Archive for December, 2011

DR. KARUME ATUNUKIWA NISHANI YA USHUJAA

rais-mstaafu-dr-karume-akipokea-nishani-ya-shujaa-wa-zanzibar-kutoka-kwa-mzee-hassan-moyo

Kituo cha Sanaa za Maonesho za Waswahili (Swahili Performing Arts Center) Zanzibar kimemtunukia Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dr. Amani Karume, nishani ya ‘Shujaa wa Zanzibar’ ikiwa ni hatua ya mwisho katika kuadhimisha kufikiwa kwa maridhiano na hatimaye serikali ya umoja wa kitaifa nchini Zanzibar.

Dr. Karume alikabidhiwa nishani hiyo na mwanasiasa mkongwe Mzee Hassan Nassor Moyo  siku ya Ijumaa tarehe 23 Desemba 2011 katika hafla fupi iliyofanyika nyumbani kwake huko Mbweni nje kidogo ya Mji Mkongwe.

Akiwasilisha risala yake katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Performing Arts Center Kheri Jumbe alitoa shukrani kwa Dr. Karume kutokana na jitihada zake katika kuleta amani ya kudumu nchini Zanzibar.

Jumbe alieleza kuwa, taasisi yake iliona umuhimu wa kuandaa sherehe za maridhiano kupitia mradi wa sanaa uliopewa utambulisho wa 100%  Zanzibari (Mzanzibari asilimia moja) ili kuwaenzi waasisi wa maridhiano hayo na kueliimisha wananchi juu ya umuhimu wake.

“Kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia Oktoba 4 hadi Desemba 3, tumekwenda katika mikoa yote ya Zanzibar na kuwasilisha ujumbe juu ya umuhimu wa kuimarisha misingi ya umoja na kuweka mbele uzalendo, ‘ alisema Jumbe.

Akikabidhi nishani hiyo kwa Rais mstaafu, Mzee Hassan Nassor Moyo alirejea wasia wake wakutaka viongozi wakuu wa Zanzibar kutowavumulia watendaji wa serikali wanaovuruga maridhiano.

Katika kuipokea nishani hiyo, Dr. Karume aliwapongeza watendaji wa Swahili Center pamoja na wasanii walioshirki katika mradi huo kwa juhudi zao katika kuyaendeleza maridhiano kupitia sanaa zilizobeba ujumbe huo.

Nishani kama hiyo ya ‘shujaa wa Zanzibar’ alitunukiwa pia Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad katika kilele cha sherehe za maridhiano huko uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba tarehe 3 Desemba 2011.

Wengine waliohudhuria katika uwasilishwaji wa nishani hiyo kwa Dr. Karume ni Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Mhe Ismail Jussa pamoja na Mkurugenzi wa Sanaa was Swahili Center, Mahsin Basalama.

Kupitia mradi wa 100% Zanzibari wasanii 130 kutoka vikundi 11 vya sanaa za maonesho walishiriki katika kambi za kjenga umoja na kufanya maonesho nchini kote.

Mradi wa 100% Zanzibari umedhaminiwa na Ubalozi wa Norway pamoja na kampuni ya mawasiliano ya Zantel

 

Advertisements

PINGENI MAFUTA KUINGIZWA KWENYE MUUNGANO-HAMAD

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi wa Chama hicho na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya demokrasia kibandamaiti mjini Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF  Maalim Seif Sharif Hamad amezungumzia tena baadhi ya mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kutoa maoni ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwataka viongozi na wananchi kuungana katika kutetea maslahi ya Zanzibar  ndani ya Muungano.

Amesema iwapo Wazanzibari wataungana na kuwa na sauti moja juu ya jambo hilo, kauli yao itakuwa na nguvu na upande wa pili wa Muungano utalazimika kuheshimu maamuzi hayo ya wazanzibari.

“Viongozi na wananchi wote tushikamane na tuweni na kauli moja juu ya jambo hili, na kamwe tusikubali kugawanywa kwa maslahi ya nchi yetu”, alisema Maalim Seif.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo katika viwanja vya demokrasia Kibandamaiti mjini Zanzibar wakati akiwahutubia maelfu ya wanachama na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliotishwa na CUF.

Amebainisha baadhi ya mambo  yanayopaswa kuzingatiwa na kuingizwa katika katiba mpya kuwa ni haja ya Zanzibar kuwa na benki kuu yake ikiwa ni nia moja wapo ya kudhibiti uchumi wake.      

Mambo mengine ni pamoja na  Zanzibar kuweza kuwa na sauti huru juu ya sera zake za fedha na uchumi ikizingatiwa kuwa suala la uchumi si katika mambo ya Muungano,sambamba na serikali kuendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka suala la mafuta liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano. 

Maalim Seif amefahamisha kuwa Zanzibar inastahiki pia kuwa na uwezo wa kuweka viwango vyake vya kodi, pamoja na kuwa na mitaala yake ya elimu inayoendana na mazingira ya Zanzibar kwa maslahi ya Wazanzibari.

Wiki iliyopita Maalim Seif alielezea umuhimu wa kuwepo utaratibu maalum wa kikatiba utakaoruhusu nafasi ya Urais wa Muungano kutumikiwa kwa awamu kati ya Tanzania bara na Zanzibar, tofauti na utaratibu uliopo sasa ambao hautoi fursa kwa Wazanzibari kuitumikia nafasi hiyo kubwa kabisa ya uongozi nchini.

Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na baadhi ya wananchi hasa wa mkoa wa Dar es Salaam kupoteza maisha yao, hali iliyosababishwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa.

Amesema mwisho mwa mwezi huu chama chake kimepanga kuzitembelea kambi wanazoishi watu walioathirika na kupoteza makaazi kutokana na mafuriko hayo kwa lengo la kutoa pole na mchango wake kwa waathirika hao.

Wakati huo huo Naibu Katibu mkuu wa CUF Zanzibar Mheshimiwa Ismail Jussa Ladhu amewataka wanachama wa chama hicho kupuuza uvumi juu ya mgogoro ndani ya Chama hicho, na kwamba chama hakina mgogoro na kiko imara wala hakitumbi.

Amesema uvumi huo unaosambazwa kupitia vyombo vya habari umekuwa ukitolewa kwa malengo maalum ya kukivuruga chama, malengo ambayo amesema hayatofanikiwa.

Nae mkurugenzi wa haki za binadamu, habari na mawasiliano ya umma wa chama hicho Bwana Salim Bimani amesema bado serikali ya Muungano haijatoa fursa zinazostahiki kwa Zanzibar katika masuala ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuinyima nafasi za kibalozi nchi za nje.

Hassan Hamad (OMKR).

SUZA MAMBO MAZURI- DR SHEIN

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, DK. ALI MOHAMED SHEIN AMBAYE PIA NI MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR KATIKA MAHAFALI YA SABA, TAREHE 24 DISEMBA 2011 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Salmin Amour; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mheshimiwa Ramadhan Abdulla Shaaban; Waheshimiwa Mawaziri; Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi; Waheshimiwa Wabunge; Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; Ndugu Wageni waalikwa; Ndugu Wahadhiri na Wana Chuo, Mabibi na mabwana. Assalaam Aleykum. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima, furaha, afya njema na kuweza kujumuika pamoja hapa leo hii. Leo ni siku nyengine muhimu inayoingia katika historia yetu kwa jumla, na hasa katika historia ya elimu ndani ya visiwa vyetu vya Zanzibar. Safari yetu iliyoanzia mwaka 2001 ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, tayari imetimiza miaka kumi; kwa mnasaba huo , napenda kuipongeza jamii ya wanachuo pamoja na wananchi wote wa Zanzibar. Hongereni sana. Kuhudhuria kwenu kwa wingi kwenye sherehe hizi ni dalili ya kutosha ya mapenzi mliyonayo kwa chuo hiki. Pia, inathibitisha imani yenu kuwa vyuo vikuu ni taasisi muhimu katika maendeleo ya nchi yo yote ikiwemo nchi yetu ya Zanzibar. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi, Ni faraja kubwa kwetu sote kwamba Serikali yenu inatambua ukweli huo na ndio sababu moja kubwa ya kuanzishwa chuo hiki ambacho leo kinatimiza miaka 10. Kwa niaba yenu nyote, nachukuwa fursa hii kutoa shukurani kwa viongozi wetu wawili ambao juhudi zao ndizo zimefanikisha kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Viongozi hao ni Rais Mstaafu Dk. Salmin Amour Juma na Rais Mstaafu na Mkuu wa Kwanza wa Chuo Kikuu hiki, Dk. Amani Abeid Karume. Wao ndio waanzilishi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Ninafakhari kwa niaba ya chuo, leo hii katika mahafali haya ya saba nimewatunukia Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa. Nawapongeza kwa heshima hiyo ambayo ni kielelezo sahihi cha juhudi zao. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Wakati Chuo chetu cha Taifa kinatimiza miaka kumi tangu kuanzishwa kwake, ni muda mzuri wa kuyatafakari baadhi ya mambo. Jambo la kwanza ni kuelewa kwamba miaka kumi ni muda mdogo tu kwa maisha ya chuo kikuu, ikizingatiwa kwamba kuna vyuo vilivyoanzishwa karne nyingi zilizopita katika Bara la Afrika. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Al Azhar kiliopo Cairo – Misri, kina zaidi ya miaka elfu moja. Vile vile, kiliwahi kuwepo Chuo Kikuu cha Timbuktu, Mali, Afrika Magharibi, ambacho wakati wa uhai wake kiliwahi kuwa na wanafunzi 25,000 wa Sayansi, Hisabati na Dini kwa wakati mmoja. Chuo hicho kilikuwa na mfumo wa aina ya peke yake wa shahada zake. Kwa upande wetu, kama utaratibu wa maumbile ulivyo, hesabu huanzia moja na ndio ikafikia mia na kuendelea. Makamu Mkuu wa Chuo ameshatueleza historia ya chuo pamoja na taarifa ya wahitimu watakaopatiwa shahada na tunzo zao leo hii. Nampongeza kwa maelezo hayo. Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo naye ametuelezea baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo. Kwa mfano, ipo misaada mbali mbali inayotolewa kwa vyuo vikuu mbali mbali lakini, haifiki huku kwetu. Namshukuru kwa kutubainishia hayo na naahidi Serikali itafanya kila juhudi katika kushughulikia jambo hilo ipasavyo. Itakumbukwa kuwa katika hotuba yangu, niliyoitoa wakati nilipotawazwa kuwa Mkuu wa Chuo hiki tarehe 29 Machi mwaka huu, nilieleza dhamira yangu ya kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010/2015 ya kuendeleza pamoja na kuimarisha fursa za elimu ya juu Zanzibar. Miongoni mwa hatua za mwanzo tulizochukua ni kuusimamia ujenzi wa Kampasi mpya huko Tunguu ulioanzishwa na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita. Tarehe 5 mwezi huu nilikagua kazi ya ujenzi unaoendelea pamoja na kulitembelea eneo lililotengewa kwa ajili ya Kampasi hiyo na nimefurahishwa na yote niliyoyaona pamoja na maendeleo mazuri ya kazi hiyo. Napenda kukuthibitishieni wananchi wa Zanzibar kwamba Serikali imejidhatiti na imesimama kidete katika kukijenga chuo hiki na Inshaallah Mwenyezi Mungu atatusaidia tufanikiwe. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu wananchi. Katika kuizingatia tathmini ya miaka kumi ya chuo chetu, hatuna budi kuzingatia kukua kwa idadi ya taaluma zinazotolewa hapa. Tulianza kwa kutoa fani chache, ikiwemo ya Elimu kwa ajili ya walimu wa sekondari. Ninafuraha kuwa dhamira yetu ya kuwa na walimu waliofuzu katika kiwango cha shahaha imeanza kufikiwa na katika kipindi kifupi kijacho walimu wetu wote wa skuli za sekondari watakuwa na Shahada ya Chuo Kikuu. Leo hii, tutatoa Shahada ya Sanaa na Elimu kwa wahitimu 139 na Shahada ya Sayansi na Elimu kwa wahitimu 63. Hao wote watakuwa ni walimu wetu wa skuli za sekondari hivi karibuni. Haya ni maendeleo ya kupigiwa mfano. Kama nilivyosema siku ile ya tarehe 29 Machi mwaka huu; kwamba karne hii tunayoishi ni karne ya Sayansi na Teknolojia ya kisasa. Kwa upande mmoja ninafuraha kuwa tumeanza kutoa wataalamu wa Fani ya Teknohoma (IT). Makamu Mkuu wa Chuo amekwishatueleza juu ya mipango ya kuanzisha vitivo vipya ambavyo vitatilia mkazo mafunzo ya Sayansi. Kwa upande wangu napenda kukuhakikishieni wanachuo nyote kwamba tutaendelea kushirikiana ili kuhakikisha chuo chetu kinatoa fani nyenginezo kama vile utalii, kilimo na udaktari. Katika tathmini yetu leo, tunapaswa pia kuangalia mchango wa chuo chetu katika maendeleo ya nchi yetu. Tunashukuru kuwa tunaendelea kupata walimu wanaohitajika kutoka kwenye Chuo Kikuu hiki, ambao tunawategemea sana na ambao watatoa mchango wao katika kupunguza tatizo la ajira na kupunguza umasikini. Benki ya Dunia imezitaka nchi za Afrika kukuza upatikanaji wa elimu ya juu, ili iwe ndio ngazi ya kuondoa umasikini. Makamu Rais wa Benki ya Dunia kwa Afrika, Obiageli Ezekwesili, hivi karibuni aliuambia mkutano wa siku mbili wa elimu ya juu katika Afrika, katika Chuo Kikuu cha Ghana, Legou kuwa: “Ni muhimu kwa vyuo vikuu kutilia mkazo ubora wa elimu unaokidhi mahitaji ya kisasa ya uchumi uliojaa ushindani.” Wito huu umetolewa kwetu kwa hivyo ni wajibu wetu tujipange vyema na tuhakikishe kwamba matunda ya vyuo vikuu vyetu ni kuchangia maendeleo ya nchi zetu. Wazo la Vyuo Vikuu vya Maendeleo (Development Universities) si geni kwa sababu lilibuniwa na wataalamu katika miaka ya sabiini na wataalamu kama Profesa Manuel Castells aliandika kuwa “Mfumo wa Elimu ya Juu uwe ni Injini ya Maendeleo katika Uchumi wa Ulimwengu Mpya.” Mtazamo huu wa kitaalamu ukitekelezwa ipasavyo, kwa hakika vyuo vikuu vyetu vitaweza kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya nchi yetu na wananchi wake. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Kutokana na haya yote, napenda kukumbusha kwamba matarajio yetu ni kuwa hapo baadae katika chuo chetu kikuu hiki, tuwe na Vitivyo vya Uhandisi, Biashara, Taasisi ya Utafiti na Taasisi ya Sayansi za Bahari. Vitivo hivi pamoja na vyenginevyo vilivyopo sasa, vitatusaidia katika kukidhi mahitaji ya nchi yetu katika kupeleka mbele maendeleo. Hili ni jukumu kubwa kwenu wanajamii na wanachuo kwa jumla, lakini nina imani nanyi kwamba mtalimudu. Naahidi tena kwamba Serikali yenu siku zote itakuwa tayari kutoa msaada kila inapowezekana. Tumeanza kwa kujenga majengo mapya, kupanua chuo, kuongeza wahadhiri na kuangalia maslahi yenu nyote kwa jumla. Nitaendelea kufanya kila jitihada katika kushajiisha na kutilia nguvu ushirikiano utakaoleta tija kwa chuo chetu kwa njia ya mahusiano na vyuo vikuu vya nchi za nje. Aidha, tutaendelea kujitahidi kadri tunavyoweza kuwasaidia wanafunzi wetu ili wawe na mazingira bora ya kujifunzia ikiwemo suala la kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar itatengewa fedha zaidi katika bajeti zijazo za Serikali kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu. Hata hivyo, napenda ifahamike kwamba idadi ya wanafunzi wanaofaulu na kupata sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, ndani na nje ya nchi inaongezeka kila mwaka na ni dhahiri kuwa hii ni changamoto kubwa kwetu sote. Natoa wito kwa wale wazazi wanaojimudu pamoja na sekta binafsi, kwa jumla waunge mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha watoto wetu kupata elimu ya juu. Ili kuleta kasi ya maendeleo katika nchi yetu, hapana budi kila mmoja wetu ajitume kwa kiasi kinachowezekana na kufanya kazi kwa bidii zaidi. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Walimu na Wahadhiri wa vyuo vikuu vyetu, nawanasihi, kuongeza bidii kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kielimu nchini ili matokeo yake yaendeleze nchi yetu kwa haraka. Katika kutekeleza jambo hilo natilia mkazo tena suala la kufanya utafiti, kwani kufanikiwa kwetu kupitia tafiti kutaongeza kiwango cha maendeleo katika chuo chetu pamoja na kutupatia sifa nzuri. Pamoja na tafiti hizo, nashauri kwamba Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni katika chuo chetu ikuzwe ili iwe mashuhuri kwa lugha hiyo duniani kama Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, kilivyo mashuhuri kwa lugha ya Kiingereza. Naamini suala hilo linawezekana na historia ya lugha hiyo nchini kwetu, itasaidia kufanikisha utekelezaji wa lengo la kukifanya chuo chetu kuwa mashuhuri katika ufundishaji wa Kiswahili duniani kote. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Sasa nataka nizungumzie suala la wahitimu. Leo hii ndugu wahitimu mmetunukiwa Shahada, Stashahada na Vyeti baada ya kuhitimu mafunzo yenu. Jambo la msingi kwenu ni kushirikiana na wananchi wenzenu katika kupambana na changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii na nchi yetu kwa jumla na kuzipatia ufumbuzi. Aidha, ninakukumbusheni umuhimu wa kushirikiana na wananchi wenzenu katika kuijenga nchi yetu. Nashauri mtumie elimu yenu mliyoipata kwa kuongeza tija katika ajira zenu na zaidi muweze kujiajiri nyinyi wenyewe kwa kila inapowezekana. Wahitimu wa Vyuo Vikuu ni watu wenye upeo mkubwa na ubunifu na ni vyema mkashirikiana katika kujitafutia ajira za kukufaeni nyinyi na nchi yetu kwa jumla. Sambamba na hilo, nakukumbusheni kuwa “elimu haina mwisho”. Ngazi mliyokwishaifikia ni mwanzo tu wa safari ndefu ya kutafuta elimu. Wasia wangu kwenu ni kuzidi kuendelea zaidi kuitafuta elimu ya Shahada za juu zaidi. Nchi yetu inahitaji wataalamu wenye elimu ya kutosha na ya juu, kwa kuwa nyinyi tayari mmeshapata msingi wa kwendea huko, nakushaurini muitumie fursa hiyo vilivyo. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Kwa mara nyengine, nakushukuruni nyote kwa kuitikia wito na kwa mahudhurio yenu makubwa. Namalizia kwa kukuombeeni afya njema na moyo wa kuendelea kuitumikia nchi yenu huku mkiamini kuwa “mtu kwao” na muungwana ni Yule anaeitumikia jamii iliyompa elimu na kumlea kwa bidii na juhudi zake zote. Nakutakieni kila kheri katika mwaka mpya wa 2012. Ahsanteni kwa kunisikiliza.

MAFURIKO DAR ES WALIOKUFA WAFIKIA 41

Idadi ya watu waliofariki katika mafuriko yaliyokumba mji mkuu wa Tanzania Dar es Salam imefikia 41 leo huku mvua kubwa ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa karibu nusu karne ikinyesha nchini humo. Zaidi ya watu elfu tano wameachwa bila makao na serikali inatenga ardhi ya kujenga makaazi ya muda ili kuwapa hifadhi waathiriwa. Kumekuwa na lawama kuwa licha ya onyo la mapema kutoka kwa mamlaka ya hali ya hewa nchini humo, hatua muafaka hazikuchukuliwa ili kuzuia vifo na uharibifu wa mali. Barabara na madaraja kadhaa nchini humo yamesombwa na mvua huku afisi za umoja wa mataifa mjini Dare es salama pia zikiathiriwa na mafuriko hayo. Mvua zaidi inatarajiwa na serikali imewaonya raia waliohamishwa kutoka maeneo yaliyoathirika  ya nyanda za chini kutorejea kwa sasa ili kuepusha maafa zaidi

ICHANGIENI REDIO IMAN

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewahimiza Waislamu nchini kote kujitokeza kwa wingi kuchangia uanzishwaji wa televisheni Imani, kwasababu televisheni hiyo itatoa mchango mkubwa kufuta dhana potofu dhidi ya Uislamu, na kutoa taaluma ya maadili mema ndani ya jamii.

Alisema hayo jana alipokuwa akihutubia kwenye hafla ya kuchangia uanzishwaji wa televisheni hiyo, inayoanzishwa chini ya Jumuiya ya Islamic Foundation, ambayo pia inaendesha Redio Imani iliyopo mkoani Morogoro.

Maalim Seif alisema vituo vingi vya televisheni hapa nchini mara nyingi huonesha vipindi vinavyokwenda kinyume na maadili mema ya jamii, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia kuharibu maadili ya jamii na zaidi vijana na watoto wadogo.

Makamu wa Kwanza wa Rais alisema mbali ya kujenga maadili mema kituo hicho cha televisheni pia kitaweza kufanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wanajamii, juu ya mazuri na mchango wa Uislamu na kufuta dhana inayoenezwa na baadhi ya watu, dhana ambazo zinapotosha na kuipaka matope dini ya Kiislamu.

“Waislamu jitokezeni mchangia mambo ya Kheri, kuanzishwa kwa televisheni hii ni jambo la Kheri, wafanyakazi serikalini, Mashirika ya Umma na taasisi binafsi changieni, na wala msione haya kujuilikana nyinyi ni Waislamu, Uislamu ndio didni sahihi” alisisitiza Maalim Seif.

Alieleza kuwa wapo waislamu wenye uwezo mkubwa na nafasi ya kuchangia mambo kama hayo yenye faida kwao na Waislamu wote, lakini kuna wengi miongoni mwao , licha ya kuwa na uwezo huo wamekuwa wagumu kutoa, na badala yake kujikita zaidi katika kuchangia mambo ya anasa.

Katika hafla hiyo, Waislamu mbali mbali walijitokeza kuchangia ambapo, Makamu wa Kwanza wa Rais alichangia shilingi milioni mbili kwa ajili ya uanzishwaji wa kituo hicho cha televisheni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh Ali Basaleh alisema vyombo vingi vya habari nchini, vikiwemo vituo vya televisheni havina tabia ya kutangaza mambo mema yanayogusa Uislamu na Waislamu, na badala yake vyombo hivyo vimekuwa vikijikita zaidi kuripoti mambo mabaya dhidi ya Uislamu na kuyapa umuhimu mkubwa.

Basaleh alieleza kwamba televisheni hiyo ya Kiislamu ikianza matangazo yake itasaidia kutangaza na kutoa taaluma juu ya mambo ya Uislamu, ikiwemo kufuta dhana hizo potofu zinazoupaka matope Uislamu.   

Mkurugenzi wa Islamic Foundation, Sheikh Arif Nahad alisema Waislamu wakiamua wanaweza, kwasababu hivi sasa wameamka baada ya miaka mingi ya kujiweka nyuma na kufunga mikono katika shughuli za kimaendeleo.

 Sheikh Nahad alieleza kuwa hakuna sababu televisheni hiyo ishindwe kuanza, na kwa kuwa jumuiya yake imeahidi itatekeleza hilo na kuwaahidi mamia ya watu waliohudhuria kuwa televisheni hiyo ipo njiani inakuja.

WANAOISHI NA UKIMWI WAPATA MAFANIKIO

JUMUIYA YA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI ZANZIBAR ZAPHA PLUS IMEELEZEA MAFANIKIO WALIYOYAFIKIA KATIKA KUPUNGUZA TATIZO LA UNYANYAPAA KWA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI. AKIZUNGUMZA KATIKA MKUTANO WA UHAMASISHAJI WANANCHI KUACHANA NA UNYANYAPAA HUKO DONGE AFISA MIPANGO WA JUMUIYA HIYO BW MASOUD HAMAD NASSOR AMESEMA WAMEWEZA KUPUNGUZA TATIZO LA UNYANYAPAA KWA KIASI KIKUBWA KATIKA VISIWA VYA ZANZIBAR LAKINI JUHUDI ZAIDI ZINAHITAJIKA ILI KUTOKOMEZA KABISA TATIZO HILO. AMEFAHAMISHA KUWA WAMEAMUA KUFANYA MKUTANO HUO ILI KUONA HAKI ZA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI ZINAPATIKANA KATIKA NGAZI YA FAMILIA NA JAMII KWA PAMOJA ILI KUWEZA KUEPUSHA MAAMBUKIZO ZAIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI. NAO WANAKIJIJI WA DONGE WAMESEMA WANAUME WAMEKUWA NA TABIA YA KUWANYANYASA WANAWAKE NA WATOTO PINDIPO WATAGUNDULIKA NA VIRUSI VYA UKIMWI HIVYO KUSABABISHA ASILIMIA KUBWA YA WATOTO WA MITAANI. AIDHA WAMEIOMBA JUMUIYA HIYO KUTOA ELIMU YA KUTOSHA KWA JAMII ILI KUEPUSHA MATATIZO MENGI YANAYOTOKANA NA UKIMWI IKIWA NI PAMOJA NA UNYANYAPAA NA WATOTO WA MITAANI.

WAKULIMA WA KARAFUU PEMBA KUINGIZA BILIONI 50

Malim Seif akizungumza na baadhi ya watendaji wa ZSTC Pemba

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema wakulima wa karafuu kisiwani Pemba wanatarajiwa kutia mifukoni kiasi cha shilingii bilioni 50 hadi mwishoni mwa msimu wa zao hilo mapema mwakani, na kuwahimiza fedha hizo zitumike kwa maendeleo na wajiepushe na tabia ya kuzitumia kwa kuongeza wake bila sababu za msingi. Maalim Seif alisema mafanikio hayo kwa wakulima wa karafuu wa Zanzibar ni matokeo ya utekelezaji ahadi za serikali za kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora, wakiwemo wakulima, wafanyakazi na wavuvi, ambao ndio wanaochukua asilimia kubwa ya wananchi wa Unguja na Pemba. Alisema serikali ya awamu ya saba iliazimia kupandisha bei ya mazao mbali mbali, ikiwemo la karafuu kwa nia ya kumuona mkulima ananufaika na mazao yake kwa asilimia 80, ambapo hivi sasa wakulima wa karafuu wanauza karafuu zao kilo moja daraja la kwanza kwa shilingi 15,000 kutoka shilingi 5000 msimu uliopita. Alisema hayo leo wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi wa kisiwa kidogo cha Kojani, mkoa wa Kaskazini Pemba akiwa katika ziara ya siku nne kisiwani Pemba. Makamu wa Kwanza wa Rais alisema bei nzuri ya karafuu ni neema kubwa kwa wakulima kwasababu huko nyuma wakulima walikuwa hawapati hata asilimia 30 ya mapato yatokanayo na mazao yao, lakini hivi sasa baada ya serikali kuona umuhimu wa mkulima kunufaika na imeweza kupandisha bei katika kiwango kwenye maslahi. “Mkulima wa karafuu sasa anapata asilimia 80 ya mazao yake, tunatarajia hadi mwishoni mwa msimu huu wa karafuu bilioni 50 zitakuwa zimeingia Pemba, zitumie fedha hizo kwa mambo ya maendeleo, na sio kuoa wake wengi zaidi bila ya sababu za msingi”, alisema Maalim Seif. Alisema baada ya mafanikio kuanza kupatikana katika zao la karafuu, serikali inaelekeza nguvu kubwa katika zao la mwani, ambalo hadi sasa wanunuzi wanawalipa wakulima kwa bei ya chini, ambayo hailingani na kazi wanayoifanya pamoja na kulihudumia hadi kufikia hatua ya kuwauzia wafanyabiashara hao. Akipokuwa katika ziara katika kisiwa kidogo cha Tumbatu, wiki mbili zilizopita, Makamu wa Kwanza wa Rais alisema serikali itaendeleza mazungumzo na wanunuzi wa zao la mwani kuwataka wapandishe bei angalau ifike shilingi 1000, lakini iwapo watakataa, serikali itafikiria zao la mwani linunuliwe na serikali kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), kama inavyofanya kwa zao la karafuu. Akielezea mafanikio mengine ya serikali hii ya awamu ya saba yenye mfumo wa umoja wa kitaifa alisema ni kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 25, kiwango ambacho ni kikubwa na kwamba ni nchi chache zinazoweza kuongeza mshahara katika kiwango kama hicho kwa mara moja. Maalim Seif alisema nyongeza hiyo ya mshahara inakwenda sambamba na kulipwa wafanyakazi ambao kwa muda mrefu walikuwa hawajapewa nyongeza zao, ambapo pia mafao ya kada muhimu kama vile madaktari yameongezwa, ili kwends sambamba na majukumu mazito wanayoyakabili, lakini pia walingane na wenzao wa Tanzania Bara. Alisema baada ya hatua hiyo ya kuzingatiwa mafao ya madaktari hakuna sababu hivi sasa wakahamie sehemu nyengine kama vile Tanzania Bara kwasababu maslahi ambayo wangeweza kuyapata huko wanalipwa hapa hapa Zanzibar. Akizungumzia sekta ya uvuvi, Maalim Seif alisema matumaini makubwa ya mafanikio yameanza kujengeka kufuatia juhudi zinazoendelea kuchukuliwa kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo, ambao wataweza kuwanufaisha wavuvu wadogo wadogo wa Unguja na Pemba. Aliwaleza wananchi wa Kojani ambao asilimia kubwa ni wavuvu kuwa, baadhi ya wawekezaji wa sekta hiyo tayari wameonesha nia ya kuja kufungua viwanda vya kusindika samaki, kutengeneza boti za kisasa kwa ajili ya wavuvi wadogo wadogo wa Zanzibar pamoja na kuleta meli kwa ajili ya shughuli za uvuvi wa bahari kuu, ambapo wavuvi wa Zanzibar ndio walengwa wakuu wa ajira katika meli hizo. Huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa hadhara, Maalim Seif alisema mbali na wawekezaji katika sekta ya uvuvi kuonesha dhamira za kuja kufungua miradi Zanzibar, juhudi nyengine zilizokwisha chukuliwa na serikali ni kuwapeleka wavuvi kutoka vikundi mbali mbali vya Zanzibar nchini China kujifunza mbinu za kufuga samaki na baadaye wao wawafundishe wananchi wengine. Hata hivyo, alionya kwamba juhudi hizo zitakuwa na mafanikio makubwa iwapo wananchi wa Zanzibar watatoa kipaumbele katika kuyalinda na kuyahifadhi mazingira ya bahari kwa kujiepusha na aina zote za uvuvi haramu na uharibifu wa matumbawe ambayo ndiyo mazalia ya samaki na kuepuka kukata miti ya mikoko. Maalim Seif alisema kwamba siri kubwa ya mafanikio yaliyoanza kujitokeza Zanzibara ni kuendelea kudumisha amani na utulivu tokea kufikiwa maridhiano ya kisasa na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo hivi sasa imetimiza mwaka mmoja na kuhimiza wananchi wote kuhakikisha umoja na mshikamano huo unalindwa, ili kuleta mafanikio zaidi. Akizungumzia mipango ya CUF akiwa kama Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif alisema lengo la chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2015 ni kushinda nafasi ya Urais wa Zanzibar na kutoa Makamu wa Pili wa Rais.