Archive for November, 2011

WANANE WAHUKUMIWA KUNYONGWA KWA MAUWAJI YA ALBINO

Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda, amesema watu wanane wamehukumiwa kunyongwa kwa kutekeleza mauaji dhidi ya malbino kwa sababu za kishirikina.

Pinda amesema mauaji hayo dhidi ya maalbino yanayofanyika kwa sababu za kishirikina, yamepaka matope Tanzania sio tu kieneo, bali kimataifa.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania imesema watu 94 wamekamatwa hadi kufikia sasa kwa tuhuma za kuua maalbino, tangu wimbi la mauaji dhidi ya watu hao miaka minne iliyopita.

Taarifa kutoka ofisi ya Mizengo Pinda imeongeza kwa sasa kuna kesi 11 za mauaji ya maalbino zinaendelea kusikilizwa katika mahakama za nchi hiyo.

Zaidi ya maalbino 60 wameuawa tangu wimbi la mauaji ya maalbino liripuke nchini Tanzania mwaka 2007.

Ingawa sheria ya Tanzania inaruhusu adhabu ya kunyongwa wahalifu wenye kupatikana na hatia ya kuua au uhaini, lakini nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika haijawahi kutekeleza adhabu hiyo tokea muongo wa 1980

Advertisements

TUNATAKA KURA YA MAONI KUHUSU MUUNGANO KABLA YA KUANDIKWA KATIBA MPYA

Baadhi ya wananchi walioshiriki mjadala wa katiba mpya ya jamhuri ya muungano Tanzania wamesema Zanzibar hahitaji katiba hiyo bila ya kuulizwa kama wanataka muungano au la kupitia kura ya maoni.

Wananchi hao wamesema hayo katika mkutano wa kutoa ufafanuzi juu ya kupitishwa mswada wa sheria wa kuunda tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuandikwa katiba mpya huko Kikwajuni.

Wamesema Zanzibar imepokonywa nafasi nyingi ikiwemo wadhifa wa urais wa Zanzibar kuwa makamo wa kwanza wa rais wa jamhuri ya muungano Tanzania pamoja na raslimali zake kuingizwa kwenye orodha ya mambo ya muungano

Nao washiriki wengine wa mkutano huo wamesema pamoja na kuundwa katiba mpya lakini wananchi hawajafahamu umuhimu wao wa kutoa maoni,  hivyo wameiomba serikali kutoa elimu hasa vijijini.

Nae waziri wa katiba na sheria Abubakar Khamis Bakar amesema mswada huo umezingatia maslahi ya Zanzibar na kuwataka wananchi wajitokeze kutoa maoni yao wakati unapowadia.

Amefahamisha kuwa katiba mpya itakayoandikwa upitishaji wake unahitaji thuluthi mbili kwa wajumbe wa Zanzibar na idadi kama hiyo kwa wajumbe wa Tanzania bara watakaounda bunge la katiba.

Hivyo amewataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao hasa kero wanazozilalamikia ndani ya muungano ikiwemo mafuta na gesi asilia

Mswada huo wa kuunda tume ya kukusanya maoni pamoja na mambo mengine umepitishwa na bunge hivi karibuni na unatarajiwa kutia saini na rais Jakaya Kikwete ili uweze kuwa sheria kamili.

CHADEMA KUZUNGUMZA NA KIKWETE JUU YA KATIBA MPYA

Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kimeunda kamati ndodgo inayotarajiwa kukutana na rais Jakaya Kikwete kuelezea msimamo wao juu undwaji wa katiba mpya.

Mwenyekiti wa chama hicho Freman Mbowe ametangaza kuundwa kwa kamati hiyo kwa wandishi wa habari mjini Dar es Salaam.

Amesema kamati hiyo ndogo imeundwa kufuatia kikao cha kamati hiyo itafanya mazungumzo na rais Kikwte juu ya mswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba mpya

Tayari mwenyekiti huyo wa CHADEMA amekwisha kutana na spika wa bunge la jamhuri ya muungano Tanzania Anna Makinda mjini Dodoma.

EU, MAREKANI WAFUATILIA UNDWAJI WA KATIBA MPYA TANZANIA

Mvutano kati ya Serikali ya Tanzania na kambi ya upinzani kuhusu kuandika katiba mpya ya nchi hiyo umesababisha nchi wahisani kutuma maafisa wao mjini Dodoma kuchunguza kiini cha mvutano huo.

Habari zinasema maafisa kutoka balozi za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya wamekutana na Spika wa bunge la Tanzania Anna Makinda pamoja na baadhi ya wabunge wa upinzani kwa ajili ya mahojiano.

Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zilihusika kwa sehemu kubwa katika undaaji wa katiba mpya nchini Kenya mwaka uliopita

Wakati huo huo

Wabunge wa upinzani kutoka chama cha NCC-MAGEUZI wametangaza kuandika katiba yao mpya na kuisambaza ili ipigiwe kura na wananchi.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wabunge hao wamesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuona mswada wa sheria juu ya katiba mpya unaweza kupitishwa na bunge na kuwa sheria.

Mwenyekiti wa wabunge wa NCC-MAGEUZI David Kafulila amedai baada ya wabunge wa CCM bungeni kukataa kusikiliza kilio cha watanzania kuhusu mswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza chama hicho kitatengeneza katiba mpya

Wabunge hao wa NCC-MAGEUZI wanaungana na wabunge wa CHADEMA waliotoka nje ya bunge wakati muswada wa sheria kuhusu kuanzishwa katiba mpya kusomwa kwa mara ya pili.

MFANYAKAZI WA SMZ AKUTWA NA MAGENDO YA KARAFUU PEMBA

Jumla ya Magunia 24 ya Karafuu yamekamatwa na Kamati ya Ulinzi ya Wilaya ya Wete ndani ya Nyumba ya Mfanyakazi Mmoja wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar huko Kiungoni Wilaya ya Wete Pemba.

 

Karafuu ambazo zimekamatwa baadhi yake zilionekana zimefichwa katika Choo nyumbani kwa Mfanyakazi huyo ambaye inadaiwa kuwa ni Mfanyakazi wa Wizara ya Afya.

 

Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Wete kufuatia kukamatwa kwa Karafuu hizo Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Karafuu Zanzibar Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa amesema kuwa Serikali haitosita kumchukulia hatua za kisheria Mfanyakazi yoyote wa Serikali atakayebainika na kuhusika na magendo ya Karafuu.

 

Amesema kuwa kitendo cha kuhifadhi karafuu ndani ya nyumba hakikubaliki hivyo kila mwananchi anatakiwa kuitikia wito wa Serikali wa kuziuza karafuu zake katika vituo vya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

 

Meja Tindwa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba amesema kuwa wafanyakazi wa Serikali wanatakiwa kuwa mfano bora kwa jamii katika kuwahimiza wananchi kuuza karafuu zao ZSTC.

 

Mapema akitoa maelezo mbele ya kamati hiyo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Wete Pemba Juma Saad amesema kuwa Jeshi hilo litaendelea na Operesheni yake ili kuliokoa zao la Karafuu ambalo ni Uti wa mgongo wa Uchumi wa Zanzibar.

 

Aidha Saad amewataka wananchi kuzidi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wanaohifadhi Karafuu zao ndani ya Nyumba zao kwa lengo la kufanya Magendo.

 

HOSPITALI YA RAS AL KHAIMAH KUSAIDIA UPASUWAJI WA FIGO, MOYO, SARATANI ZANZIBAR

Dr. Shein akizungumza na mwenyeji wake Sheikh Saud bin Saqr Al Kassim kiongozi wa Ras Al- Khaimah wakati alipowasili katika kasri ya kiongozi huyo, mjini Ras al-Khaimah

HOSPITALI Kuu ya Rufaa ya Ras Al Khaimah imeahidi ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na azma ya kusaini makubaliano ya kushirikiana katika kutoa huduma za upasuaji kwa maradhi ya figo, moyo na saratani.

 
Ahadi hiyo imetolewa na uongozi wa Hospitali ya RAK wakati wa ziara ya Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, alitembelea hospitali hiyo.
Dk.  Mkuu wa Upasuaji katika hospitali hiyo Dk. J. M. Gauer alimueleza Dk Shein kuwa Hospital ya RAK iko tayari kusaini Mkataba wa Makubaliano juu ya ushiikiano kati yake na Zanzibar.
Katika makubaliano hayo Zanzibar itaweza kufaidika katika utoaji huduma ya afya ikiwa ni pamoja na upasuaji wa maradhi mbali mbali.
Miongoni mwa maradhi hayo ni pamoja na maradhi ya figo, moyo, saratani pamoja na maradhi mengineyo.
Nae Rais Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa uwamuzi huo wa Hospitali ya RAK na kueleza kuwa hatua za haraka zitachukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Alisema kuwa Zanzibar inatarajia kutuma ujumbe mzito hivi karibun kwa ajili ya kukaa pamoja na uonozi huo na kusaini makubaliano hayo kwa pamoja ili kuweza kuanza kutoa huduma hizo kwa haraka.
Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua hatua za makusudi katika kuhakikisha mchakato wa kuazisha vituo vya utoaji wa huduma hiyo katika hospitali zake kuu ikiwemo hospitali ya MnaziMmoja.
Alieleza kuwa kufikiwa kwa lengo hilo kutaweza kupanua utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa Hospitali hiyo ya RAK kushirikiana pamoja na Zanibar katika kuendeleza programu kwa pamoja ili kuweza kuimarisha huduma za afya Zanzibar.
Wakati huo huo Kiongozi Mkuu wa Ras Al Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi ameelezaa azma yake ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika uhifadhi wa nyaraka hasa zile zilizoanza kuharibika.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuzifanyia utaratibu wa kitaalamu nyaraka kwa kuweza kuzihifadhi ili zisiweze kutoweka.
Katika hatua hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ras-Al-Khaimah zitaweza kushirikiana pamoja na kusaidia uhifadhi wa nyaraka pamoja na kuziendeleza.
Alieleza kuwa hivi karibuni atatuma wataalamu kuja kuangalia namna ya kuanza mchakato huo huo huko Zanzibar.
Aidha, Ras Al Khaimah imeeleza kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuendelea kutoa nafasi za masomo hasa ya Sayansi ya Afya ambapo tayari imeshatoa nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar ambao hivi sasa wanasoma Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya kilichopo Ras Al Khaimah.
Dk. Shein amemaliza ziara yake Ras-Al Khaimah na leo anaendelea na ziara yake Sharja ambako mbali ya kutembelea sehemu mbali mbali pamoja na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya wafanyabiashara, wenyeviwanda na wawekezaji.
Dk. Shein pia, atakutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Sharja Sheikh Sultan Mohamed Al Qasimi.
Katika ziara yake hiyo Dk. Shein amefuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein, Mawaziri na watedaji wengine wa serikali ambapo miongoni mwa viongozi hao ni  Waziri wa Kazi Uwezesaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mhe. Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazurui.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Mahadhi Juma Maalim,Mshauri wa Rais wa Zanzibar Uhusiano wa Kimataifa na Uwezeshaji Mhe. Balozi Mohammed Ramia na watendaji wengine wa serikali

INDONESIA KUISAIDIA ZANZIBAR MELI ZA ABIRIA NA MIZIGO

Indonesia imeahidi kulifanyia kazi mara moja ombi la Zanzibar la mpango wake wa kuimarisha huduma za usafiri wa kudumu wa  meli kubwa  za abiria na mizigo kati ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Ahadi hiyo imetolewa na Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka   Indonesia Unaoongozwa na Waziri wa Nchi anayesimamia Wizara za Biashara na Viwanda na ile ya Maendeleo ya Taifa  ya Nchi hiyo Bw. Lee Shyan wakati ulipokutana kwa mazungumzo  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Ujumbe huo umesema juhudi za haraka zitaanzishwa kwa kuwasiliana na Makampuni ya Meli Huko Japan ili kuona utekelezaji ya ombi hilo unafanikiwa katika kipindi kifupi kijacho.

Waziri wa Nchi anayesimamia Wizara ya Biashara ya Indonesia  Bw. Lee Shyan alimueleza Balozi Seif kwamba Ujumbe wake umekuja Zanzibar kuangalia maeneo ambayo wanaweza wakashirikiana na Zanzibar katika kuwekeza Vitega Uchumi.

“ Naimani kwamba yapo maeneo mengi hasa katika sekta za  Biashara, Kilimo na Mtandao wa Mawasiliano ambayo tunaweza kuwekeza au kuingia katika ubia ”. Alisema Bwana Lee Shyan.

Bwana Lee alifahamisha kwamba miradi ya pamoja kati ya pande hizo mbili inaweza kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo na kustawisha jamii za sehemu hizo.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuambia Ujumbe huo kwamba Zanzibar hivi sasa iko katika Mipango ya kukabiliana na Tatizo la Usafiri wa Baharini Kati ya Unguja na Pemba.

Balozi Seif alisema Uanzishwaji wa mradi wa usafiri kati ya Visiwa Hivi mbali ya kutoa ajira pia utatoa kiwango kikubwa cha mapato kwa vile jamii ya Visiwa hivi inategemea sana meli kulingana na mazingira yao ya kimaisha.

“ Wananchi wengi hasa wafanyabiashara ndogo ndogo wa Zanzibar hutegemea zaidi usafifi wa Meli katika kuendesha Biashara zao zinazozunguuka ndani ya mwambao wa Afrika Mashariki ”. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Indonesia kuingia katika soko la Zanzibar kwenye maeneo ya viwanda vya samaki, Utalii na hata kwa kubadilishana Utaalamu katika masuala ya Biashara ili kustawisha kizazi cha sasa.

Alisema Zanzibar imekuwa na mawasiliano ya Kibiashara ya muda mrefu kati yake  na Mataifa mengi ya Barala Asia.