From Habari Leo Newspaper

MBUNGE wa Mbarali, Modestus Kilufi (CCM) amehukumiwa kifungo cha miezi 10 jela au kulipa faini ya Sh 500,000 baada ya kupatikana na hatia ya kutishia kuua kwa maneno.

Mbunge huyo (51) alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 10 akidaiwa kutishia kwa maneno kumuua Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruiwa, Mbarali, Jordan Masweve.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, Michael Mteite, alisema ameridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Epimack Mabrouk na Griffin Mwakapeje. Upande wa utetezi uliongozwa na Wakili Edson Mbogoro.

Alieleza kuwa, mshitakiwa kwa makusudi alitenda kosa hilo Machi 16 eneo la Rujewa, Mbarali.

Alisema, mshitakiwa alitamka kuwa atamtoa roho mlalamikaji, huku akimtukana pumbavu asipofuta kesi ndani ya wiki moja, ambayo ilifunguliwa dhidi ya Mbunge huyo mwaka 2009 katika Mahakama ya Wilaya ya Mbarali.

“Kutokana na maelezo hayo na ushahidi ulioletwa mahakamani, ninakuhukumu kifungo cha miezi 10 jela au kulipa faini ya Sh 500,000,” alisema Hakimu Mteite.Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili wa upande wa mashitaka walimwomba Hakimu Mteite kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Kupitia Wakili wake, Mbunge aliomba Mahakama impunguzie adhabu, kwani ana watoto watano kati yao wawili wanasoma Chuo Kikuu na wananchi wanamtegemea kuwasilisha matatizo yao bungeni.

Baada ya kusomewa hukumu, Mbunge huyo alilipa Sh 500,000 na kuachiwa huru.

Advertisements