Dr. Shein akizungumza na mwenyeji wake Sheikh Saud bin Saqr Al Kassim kiongozi wa Ras Al- Khaimah wakati alipowasili katika kasri ya kiongozi huyo, mjini Ras al-Khaimah

HOSPITALI Kuu ya Rufaa ya Ras Al Khaimah imeahidi ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na azma ya kusaini makubaliano ya kushirikiana katika kutoa huduma za upasuaji kwa maradhi ya figo, moyo na saratani.

 
Ahadi hiyo imetolewa na uongozi wa Hospitali ya RAK wakati wa ziara ya Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, alitembelea hospitali hiyo.
Dk.  Mkuu wa Upasuaji katika hospitali hiyo Dk. J. M. Gauer alimueleza Dk Shein kuwa Hospital ya RAK iko tayari kusaini Mkataba wa Makubaliano juu ya ushiikiano kati yake na Zanzibar.
Katika makubaliano hayo Zanzibar itaweza kufaidika katika utoaji huduma ya afya ikiwa ni pamoja na upasuaji wa maradhi mbali mbali.
Miongoni mwa maradhi hayo ni pamoja na maradhi ya figo, moyo, saratani pamoja na maradhi mengineyo.
Nae Rais Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa uwamuzi huo wa Hospitali ya RAK na kueleza kuwa hatua za haraka zitachukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Alisema kuwa Zanzibar inatarajia kutuma ujumbe mzito hivi karibun kwa ajili ya kukaa pamoja na uonozi huo na kusaini makubaliano hayo kwa pamoja ili kuweza kuanza kutoa huduma hizo kwa haraka.
Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua hatua za makusudi katika kuhakikisha mchakato wa kuazisha vituo vya utoaji wa huduma hiyo katika hospitali zake kuu ikiwemo hospitali ya MnaziMmoja.
Alieleza kuwa kufikiwa kwa lengo hilo kutaweza kupanua utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa Hospitali hiyo ya RAK kushirikiana pamoja na Zanibar katika kuendeleza programu kwa pamoja ili kuweza kuimarisha huduma za afya Zanzibar.
Wakati huo huo Kiongozi Mkuu wa Ras Al Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi ameelezaa azma yake ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika uhifadhi wa nyaraka hasa zile zilizoanza kuharibika.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuzifanyia utaratibu wa kitaalamu nyaraka kwa kuweza kuzihifadhi ili zisiweze kutoweka.
Katika hatua hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ras-Al-Khaimah zitaweza kushirikiana pamoja na kusaidia uhifadhi wa nyaraka pamoja na kuziendeleza.
Alieleza kuwa hivi karibuni atatuma wataalamu kuja kuangalia namna ya kuanza mchakato huo huo huko Zanzibar.
Aidha, Ras Al Khaimah imeeleza kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuendelea kutoa nafasi za masomo hasa ya Sayansi ya Afya ambapo tayari imeshatoa nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar ambao hivi sasa wanasoma Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya kilichopo Ras Al Khaimah.
Dk. Shein amemaliza ziara yake Ras-Al Khaimah na leo anaendelea na ziara yake Sharja ambako mbali ya kutembelea sehemu mbali mbali pamoja na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya wafanyabiashara, wenyeviwanda na wawekezaji.
Dk. Shein pia, atakutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Sharja Sheikh Sultan Mohamed Al Qasimi.
Katika ziara yake hiyo Dk. Shein amefuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein, Mawaziri na watedaji wengine wa serikali ambapo miongoni mwa viongozi hao ni  Waziri wa Kazi Uwezesaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mhe. Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazurui.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Mahadhi Juma Maalim,Mshauri wa Rais wa Zanzibar Uhusiano wa Kimataifa na Uwezeshaji Mhe. Balozi Mohammed Ramia na watendaji wengine wa serikali

Advertisements