Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema haitakivumilia kikundi chochote kitakachoendesha makongamano na mihadhara itakayonekana kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa wananchi.
Akiakhirisha kikao cha baraza la wawakilishi makamo wa pili wa rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesema kumejitokeza kikundi cha wachache kinachoendesha makongamano na mihadhara inayotishia amani na utulivu.
Amesema makongamano na mihadhara inayoendeshwa na vikundi hivyo imebadili sura na kuwa kashfa, kejeli na matusi ya nguoni dhidi ya viongozi na wale wanaunga mkono muungano jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa mzanzibari na misingi ya demokrasia

Hata hivyo Balozi Iddi amewataka watanzania kuitumia fursa iliyotolewa na serikali ya kuandaa katiba mpya inayonesha kukuwa kwa demokrasia badala ya baadhi ya watu kujitokeza kuharibu dhamira hiyo.
Kuhusu taarifa ya kamati teuli iliyowasilishwa katika baraza la wawakilishi balozi Iddi amesema taarifa hiyo itasaidia kuwabadilisha viongozi wandamizi wa serikali kwa kufanya kazi kwa kujituma badala ya kimazowea.
Amesema rais Shein ametoa nafasi kwa kiongozi asietaka kubadilika kumuona kwa ajili ya kumpumzisha, hivyo amewataka mawaziri kusimamia kazi zao kwa uadilifu na uwajibikaji

Kikao cha baraza la wawakilishi kimeghirishwa hadi june 13 mwaka huu.

Advertisements