizuizi cha upelelezi unaoendelea juu kadhia nzima ya utoroshwaji wa nyara hizo.

Kwa upende wake Mkuu wa Polisi katika bandari ya Zanzibar, Mrakibu wa Polisi Martin Lissu, alisema magunia ya dagaa hilo lilokuwa katika makontena mawili walilitilia mashaka na wakati wa ukaguzi wakilibaini ndani ya magunia hayo kuwemo vitu visivyo vya kawaida.

Alisema taarifa zilizopo ni kwamba magunia hayo yaliokuwa na pembe za ndovu yaliingia Zanzibar wiki mbili zilizopita yakitokea Dar es Salaam kwa meli ya MV Burak.

Mrakibu Lissu alisema baada ya kuingia Zanzibar mzigo huo moja kwa moja ulipelekwa katika makaazi ya wakala Ramadhan Makame huko Mwanakwerekwe mjini hapa.

“Tumefanya mahojiano ya awali na wakala wa mzigo huu bwana Makame ametueleza yeye ni wakala tu wa mizigo na alijua ndani ya magunia hayo kuna dagaa tu na si vipande vya pembe za ndovu”,alisema.

Alisema juzi ilikuwa ndiyo siku ya kusafirishwa ambapo kabla ya kuingizwa katika meli kwa safari ya Malysia waliyafanyia upekuzi makontena hayo baada ya kuyatilia mashaka, ambapo ndani yake katika baadhi ya makontena walikuta vipande vya pembe za ndovu zikiwa zimefungwa vizuri.

“Ni vugumu kukuelezeni wapi tumepata habari na kugundua kuwepo kwa pembe hizi, ila kwa ufupi ni suala la kiitelijensia la jeshi letu”,alisema Mrakibu huyo.

Alisema mbali ya kumshikilia wakala Ramadhan Makame, pia inamshikilia mkaazi wa Dar es Salaam, Ruben Msigano ambaye aliletwa Zanzibar kuja kusimamia na kuhakikisha kuwa mzigo huo unasafirishwa kuelekea nchini Malyasia.

Lissu alisema walipofanya mahojiano na Ruben alisema kilichomtela kuja kusimamia mzigo unasafrishwa na kazi hiyo alipewa na mkaazi mmoja wa Kariakoo jijini Dar es Salaam mwenye asili ya Mashariki ya mbali aitwae Mr. Lee.

“Mimi nimekuja kusimamia sikujua kama kuna pembe za ndovu, nimetumwa na Mr. Lee kuusafirisha”,alisema Ruben ambaye kwa sasa anashikiliwa jeshi la Polisi na wakala wa mzigo huo Ramadhna Makame.

Zanzibar Leo ambayo ilikuwepo kwenye zoezi hilo la kupekuliwa dagaa hilo ambapo ambapo 135 yaligunduliwa kuwa na vipande kati ya vinane hadi 11 vilivyofungwa vizuri na kuchomekwa katikati ya magunia hayo

WAISLAMU WACHENI MIGOGORO MISKITINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewanasihi waislamu kujiepusha na mivutano na ugomvi wa kugombania uongozi misikitini na badala yake waitumie kwa ibada na kuimarisha mapenzi baina yao.

Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kuufungua msikiti wa Mzuri Makunduchi ambao umejengwa upya na kuzidishwa ukubwa wake.

Katika maelezo yake Aljah Dk. Shein alisema kuwa mivutano hiyo ambayo huwa haipendezi wengi, husababishwa na ubinafsi na kwa kweli ni amali za kishetani na kwa vile misikiti ni nyumba ya MwenyeziMungu waumi watapaswa kuiheshimu.

Alieleza kuwa tarekh ya Kiislamu inafunza kuwa wakati wa Bwana Mtume (S.A.W) na Masahaba zake misikiti ilitumika kwa shughuli mbali mbali zikiwemo za kitaaluma, kusuluhisha migogoro, kupokelea wageni na hata kujuliana hali.

“Waislamu waliweza kubaini wenzao wanaoumwa kwa kuangalia mahudhurio yao katika vipindi vya sala, Waumini walipogundua hali hii walitenga muda kwenda kuwakagua waislamu wenzano na kuwaombea dua”,alisema Alhaj Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kwa hali kama hiyo misikiti iliimarisha mapenzi miongoni mwa waumini na hayo ndio mafunzo makubwa yanayopatikana na hakuna budi yafuatwe.

Alhaj Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na Kamati ya Msikiti huo kuwa inawaandaa vijana kwa ajili ya mafunzo ya kuwapata Maimam na Mkhatib watakaoshughulikia na kusaidia kwa ukaribu zaidi masuala ya msikiti huo na mengine.

Alisema kuwa hatuan hiyo bila shaka haitowanufaisha waumini kupata Maulamaa tu, bali pia, itawakuza imani vijana hao na kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuwaharibia maisha yao.

Dk. Shein alieleza kuwa kujengwa kwa msikiti huo ni neema kubwa hivyo waumini hao wanawajibu wa kumshukuru MwenyeziMungu kwa kuutumia msikiti huo hasa kwa sala na ibada nyenginezo ikiwemo kusoma Quran na darsa hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ambapo ibada za waja huwa na malipo makubwa.

Alhaj Dk. Shein alitoa pongezi kwa Waislamu ambao kila mmkoja alitaka awe mbele katika kufanikisha ujenzi wa msikiti huo kwa kutoa fedha, Aidha, alitoa shukurani kwa waislamu waliojihimu katika kuchangia nguvu zao.

Pia, Alhaja Dk. Shein alisisitiza haja ya kuutunza na kuuenzi msikiti huo na kuchukua fursa hiyo kuwakumbusha Waumini juu ya umuhimu wa kuzitumia vyema neema za Mwezi Mktukufu wa Ramadhani.

Dk. Shein aliwasisitiza Waumini kujitahidi kufanyiana ihsan, kuoneana huruma, kuzitumia neema alizotoa MwenmyeziMungu ili kuweza kwuasaidia wahitaji, kusoma Quran na kufanya bidii katika sala za Faradhi na Sunna.

Kwa upande wa Wafanyabiasahara, Alhaj Dk.Shein alisisitiza kuwa waadilifu, kufanya tahfifu katika bei na wasitawaliwe na tamaa.

“Tukifanya hivi ni dhahiri tutakuwa tumezivuna zile fadhila alizotuadidi Mwenyezi Mungu”,alisema Alhaj Dk. Shein.

Aidha, Alhaj Dk. Shein alitoa pongezi kwa wakulima wote walikiwemo wakulima wa Makunduzi kwa kujidhatiti na kulima kwa juhudi kiasi cha kupatikana chakula cha kutosha kwenye mwezi huu wa Ramadhan

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kuwapongeza wananchi wa Makunduchi kwa kuimarisha sekta ya kilimo na kutoa wito kuongeza juhudi katika kilimo kwani kilimo hutoa chakula cha kutosha na hakina mbadala.

Pamoja na hayo alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zazibar itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha tatizo la maji linapatiwa ufumbuzi katika Jimbo hilo la Makunduchi kwani tayari ameshaiagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ifanye jitihada ili maji ya uhakika yapatikane.

Nayo Kamati ya Msikiti huo katika risala yao walitoa shukurani kwa Alhaj Dk. Shein kwa kuufungua msikiti wao ambao hadi kumalizika umegharimu Shilingi milioni 85 za Kitanzania, ambao unakisiwa kusaliwa waumini wapatao 350 hadi 400.

Aidha, walieleza kuwa ujenzi wa msikiti huo alianza mwamzoni mwa huu ambapo kabla ya kutokea mfadhili Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Haroun Ali Suleiman alikuwa tayari amejitolea kuujenga msikiti huo.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika uzinduzi huo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri, Masheik, Maulamaa pamoja na viongozi wengine wa dini na serikali.