Eneo la rasi ya Nungwi

Baadhi ya mili ya watu waliozama kwenye meli ya abiria na mizigo ya Spice iliyokuwa ikitokea Unguja kwenda Pemba imeanza kuletwa nchi kavu katika bandari ya Nungwi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye eneo la tukio vikosi vya ukozi vya KMKM pamoja na vyombo vingine vya wananchi vinaendelea na shughuli za ukozi.

Akizungumza na vyombo vya habari naibu waziri wa miundo mbinu na mawasiliano Issa Haji Gavu amesema vyombo vya uokozi vimeondoka bandari ya Malindi kuelekea katika eneo la tukio.

Gavu amesema msiba huo ni wa kitaifa na kuwataka wananchi kuendelea kuvuta subra na serikali itatoa taarifa rasmi juu ya maafa hayo.

Hata hivyo idadi ya watu waliokuwemo ndani ya meli hiyo na walionusurika bado haijafahamika, lakini baadhi ya viongozi wa serikali waliozungumza na vyombo vya habari wamesema watu kadhaa wamefariki dunia.

Meli hiyo ya Spice imezama usiku wa manane katika mkondo wa Nungwi na chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika.

Wananchi wa Tanzania wameingiwa na simazi kutokana na kuguswa na msiba huo

        Taarifa za hivi karibuni zinasema meli hiyo inaendelea kukokowata na maji na mawimbi ya bahari ikielekea katika mkoa wa Tanga

NEW  NEW  NEW

Meli ya LCT  SPICE ISLANDERS imebiruka na kuzama katika Bahari ya Hindi katika Pwani ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ikielekea Pemba.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi amesema tukio hilo limetokea saa 8:30 za usiku ambapo meli hiyo ilikuwa imebeba abiria 610 pamoja na mizigo.

Naibu Waziri huyo amesema meli hiyo imeondoka katika Bandari ya Malindi Unguja ikiwa katika hali ya uzima,lakini katikati ya safari ikapata hitilafu na kusababisha kubiruka na hatimaye kuzama.

Hadi sasa haijaweza kufahamika idadi kamili ya watu waliofariki,lakini vyombo vya uokozi vimefika katika eneo la tukio kutoa msaada.

Naibu Waziri Issa amesema Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usafiri  vya binafsi boti ziendazo kasi zimekwenda eneo la tukio kutoa msaada unahitajika.Jeshi la Polisi Tanzania imetuma  Helkopta yake kwenye eneo la tukio.

Awali, amesema Mamlaka zinazohusika zilipata taarifa za kuzama kwa meli hiyo baada ya Meli ya Mv Jitihada inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuripoti kuzama kwa meli ya Spice Islanders ambayo ililazimika kukatisha safari yake kuelekea Kisiwani Pemba na kwenda kwenye tukio.

Serikali imesema taarifa zaidi zitakuwa zikitolewa na wananchi wameombwa kuwa watulivu.

 

TAARIFA YA RAIS WA ZANZIBAR KUHUSU AJALI YA MELI

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein ametoa salamu za rambi rambi kwa ndugu na jamaa kufuatia ajali ya meli ya Spice Islander na kusababisha watu kadhaa kufariki dunia.

Akizungumza katika eneo la kupokelea majeruhi na maiti wa ajali hiyo huko Nungwi amesema msiba huo ni mkubwa na umegusa taifa na wananchi wote wa Zanzibar.

Hivyo amewataka ndugu, jamaa na wananchi kwa ujumla kuwa na moyo wa subra katika kipindi hiki cha msiba.

Dr. Shein amesema serikali imeandaa utaratibu wa kuwahudumia waliokufikwa na maafa hayo na wale waliopoteza maisha, serikali itafanikisha mazishi yao.

Hata hivyo Dr. Shein amewapongeza wananchi wa kijiji cha Nungwi waliochukua hatua za awali za kuokoa maisha ya watu.

Aidha Dr. Shein amevitaka vyombo vya habari kutoa habari zenye usahihi ili kuwasaidia wananchi kupata taarifa za maafa hayo kwa usahihi.

Taarifa za hivi karibuni meli hiyo iliyokuwa na zaidi ya watu 610 hadi sasa watu 260 wameokolewa wakiwa hai.

Advertisements