Dr. Emanuel Nchimbi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Dk. Emmanuel Nchimbi ametua Visiwani Zanzibar leo ambapo amekemea vitendo vya vurugu,akiahidi Serikali kuwachukulia hatua ikibidi hata kuwavizia nje ya misikiti kwa wale watakaohusika na uvunjifu wa amani .
 
Waziri Nchi aliwasili Mjini Zanzibar akiwa na Mkuu wa Jeshi  la Polisi,Inspekta Jenerali Said Mwema kwa pamoja waliitisha mkutano uliowakutanisha viongozi wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar(JUMAZA),Mabalozi,Kamisheni ya Utalii, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar(JUMIKI).
 
“Suala la kufuata sheria halina mjadala,lazima kila mmoja wetu afuate na kutii sheria hatutawavumilia watakaovuruga amani ya nchi…maandamano yoyote lazima yapate kibali” Aliwaambia wadau katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar,Ziwani.
 
Waziri Nchi alisema busara ya Polisi imefikia kikomo na kwamba atashangaa sana akiona busara hiyo ikiendelea wakati kuna watu au kikundi kinavunja amani ya nchi.
“Tutashangaa busara ya Polisi ikiendelea wakati watu wanaumia kwa watu wengine kuvunja amani…hatutakubali, tutaendelea kuviziana hata nje ya misikiti tutawakamata” Alisisitiza Waziri Nchi.
 
Waziri huyo alisema kila mtu anawajibika kitunza amani iliyopo ambapo pia alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa imefanyakazi nzuri katika kipindi kifupi na kuwapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.
 
 “Jamani Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatufanyia kazi nzuri kwanini mnataka kuwachafua viongozi wetu,lazima mfuate sheria hakuna mbadala wa hilo kwani dini zote zinahimiza amani,umoja na mshikamano.
 
Alisema Serikali inataka utulivu ndani ya mioyo ya watu na sio utulivu huo usiishie kuonekana barabarani tu, “watu waishi bila hofu kwa utulivu kabisa huku mioyo yao ikiwa imetulia” Aliongeza Dk. Nchimbi.
 
Alitoa wito kwa viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kuwafichua wahalifu wote waliohusika na matukio ya wizi,uporaji wa mali na uharibifu wa vitu na mali mbalimbali wakati wa matukio ya wiki iliyopita.
 
“Wananchi wafichueni wahalifu ,tusichanganye uislamu na uhalifu” alisisitiza Waziri Nchi katika mkutano huo ambapo viongozi wa dini waliahidi kuchukua hatua kusambaza ujumbe wa Waziri huyo kwa waumini na wananchi wengine kutunza amani na kujieepusha na vurugu.
 
Katibu wa JUMAZA,Sheikh Muhidin Zubeir Muhidin alisema Jumuiya yake ni tofauti na Jumuiya ya Uamsho hivyo watu wasizichanganye. Alisema Maimamu wataelezana ulazima wa kuwaeleza waumini kufuata na kuzitii sheria sio tu za Mwenyezimungu bali hata za Serikali.
 
Katika mkutano huo kulikuwa na wawakilishi wa Balozi za Marekani, Canada, Uingereza na Norway.

Advertisements