Maalim Seif akizungumza na Balozi Alfonso Lenhadrt wa Marekani Movenpick hoteli. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Marekani imeahidi kuisaidia Zanzibar vifaa vya uokozi wa baharini kwa nia ya kuiwezesha kufanikisha mipango yake ya kuweka na kukabiliana na majnga yanapotokea.

Ahadi hiyo imetolewa jana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad yaliyofanyika hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam.

Balozi Alfonso alisema nchi yake inaona kuna haja ya kusaidia vifaa vya uokozi kama vile boti na redio kwa kufanikisha mawasiliano na kufika kwa wakati katika maeneo ya matukio na hatua hiyo itaiwezesha Zanzibar kujiandaa kuepuka maafa ya baharini.

Alisema Marekani imefurahishwa sana na mshikamano na uwezo wa hali ya juu uliooneshwa na serikali pamoja na wananchi wa Zanzibar, baada ya tukio la kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders Septemba 10 mwaka huu na kuwezesha idadi kubwa ya abiria kuokolewa

Balozi Lenhardt alieleza kuwa licha ya kuwepo uhaba wa vifaa na wataalamu wa masuala ya uokozi Wazanzibarui pamoja na raia wa kigeni waliokuwepo baada ya tukio hilo walishikamana na kufanya kazi ya kupigiwa mfano.

“Mshikamano wa wananchi wa Zanzibar, wakati ule wa maafa ya meli ni wa kupigiwa mfano, kwakweli umetuvutia sana na hali hii inaonesha kwamba Serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar inafanikiwa vizuri kuleta umoja”, alisema Balozi Lenhardt.

Alisema nchi yake imeona itakuwa imetoa mchango mkubwa katika suala hilo iwapo itasaidia boti za uokozi na redio za mawasiliano na Zanzibar itaweza kujijengea uwezo wa kiuokozi katika siku zijazo.

Naye, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad alisema uamuzi huo wa Marekani ni muafaka kwasababu Zanzibar inahitaji sana vifaa vya uokozi pamoja na kutoa taaluma kwa wananchi, wakiwemo wavuvi wadogo wadogo.

“Msaada kama huo unahitajika sana kwa Zanzibar na nimefurahi sana kusikia ahadi hii, wananchi wetu walitumia uzoefu na juhudi kubwa kuokoa maisha ya watu baada ya maafa yale”, alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.

Maalim Seif alisema iwapo kungekuwa na vifaa vya kisasa na elimu ya kutosha ya masuala ya uokozi, kazi nzuri zaidi ingeweza kufanywa na idadi ya watu wengi zaidi wangeokolewa.

Akizungumzia mradi wa umeme upitia chini ya bahari hadi Zanzibar unaofadhiliwa na Marekani, Balozi huyo alisema hivi sasa kazi ya uzalishaji waya inaendelea vizuri, baada ya kusita kufuatia kampuni ya ujenzi kutoka Japan inayofanya kazi hiyo kusitisha kufuatia maafa yaliyotokea Japan mwezi Machi mwaka huu.

Alieleza kwamba kuna matumaini makubwa mradi huo utakuwa umekamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao, ambapo utaongeza kiwango cha upatikanaji huduma ya umeme Zanzibar.

 

Advertisements