Archive for January, 2012

TIBAIJUKA AMJIBU JUSSA

 

Waziri wa nyumba na maendeleo ya makaazi Prifisa Anna Tibaijuka

Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makaazi Profisa Anna Tibaijuka amesema suala ya kugawanya raslimali ndani ya muungano linaweza kujadilika badala ya kuendelea kuzozana juu ya pendekezo la kuomba eneo la maili 200 la bahari kuu ya hindi kwenye umoja wamataifa.

          Akizungumza na Zenji Fm radio juu ya mvutano huo ameseema wananchi wanao uhuru wa kujadili raslimali zao kwa kila upande wa muungno na hatimae kupatikana muafaka.

Profisa Tibaijuka amesema wananchi wanaweza kutoa maoni yao juu ya waganaji wa raslimali zitakazopatikana katika eneo hilo wakati huu wa kuunda katiba mpaya badala ya kuendelea kubaki chini ya umoja wamataifa.

Aidha Profisa Tibaijuka amesema suala hilo linagusa mipaka ya nchi na limo kwenye mamalaka yake na iwapo eneo hilo litapatikana wizara yake haitakua na mamlaka na raslimali zitakazopatikana ikiwemo nishati ya mafuta.

Hivi karibuni mwakilishi wa jimbo la Mkongwe Ismail Jussa Ladhu ameiomba serikali ya mapinduzi Zanziba kuiandikia serikali ya jamhuri ya muungano kuitaka kusimamisha mpango wake huo wa kuongezewa eneo hilo kwenye umoja wa mataifa.

          Akiwasilisha hoja ya dharura katika baraza la wawakilishi amesema suala hilo bado halijapatiwa ufumbuzi kutokana na baraza la wawakilishi kutoa mapendekezo ya eneo la bahari kuu na raslimali zake liwe chini ya mamlaka ya Zanzibar.

Eneo lililombwa na Tanzania kwenye umoja wa mataifa la maili 200 za ziada katika bahari kuu ya Hindi sehemu kubwa liko kaskazini mashariki mwa kisiwa cha Pemba.

Serikali ya jamhuri ya muungano Tanzania imetumia zaidi ya shilingi bilioni moja kama gharama za kuwasilisha pendekezo hilo kwenye umoja wa mataifa huku wajumbe wa baraza la wawakilishi wakidai Zanzibar haikushikishwa kikamilifu.

 

 

Advertisements

HAKUNA UWIANO WA UAJIRI NAFASI ZA KIBALOZI

Serikali ya mapinduzi Zanzibar imesema hakuna uwiano wa kutosha katika nafasi za kazi za utendaji kwenye afisi za kibalozi nje ya nchi kati ya vijana wa Zanzibar na Tanzania bara. Waziri wa nchi afisi ya makamu wa pili wa rais Mohammed Aboud amesema tatizo hilo ni moja ya kero za muungano zinazoshughulikiwa ili wanzanibari waweze kuajiriwa katika afaisi hizo. Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi amesema serikali imeona upo umuhimu kwa nafasi za ajira katika ofisi za kibalozi kuajiriwa kwa usawa kati ya vijana wa Zanzibar na Tanzania bara. Hata hivyo waziri Aboud amesema kuchelewa kuyapatia ufumbuzi matatizo ya muungano likiwemo suala hilo kunaweza kuwafanya wazanzibari kutokuwa na imani kwa vile hawafaidiki na matunda ya muungano.

RAZA AWEKEWA PINGAMIZI

Ali MBAROUK MSHIMBA Mgombea wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Uzini kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amewasilisha pingamizi dhidi ya uteuzi wa Bwana. Mohammedraza Hassanali kuwa mgombea wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi mdogo Jimbo la Uzini utakaofanyika tarehe 12, Februari 2012.
Kwa kuwa hati ya kiapo ya Mohammed raza Hassanali Mohamedali mgombea wa Uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) inakwenda kinyume na Sheria ya uchaguzi namba 11/1984 Kifungu cha 46 (3) (a).
SABABU ZA PINGAMIZI.
1.    Kwamba kiapo cha Muombaji na au Mgombea wa Uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kukidhi matakwa ya kisheria za viapo kwa sababu hakuna kumbukumbu za nambari katika kuonyesha stakabadhi halali za malipo (Paid in Receipt no) na kwamba mlaji kiapo hakulipa malipo halali kwa mujibu wa Sheria na wala hakuomba nafuu yeyote iwapo uwezo wa malipo hayo hana.

2.    Kwamba kiapo cha muombaji kimeliwa kinyume cha sheria za viapo Zanzibar (Laws and Decree) pamoja na kukosa stempu halali na ambapo ni kinyume na matakwa ya sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Namba 11 ya mwaka 1984 pamoja na marekebisho yake, kifungu 46 (3) (a).

3.    Kwamba Kiapo cha Muombaji kimekosa sifa kwa mujibu wa Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka 1984, (3) (a) ambapo Mlaji kiapo alitakiwa aape mbele ya Hakimu kwa mujibu wa kifungu nilichokitaja kwenye aya hii, badala yake yeye alikula kiapo aidha mbele ya Jaji au amegushi muhuri wa Mahakama Kuu.

4.    Kwamba Mlaji kiapo hakuweza kufuata utaratibu wa kisheria ambapo alitakiwa ale kiapo mbele ya Hakimu, na badala yake alikiuka utaratibu huo  na kwa vyovyote vile kiapo hicho hakiwezi kukidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa kinapingana na Sheria za Viapo na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar.

Kwa Hivyo basi kutokana na sababu za pingamizi tulizozieleza hapo juu kutoka kwenye aya ya 1, 2, 3, na 4 na kwa mujibu wa Kifungu namba 46 (4) ninaiomba Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Uzini kama ifuatavyo:-

Msimamizi wa Uchaguzi utengue Uteuzi wa Mohammedraza Hassanali Mohamedali kuwa ni Mgombea halali, na kumuondoa katika orodha ya wagombea wa Uwakilishi Jimbo la Uzini katika uchaguzi mdogo, kwa kuwa hakuweza kutimiza sifa za kuwa mgombea kwa mujibu wa sheria.
   
Pingamizi hili limetiwa saini leo Tarehe 25 Januari, 2012 na kuwasilishwa mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Uzini.

Taarifa imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uenezi kwa niaba ya ALI MBAROUK MSHIMBA, MGOMBEA WA UWAKILISHI-CHADEMA JIMBO LA UZINI

SERIKALI YA KIKWETE YASALIM AMRI KWA MADAKTARI

Serikali ya jamhuri ya muungano Tanzania imewataka madaktari waliogoma kurudi kazini ili kutoa mapendekezo yao ya kumaliza mgomo huo.

          Akizungumza na wandishi wa habari waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema wataalamu hao wanapaswa kuwajali wagonjwa na mvutano kati yao na serikali utamalizwa katika meza ya mazungumzo)

          Mgomo huo wa madaktari ulioingia kwa siku ya pili leo umeathiri utowaji huduma katika hospitali za Muhimbili, Dodoma na Ocean road.

Baadhi ya hospitali serikali imelazimika kuwarejesha kazini madaktari waliostaafu kwa kuingia mkataba.

 

PINDA AJITOA KWENYE SIASA

Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ametangaza hatagombea nafasi yoyote ya uongozi wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015.

          Pinda amesema anakusudia kustaafu rasmi katika siasa wakati muhula wake utakapomalizika mwaka huo.

          Waziri mkuu ametangaza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es salaam kuzungumzia masuala mbali mabali yanayohusu serikali na utendaji wake.

          Uwamuzi wa waziri mkuu Pinda unakuja katika wakati huu baadhi ya vigogo wa CCM wakiwa katika harakati za kutaka kumrithi rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muhula wake wa mwisho mwaka 2015.

Hata hivyo Pinda amewaonyeshea kidole wanasiasa wanaowania nafasi ya urais kutokuwa na pupa ya kukimbilia ikulu

DR. SHEIN AKUTANA NA SHAMHUNA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, leo amenza vikao maalum vya muendelezo wa kukutana na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia mpango kazi wa Wizara hizo katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa kipindi cha robo ya pili.

 

Katika vikao hivyo vinavyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Rais Dk. Shein leo ameanza kukutana na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji, Nishati na baadae alikutana na Uongozi wa Wizara ya Afya.

 

Akizungumza na Uongozi wa Wizara hizo kwa nyakati tofauti, Dk. Shein alisema kuwa utaratibu huo utazisaidia kwa kiasi kikubwa Wizara zote kuweza kujitathmini wenyewe kwa kuangalia kila robo mwaka hatua iliyofikiwa pamoja na mambo waliyoyafanya.

 

Alieleza kuwa hatua hiyo pia, itasaidia kupata kujua mambo waliyoyapanga wanaweza kuyatekekeza vipi kutokana na nyenzo walizozipata sanjari na bajeti yao waliyoiandaa.

 

Kwa upande wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, uongozi wa Wizara hiyo ulieleza mafanikio yaliopatikana kutokana na vikao hivyo na kueleza kuwa kwa upande wa sekta ya maji lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kufikia asilimia 95 kwa watumiaji wa mjini na asilimia 75 kwa watumiaji wa vijijini ifikapo mwaka 2015 lipo pale pale.

 

Uongozi huo ulieleza kuwa utafiti wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi bado unaendelea baada ya kumpata mshauri mwelekezi kutoka Kampuni ya NIRAS ya Denmark ambapo pia, ulieleza hatua inazozichukua ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu.

 

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa kazi ya uchimbaji wa visima viwili vya Chumbuni,ulazaji wa mambomba ya maji katika maeneeo ya Kijichi na Kinuni,uwekaji wa pampu na Mota katika maeneo ya Dimani pamoja na uchimbaji wa visima viwili vya Chokocho Michenzani Pemba vimekamilika.  

 

Pia, uongozi huo ulieleza kuwa ujenzi wa tangi la maji Kizimkazi, Micheweni na Kama tayari umekamilika na wananchi wameshaanza kutumia huduma hiyo ambapo ujenzi wa tangi la Ziwani Pemba umo katika hatua za kumalizika.

 

Uongozi ulieleza kuwa ulazaji wa mabomba ya maji katika maeneo ya Kizimkazi tayari umekamilika na kwa upande wa Shumbavyamboni kazi bado inaendelea.

 

Kwa upande wa Sekta ya Nishati uongozi huo ulieleza kuwa tathmini na malipo ya fidia ya mali na mazao kwa waathirika wa mradi wa MCC imekamilika.

 

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa kupitia shirika lake la umeme Zanzibar ZECO, limo katika juhudi za kuzungumza na Benki za hapa nchini zikiwemo PBZ na NMB kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kuungiwa huduma hiyo kwa njia ya mkopo.

 

Uongozi huo ulieleza kuwa kwa upande wao hivi sasa Shirika hilo limesitisha mkopo wa kuungiwa huduma hiyo kutokana na ukosefu wa fedha na inachofanya hivi sasa ni kuendelea kukusanya kile waliochowakopesha wananchi waliyowaungia huduma hiyo hapo siku za nyuma.

 

Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa hatua za ukamilishaji wa waya wa baharini  wenye kilomita 39.5 kutoka Ras Kiromoni Dar-es-Salam hadi Ras Fumba Unguja zinaendelea na unatarajiwa kukamilika wakati wowote. Pia, umeeleza azma na mikakati iliyowekwa ya kuepeleka huduma ya umeme katika visiwa vidogo vidogo vya Pemba.

 

Kwa upande wa uongozi wa Wizara ya Afya, uongozi huo ulieleza mikakati na mipango yake katika kuendeleza huduma ya afya hapa nchini. Aidha, Wizara hiyo ilitoa shukurani kwa Dk. Shein kutokana na hatua yake hiyo ambayo wameielezea kuwa ni chachu ya utendaji wa kazi zao

 

 

 

SHAMHUNA ATAKIWA KUJIUZULU

Wajumbe wa baraza la wawakilishi wameliomba baraza la mapinduzi kumchukulia hatua za kinidhamu waziri wa ardhi, makaazi, maji na nishati Ali Juma Shamhuna kwa kukiuka mamlaka ya serikali ili kuwa fundisho kwa mawaziri wengine.

        Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma ametoa ombi hilo alipokuwa akichangia hoja binafsi ya kuitaka serikali kuchukua hatua za kuzuwia azimio la Tanzania kutaka kuengezewa maili 200 za ziada na umoja wa mataifa iliyowasilishwa na mwakilishi wa jimbo la Mji mkongwe Ismail Jussa Ladhu.

        Amesema mwaka 2009 wajumbe wa baraza la wawakilishi walipitisha azimio la kuiagiza serikali kuondoa suala la mafuta na gesi asilia na eneo la bahari kuu kwenye orodha ya muungano na badala yake kushughulikiwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

        Amesema kauli ya waziri Shamhuna kutamka azimio hilo halijui ni kukosa umakini kwa kiongozi na kumtaka waziri huyo ajiuzulu

        Nae mwakilishi wa jimbo la Chakecheke Omar Sheikh amesema kitendo hicho kimeabisha baraza la wawakilishi na wananchi, hivyo ametaka waziri huyo kabla ya kufika kwenye abaraza la mapinduzi ajiuzulu.

        Amesema iwapo atashindiwa kufanya hivyo amemuomba rais wa zanziba na mwenyuekiti wa baraza la mapdinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kuchukua hatua za kumfuta kazi

        Waziri Shamhuna ambae ni mwakilishi wa jimbo la Donge anadaiwa kukiuka katiba ya Zanzibar kwa kutamka mapendekezo hayo anayafahamu, lakini, ameshindwa kutoa taarifa kwa baraza la mapinduzi.

        Mapendekezo hayo ya Tanzania kutaka kuongezewa maili 200 zaidi ya eneo la bahari kuu yamewasilishwa umoja wa mataifa tarehe 18 mwezi huu, hatua inayopingwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi wakidai suala hilo bado halijapatiwa ufumbuzi ndani ya muungano