Archive for May, 2012

DR. NCHIMBI AKEMEA VITENDO VYA VURUGU ZANZIBAR

Dr. Emanuel Nchimbi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Dk. Emmanuel Nchimbi ametua Visiwani Zanzibar leo ambapo amekemea vitendo vya vurugu,akiahidi Serikali kuwachukulia hatua ikibidi hata kuwavizia nje ya misikiti kwa wale watakaohusika na uvunjifu wa amani .
 
Waziri Nchi aliwasili Mjini Zanzibar akiwa na Mkuu wa Jeshi  la Polisi,Inspekta Jenerali Said Mwema kwa pamoja waliitisha mkutano uliowakutanisha viongozi wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar(JUMAZA),Mabalozi,Kamisheni ya Utalii, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar(JUMIKI).
 
“Suala la kufuata sheria halina mjadala,lazima kila mmoja wetu afuate na kutii sheria hatutawavumilia watakaovuruga amani ya nchi…maandamano yoyote lazima yapate kibali” Aliwaambia wadau katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar,Ziwani.
 
Waziri Nchi alisema busara ya Polisi imefikia kikomo na kwamba atashangaa sana akiona busara hiyo ikiendelea wakati kuna watu au kikundi kinavunja amani ya nchi.
“Tutashangaa busara ya Polisi ikiendelea wakati watu wanaumia kwa watu wengine kuvunja amani…hatutakubali, tutaendelea kuviziana hata nje ya misikiti tutawakamata” Alisisitiza Waziri Nchi.
 
Waziri huyo alisema kila mtu anawajibika kitunza amani iliyopo ambapo pia alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa imefanyakazi nzuri katika kipindi kifupi na kuwapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.
 
 “Jamani Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatufanyia kazi nzuri kwanini mnataka kuwachafua viongozi wetu,lazima mfuate sheria hakuna mbadala wa hilo kwani dini zote zinahimiza amani,umoja na mshikamano.
 
Alisema Serikali inataka utulivu ndani ya mioyo ya watu na sio utulivu huo usiishie kuonekana barabarani tu, “watu waishi bila hofu kwa utulivu kabisa huku mioyo yao ikiwa imetulia” Aliongeza Dk. Nchimbi.
 
Alitoa wito kwa viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kuwafichua wahalifu wote waliohusika na matukio ya wizi,uporaji wa mali na uharibifu wa vitu na mali mbalimbali wakati wa matukio ya wiki iliyopita.
 
“Wananchi wafichueni wahalifu ,tusichanganye uislamu na uhalifu” alisisitiza Waziri Nchi katika mkutano huo ambapo viongozi wa dini waliahidi kuchukua hatua kusambaza ujumbe wa Waziri huyo kwa waumini na wananchi wengine kutunza amani na kujieepusha na vurugu.
 
Katibu wa JUMAZA,Sheikh Muhidin Zubeir Muhidin alisema Jumuiya yake ni tofauti na Jumuiya ya Uamsho hivyo watu wasizichanganye. Alisema Maimamu wataelezana ulazima wa kuwaeleza waumini kufuata na kuzitii sheria sio tu za Mwenyezimungu bali hata za Serikali.
 
Katika mkutano huo kulikuwa na wawakilishi wa Balozi za Marekani, Canada, Uingereza na Norway.

CCM YALAANI VITENDO VYA GHASIA NA VURUGU ZENJI

Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai

Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar kimesema kinasikitishwa na vurugu zilizotokea usiku wa kuamkia juzi zilizoandaliwa kwa makusudi na baadhi ya watu wasiopenda amani.

        Katika taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari imelaani vitendo hivyo na kuitaka serikali kuchukua tahadhari kubwa ili kudhibiti haraka vitendo hivyo kabla ya kuarhiri zaidi.

        Taarifa hiyo imetaja maeneo ya Mwanakwerekwe, Jang’ombe, Magogoni, Darajabovu na Kwamchina yaliotokea vurugu za jana jioni zinaweza kusimamisha shughuli zote za wananchi za kujitafutia maisha.

        Aidha chama hicho kimesema vijana wanaoendelea na vitendo vya hujuma kwa kuchoma moto gari, nyumba, makanisa matatu, baa tatu vinaweza kuhatarisha amani ya nchi.

        Taarifa hiyo imesema vurugu hizo hazipaswi kupuzwa na badala yake kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na baadhi ya watu kuendelea kuwahamasisha vijana kufanya fujo.

        Chama hicho kimetoa pole kwa wale walioathirika na vurugu hizo kwa kuharibiwa mali zao na kutoendelea na shughuli za kujitafutia maisha

HALI YA UTULIVU IMEANZA KUREJEA KATIKA MJI WA ZANZIBAR

Eneo la Michenzani Roud About lililokuwa kitovu cha ghasia na urushaji wa mabomu ya kutoa machozi kufuatia kuzuka vurugu katika mji wa Zanzibar

Hali ya utulivu imerejea kuwa ya kawaida katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Amani, Magogoni na Darajabovu kufuatia jeshi la polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu wanaodaiwa kutaka kufanya fujo katika maeneo hayo.

        Mwandishi wetu alietembelea maeneo hayo amesema mabomu ya kutoa machozi yalirushwa katika maeneo hayo na kusababisha barabara kufungwa, lakini hali hivi sasa imerejea kuwa shwari.

        Wakati huo huo maeneo yaliokuwa kitovu cha ghasia zilizoanza juzi usikukamavile Darajani, Michenzani, Kariakoo na Madema leo yameripotiwa kuwa salama.

        Hata hivyo kumekuwepo na hali ya taharuki katika maeneo hayo na kusababisha baadhi ya maduka kufungwa, lakini ulinzi mkali umeimarishwa katika majengo nyeti ya serikali na mabenki.

        Na taarifa za hivi karibuni zinasema kanisa la Tomondo limechomwa moto na watu wasiojulikana na hakuna taarifa za watu kujeruhiwa.

        Hata hivyo kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar amesema jeshi hilo bado halijapokea taaria hizo

WATU 30 WAKIWEMO VIONGOZI WATATU WA UAMSHO WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Gari la la mahabusu la Jeshi la Polisi likishusha watuhumiwa wa vurugu katika mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwwe

Watu 30 wakiwemo viongozi watatu wa jumuiya ya Uamsho wamefikishwa katika mahakama za wilaya Mwanakwerekwe kwa tuhuma za kukusanyika, kuandamana bila ya kibali, udhururaji na kufanya fujo.

        Viongozi watatu wa jumuiya ya Uamsho akiwemo Mussa Juma Issa na Said Khalfan wameshitakiwa kwa makosa ya kufanya mikusanyiko ya watu na kuandamana bila kibali.

        Viongozi hao walidaiwa mahakamani hapo siku ya tarehe 26 mwezi huu walikusanyika katika viwanja vya Malindi na kufanya maandamano bila ya kibali.

        Hata hivyo watuhumiwa hao wamekana tuhuma hizo, na hakimu wa mahakama hiyo Mohammed Ali Shein amekubali kuwapa dhamana ya shilingi laki tatu kwa maandishi na wadhamini watatu.

        Wakati huo huo watu wengine 28 wamefunguliwa mashtaka ya kufanya fujo, uzembe, udhururaji na ukorofi kwa kuweka mawe na kuchoma moto mipira ya gari katika barabara za Michenzani, Kariakoo, Mfereji wa wima na Amani.

Watuhumiwa hao wanadaiwa usiku wa tarehe 26 walidaiwa kufanya kosahilona kusababisha fujo. Hata hivyo watuhumiwa hao wamekana tuhuma hizo na kuiomba mahakama kuwapatia dhamana.

Mahakimu waliosikiliza kesi hizo Janeti Sakihola Nora na Valentine Andrew wamekubali kuwapatia dhamana watuhumiwa hao kwa shilingi laki tano kila mmoja na wadhamini wawili.

Kesi hizo zitasikilizwa tena tarehe 11 mwezi ujao.

 

MABOMU YA MACHOZI YATAWALA KATIKA KITOVU CHA MJI WA ZANZIBAR

Baadhi ya polisi wakionekana kutupa mabomu ya kutoa machozi

Jeshi la polisi Zanzibar linaendelea kutupa mabomu ya kutowa machozi katika maeneo ya Darajani na Michenzani yenye harakati nyingi ya shughuli za biashara kuwatawanya watu wanaokusanyika.

Mwandishi wetu Juma Abdallah Ali alietembelea maeno hayo amesema jeshi la polisi limekuwa kitawanya watu wanaokusanyika katika maeneo hayo kwa kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.

Watu wanaoishi katika maneo hayo wanaendelea kusalia ndani ya nyumba zao, lakini harakati za watu kupita huku na kule bado zinaendelea kama kawaida.

Baadhi ya maeneo mwandishi wetu ameshuhudia mabomu ya kutoa machozi ambayo hajaripuka.

Taasisi za fedha ikiwemo benki ya tu wa Zanzibar na benki nyengine katika maeneo ya Mji Mkongwe zimeimarisha ulinzi kwa kuhofia watu kuvamia majengo hayo.

Baadhi ya watu waliohojiwa na wandishi wete wameiomba serikali kuimarisha ulinzi na kuwasikiliza wananchi wake badala ya kutumia nguvu.

Hapo jana polisi pia walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu waliotaka kukivamia kituo cha polisi Madema mkoa wa mjini Magharib wakitaka kuwachiliwa huru kwa baadhi ya viongozi wa taasisi za dini ya Kislamu walioshilikiwa na jeshi hilo.

Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Khamis amesema jeshi hilo bado linaendelea na msako kuwatafuta watu wengine wanaodaiwa kuchochea wananchi kufanya fujo.

Kabla ya kutokea ghasia hizo baadhi ya watu wanaodaiwa wanachama wa jumuiya ya Mihadhara ya Kislamu UAMSHO walifanya maandamano yaliodaiwa kupeleka ujumbe kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Umoja wa mataifa kutaka Zanzibar huru.

UAMSHO WADAIWA KUVAMIA KITUO CHA POLISI MADEMA

 

Baadhi ya wanajumuiya ya Uamsho wakiandamana kabla ya kutokea ghasia

Polisi katika mkoa wa mjini magharibi wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu wanaodaiwa kukivamia kituo cha polisi Madema wakitaka kuachiliwa huru viongozi watano wa jumuiya ya Uamsho waliokamatwa na jeshhilo.

Viongozi hao wanadaiwa kushikiliwa na jeshi la polisi katika kituo cha Madema kwa madai ya kuchochea kufanya maandamano yasiokuwa na kibali.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu aliefika katika eneo la tukio Ramadhan Madogo polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu waliofika katika kituo hicho.

Hata hivyo amesema polisi wamefanikiwa kuweka hali ya utulivu katika eneo la tukio kwa kuwarejesha nyuma watu waliofka kwenye kituo hichoo

Akizungumzia juu ya ghasia hizo kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Khamis amesema viongozi wa Uamsho waliwashajihisha watu kwenda kumtoa kiongozi huyo.

Amesema kiongozi huyo amekamatwa kwa kile alichodai kufanya maandamano bila ya kibali na kusema jeshihilolinaendelea kuwatafuta viongozi wengine wa jumuiya hiyo wanaochochea uvunjifu wa amani.

Hata hivyo Kamishna Mussa amesema jeshi la polisi linaendelea kulinda hali ya amani na utulivu na kuwataka wananchi kutii sheria za nchi

Kabla ya kuripotiwa ghasia hizo baadhi ya wananchi wakiongozwa na Taasisi za Kiislamu walifanya maandamano kuanzia viwanja vya Lumba hadi Mnazi mmoja kulikofanyika muhadhara wa kislamu.

Maandamano hayo yalikuwa na lengo la kupeleka ujumbe kwa viongozi wa serikali yaZanzibar, Jamhuri ya Muungano na Umoja wa Mataifa kwa kile kinachodai kutakaZanzibarhuru.

Hata hivyo maandamano hayo yameripotiwa kufanyika kwa amani na utulivu, huku jeshi la polisi la kutuliza ghasia yakifanya doria wakati wa maandamano hayo.

Taarifa nyingine zinasema baadhi ya watu wameweka vizuzi kwa kuchoma mopo mipira ya gari katika barabara za maeneo ya Kariakoo, Michenzani na Miembeni.

KANISA LA ASSEMBLES OF GOD ZANZIBAR LACHOMWA MOTO

ASKOFU WA MADHEHEBU YA KANISA LA TANZANIA ASSEMBLES OF GOD LA KARIAKOO DICKSON KAGANGA AMESEMA WATU WASIOJULIKANA WAMECHOMA KANISA HILO JANA USIKU MAJIRA YA SAA 3.30 USIKU NA KUSABABISHA HASARA KUBWA.

AMESEMA MNAMO SAA HIZO WATU WASIOJULIKANA WALIVAMIA KANISA HILO HUKU WAKITOA LUGHA CHAFU ZENYE KUASHIRIA UVUNJIFU WA AMANI AMBAPO WALINZI WA KANISA HILO WALIBIDI WAJIFICHA KUOKOA MAISHA YAO.

AMEFAHAMISHA KUWA VITU VILIVYOUNGUA NI PAMOJA NA GARI NDOGO AINA YA KOROLA, VITI VYA PLASTIKI, VYOMBO VYA MUZIKI, KUTA ZA KANISA PAMOJA NA VIFAA VINGINE.

ASKOFU KAGANGA AMEFAHAMISHA JENGO LA KANISA NALO HALIFAI KWA MATUMIZI YA SALA AMBALO LINAHITAJI MATENGENEZO MAKUBWA IKIWEMO VIUNGO VYA UMEME, KWANI HADI SASA HAWAJAWEZA KUFANYA TATHIMINI KUJUA HASARA ILIYOPATIKANA.

AMEONGEZA KUWA  WAHALIFU HAO WALIOFANYA VITENDO VYA KUCHOMA KANISA HILO WALIDHAMIRIA KUFANYA MAUWAJI, KWANI ZANA WALIZOKUWA NAZO NI VISU, MAWE NA SILAHA ZA KIENYEJI.

AMESEMA KUWA ALIWAELEKEZA WALINZI WA KANISA HILO KUJIFICHA KATIKA SEHEMU AMBAYO ISINGEKUWA RAHISI KUONEKANA KUTOKANA NA NYIMBO NA MANENO WALIYOKUWA WAKISEMA YALIASHIRIA KABISA KUFANYA UHALIFU MKUBWA..

ASKOFU KAGANGA AMEIOMBA SERIKALI YA MAPINDUZIZANZIBARKUVIANGALIA KWA MAKINI VIKUNDI VYENYE KUASHIRIA SHARIILIKUITUNZA NA KUIENZI AMANI YA TAIFA HILI.