HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, DK. ALI MOHAMED SHEIN AMBAYE PIA NI MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR KATIKA MAHAFALI YA SABA, TAREHE 24 DISEMBA 2011 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Salmin Amour; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mheshimiwa Ramadhan Abdulla Shaaban; Waheshimiwa Mawaziri; Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi; Waheshimiwa Wabunge; Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; Ndugu Wageni waalikwa; Ndugu Wahadhiri na Wana Chuo, Mabibi na mabwana. Assalaam Aleykum. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima, furaha, afya njema na kuweza kujumuika pamoja hapa leo hii. Leo ni siku nyengine muhimu inayoingia katika historia yetu kwa jumla, na hasa katika historia ya elimu ndani ya visiwa vyetu vya Zanzibar. Safari yetu iliyoanzia mwaka 2001 ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, tayari imetimiza miaka kumi; kwa mnasaba huo , napenda kuipongeza jamii ya wanachuo pamoja na wananchi wote wa Zanzibar. Hongereni sana. Kuhudhuria kwenu kwa wingi kwenye sherehe hizi ni dalili ya kutosha ya mapenzi mliyonayo kwa chuo hiki. Pia, inathibitisha imani yenu kuwa vyuo vikuu ni taasisi muhimu katika maendeleo ya nchi yo yote ikiwemo nchi yetu ya Zanzibar. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi, Ni faraja kubwa kwetu sote kwamba Serikali yenu inatambua ukweli huo na ndio sababu moja kubwa ya kuanzishwa chuo hiki ambacho leo kinatimiza miaka 10. Kwa niaba yenu nyote, nachukuwa fursa hii kutoa shukurani kwa viongozi wetu wawili ambao juhudi zao ndizo zimefanikisha kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Viongozi hao ni Rais Mstaafu Dk. Salmin Amour Juma na Rais Mstaafu na Mkuu wa Kwanza wa Chuo Kikuu hiki, Dk. Amani Abeid Karume. Wao ndio waanzilishi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Ninafakhari kwa niaba ya chuo, leo hii katika mahafali haya ya saba nimewatunukia Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa. Nawapongeza kwa heshima hiyo ambayo ni kielelezo sahihi cha juhudi zao. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Wakati Chuo chetu cha Taifa kinatimiza miaka kumi tangu kuanzishwa kwake, ni muda mzuri wa kuyatafakari baadhi ya mambo. Jambo la kwanza ni kuelewa kwamba miaka kumi ni muda mdogo tu kwa maisha ya chuo kikuu, ikizingatiwa kwamba kuna vyuo vilivyoanzishwa karne nyingi zilizopita katika Bara la Afrika. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Al Azhar kiliopo Cairo – Misri, kina zaidi ya miaka elfu moja. Vile vile, kiliwahi kuwepo Chuo Kikuu cha Timbuktu, Mali, Afrika Magharibi, ambacho wakati wa uhai wake kiliwahi kuwa na wanafunzi 25,000 wa Sayansi, Hisabati na Dini kwa wakati mmoja. Chuo hicho kilikuwa na mfumo wa aina ya peke yake wa shahada zake. Kwa upande wetu, kama utaratibu wa maumbile ulivyo, hesabu huanzia moja na ndio ikafikia mia na kuendelea. Makamu Mkuu wa Chuo ameshatueleza historia ya chuo pamoja na taarifa ya wahitimu watakaopatiwa shahada na tunzo zao leo hii. Nampongeza kwa maelezo hayo. Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo naye ametuelezea baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo. Kwa mfano, ipo misaada mbali mbali inayotolewa kwa vyuo vikuu mbali mbali lakini, haifiki huku kwetu. Namshukuru kwa kutubainishia hayo na naahidi Serikali itafanya kila juhudi katika kushughulikia jambo hilo ipasavyo. Itakumbukwa kuwa katika hotuba yangu, niliyoitoa wakati nilipotawazwa kuwa Mkuu wa Chuo hiki tarehe 29 Machi mwaka huu, nilieleza dhamira yangu ya kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010/2015 ya kuendeleza pamoja na kuimarisha fursa za elimu ya juu Zanzibar. Miongoni mwa hatua za mwanzo tulizochukua ni kuusimamia ujenzi wa Kampasi mpya huko Tunguu ulioanzishwa na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita. Tarehe 5 mwezi huu nilikagua kazi ya ujenzi unaoendelea pamoja na kulitembelea eneo lililotengewa kwa ajili ya Kampasi hiyo na nimefurahishwa na yote niliyoyaona pamoja na maendeleo mazuri ya kazi hiyo. Napenda kukuthibitishieni wananchi wa Zanzibar kwamba Serikali imejidhatiti na imesimama kidete katika kukijenga chuo hiki na Inshaallah Mwenyezi Mungu atatusaidia tufanikiwe. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu wananchi. Katika kuizingatia tathmini ya miaka kumi ya chuo chetu, hatuna budi kuzingatia kukua kwa idadi ya taaluma zinazotolewa hapa. Tulianza kwa kutoa fani chache, ikiwemo ya Elimu kwa ajili ya walimu wa sekondari. Ninafuraha kuwa dhamira yetu ya kuwa na walimu waliofuzu katika kiwango cha shahaha imeanza kufikiwa na katika kipindi kifupi kijacho walimu wetu wote wa skuli za sekondari watakuwa na Shahada ya Chuo Kikuu. Leo hii, tutatoa Shahada ya Sanaa na Elimu kwa wahitimu 139 na Shahada ya Sayansi na Elimu kwa wahitimu 63. Hao wote watakuwa ni walimu wetu wa skuli za sekondari hivi karibuni. Haya ni maendeleo ya kupigiwa mfano. Kama nilivyosema siku ile ya tarehe 29 Machi mwaka huu; kwamba karne hii tunayoishi ni karne ya Sayansi na Teknolojia ya kisasa. Kwa upande mmoja ninafuraha kuwa tumeanza kutoa wataalamu wa Fani ya Teknohoma (IT). Makamu Mkuu wa Chuo amekwishatueleza juu ya mipango ya kuanzisha vitivo vipya ambavyo vitatilia mkazo mafunzo ya Sayansi. Kwa upande wangu napenda kukuhakikishieni wanachuo nyote kwamba tutaendelea kushirikiana ili kuhakikisha chuo chetu kinatoa fani nyenginezo kama vile utalii, kilimo na udaktari. Katika tathmini yetu leo, tunapaswa pia kuangalia mchango wa chuo chetu katika maendeleo ya nchi yetu. Tunashukuru kuwa tunaendelea kupata walimu wanaohitajika kutoka kwenye Chuo Kikuu hiki, ambao tunawategemea sana na ambao watatoa mchango wao katika kupunguza tatizo la ajira na kupunguza umasikini. Benki ya Dunia imezitaka nchi za Afrika kukuza upatikanaji wa elimu ya juu, ili iwe ndio ngazi ya kuondoa umasikini. Makamu Rais wa Benki ya Dunia kwa Afrika, Obiageli Ezekwesili, hivi karibuni aliuambia mkutano wa siku mbili wa elimu ya juu katika Afrika, katika Chuo Kikuu cha Ghana, Legou kuwa: “Ni muhimu kwa vyuo vikuu kutilia mkazo ubora wa elimu unaokidhi mahitaji ya kisasa ya uchumi uliojaa ushindani.” Wito huu umetolewa kwetu kwa hivyo ni wajibu wetu tujipange vyema na tuhakikishe kwamba matunda ya vyuo vikuu vyetu ni kuchangia maendeleo ya nchi zetu. Wazo la Vyuo Vikuu vya Maendeleo (Development Universities) si geni kwa sababu lilibuniwa na wataalamu katika miaka ya sabiini na wataalamu kama Profesa Manuel Castells aliandika kuwa “Mfumo wa Elimu ya Juu uwe ni Injini ya Maendeleo katika Uchumi wa Ulimwengu Mpya.” Mtazamo huu wa kitaalamu ukitekelezwa ipasavyo, kwa hakika vyuo vikuu vyetu vitaweza kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya nchi yetu na wananchi wake. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Kutokana na haya yote, napenda kukumbusha kwamba matarajio yetu ni kuwa hapo baadae katika chuo chetu kikuu hiki, tuwe na Vitivyo vya Uhandisi, Biashara, Taasisi ya Utafiti na Taasisi ya Sayansi za Bahari. Vitivo hivi pamoja na vyenginevyo vilivyopo sasa, vitatusaidia katika kukidhi mahitaji ya nchi yetu katika kupeleka mbele maendeleo. Hili ni jukumu kubwa kwenu wanajamii na wanachuo kwa jumla, lakini nina imani nanyi kwamba mtalimudu. Naahidi tena kwamba Serikali yenu siku zote itakuwa tayari kutoa msaada kila inapowezekana. Tumeanza kwa kujenga majengo mapya, kupanua chuo, kuongeza wahadhiri na kuangalia maslahi yenu nyote kwa jumla. Nitaendelea kufanya kila jitihada katika kushajiisha na kutilia nguvu ushirikiano utakaoleta tija kwa chuo chetu kwa njia ya mahusiano na vyuo vikuu vya nchi za nje. Aidha, tutaendelea kujitahidi kadri tunavyoweza kuwasaidia wanafunzi wetu ili wawe na mazingira bora ya kujifunzia ikiwemo suala la kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar itatengewa fedha zaidi katika bajeti zijazo za Serikali kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu. Hata hivyo, napenda ifahamike kwamba idadi ya wanafunzi wanaofaulu na kupata sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, ndani na nje ya nchi inaongezeka kila mwaka na ni dhahiri kuwa hii ni changamoto kubwa kwetu sote. Natoa wito kwa wale wazazi wanaojimudu pamoja na sekta binafsi, kwa jumla waunge mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha watoto wetu kupata elimu ya juu. Ili kuleta kasi ya maendeleo katika nchi yetu, hapana budi kila mmoja wetu ajitume kwa kiasi kinachowezekana na kufanya kazi kwa bidii zaidi. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Walimu na Wahadhiri wa vyuo vikuu vyetu, nawanasihi, kuongeza bidii kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kielimu nchini ili matokeo yake yaendeleze nchi yetu kwa haraka. Katika kutekeleza jambo hilo natilia mkazo tena suala la kufanya utafiti, kwani kufanikiwa kwetu kupitia tafiti kutaongeza kiwango cha maendeleo katika chuo chetu pamoja na kutupatia sifa nzuri. Pamoja na tafiti hizo, nashauri kwamba Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni katika chuo chetu ikuzwe ili iwe mashuhuri kwa lugha hiyo duniani kama Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, kilivyo mashuhuri kwa lugha ya Kiingereza. Naamini suala hilo linawezekana na historia ya lugha hiyo nchini kwetu, itasaidia kufanikisha utekelezaji wa lengo la kukifanya chuo chetu kuwa mashuhuri katika ufundishaji wa Kiswahili duniani kote. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Sasa nataka nizungumzie suala la wahitimu. Leo hii ndugu wahitimu mmetunukiwa Shahada, Stashahada na Vyeti baada ya kuhitimu mafunzo yenu. Jambo la msingi kwenu ni kushirikiana na wananchi wenzenu katika kupambana na changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii na nchi yetu kwa jumla na kuzipatia ufumbuzi. Aidha, ninakukumbusheni umuhimu wa kushirikiana na wananchi wenzenu katika kuijenga nchi yetu. Nashauri mtumie elimu yenu mliyoipata kwa kuongeza tija katika ajira zenu na zaidi muweze kujiajiri nyinyi wenyewe kwa kila inapowezekana. Wahitimu wa Vyuo Vikuu ni watu wenye upeo mkubwa na ubunifu na ni vyema mkashirikiana katika kujitafutia ajira za kukufaeni nyinyi na nchi yetu kwa jumla. Sambamba na hilo, nakukumbusheni kuwa “elimu haina mwisho”. Ngazi mliyokwishaifikia ni mwanzo tu wa safari ndefu ya kutafuta elimu. Wasia wangu kwenu ni kuzidi kuendelea zaidi kuitafuta elimu ya Shahada za juu zaidi. Nchi yetu inahitaji wataalamu wenye elimu ya kutosha na ya juu, kwa kuwa nyinyi tayari mmeshapata msingi wa kwendea huko, nakushaurini muitumie fursa hiyo vilivyo. Ndugu Wahadhiri, Wanachuo na Ndugu Wananchi Kwa mara nyengine, nakushukuruni nyote kwa kuitikia wito na kwa mahudhurio yenu makubwa. Namalizia kwa kukuombeeni afya njema na moyo wa kuendelea kuitumikia nchi yenu huku mkiamini kuwa “mtu kwao” na muungwana ni Yule anaeitumikia jamii iliyompa elimu na kumlea kwa bidii na juhudi zake zote. Nakutakieni kila kheri katika mwaka mpya wa 2012. Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Advertisements