Makamu wa kwanza wa rais Malis Seif Sharif Hamad akiwa na wasanii wa filam ya Toba baada ya hafla ya uzinduzi ulifoanyika hoteli ya Bwawani

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wasanii mbali mbali katika kuitangaza Zanzibar Kimataifa.
Amesema wasanii hasa wa filamu wana mchango mkubwa  katika kuitangaza nchi na utamaduni wake, na kuwataka wasanii kutumia hiyo kuelezea hali halisi ya nchi badala ya kupotosha na kuiga mambo yasiyokuwa na faida kwa jamii.
Maalim Seif ameeleza hayo huko hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar katika hafla ya uzinduzi wa filamu ya “Touba” iliyoandaliwa na kampuni ya CY&CL ya Mjini Dar es Salaam.
Amesema filamu hiyo ambayo imeonyesha mafanikio mazuri kutokana na umahiri wa waigizaji wake na maudhui ya dini ya kiislamu yaliyomo, ni mfano wa kuigwa na wasanii wengine katika kujenga picha halisi ya utamaduni wa Zanzibar.
“Sanaa yoyote ile iwayo ni kielelezo muhimu cha utamaduni wa watu na jamii maalum, kwa maana hiyo sanaa haina budi kulindwa, kuenziwa na kuendelezwa,  lakini vile vile jamii inayohusika ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha sanaa hiyo ndiyo halisi, na wala haiharibiwi na kusababisha utamaduni, silka na mila zao kupotoshwa”, alifafanua.
Amefahamisha kuwa Tanzania inao wasanii wazuri ambapo iwapo watajiendeleza wanaweza kufikia upeo wa kutengeneza filamu za kuvutia kama zilivyo za Hollywood na Bollywood za Marekani na India.
Akielezea kuhusu historia ya Filamu Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema nyanja ya filamu Zanzibar ni kongwe na inaelezwa kuwa nchi ya kwanza kuwa na Sinema katika eneo la Afrika Mashariki mnamo miaka ya 1920s.
Ameongeza kuwa licha ya sanaa ya filamu kuwa na mafanikio lakini inakabiliwa na changamoto kadhaa  zikiwemo  kuporomoka kwa mila na tamaduni za nchi mbali mbali hasa nchi maskini, na kuwataka wasanii kuwa makini wakati wanapowasilisha sanaa zao, ili kulinda mila na silka za jamii zao.
Mapema akisoma risala kwa ajili ya uzinduzi huo mjumbe wa kamati ya maandalizi Zanzibar bwana Nassor Ameir Nassor amesema wameamua kufanya uzinduzi huo Zanzibar ili kutoa fursa kwa wasanii chipukizi wa Zanzibar kujifunza na kupata ukomavu wa sanaa hiyo.
Amezitaja sababu nyengine kuwa ni pamoja na kuona kuwa Wazanzibari wamefungamana na tabia njema kutokana na mila na silka zao wa asili, pamoja na kuitaja Zanzibar kuwa kitovu cha elimu ya dini ya Kiislamu.
Uzinduzi wa filamu hiyo ya “Touba” yenye maudhui ya kiislamu ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa wakiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk ambaye alikuwa mteja wa mwanzo kuinunua filamu hiyo kwa shilingi laki mbili.

Advertisements