gari lililopata ajali na kusababisha kifo cha Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Regia Mtema. Picha na Yusuf Badi).

MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Regia Mtema amekufa katika ajali ya gari iliyotokea saa 5:15 asubuhi jana. Katika tukio hilo, Mbunge huyo aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Landcruiser VX (V8) lenye namba za usajili T 296 BSM, alipasuka kichwa na ubongo wake kutapakaa katika eneo la ajali mita chache kabla ya kulifikia Daraja la Ruvu kutokea Dar es Salaam. Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Saleh Mbaga alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa ilitokana na hatua ya Mbunge huyo kulipita gari lililokuwa mbele yake na ghafla likatokea roli la mafuta na alipotaka kurejea upande wake gari hilo lilimshinda na kubiringita mara saba. Mbaga alisema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, polisi walifika na kumkuta Mbunge huyo akiwa tayari amekufa huku akibubujikwa na damu nyingi kutokana na kichwa kupasuka huku ubongo ukiwa umemwagika ardhini. “Askari walipofika kwanza walianza kuwakimbiza majeruhi Hospitali ya Tumbi, waliwachukua kwanza majeruhi watano halafu baadaye wakawachukua wengine wawili na baadaye ndio tukafanya mpango wa kuondoa mwili wa marehemu eneo la tukio kuupeleka Hospitali ya Tumbi,” alisema Mbaga. Alisema hata hivyo ajali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua ya Mbunge huyo kuwa na ulemavu wa mguu na hivyo kuwa na mguu mmoja tu wa kushoto ambao alisema inadhaniwa ulimpa tabu katika kufanya uamuzi baada ya kutokea kwa lori hilo la mafuta mbele yake. “Kama mnavyojua pedeli za gari zipo upande wa kulia lakini yeye alikuwa anatumia mguu wa kushoto kwa hiyo inawezekana kutokana na mshituko wa kutokea gari mbele, alibabaika katika kuutumia mguu huo wa kushoto kufanya uamuzi na hivyo kusababisha gari kumshinda na kupinduka,” alisema Mbaga. Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mlandizi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Emmanuel Bondo alisema mbunge huyo alikuwa na abiria wengine saba ndani ya gari hilo ambao ni wa familia yake na walikuwa wakielekea katika kijiji cha Mperamumbi katika Tarafa ya Ruvu kukagua mashamba. Alisema muda mfupi baada ya ajali hiyo, gari la Mbunge huyo liliondolewa kutoka eneo la ajali ili kuepusha msururu wa magari katika eneo hilo. “Sasa hivi nasubiri kufika kwa Kamati ya Bunge ambayo nimeambiwa itafika mahali hapa wakati wowote ili kuja kutembelea eneo la tukio,” alisema Mkuu huyo wa Kituo cha Polisi cha Mlandizi. Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alithibitisha kutokea kwa kifo cha Mtema aliyekuwa mmoja wa wabunge 48 wa chama hicho na akakiri kuwa Chadema imepata pigo kubwa kutokana na msiba wa ghafla wa mbunge huyo akisema kuwa, mchango wake ulikuwa ukihitajika kwa chama na taifa kwa ujumla. Aliongeza kuwa, mipango ya mazishi ya marehemu ilikuwa inapangwa nyumbani kwa baba wa marehemu, Estelatus Mtema, Tabata Chang’ombe, katika Manispaa ya Ilala na kwamba ratiba ya maziko itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zilizotarajiwa kupangwa na familia ya marehemu, Ofisi ya Bunge na chama. Kutokana na kifo hicho, salamu za rambirambi zimemiminika kwa Chadema na familia ya marehemu, zikiwamo kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete. Katika salamu zake za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Rais Kikwete alisema amesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha mbunge huyo ambaye amepoteza maisha akiwa bado kijana na kwamba pigo hilo siyo la Chadema pekee, bali ni kwa taifa zima. “Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi habari za kifo cha Mheshimiwa Mtema katika ajali ya gari. Siyo kwamba ajali hii imechukua maisha ya kijana bali imelinyang’anya taifa mbunge hodari na kwa hakika, kifo chake siyo tu ni pigo kwa chama chako cha Chadema bali ni pigo kwa sote na kwa taifa letu kwa jumla. Nakutumia wewe binafsi, chama chako na wanachama wake salamu za dhati za moyo wangu kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa.” “Napenda ujue kuwa niko nanyi katika msiba huu. Napenda vilevile uniwasilishie salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa kwa wana-familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mheshimiwa Mtema. Wajulishe kuwa nimepokea habari hizo kwa uchungu mwingi na kuwa moyo wangu uko nao katika wakati huu mgumu wa maombolezo, “ amesema Mheshimiwa Rais na kuongeza. “Aidha, wajulishe kuwa nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, awajalie uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake. Naungana nawe, Mheshimiwa Mwenyekiti, na wanafamilia wa marehemu kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya Mheshimiwa Regia Mtema. Amen.” Naye John Nditi anaripoti kutoka Kilombero kuwa, wananchi wa mjini Ifakara na vitongoji vyake wamepokea taarifa za msiba huo kwa mshtuko mkubwa kufuatia taarifa ya kifo cha mbunge huyo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Ifakara, kwa majonzi baadhi ya wananchi walisema kuwa wana-Kilombero wamempoteza mbunge kijana na mchapakazi aliyewatumikia wananchi wake bila kujali jinsia na itikadi ya vyama vya siasa. Baba mkubwa wa marehemu Bartholomew Mtemanyenja alisema walipata taarifa za ajali hiyo, na baadaye baba mzazi wa marehemu, Estelatus Mtema alithibitisha akiwa njiani kwenda eneo la tukio akitokea Kilombero ambako juzi alishiriki katika maziko ya mmoja wa madaktari wa Hospitali ya St. Francis. “Tulipata taarifa mchana wa saa saba na nusu saa baadaye, baba yake mzazi aliamua kuondoka kwa kupanda magari tofauti kwenda eneo la tukio, lakini akiwa njiani alituarifu kuwa Regia amefariki dunia,” alisema baba mkubwa. Awali, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abdul Mteketa alisema amesikitishwa na kifo hicho na kumwelezea marehemu kuwa ni kijana mdogo, na mchango wake ulikuwa bado unahitajika kwa wananchi wa Kilombero na Taifa kwa ujumla. Naye Katibu wa Mbunge, Mashaka Manjoti alisema kuwa Wilaya ya Kilombero na Chama chao kimepoteza mpigania maendeleo ya wananchi wanyonge wakiwemo na watumishi wa nyanja mbalimbali. Historia ya marehemu ambaye mwaka 2006 alihitimu Shahada ya Sayansi ya Uchumi na Lishe katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA). Alizaliwa miaka 31 iliyopita na Aprili 21 mwaka huu angetimiza miaka 32. Alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Mchikichini, Ilala kuanzia mwaka 1989 hadi 1995, huku elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne aliipata katika Shule ya Sekondari ya Forodhani kuanzia mwaka 1996 hadi 1999 zote za Dar es Salaam. Alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa katika Mchepuo wa Kemia, Biolojia na Lishe (CBN) mwaka 2000, lakini aliomba uhamisho ili kwenda Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bweni Machame, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Habari na picha kutoa gazeti la habari leo

Advertisements