Jumla ya tani 789 za karafuu zimenunuliwa hadi kufikia jana zenye thamani ya Shs billion 11 million 631 laki nane sabiini na saba elfu mia mbili na hamsini.

 

Ununuzi huo ni kuanzia kipindi cha Mwezi wa Julai hadi hapo jana ambapo karafuu zote hizo zimeuzwa katika Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) katika vituo mbali mbali kisiwani Pemba.

 

Akitoa taarifa leo mbele ya Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Fedha Biashara na Kilimo Zanzibar huko katika ofisi ya ZSTC Wete Pemba Afisa Mdhamini wa Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar Hemed Suleiman Abdallah, amesema kuwa ununuzi huo umetokana na mashirikiano yaliyopo kati ya wakulima na ZSTC.

 

Akielezea mchanganuo wa ununuzi wa karafuu hizo amesema kuwa kwa Mkoa wa Kusini Pemba Wilaya ya Mkoani imenunua Tani 402 sawa na shs Bilion 5.9, Wilaya ya Chake Chake Tani 184 sawa na shs Bilion 2 na Milion 72.

 

Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Wilaya ya Wete imenunua Tani 155 sawa na Bilion 2 na Milion 31 na Wilaya ya Micheweni Tani 45 sawa na Milion 68 Sitini na tisa elfu, elfu mbili mia tisa na sabiini na tano.

 

Amesema kuwa wananchi wa Pemba wametambua athari ya magendo ya Karafuu hivyo wamehamasika kuuza karafuu zao katika vituo vya ununuzi vya ZSTC kwa kutambua umuhimu wa kupeleka zao hilo huko kwa faida ya maendeleo ya Zanzibar.

 

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Fedha, Biashara na Kilimo, Salmin Awadh Salmin amelipongeza Shirika la ZSTC kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kufanikisha ununuzi wa tani hizo tokea kuanza msimu wa ununuzi wa karafuu mwezi Julai mwaka huu.

 

Amesema kuwa ZSTC imepiga hatua kubwa kwa kusimamia upatikanaji wa Tani hizo kwani imeonesha tofauti kubwa ya ununuzi wa karafuu hizo ikilinganishwa na msimu uliopita.

 

Salmin Awadh Salmin amewataka ZSTC kuwahamasisha wananchi kupanda Mikarafuu mipya na kuzidisha kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha karafuu zao wanazozipeleka ZSTC zipo katika hali nzuri ili waweze kupata daraja la kwanza kwa faida zaidi.

 

Wajumbe hao walitembelea ofisi kuu ya ZSTC iliyopo Wete, Banda la Karafuu la Wete vituo vya ununuzi wa karafuu vya Mzambarauni na kituo cha ununuzi cha Wete kisiwani Pemba.

 

Advertisements