Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewanasihi waislamu kujiepusha na mivutano na ugomvi wa kugombania uongozi misikitini na badala yake waitumie kwa ibada na kuimarisha mapenzi baina yao.

Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kuufungua msikiti wa Mzuri Makunduchi ambao umejengwa upya na kuzidishwa ukubwa wake.

Katika maelezo yake Aljah Dk. Shein alisema kuwa mivutano hiyo ambayo huwa haipendezi wengi, husababishwa na ubinafsi na kwa kweli ni amali za kishetani na kwa vile misikiti ni nyumba ya MwenyeziMungu waumi watapaswa kuiheshimu.

Alieleza kuwa tarekh ya Kiislamu inafunza kuwa wakati wa Bwana Mtume (S.A.W) na Masahaba zake misikiti ilitumika kwa shughuli mbali mbali zikiwemo za kitaaluma, kusuluhisha migogoro, kupokelea wageni na hata kujuliana hali.

“Waislamu waliweza kubaini wenzao wanaoumwa kwa kuangalia mahudhurio yao katika vipindi vya sala, Waumini walipogundua hali hii walitenga muda kwenda kuwakagua waislamu wenzano na kuwaombea dua”,alisema Alhaj Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kwa hali kama hiyo misikiti iliimarisha mapenzi miongoni mwa waumini na hayo ndio mafunzo makubwa yanayopatikana na hakuna budi yafuatwe.

Alhaj Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na Kamati ya Msikiti huo kuwa inawaandaa vijana kwa ajili ya mafunzo ya kuwapata Maimam na Mkhatib watakaoshughulikia na kusaidia kwa ukaribu zaidi masuala ya msikiti huo na mengine.

Alisema kuwa hatuan hiyo bila shaka haitowanufaisha waumini kupata Maulamaa tu, bali pia, itawakuza imani vijana hao na kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuwaharibia maisha yao.

Dk. Shein alieleza kuwa kujengwa kwa msikiti huo ni neema kubwa hivyo waumini hao wanawajibu wa kumshukuru MwenyeziMungu kwa kuutumia msikiti huo hasa kwa sala na ibada nyenginezo ikiwemo kusoma Quran na darsa hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ambapo ibada za waja huwa na malipo makubwa.

Alhaj Dk. Shein alitoa pongezi kwa Waislamu ambao kila mmkoja alitaka awe mbele katika kufanikisha ujenzi wa msikiti huo kwa kutoa fedha, Aidha, alitoa shukurani kwa waislamu waliojihimu katika kuchangia nguvu zao.

Pia, Alhaja Dk. Shein alisisitiza haja ya kuutunza na kuuenzi msikiti huo na kuchukua fursa hiyo kuwakumbusha Waumini juu ya umuhimu wa kuzitumia vyema neema za Mwezi Mktukufu wa Ramadhani.

Dk. Shein aliwasisitiza Waumini kujitahidi kufanyiana ihsan, kuoneana huruma, kuzitumia neema alizotoa MwenmyeziMungu ili kuweza kwuasaidia wahitaji, kusoma Quran na kufanya bidii katika sala za Faradhi na Sunna.

Kwa upande wa Wafanyabiasahara, Alhaj Dk.Shein alisisitiza kuwa waadilifu, kufanya tahfifu katika bei na wasitawaliwe na tamaa.

“Tukifanya hivi ni dhahiri tutakuwa tumezivuna zile fadhila alizotuadidi Mwenyezi Mungu”,alisema Alhaj Dk. Shein.

Aidha, Alhaj Dk. Shein alitoa pongezi kwa wakulima wote walikiwemo wakulima wa Makunduzi kwa kujidhatiti na kulima kwa juhudi kiasi cha kupatikana chakula cha kutosha kwenye mwezi huu wa Ramadhan

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kuwapongeza wananchi wa Makunduchi kwa kuimarisha sekta ya kilimo na kutoa wito kuongeza juhudi katika kilimo kwani kilimo hutoa chakula cha kutosha na hakina mbadala.

Pamoja na hayo alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zazibar itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha tatizo la maji linapatiwa ufumbuzi katika Jimbo hilo la Makunduchi kwani tayari ameshaiagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ifanye jitihada ili maji ya uhakika yapatikane.

Nayo Kamati ya Msikiti huo katika risala yao walitoa shukurani kwa Alhaj Dk. Shein kwa kuufungua msikiti wao ambao hadi kumalizika umegharimu Shilingi milioni 85 za Kitanzania, ambao unakisiwa kusaliwa waumini wapatao 350 hadi 400.

Aidha, walieleza kuwa ujenzi wa msikiti huo alianza mwamzoni mwa huu ambapo kabla ya kutokea mfadhili Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Haroun Ali Suleiman alikuwa tayari amejitolea kuujenga msikiti huo.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika uzinduzi huo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri, Masheik, Maulamaa pamoja na viongozi wengine wa dini na serikali.

Advertisements