Baadhi ya wananchi walioshiriki mjadala wa katiba mpya ya jamhuri ya muungano Tanzania wamesema Zanzibar hahitaji katiba hiyo bila ya kuulizwa kama wanataka muungano au la kupitia kura ya maoni.

Wananchi hao wamesema hayo katika mkutano wa kutoa ufafanuzi juu ya kupitishwa mswada wa sheria wa kuunda tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuandikwa katiba mpya huko Kikwajuni.

Wamesema Zanzibar imepokonywa nafasi nyingi ikiwemo wadhifa wa urais wa Zanzibar kuwa makamo wa kwanza wa rais wa jamhuri ya muungano Tanzania pamoja na raslimali zake kuingizwa kwenye orodha ya mambo ya muungano

Nao washiriki wengine wa mkutano huo wamesema pamoja na kuundwa katiba mpya lakini wananchi hawajafahamu umuhimu wao wa kutoa maoni,  hivyo wameiomba serikali kutoa elimu hasa vijijini.

Nae waziri wa katiba na sheria Abubakar Khamis Bakar amesema mswada huo umezingatia maslahi ya Zanzibar na kuwataka wananchi wajitokeze kutoa maoni yao wakati unapowadia.

Amefahamisha kuwa katiba mpya itakayoandikwa upitishaji wake unahitaji thuluthi mbili kwa wajumbe wa Zanzibar na idadi kama hiyo kwa wajumbe wa Tanzania bara watakaounda bunge la katiba.

Hivyo amewataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao hasa kero wanazozilalamikia ndani ya muungano ikiwemo mafuta na gesi asilia

Mswada huo wa kuunda tume ya kukusanya maoni pamoja na mambo mengine umepitishwa na bunge hivi karibuni na unatarajiwa kutia saini na rais Jakaya Kikwete ili uweze kuwa sheria kamili.

Advertisements