Waziri wa afya Zanzibar Juma Duni Haji akizungumza na waandishi wa habari

Wizara ya afya Zanzibar imewaomba watu wenye uwezo kusaidia matibabu ya watoto zaidi ya 100 wanaotaka kusafirishwa nje ya nchi kutokana na serikali kukabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa hao.

Waziri wa wizara hiyo Juma Duni Haji amesema gharama za kuwasafirisha watoto hao ni kubwa na serikali haina uwezo wa kuwatosha kuwasafirisha watoto hao wanaougua maradhi ya figo, moyo na saratani.

Akizungumza na wandishi wa habari juu ya utekelezaji wa majukumu ya wizara katika kipindi cha miezi sita amesema kuanzia Julai 2011 hadi Desemba mwaka jana serikali imetumia zaidi ya shilingi milioni 255 kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi.

Hata hivyo amesema idadi ya wagonjwa ya watoto na watu wazima wanaohitaji kusafirishwa nje ya nchi inazidi kuongezeka, hivyo ni vyema  kwa watu wenye uwezo kusaidia juhudi za kuokoa maisha ya watu hao

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikipeleka wagonjwa wanaoshindikana kutibiwa katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja katika nchi za India na Israeli. 

Akizungumzia ujenzi wa chumba cha wagonjwa mahuti katika hospitali ya Mnazi mmoja Duni amesema wizara inaendelea na matengenezo ya chumba na serikali  imetoa shilingi milioni 500 kati ya milioni 900.

Amesema matengenezo hayo yanendelea vizuri na yanatarajiwa kukamilika kabla ya bajeti ya mwakani.

Kuhusu upungufu wa madaktari bingwa amesema madaktari waliopo 20 wanasaidiana na madaktari kutoka nchi za Cuba, Norway, Misri na China.

Amesema katika kukabiliana na hali hiyo serikali inawapa mafunzo zaidi ya vijana 30 chini ya usimamizi wa madaktari bingwa wa Cuba pamoja na kuingia mkataba na Norway kuleta madaktari bingwa na kupeleka madaktari wazalendo nchini humo kupata uzowefu.

Advertisements