Ali MBAROUK MSHIMBA Mgombea wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Uzini kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amewasilisha pingamizi dhidi ya uteuzi wa Bwana. Mohammedraza Hassanali kuwa mgombea wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi mdogo Jimbo la Uzini utakaofanyika tarehe 12, Februari 2012.
Kwa kuwa hati ya kiapo ya Mohammed raza Hassanali Mohamedali mgombea wa Uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) inakwenda kinyume na Sheria ya uchaguzi namba 11/1984 Kifungu cha 46 (3) (a).
SABABU ZA PINGAMIZI.
1.    Kwamba kiapo cha Muombaji na au Mgombea wa Uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kukidhi matakwa ya kisheria za viapo kwa sababu hakuna kumbukumbu za nambari katika kuonyesha stakabadhi halali za malipo (Paid in Receipt no) na kwamba mlaji kiapo hakulipa malipo halali kwa mujibu wa Sheria na wala hakuomba nafuu yeyote iwapo uwezo wa malipo hayo hana.

2.    Kwamba kiapo cha muombaji kimeliwa kinyume cha sheria za viapo Zanzibar (Laws and Decree) pamoja na kukosa stempu halali na ambapo ni kinyume na matakwa ya sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Namba 11 ya mwaka 1984 pamoja na marekebisho yake, kifungu 46 (3) (a).

3.    Kwamba Kiapo cha Muombaji kimekosa sifa kwa mujibu wa Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka 1984, (3) (a) ambapo Mlaji kiapo alitakiwa aape mbele ya Hakimu kwa mujibu wa kifungu nilichokitaja kwenye aya hii, badala yake yeye alikula kiapo aidha mbele ya Jaji au amegushi muhuri wa Mahakama Kuu.

4.    Kwamba Mlaji kiapo hakuweza kufuata utaratibu wa kisheria ambapo alitakiwa ale kiapo mbele ya Hakimu, na badala yake alikiuka utaratibu huo  na kwa vyovyote vile kiapo hicho hakiwezi kukidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa kinapingana na Sheria za Viapo na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar.

Kwa Hivyo basi kutokana na sababu za pingamizi tulizozieleza hapo juu kutoka kwenye aya ya 1, 2, 3, na 4 na kwa mujibu wa Kifungu namba 46 (4) ninaiomba Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Uzini kama ifuatavyo:-

Msimamizi wa Uchaguzi utengue Uteuzi wa Mohammedraza Hassanali Mohamedali kuwa ni Mgombea halali, na kumuondoa katika orodha ya wagombea wa Uwakilishi Jimbo la Uzini katika uchaguzi mdogo, kwa kuwa hakuweza kutimiza sifa za kuwa mgombea kwa mujibu wa sheria.
   
Pingamizi hili limetiwa saini leo Tarehe 25 Januari, 2012 na kuwasilishwa mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Uzini.

Taarifa imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uenezi kwa niaba ya ALI MBAROUK MSHIMBA, MGOMBEA WA UWAKILISHI-CHADEMA JIMBO LA UZINI

Advertisements