Jumla ya Magunia 24 ya Karafuu yamekamatwa na Kamati ya Ulinzi ya Wilaya ya Wete ndani ya Nyumba ya Mfanyakazi Mmoja wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar huko Kiungoni Wilaya ya Wete Pemba.

 

Karafuu ambazo zimekamatwa baadhi yake zilionekana zimefichwa katika Choo nyumbani kwa Mfanyakazi huyo ambaye inadaiwa kuwa ni Mfanyakazi wa Wizara ya Afya.

 

Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Wete kufuatia kukamatwa kwa Karafuu hizo Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Karafuu Zanzibar Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa amesema kuwa Serikali haitosita kumchukulia hatua za kisheria Mfanyakazi yoyote wa Serikali atakayebainika na kuhusika na magendo ya Karafuu.

 

Amesema kuwa kitendo cha kuhifadhi karafuu ndani ya nyumba hakikubaliki hivyo kila mwananchi anatakiwa kuitikia wito wa Serikali wa kuziuza karafuu zake katika vituo vya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

 

Meja Tindwa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba amesema kuwa wafanyakazi wa Serikali wanatakiwa kuwa mfano bora kwa jamii katika kuwahimiza wananchi kuuza karafuu zao ZSTC.

 

Mapema akitoa maelezo mbele ya kamati hiyo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Wete Pemba Juma Saad amesema kuwa Jeshi hilo litaendelea na Operesheni yake ili kuliokoa zao la Karafuu ambalo ni Uti wa mgongo wa Uchumi wa Zanzibar.

 

Aidha Saad amewataka wananchi kuzidi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wanaohifadhi Karafuu zao ndani ya Nyumba zao kwa lengo la kufanya Magendo.

 

Advertisements