Meli ya Spice Islander ikiwa chini ya bahari mkondo wa Nungwi

Watuhumiwa 11 wanaodaiwa kufanya uzembe uliosababisha ajali ya kuzama Meli ya Mv Spice Islander akiwemo mwakilishi wa jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub wamefikishwa katika mahakama kuu ya Zanzibar leo.

Mwendesha mashitaka wa serikali Mohammed Khamis Hamad amewataja watuhumiwa hao ni Said Abdalla Kinyanyika nahodha wa meli, Abdalla Mohammed Ali, Yusuf Sleiman Issa na Simai Nyange.

Wengine ni Haji Vuai Haji, Abdalla Mohd Abdalla, Juma Seif Juma, Hasan Mussa Mwinyi, Salim Said na Makame Hasnou.

Watuhumiwa wakati kesi inatajwa mahakamani hapo walikuwa hawapo akiwemo nahodha wa meli na Makame Hasnuu.

Amesema watuhumiwa hao wakiwa na dhamana ya meli ya MV Spices Ilander hawakutekeleza majukumu yao kwa kujaza mizigo na abiria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

 Hata hivyo mwendesha mashata huyo amesema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na watuhumiwa wamerejeshwa rumande, lakini dhamana yao iko wazi.

Amesema watuhumiwa hao wanaweza kuwa nje iwapo watakuwa na wadhamini wawili kila mmoja, warka ya mali usiohamishika wenye thamani ya shilingi milioni 20 au pesa taslimu shilingi milioni tano.

Nae wakili wa watuhumuwa hao Salum Mkonja aliomba mahakama kuharakisha upelezi ili kesi ipate kusikilizwa.

Kesi hiyo itakayotajwa tena tarehe pili mwezi ujao inasimamiwa na waendesha mashtaka watano wa serikali na watuhumiwa wanatetewa mawakili wawili.

 

Advertisements