Archive for June, 2012

SMZ KUANDAA MIKAKATI YA MIAKA MITANO YA DIASPORA KUCHANGIA MAENDELEO YA ZANZIBAR

 

wizara ya nchi ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dr. Mwinyihaji Makame

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema imetayarisha mpango wa miaka mitano wa kuwashajihisha wazanzibari wanaoishi nchi za nje kuchangia maendeleo ya uchumi ya nchi yao.

        Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara ya nchi ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi waziri Dr. Mwinyihaji Makame amesema mpango huo utasaidia kupatikana michango na utekelezaji wa sekta za kijamii na kiuchumi kutoka kwa wazalendo hao.

        Amesema serikali inaendelea kuwatafuta na kuwasiliana na jumuiya za wanzibari wanaoishi nchi za Ughaibuni zikiwemo Uingereza, Canada ili kuwashajihisha kusaidia maendeleo ya nchi yao 

MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/ 2013

 

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyeezi Mungu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana kwa mara nyengine ili tuendelee kujadili majukumu tuliyopewa na Wananchi wetu, likiwemo jukumu hili la kujadili suala la Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Taasisi mbali mbali za Serikali ikiwa leo tunajadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Mwaka wa Fedha wa 2012/2013.

 

Mheshimiwa Spika, pili, naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama  mbele ya Baraza lako tukufu ili niweze kuwasilisha Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi  Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Mwaka wa Fedha wa 2012/2013.

 

Mheshimiwa Spika, naomba nisiwe mwizi wa fadhila kwa kumpongeza  Mheshimiwa Waziri na Watendaji wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mashirikiano yao wanayotupa katika shughuli za   kamati na Baraza kwa ujumla. Vile vile napenda kuishukuru Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuwasilisha mbele ya kamati yetu pamoja na Baraza lako tukufu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2012/2013 ili, kama Katiba na Kanuni zetu zinavyoelekeza, yaridhiwe na Wajumbe wako kwa njia ya mjadala kwa maslahi ya nchi yetu.

 

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa kuwashukuru kwa dhati Wajumbe wa Kamati yetu kwa mashirikiano yao makubwa wanayonipa katika kutekeleza majukumu ya kazi zetu. Aidha, naomba niwashukuru Wajumbe wa Kamati kwa michango, maoni na ushauri wanaoutoa wakati tunapokuwa pamoja katika shughuli zetu za Kamati pamoja na shughuli za Baraza letu kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, naomba niwataje waheshimiwa Wajumbe wa Kamati kama ifuatavyo:-

 

1.       Mhe. Hamza Hassan Juma                –         Mwenyekiti

2.       Mhe. Mwanajuma Faki Mdachi           –         Makamu Mwenyekiti

3.       Mhe. Ali Salum Haji                            –          Mjumbe

4.       Mhe. Mgeni Hassan Juma                 –         Mjumbe

5.       Mhe. Mohammed Haji Khalid            –        Mjumbe

6.       Mhe. Salma Mohammed Ali                 –        Mjumbe

7.       Mhe. Ussi Jecha Simai                          –        Mjumbe

8.       Ndg. Rahma Kombo Mgeni              –         Katibu

9.       Ndg. Ramadhan Kh. Masoud           –         Katibu

 

 

Mheshimiwa Spika, baada ya Utangulizi huo, sasa kwa niaba ya Kamati yetu, sasa  naomba nianze kuichangia Hoja ya Waziri kwa uniruhusu kuwasilisha maoni ya kamati yetu kama ifuatavyo:-

 

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI

Mheshimiwa Spika, kamati inaipongeza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Idara ya Mipango, Sera na Utafiti kwa kuanzisha Tovuti ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na kutayarisha barua pepe za watendaji wa ofisi hiyo. Mheshimiwa Spika, kamati yetu inaipongeza Idara hii kwa kuanzisha Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kamati inaamini kuwa kuanzishwa kwa tovuti na kitengo hicho kutaiwezesha Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kufanya kazi zake kwa ufanisi lakini pia kuiwesha Ofisi hii kufahamika nje na ndani ya nchi yetu.

 

OFISI YA FARAGHA YA RAIS

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza kwa dhati ziara za nje na ndani ya nchi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais na wajumbe wake mbali mbali. Kamati yetu inaamini kuwa ziara hizi zinaongeza chachu ya maenedeleo katika nchi yetu. Hata hivyo, kamati inaishauri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Ofisi ya Faragha kuwa katika ziara hizo kadri itavyowezekana kuwakumbuka kuwajumuisha Wajumbe wa Kamati ili nao wapate nafasi ya kujifunza na kuishauri Serikali ipasavyo.

 

Mheshimiwa Spika, kamati vile vile imefarajishwa na maelezo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Mkataba wa Makubaliano na Serikali ya Ras el Khaimah katika nyanja kadhaa za kiuchumi na maendeleo, kama vile masuala ya Afya kwa kusaidiwa katika matibabu ya maradhi ya kisukari, figo, moyo na saratani. Mheshimiwa Spika, kamati inaomba ipatiwe ufafanuzi wa makubaliano hayo kwa maana Zanzibar iatapatiwa madaktari na vifaa kutoka Ras el Khaimah? Au madakatari wetu watakwenda kujifunza huko? Au tutajengewa hospitali itakayojihusisha na maradhi hayo? Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yatakayotolewa na Mheshimiwa Waziri, ni muhimu kukumbuka kuwa miongoni mwa mashaka makubwa yanayoikabili sekta ya Afya katika nchi yetu ni ukosefu wa vifaa vya kisasa pamoja na uhaba mkubwa wa wataalamu kwa maana ya madaktari wa maradhi ya tofauti. Hivyo, kamati yetu inawaomba viongozi wetu wanapopata fursa ya kupatiwa misaada ya Afya basi washawishi sana misaada hiyo ijikite kwa kupatiwa vifaa na kuwapatia madakatari wetu nafasi za masomo nje ya nchi ili wakapate mafunzo katika maradhi ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa sana hapa Zanzibar. Mheshimiwa Spika, Sukari, Saratani, figo, sindikizo la damu na maradhi ya baridi ni miongoni mwa maradhi kadhaa na mazito yanayoitesaZanzibar, amabayo yanahitaji vifaa na wataalamu wa kutosha.

 

Mheshimiwa Spika, kamati inaendelea kuipongeza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuweza kulifanyia matengenezo Jengo la Ikulu ya Mnazi mmoja na lile la Chake Chake. Hata hivyo, kamati yetu inaikiumbusha Seriakali kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuyafanyia matengenezo makubwa Majengo ya Ikulu ya Mkoani na Dodoma. Kwa ujumla majengo haya ni chakavu na hayana hadhi ya makaazi ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Spika, kamati yetu pia inaomba ipatiwe ufafanuzi wa kutosha kuhusu suala la kuliimarisha Jengo la Ikulu ya Kibweni kwa kulipaka rangi katika kuta zake za nje pamoja na kuimarisha bustani ya Ikulu hiyo. Mheshimiwa Spika, tunaomba ufafanuzi kwa sababu Jengo hilo lilipakwa rangi ambayo inaonekana haikuwa na kiwango lakini mazingira ya bustani yake hayaridhishi. Mheshimiwa Spika, kamati yetu pia inaikumbusha Ofisi hii kuyafanyia matengenezo majengo ya Ikulu ya Mkoani na Dodoma ambayo kiukweli hayana hadhi ya kuwa Makaazi ya Mheshimiwa Rais. Aidha, tunakumbushia suala la kuwekwa uzio katik eneo la Nyumba ya Seriakali iliyopo Mkokotoni, ambako mazingira yake yanachafuliwa na wanyama wanaofungwa katika eneo hilo. Kamati bila ya kusahau, inaiuliza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ule mpango wa kulihami Jengo la Serikali liliopo Fumba, ambalo eneo lake linanyemelewa kuliwa na bahari, umefikia wapi? Au ndio limetiwa kapuni?

 

IDARA YA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA URATIBU WA SHUGHULI A WAZANZIBARI

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza jitihada zinazochukuliwa na Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Shughuli za Wazanzibari wanaoishi nchi za nje. Kamati inaamini kuwa wazo la kuanzishwa kwa Idara hii pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Idara hii kutawawezesha Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kuisadia nchiyao kiuchumi na kijamii. Kamati katika kazi zake ilipewa taarifa kuwa Idara hii katika siku za usoni inatarajiwa kuhamishiwa katika eneo ambalo itaweza kufanya kazi zake kwa ufanisi. Kamati inafarajishwa na taarifa hii kwa sababu eneo wanalolitumia hivi sasa ni finyu na halitoshelezi kwa shughuli zao za kiofisi. Kamati vile vile inaishauri Idara hii kushirikiana na Wazanzibari waliopoZanzibar ambao waliishi nje ya nchi kwa miaka mingi kwa lengo la kupata taarifa zitakazawasaidia katika kazi zao. Kamati yetu pia inaishauri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Idara hii kuendelea kujifunza katika nchi zilizofanikiwa na utekelezaji wa dhana ya Diaspora. Miongoni mwa nchi hizo ni Ghana, India na nchi za “latin America”.

 

Mheshimiwa Spika, Idara hii kwa mujibu wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri hutangaza dhana ya Diaspora kupitia ZBC TV na Redio. Kamati yetu inaamini kuwa kuitangaza dhana hii mpya kwa kutumia vyombo hivi pekee haitoshelezi. Hivyo, kuna haja ya kuitangaza dhana hii kwa kutumia vyombo vya habari zaidi ya hivyo ili iweze keeleweka vyema. Aidha, kwa kuwa dhana hii bado ni mpya kuna haja kwa viongozi mbali mbali wa nchi hii kupatiwa elimu ambayo itawapa uelewa zaidi kuhusu suala la diaspora na umuhimu wake katika maendeleo ya uchumi.

 

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuanzishwa kwa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Shughuli za Wazanzibari wanaoishi nchi za nje kwa lengo la kuwawezesha Wazanzibari wanaoishi za nje kuisaidia nchi yao, kamati yetu inaona kuwa, kuna changamoto za msingi zinazoikabili Zanzibar katika utekelezaji wa Ushirikiano wa Kimataifa na dhana nzima ya Diaspora. Miongoni mwa   changamoto kubwa inayoikabili Zanzibar katika suala la Ushirikiano wa Kimataifa ni kwamba kwa kuwa suala la Ushirikiano wa Kimataifa limewekwa katika masuala ya Muungano, Zanzibar imekuwa ikishiriki katika Vikao vya Kikanda na vya Kimataifa kwa mwa mvuli wa Muungano huku ikichukuliwa kama vile kushiriki kwake katika vikao hivyo sio suala la lazima bali ni ihsani ya Jamhuri ya Muungano. Baya zaidi katika vikao hivyo kuna mambo yanayojadiliwa na kupitishwa si ya Muungano lakini bado Zanzibar inashiriki kwa mwa mvuli huo ambao kwa muda mrefu sasa umeonekana kuwa ni kero kwa wananchi wa Zanzibar.

 

Mheshimiwa spika, kwa kuwa kuna mchakato wa utoaji wa maoni ya uundwaji wa Katiba mpya, kuna umuhimu kwa Wazanzibari kuhakikisha kuwa masuala ya Mambo ya Nje yanakuwa si ya Muungano ili Zanzibar iwe na uwezo wa kushiriki katika vikao mbali mbali ikiwa nchi kamili.

 

KITENGO CHA USALAMA WA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, kitengo cha Usalama wa Serikali kimepewa Majukumu muhimusana kwa lengo la kuimarisha usalama katika taasisi na vituo muhimu vya Serikali. Hata hivyo, Kitengo hiki, mbali na jitihada kinazozichukua katika kutekeleza majukumu yake, hakipatiwi fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza kazi ilizopangiwa. Aidha, kitengo hiki hakina usafiri wa kufuatilia kazi zao, ingawa kwa mujibu wa Bajeti ya mwaka 2012/2013, kimetengewa fedha kwa ajili ya usafiri. Kamati inaisistiza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kukipatia kitengo hiki fedha za kutosha ili kiweze kutekeleza kazi zake kwa ufanisi zikiwemo kazi za kuyakagua majengo ya Taasisi za Serikali yaliyopo Tanzania Bara, ambayo yanashindwa kukaguliwa kutokana na ukosefu wa fedha. Aidha, kamati inaona kuwa kuna haja kwa kitengo hiki kupatiwa usafiri wa gari na vespa ili kiweze kufuatilia kwa ufanisi kazi ilizopangiwa. Kamati pia inaiomba Serikali kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kukisaidia kitengo hiki kwa kukiwezesha watendaji wake kupatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili nao waweze kuimarisha utendaji wao.

 

Mheshimiwa Spika, kamati kwa mara nyengine inakikumbusha Kitengo cha Usalama wa Serikali kuhakikisha kuwa Taasisi zote za Serikali zinafuata Sheria na taratibu kwa kuhakikisha kuwa Watumishi wa Serikali wanaajiriwa baada ya kufanyiwa upekuzi kwa maana ya “Vetting”. Kamati kwa upande mwengine inaona kuwa kuna haja kwa Serikali kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa kigeni wanaofanya kazi katika sekta binafsi nao wanafanyiwa upekuzi kwa lengo la kuimarisha usalama katika sehemu wanazofanyia kazi pamoja na nchi kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, kuna umuhimu mkubwa suala hili likafanyiwa kazi ili kuweza kuzifahamu tabia za wafanyakazi hao wanaofanyakazi katika sekta binafsi ili tuepukane na madhara yanayoweza kutokea.

 

Mheshimiwa Spika, kamati imebaini kuwa Sheria ya Upekuzi kwa wafanyakazi ina mapungufu kwa maana kitengo cha Usalama wa Serikali (GSO) kinapobaini kuwa kuna udanganyifu umefanyika katika suala la upekuzi wa wafanyakazi wapya, wao hutoa ushauri tu kuwa wafanyakazi hao wasiajiriwe lakini Sheria haianishi waajiri na waajiriwa waliodanganya katika zoezi zima la uajiri wachukuliwe hatua gani. Mheshimiwa Spika, kamati yetu inapendekeza Sheria hiyo kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kukiwezesha Kitengo cha Usalama wa Serikali kuweza kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki katika udanganyifu wa ajira.

 

Mheshimiwa Spika, katika kuunganisha suala la usalama katika utekelezaji wa Sughuli za Serikali, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya Taasisi za Seriakali wahasibu na washika fedha wao huchukua pesa za mishahara kutoka benki bila ya kuwepo Uinzi wa Polisi, ambao kupatikana kwake huwa hauna gharama yoyote ile.Mheshimiwa Spika, Suala hili kiusalama ni hatari na halikubaliki. Hivyo, kamati inaziagiza Taasisis za Serikali kuhakikisha kuwa pesa za mishahara zinazochukuliwa benki zinakuwa na ulinzi wa polisi. Aidha, Kamati inaziagiza Taasisi za Serikali kuhakikisha kuwa watumishi wao wakiwemo washika fedha na wahasibu kutozilaza funguo za ofisi majumbani mwao ili kuepuka uwezekano wa upotevu wa funguo hizo. Kamati inazishauri taasisi za Serikali kuweka sehemu maalum za kuweka funguo hizo (combination lock.) Kamati pia inaona kuwa kuna umuhimu katika milango ya wahasibu na washika fedha kuwekwa milango ya “Grills” kwa lengo la kuimarisha usalama katika ofisi hizo. Kamati yetu bila ya kusahau inazikumbusha Tasisi za Serikali kuweka vifaa vya kuzimia moto “Fire Extinguishers” katika majengoyao ili ziweze kukabiliana na maafa ya moto yanayoweza kutokea.

 

OFISI YA USAJILI NA KADI ZA UTAMBULISHO

Mheshimiwa Spika, kamati inaipongeza Ofisi hii kwa kuendelea na jukumu la kusajili na kutoa Vitambulisho vya Ukaazi vya Mzanzibari. Hata hivyo, kamati inaona kuwa kuna haja ikatolewa elimu zaidi kwa wananchi kwa lengo la kuwahamasisha kuchukua vitambulisho vyao katika vituo walivyopangiwa. Mheshimiwa Spika, tunalisema hili kwa sababu wakati kamati ilipokuwaPemba kikazi ilifahamishwa kuwa kuna idadi kubwa ya wananchi waliokuwa hawajachukua vitambulisho vyao.

 

Mheshimiwa Spika, kamati inaipongeza Ofisi hii kwa kutoa elimu kuhusu kuelimisha matumizi bora ya Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kupitia ZBC TV. Hata hivyo, kuna haja kwa Ofisi hii kutoa elimu hiyo kwa kuvitumia vyombo vya habari zaidi ili elimu hiyo iwafikie wananchi wengi zaidi.

 

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza hatua ya utayarishaji wa Rasimu ya Marekebisho ya Usajili Nambari 7 ya 2005 inayoruhusu Utoaji wa Vitambulisho vya Wageni wanaoishi nchini. Kamati inashauri kuwa marekebisho ya rasimu hiyo yanahitajika kuwa madhubuti ili kuepuka changamoto zilizojitokeza hapo kabla katika suala zima la utoaji wa vibali vya ukaazi kwa wageni wanaoingia nchini.

 

IDARA YA URATIBU WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Waziri inaeleza kuwa Idara hii kupitia Mabaraza ya Halamashauri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imekamilisha utayarishaji wa Sheria ndogo ndogo za Serikali za Mitaa. Kamati inaikumbusha Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuziwasilisha Sheria hizo hapa Barazani ili zipitiwe na Kamati ya Sheria Ndogo Ndogo ambayo imejumuishwa katika Kanuni mpya za Baraza, toleo la mwaka 2012.

 

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Mradi wa ZUSP kwa kununu vifaa kama vile gari, vespa na Honda kwa ajili ya kuliimarisha Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji Pemba, Idara ya Mipango Miji na Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kamati inaamini kuwa upatikanaji wa vifaa hivyo utaziwezesha taasisi hizi kufanya kazi zao zikiwemo kazi za kusafisha miji kwa ufanisi.

 

Mheshimiwa Spika, kamati vile vile inafarajishwa na maelezo ya kuwa Serikali imekwishaziwasilisha katika Benki ya Dunia hadudi rejea za kumtafuta mshauri wa Kusimamia Uwekaji wa Taa za Barabarani. Mheshimiwa Spika, suala la uwekaji wa taa hizi katika mitaa na miji yetu lina umuhimu wa pekee hasa ikitiiliwa maanani kwamba maeneo mengi ya Manispaa yaZanzibar kutokana na ukosefu wa taa hizo nyakati za usiku huwa hayako salama kwa wananchi wetu.

 

Mheshimiwa Spika, tunaipongeza kwa dhati Serikali kwa kuchukua hatua za kulenga kumtafuta mjenzi wa utanunuzi wa ukuta unaopita pembezoni mwa pwani ya Forodhani bila shaka kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya maeneo hayo na kuweka usalama wa wananchi wanaoutumia maeneo hayo.

 

MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MIKOA

 

Mkoa wa Mjini Magharibi

Mheshimiwa Spika, kamati inatoa pongezi kwa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuwapatia mafunzo mbali mbali Masheha pamoja na Kamati zao za Maendeleo. Bila shaka mafunzo hayo yatawawezesha kutakeleza majukumu yao kwa ufanisi. Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Waziri inaainisha kuwa Mkoa umefanya ziara kufuatilia uharibifu wa mazingira na kufanya vikao na wadau wengine ili kuzungumzia usafi wa mji na uzururaji wa wanyama. Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihda hizo, uharibifu wa mazingira katika Mkoa wa Mjini Magharibi umeenea kila pahala kuanzia nchi kavu hadi baharini. Kamati inataka kuelewa baada ya ufuatiliaji huo, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Mkoa wa Mjini Magharibi imechukua hatua gani katika kudhibiti uharibifu huo katika maeneo hayo hususani maeneo ya Mbuyu Mnene, Amani, Maruhubi, Ukanda wa bahari wa kizingo na kadhalika. Kuhusu suala la usafi kamati inaipongeza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia taasisi zake pamoja na vikundi mbali mbali vya mazoezi na Jumiya zisizo za Kiserkali kwa kuchukua hatua za kuusafisha mji wetu kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi. Hata hivyo, tunaiomba Serikali kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuongeza vifaa vya usafishaji kwa lengo la kuimarisha usafi katika miji yetu.

 

Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa malengo ya Mkoa kwa mwaka 2012/2013 ni kutatua migogoro ya ardhi inayoukabili Mkoa. Kamati inataka kufahamu kwa mwaka 2011/2012, Mkoa ulikuwa na migogoro mingapi ya ardhi na mpaka sasa imeshaitatua migogoro mingapi? Mheshimiwa Spika, tunalisema hili kwa sababu suala la migogoro ya ardhi limedumu kwa miaka mingi sasa na kila mwaka liwekwa kama ni malengo ya Mikoa na taasisi nyenginezo. Mheshimiwa Spika, kamati yetu ina wasi wasikama migogoro hiyo itaweza kutatuliwa kwa sababu kuna shutuma kwamba migogoro hiyo inawahusisha baadhi ya wale waliopewa madaraka katika Mikoa, Wilaya na Shehia. Hivyo, kamati inashauri kuna haja migogoro hiyo ikatatuliwa na watu au taasisi ambazo hazikuhusika ama kushutumiwa kuwemo katika migogoro hiyo.

 

Mheshimiwa Spika, ofisi ya Mkuu wa Mkoa inaanza matayarisho ujenzi wa jengo jipya la Ofisi yake huko Amaan na kufanya matengenezo ya jengo la ofisi yake hapo Vuga. Kamati inapongeza hatua hizo zinazotaka kuchukuliwa na Ofisi hii. Lakini kamati yangu haifurahishwi na matumizi mabaya ya eneo la mbele ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi hapo Amani kwa kuwekwa yadi ya Magari jambo ambalo limeharibu mandhari nzima ya eneo hili. Kamati inaikumbusha Serikali  kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  kuwa na mkakati wa  kujenga Majengo mapya na ya kisasa ya Serikali kwa Wakuu wa Mikoa na taasisi za Serikali ili kuwawezesha wafanyakazi wa taasisi hizi kufanyakazi katika mazingira mazuri. Mheshimiwa Spika, .Kuna haja kwa Serikali kuwa makini na suala la kupanga utekelezaji wa ujenzi wa majengo mapya ya taasisi za Serikali, vyenginevyo kuachiwa taasisi moja pekee kutaka kujenga jengolakekwa kutegemea pesa za Matumizi Mengineyo, kutapelekea ujenzi wa nyumba hizo kuchukuwa muda mrefu hadi kukamilika kwake.

 

Mkoa wa Kaskazini, Unguja

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini, Unguja, kamati inautaka Mkoa huu kulitekeleza suala la kusimamia shughuli za Ulinzi na Usalama kwa vitendo kwa sababu katika eneo la Mkoa huo kumejitokeza vitendo vingi vya uhalifu katika baadhi ya hoteli za kitaalii jambo ambalo linatishia usalama wa wenyaji na wageni kwa maana ya watalii na mali zao. Aidha, kuna haja kwa Mkoa huu kusimamia masuala ya ulinzi na usalama kwa vitendo kwa kuwa katika Mkoa huu kuna baadhi ya maeneo zipo bandari bubu zinazotumika kusafirisha na kuingiza wageni kinyume na Sheria na taratibu.

 

Mheshimiwa Spika, kamati yetu inaukumbusha Mkoa huu kuhakikisha kuwa vibanda vilivyojengwa katika fukwe za bahari pembezoni mwa hoteli za kitalii vinabomolewa kwani vinaharibu mazingira ya fukwe lakini pia vinaikosesha Serikali mapato kwa kuwa tumebaini kuwa vibanda hivi vimejengwa kwa maslahi ya wenye hoteli na pengine baadhi ya watendaji katika Ofisi za Wilaya na Mikoa.

 

Mkoa wa Kusini, Unguja

Mheshimiwa Spika, kamati inaupongeza Mkoa huu kwa kuwa na jengolakeambalo hivi sasa linatumika kwa shughuli za ofisi. Tunaiomba Mikoa mengine iige mfano wa Mkoa huu kwa kuwa na majengoyao ya kisasa. Hata hivyo, Kamati yetu inauagiza Mkoa wa Kusini kupitia kamati yake na Ulinzi na Usalama kufuatilia kwa kina masuala ya ulinzi na usalama katika Mkoa huo  kwani kumebainika kuwa kuna baadhi ya wenyeji na hata wageni wanamiliki nyumba wanazikodisha kinyume na Sheria kwa wageni na kupelekea kutishia usalama wa Mkoa na kuikosesha Serikali mapato.

 

Mheshimiwa Spika, kamati pia inauagiza Mkoa huu kuhakikisha kuwa vibanda vyote na miamvuli iliyojengwa katika fukwe za bahari na kupelekea kuharibu mazingira vinabomolewa mara moja kwa lengo la kdhibiti mazingira katika maeneo hayo. Aidha, kamati inauagiza Mkoa wa Kusini Unguja kwa kushirikiana na Ofisi za Wilaya na Masheha, Idara ya Ardhi kuhakikisha kuwa nyumba zote walizokodishwa wageni zinaorodheshwa na kutoa taarifa  Polisi,Uhamiaji, Zipa, na ZRB ili kila taasisi iwajibike kwa lile linalowahusu. Pia kamati yangu inazitaka Ofisi zote za Wakuu wa wilaya kushirikiana na masheha kuzibua njia zote zilizozibwa na wawekezaji za kuteremkia Pwani ili wananchi kuweza kupita kwa urahisi wanapokwenda na shughuli zao mbali mbali za kiuchumi na kawaida huko pwani.

 

Mheshimiwa Spika, kamati pia inawakumbusha Viongozi katika Mkoa, Wilaya na Shehia za Mkoa wa Kusini kuhakikisha kuwa mapato yanayokusanywa katika hoteli za kitalii yanasimamiwa ipasavyo kwa lengo la kufaidisha Serikali na wananchi wake. Mheshimiwa Spika, kamati inalikumbusha suala hili kwa viongozi hawa kwa kuelewa kuwa katika Mkoa wa Kusini, mapato yanayotokana na kodi ya hoteli za kitalii yanavuja kutokana na kutosimamiwa vyema na viongozi hao. Kamati yetu pia inawakumbusha viongozi hawa kuwa kwa mujibu wa Sheria za Kodi wanatakiwa wajielewe wao ndio wasimamizi wa kodi ktika maeneoyao.

 

Mheshimiwa Spika, kutokana na udhaifu unaoneshwa na baadhi ya viongozi hao na wengineo pamoja na baadhi ya watendaji wa Serikali wanaopelekea kupotea kwa mapato ya Serikali, kamati inashauri pale inapobainika kutokea kwa upotevu huo, hatua za kisheria zinafaa zichukuliwe kwa wahusika. Aidha, kamati inashauri kuwa somo la kodi liingizwe katika mitaala ya skuli za sekondari ili kuwawezesha wananchi kuyajua majukumuyao ya kulipa kodi tangu wakiwa wadogo, vyenginevyo wananchi wengi huwa hawana utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari zao lakini pia huchangia kuwasaidia wageni nao kwa njia moja au nyengine kushiriki kutolipa kodi.

 

 

 

Mkoa wa Kusini, Pemba

Mheshimiwa Spika, kamati inaupongeza Mkoa wa Kusini Pemba kwa jitihada inazozichukua katika kutekeleza majukumu iliyojipangia likiwemo jukumu la kuwa na mpango wa kujenga nyumba ya Mkuu wa Mkoa, kuanza matayarisho ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chake na kununua jengo kwa ajili ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani. Mheshimiwa spika, jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Pemaba kiukweli halina hadhi ya kuwa Ofisi ya Mkoa. Aidha, haipendezi kwa Mkuu wa Mkoa kutokuwa na nyumba ya Serikali na badala yake kutegemea nyumba ya kukodi ambayo bila shaka huwa na gharama zake. Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa nyumba na Ofisi za Serikali kwa Viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya lina umuhimu wa pekee na linahitaji kutekelezwa kwa vitendo, vyenginevyo suala hili litaishia kwa kuelezwa katika Hotuba mbali mbali za viongozi pasina kutekelezwa. Mheshimiwa Spika, kamati yetu inaona kuwa, mbali na jitihada za Serikali kuzitengea pesa taasisi zake kwa ajili ya ujenzi wa Majengo ya Serikali, kiuhalisia pesa hizo hazitoshi katika kufanikisha ujenzi wa majengo ya kisasa na yanayokubalika kiofisi na hasa ikitiiliwa maanani katika miaka hii tuliyonayo wakati gharama za ujenzi zinapanda kila leo, bajeti ya majengo na masuala mengine ya maendeleo inapungua. Kamati yetu bado ina mashaka kuwa ujenzi uliokusudiwa, utaendelea kutekelezwa kwa utaratibu ule ule uliozoeleka wa Ofisi hii na nyenginezo kusubiri pesa za Matumizi Mengineyo kila baada ya mwezi ama miezi. Ukweli ni kuwa pesa za Matumizi Mengineyo hazina uwezo wa kujenga jengo linalohitajika kiofisi bali litajengwa jengo la kubahatisha, lisilovutia na ukamilkaji wake huchukua miaka na miaka.

 

Mheshimiwa spika, kamati yetu haitochoka kupiga mayowe hapa Barazani kuhusu Serikali kuwa “serious” katika kuhakikisha kuwa linakuwa na Mradi utakaotekelezwa kwa Ujenzi wa nyumba na ofisi mbali mbali za Serikali. Mheshimiwa Spika, suala hili linawezekana ikiwa Serikali itafikiria kukaa kitako na kuwatafuta marafiki wetu wa kweli kwa maana ya Wachina na wengineo ili waangalie uwezekano wa kutusaidia.

 

Mkoa wa Kaskazini, Pemba

Mheshimiwa spika, kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini, Pemba, ingawa jengo lao ni la kale, angalau wanafanya kazi zao katika eneo linalotizamika. Hata hivyo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kaskazini, Pemba, ni miongoni mwa Ofisi za Wakuu wa Mikoa ambazo zinakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na Watumishi wa Serikali kwa maana ya wawakilishi kutoka taasisi mbali mbali za Serikali, hali ambayo imepelekea kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Mheshimiwa Spika, kamati inaishauri Serikali, ili kuitafutia ufumbuzi changamoto hii, kuweka mipango ya kuhakikisha kuwa Ofisi za Mikoa na Wilaya zinakuwa na watumishi wa kutosha kutoka kila taasisi inayohitajika.

 

MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

 

Baraza la Manispa,

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza jitihada zinazochukuliwa na Baraza la Manispaa katika kutekeleza majukumu yake yakiwemo majukumu ya kusimamia na kuimarisha usafi katika Manispaa ya Zanzibar. Kamati inalitaka Baraza hili kuendelea na jitihada hizo ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa Rwanda ya pili katika masuala ya usafi. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ili Baraza hili liweze kufikia lengo la kuhakikisha kuwa Manispaa yetu inakuwa katika mazingira ya usafi tunayoyataka, kunahitajika mashirikiano ya dhati kati ya Baraza la Manispaa na wadau wengine kama vile Serikali kuu, vikundi mbali mbali vinavyotunza mazingira na masuala ya usafi, viongozi pamoja na wananchi kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, tunalianisha hili kwa sababu wengi wetu tuna fikra suala la kusafisha Manispaa na kuimarisha mazingira ni la Baraza la Manispaa pekee na kushau kuwa wadau wengine mbali mbali nao wanahitajika kuhakikisha kuwa wanachangi nguvu zao kwa kuhakikisha kuwa wanasafisha maeneo yao kwa lengo la kutunza mazingira. Serikali kwa upande wake inahitajika kulisaidia Baraza hili kwa kulipatia vitendea kazi vya kutosha na maslahi bora kwa watumishi ili Baraza liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, Serikali inahitajika kulisaidia Baraza la Manispaa kwa kuliachia vianzo vya mapato ambavyo vitaliwezesha Baraza kujiendesha. Hata hivyo, kuna umuhimu mkubwa kwa Baraza la Manispaa kujielewa kuwa mapato ya Serikali si mali ya mtu bali ni mali ya Serikali. Hivyo lihakikishe kuwa kodi zinazokusanywa ni kwa ajili ya maslahi ya wananchi wetu

 

Mheshimiwa spika, katika kazi zake, mwezi wa Mei mwaka huu. Kamati yetu ilipata fursa ya kukutana kwa pamoja na Uongozi wa Baraza la Manispaa na vikundi vinavyojihusisha na masuala ya utunzaji mazingira na masuala ya usafi kwa lengo la kubadilishana mawazo na kuhamasisha utekeleza wa dhana ya Ushirikishwaji wa Pamoja kati ya Sekta ya Umma, na Binafsi (PPP). Kamati kwa ujumla imefarajishwa na matokeo ya kikao kile kwa sababu kimepelekea washiriki wa kikao hicho sio tu kuilewa dhana hiyo bali pia kujenga mashirikiano katika shughuli zao za utunzaji mazingira na masuala ya usafi.

 

Mheshimiwa spika, ili kufanikisha kwa pamoja shughuli za Serikali kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali na Jamii kuhamasisha utekeleza wa dhana ya Ushirikishwaji wa Pamoja kati ya Sekta ya Umma, na Binafsi (PPP). Hivyo, kamati yetu inatoa wito kwa Serikali na jamii kutoa elimu kwa viongozi, watendaji wa Serikali na wananchi kwa ujumla ili kuweza kuielewa dhana hii mpya. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna haja kwa Serikali kuijengea uwezo sekta binafsi ili iwe nayo iwe na uwezo wa kuitekeleza kwa ufanisi dhana hii.

 

Mheshimiwa spika, kamati inalitaka Baraza la Manispaa kuwa na utaratibu mzuri katika utekelezaji wa miradi kati wadi mbali mbali zilizopo katika Manispaa ya Zanzibar. Kamati inalianisha hili kwa sababu imekuwa na mashaka kuwa Baraza limekuwa likitoa fedha za miradi hiyo lakini utekelezaji wa miradi hiyo huwa hauonekani.

 

Mheshimiwa Spika, kuna haja kuwashirikisha madiwani na masheha katika Utekelezaji wa Miradi katika wadi ili kuhakikisha ufanikishaji wa miradi   hiyo.

 

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza jitihada zinazofanywa na Halamashauri na Mabaraza ya Miji mbali mbali Unguja na Pemba. Hata hivyo, mbali na jitihada zinazofanywa na taasisi hizi, Halmashauri na Mabaraza mengi ya Miji yanakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile ukosefu wa wataalamu hususani wanasheria na watoza kodi, ukosefu wa vitendea kazi, kuchelewa kukamilika kwa Mabadiliko ya Sheria ya Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Miji, kukosekana kwa mashirikiano kati yao na taasisi nyengine za Serikali katika suala zima la ukusanyaji mapato na udhibiti wa mazingira. Hali hii kwa ujumla inazipelekea tasisi hizi kutofanya kazi zao kwa ufanisi hususani katika suala la ukusanyaji wa kodi.

 

IDARA YA URATIBU WA IDARA MAALUM ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

 

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inavipongeza vikosi vyote vya SMZ kwa kazi kubwa wanazofanya kwa kusaidia ulinzi katika Nchi yetu, lakini pia kushiriki katika kujenga uchumi wa Nchi yetu. Hata hivyo, kamati yetu inaikumbusha Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa suala la nyongeza za mishahara katika Vikosi vya SMZ bado ni tatizo kwa maana wapo walioongezwa lakini nyongeza hiyo ni ndogo lakini nyongeza hizo hazikuzingatia muda wa mtu kuwepo kazini kwa maana mpiganaji mwenye cheo cha koplo ambaye amekipata cheo hicho leo hii, mshahara wake utakuwa sawa na koplo aliyedumu katika cheo hicho kwa miaka mingi. Mheshimiwa Spika, hili ni tatizo ambalo ukweli limechangiwa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutekeleza majukumu ya kurekebisha mishahara ya vikosi na taasisi nyenginezo bila ya kuzishirikisha Tume za Utumishi za taasisi husika. Mheshimiwa Spika, kamati yetu bado inaisisitiza Serikali kufanya marekebisho hayo kwa kuwapatia wapiganaji wetu haki zao za msingi wanazozidai. Aidha, kamati inaishauri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwapatia “salary sleeps” mara baada ya kulipwa mishaharayao ili kuepusha malalamiko miongoni mwa wapiganaji.

 

Kikosi cha Zima Moto na Uokozi

Mheshimiwa Spika, kamati inazipongeza kwa dhati kazi zinazotekelezwa na kikosi hiki. Aidha, kamati inakipongeza kikosi hiki kwa kupatiwa eneo la Mwanakwerekwe ili kiweze kutanua shughuli zake. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla kikosi hiki kinafanya kazi kubwa usiku na mchana kwa lengo la kufanya uokozi wa aina mbali mbali. Hata hivyo, kikosi hiki kinakabiliwa na changamoto kadhaa na miongoni mwa hizo ni ukosefu wa vitendea kazi, kutoshirikishwa na Idara ya Ardhi pamoja na jamii katika masuala ya ujenzi wa nyumba ili kiweze kutoa ushauri wake, kupewa mawasilano ya uongo na baadhi ya wananchi, hali ambayo inapelekea kupoteza mafuta ambayo nayo hayatoshelezi kwa matumizi ya kikosi. Changamoto nyengine kwa kikosi hiki ni kutokuwa na majengo katika maeneo ya Viwanja vya ndege na kupelekea kufanya kazi katika mazingira magumu.

 

Mheshimiwa Spika, kamati yetu kwanza inaipongeza Serikali kwa kukiongezea kikosi hiki fungu la pesa kwa mwaka 2012/2013. Hata hivyo, kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kukifikiria kikosi hiki kadri inavyowezekana kwa kukipatia pesa zaidi ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.

 

Mheshimiwa Spika, kamati inaiomba Serikali kukiwezesha kikosi hiki kwa kukipatia majengo ya kudumu katika maeneo ya uwanja wa ndege ili kiondokane na usumbufu uliopo.

 

 

Jeshi la Kujenga Uchumi (J. K.U)

Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza jitihada zinazofanywa na kikosi hichi kwa kuendeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Lakini pia kikosi kinapongezwa kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana wanaojitolea kupitia kikosi hichi ambao ni nguvu kazi ya taifa letu.Mbali na hayo kikosi kinakabiliwa na changamoto ikiwemo madeni wanayodaiwa na wafanyabiashara binafsi, ukosefu wa hati miliki katika maeneo yao, ukosefu wa umeme kwa baadhi ya kambi pamoja na vitendea kazi, huduma duni kwa vijana wanaojitolea katika kikosi na uhaba wa bajeti hali ambayo inapelekea kukwama kwa baadhi ya malengo waliojipangia.

 

Mheshimiwa Spika, kamati yangu kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inaomba Serikali kukiangalia kikosi hichi kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba ya kamanda huko Pemba, kuimarisha mashamba yao kwa kuchimba visima kwa ajili ya umwagiliaji maji,pamoja na kuwafikiria vijana wanaojitolea kwa kuwaajiri inapotokezea nafasi za ajira ili kuwatia moyo na wengine kuweza kujitolea.

 

Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo (K.M.K.M)

Mheshimiwa Spika, tunatoa pongezi kwa kikosi Kikosi cha KMKM kwa kujiimarisha kwa kukipatia wataalam waliokuja kutoa mafunzo kwa ajili ya uokozi pamoja na kuongeza vifaa vya kuzamia jambo ambalo litasaidia kuwa na nyenzo za kuokolea pale maafa yatakapotokea. Pia kikosi hiki kinakabiliwa na uchakavu wa majengo yake ambayo huwafanya baadhi ya Askari wake kuishi katika mazingira magumu kwenye majengo ambayo hayastahiki kuishi Askari. Changamoto nyingine tulioiona ni kuwepo kwa rasilimali ya chelezo hapo Kibweni. Kamati yangu inaitaka Serikali kukitengeneza chelezo hichi ili kuongeza mapato na pia kurahisisha matengenezo ya vyombo vyao. Kamati yangu bado inakitaka kikosi kuwa na kitengo cha kuzamia katika kisiwa cha Pemba ili kusaidia uokozi pindipo itakapo tokea maafa. Changamoto nyingine ni upungufu wa mafuta ya kufanyia Doria kwani maumbile ya kazi yao ni kulinda baharini.

 

Idara ya Chuo Cha Mafunzo

Mheshimiwa Spika, Kamati inathamini kazi zinazofanywa na Chuo cha Mafunzo. Hata hivyo, pamoja na kazi kubwa zinazotekelezwa na Chuo hiki, Chuo cha Mafunzo kinakabiliwa na changamotokama vile kuwa na uhaba wa pesa zinazoingiziwa kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa. Hali hii husababisha Chuo kupata mzigo mkubwa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya mahabusu ukilinganisha na idadi ya wanafunzi (wafungwa). Hivyo, tunaitaka Serikali kuongeza fungu hili ili kuweza kukidhi mahitaji ya chakula kwa wafungwa na na mahabusu. Pia kamati yangu inaitaka Serikali kupitia Kikosi cha mafunzo kujenga magereza yanayokwenda na wakati kwani haya yaliyopo yamepitwa na wakati na mazingira yake hayaridhishi kiafya. Pia tunaomba kujengwa majengo maalum ya watoto ili wasichanganywe na wanafunzi watu wazima,

 

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inaiomba Serikali kupitia Chuo cha Mafunzo kuyafanyia ukarabati mkubwa majengo wanayoishi Askari, Unguja na Pemba kwani mengi yao yamezeeka na kuchakaa sana. Pamoja na hayo kamati yangu imepata malalamiko kutoka kwa baadhi ya Askari kuwa kuna baadhi yao wamepewa barua za uhamisho kutoka Pemba kuja Unguja lakini wanaambiwa wajitegemee kwa kuwa hakuna pesa za uhamisho.  Sasa Mhe Waziri, ukija hapa kutujibu tunaomba jawabu katika hilo. Pia Kamati yangu inaitaka Serikali kupitia ushauri wa kamati kuwa Askari wote wa Vikosi vya SMZ wasilazimishwe kukatwa pesa katika mishahara yao bila ya kushauriwa kwani mshahara ni haki ya muajiriwa na inabidi kila atakachokatwa basi iwe ni lazima kwa mashauriano na muajiri wake, Mheshimiwa Spika, kamati yangu pia inaitaka Serikali kupitia chuo cha mafunzo, kuwapeleka mawakili ili kwenda vyuo vya Mafunzo kuwasaidia wanafunzi kukata rufaa kwa wale wanaohitaji.

 

Kikosi cha Valantia, Zanzibar (KVZ)

Mheshimiwa Spika, kamati vile vile inakipongeza kikosi hichi kwa kazi kubwa wanazozifanya hasa katika suala la kuimarisha ulinzi kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini, lakini tunaomba uongozi wa kikosi hicho kwanza wao wenyewe viongozi wakuu, wawe na maelewano makubwa kwani bila ya mashirikiano yao basi, kikosi kitayumba. Kamati yetu pia inaitaka Serikali kumtafutia makaazi yanayostahiki Mkuu wa kikosi hiki kwa upande wa Pemba kwani kumpatia chumba kimoja yeye na familia yake ni kumdhalilisha kwa hiyo tunaomba suala hili lifanyiwe kazi mara moja. Pia kamati yangu inakitaka kikosi kutafuta hati miliki za maeneo yao yote ya kambi zao kwani tumegundua kuwa maeneo mengi ya kikosi hayana hati miliki. Pia kamati inakiomba kikosi hiki kupatiwa vitanda na magodoro kwa Unguja na Pemba kwani katika baadhi ya kambi mfano mzuri Pemba maofisa na askari wanalala chini. Hili ni jambo la kusikitisha Mheshimiwa Spika, nani kati yetu sisi anataka alale chini bila ya godoro? Kamati yetu pia inaishauri Serikali kukisaidia kikosi hiki kwa upande waPemba kwa kukipatia pesa ili kilipe madeni mengi inayodaiwa.

 

Mheshimiwa spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru kwa mara nyengine na nawashukuru Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa kunisikiliza kwa makini.

 

Mheshimiwa spika, baada ya maelezo hayo, naomba nitamke kwamba, kwa niaba ya Kamati yetu naunga mkono hoja mia kwa mia.

 

Mheshimiwa spika, naomba kuwasilisha.

 

                                    …………………………..

                                    Mhe Ali Salum Haji

Kny: Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa

                             Baraza la Wawakilishi

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Advertisements

SMZ YAKANUSHA KUSAJILI MELI ZA 10 ZA IRAN

 

Waziri wa miundo mbinu na mawasiliano Zanzibar Hamad Masoud

Serikali ya mapinduzi Zanzibar imekanusha taarifa za vyombo vya habari zinazodai zimesajili meli 10 za kampuni za mafuta zinazofanya biashara na Iran ambayo imewekewa vikwazo vya kimataifa kusafirisha mafuta duniani.

        Taarifa hiyo ya serikali imekuja baada gazeti la Citzen la jana na shirika la habari la International News kuripoti meli 10 za mafuta za Iran zimesajiliwa Zanzibar na kupeperusha bendera ya Tanzania.

Waziri wa miundo mbinu na mawasiliano Hamad Masoud amesema taarifa hizo zilizochapishwa na vyombo hivyo hazina ukweli na lengo lake ni kuwavunja moyo wamiliki wa meli za kigeni kusajili meli zao Zanzibar.

Amesema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita Zanzibar ilisajili meli 11 kutoka nchi za Cyprus na Malta zenye uzito wa zaidi ya tani milioni 1.3 ambazo wamiliki wa kampuni za meli hizo hawana uhusiano wa kibiashara na makampuni ya mafuta ya Iran.

Waziri Hamad amesema suala la usajili wa meli za kigeni sio la muungano hivyo Zanzibar inahaki ya kusajili meli hizo kwa lengo la kuimarisha uchumi

        Aidha waziri Hamad amesema serikali itaendelea kufanya mazungumzo na wamiliki wa meli duniani ili kuongeza idadi ya meli zinazosajili nchi za nje katika juhudi za kuimarisha mapato.

        Amefahamisha taarifa za Zanzibar za kupokea maombi matano ya kusajili meli za kigeni zenye uzito wa zaidi ya tani laki tano imeshitua makampuni mengi na nchi nyingine zisizoitakia mema Zanzibar.

        Mamlaka ya usafiri wa vyombo vya baharini Zanzibar kupitia wakala wake imesajili meli mia tatu na 96 zikiwemo meli za mafuta, mizigo na abiria.

        Nchi ya Iran na makampuni ya mafuta yanayofanya biashara na Iran yameekewa vikwazo na nchi za Magharibi na Marekani kusafirisha mafuta dunaini kwa madai nchi hiyo inajishughulisha na utengenezaji wa silaha za nyuklia.

        Hivi karibuni Marekani ilitishia kupunguza misaada yake kwa nchi ya India kufuatia nchi hiyo kufanya biashara ya mafuta na Iran.

SOMA HOTUBA KAMILI YA WAZIRI HAMAD

 

TAARIFA KWA BARAZA LA WAWAKILISHI JUU YA

USAJILI WA MELI ZA NJE  ULIOFANYWA NA SMZ

KUPITIA MAMLAKA YA USAFIRI BAHARINI

ZANZIBAR MARITIME AUTHORITY  – ZMA

 

Mhe. Spika,

 

Tarehe 27/06/2012 Vyombo vya Habari hapaTanzania(The Citizen) na nchi za nje (International news Agency – Bloomberg) viliandika makala kuhusu usajili wa meli 10 za mafuta (Tankers).  Ilidaiwa katika makala hayo kuwa Meli hizo zilisajiliwaZanzibarna zinapeperusha Bendera yaTanzaniana kwamba zinafanya biashara na Kampuni ya Serikali yaIRAN.  Gazeti la “The Citizen la tarehe 27 Juni, 2012 lilikuwa na kichwa cha habari “Iran Tankers adopt TZ Flag to avoid embargo” (meli za mafuta za Iran zinatumia bendera ya Tz kukwepa vikwazo.

 

TAARIFA YA ZMA

 

Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar Maritime Authority – ZMA ni Mamlaka iliyoundwa kwa sheria No. 3 ya mwaka 2009 ambayo pamoja na kazi nyengine inasimamia utekelezaji wa Sheria ya usafiri wa Bahari Zanzibar ya mwaka 2006 (Zanzibar Maritime Transport Act 2006).

 

Sheria ya Zanzibar Maritime Transport Act 2006, kifungu no. 8 cha sheria hii, kinasomekakamaifuatavyo:

 

Section 8 (1). There shall be established the registers of   Tanzania Zanzibar ships           to be Known as:-

  • (a). Tanzania Zanzibar International Register of Shipping for ocean going ships; and
  •  (b) Tanzania Zanzibar Register of Shipping for coastal   Ships.
  •      (2). A ship shall be a Tanzania Zanzibar ship for the purpose of       this Act if that ship is registered under this part.

Katika kutekeleza jukumu la usajili wa meli kama ilivyoelekezwa katika kifungu 8(1)(a) hapo juu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetiliana mkataba na kampuni ya PHILTEX yaDubaikufanya usajili wa meli za kimataifa. (Open Registry). Usajili huu umekuwa ukifanyika tangu mwaka 2009 na mpaka sasa ZMA kupitia Wakala wake imesajili meli 399 ikiwa ni pamoja na meli za mafuta, makontena, General cargo na meli za Abiria.

 

Kama nilivyoeleza hapo awali, vyombo vya habari vimechapisha makala ya usajili wa meli 10 ambazo zinadaiwa ni meli zaIRANkulingana na makala zao hizo.

 

SMZ inatoa taarifa rasmi juu ya meli za mafuta ilizosajiliwa wiki mbili zilizopita pamoja na majina ya meli, ukubwa wake, majina ya makampuni inayomiliki meli hizo na nchi zilizotoka kabla ya kupata usajili kwa ZMA,kamaifuatavyo:

 

Jina la meli          GRT (Ukubwa)     Company name              Ilikotoka

 

1. Daisy                      81479              Daisy Shipping Co. Ltd                       Malta

2. Justice                  164241             Justice Shipping Co. Ltd                     Cyprus

3. Magnolia               81479               Magnolia Shipping Co. Ltd                  Malta

4. Lantana                 81479               Lantana Shipping Co. Ltd                   Malta

5. Leadership           164241              Leadership Shipping Co. Ltd              Cyprus

6. Companion           164241             Companion Shipping Co. Ltd               Malta

7. Camellia                81479              Camellia Shipping Co. Ltd                    Malta

8. Clove                     81479              Clove shipping Co. Ltd                          Malta

9. Courage                163660            Courage Shipping Co. ltd                      Cyprus

10. Freedom             163660             Freedom shipping Co. Ltd                    Cyprus

11. valor                   160930             valor Shipping Co. Ltd.                         Cyprus

 

Jumla ya GRT ni 1,388,368 tons

 

Meli hizi ni 11kamazinavyoonekana katika orodha hapo juu ni miongoni mwa meli nyingi zinazobadilisha usajili wao (De registration). Meli zilizosajiliwa na ZMA zinatoka nchiniCyprusnaMalta.  Sambamaba na meli hizi 11 zilizosajiliwa na ZMA, meli za mafuta nyengine 20 ambazo zinasemekana zilikuwa kwenye usajili wa nchi za Ulaya zimebadilisha usajili wao na kwenda usajili wa “TUVALU Islands”.

 

ZMA ilimtaka Wakala wake Philtex Corporation kuwaita wenye meli hizi na kuwataka kujieleza kuhusu uhusuiano wao na Serikali ya au makampuni ya mafuta ya  IRAN. Philtex ilikutana na Wamiliki hao siku ya Alkhamis tarehe 28/06/2012 katika afisi za Philtex Corporation na Wamiliki hao wameeleza kwamba hawana uhusianao na Serikali au mamlaka yoyote nchini Iran na wameamua kuja kusajili meli ZMA kwa ridhaa yao na kwa kufata matangazo ya usajili wetu wa nje (Open Registry).

 

Pamoja na maelezo hayo, wamiliki hao wametangaza kwamba ikiwa ZMA haiko tayari kuendelea na usajili wa meli zao, wanaweza kufuta usajili wao na tayari wanafikiria kufanya mazungumzo na open Registry nyengine (PANAMA) lakini hawana nia ya kurudi walikotoka, yaaniCyprusnaMalta.

 

Kinyume na maelezo yaliyotolewa na vyombo vya habari juu ya uraia wa wamiliki wa meli hizi, Wamiliki wa meli hizi kama walivyojieleza katika usajili wa meli zao wana uraia wa British Vergin Islands na Sychelles.

 

Kulingana na “United Nations Convention Law of the Sea”, Article 91, na za “Geneva convection of Registration” articles 6, 7 na 8, na kulingana na  Zanzibar Maritime Transport Act of 2006, section 8, Zanzibar ikiwa ni nchi moja kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayo haki ya kusajili meli yeyote kulingana na taratibu na Sheria za Zanzibar, na sheria za Kimataifa zinazoongoza usajili huo.

 

Maelezo haya yanatolewa ili kutoa usahihi wa uvumi kuwaZanzibarimesajili meli zaIRANambazo zimewekewa vikwazo na Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya (European Union) juu ya usafirishaji na uuzaji wa mafuta kutokaIran.

 

Mhe. Spika, taarifa hizi za vyombo vya habari hazina madhumuni yeyote zaidi ya kuwavunja moyo wenye Makampuni ya meli wanaotaka kusajili meli zao kwetu.

 

Hivyo basi Serikali inatamka wazi kwamba Usajili uliofanywa kwa meli hizi umefuata taratibu zote zilizowekwa kisheria na kwamba Serikali imekuwa ikifanya na itaendelea kufanya mazungumzo na wenye meli mbalimbali ili kuongeza idadi na ukubwa wa meli inazosajili nje ya nchi.  Biashara hii ya ukubwa wa GRT 1,388,368 Tons katika kipindi cha wiki mbili na maombi mapya matano kwa meli zitakazokuwa na ukubwa wa zaidi ya GRT 500,000 imeshtua Makamuni mengine na hata nchi nyengine zisizoitakia memaZanzibarkatika juhudi zake za kukuza mapato na uchumi wake.

 

Hata hivyo mamlaka itafata sheria zote zilizowekwa kitaifa na kimataifa katika biashara ya usafiri baharini na itahakikisha meli zinasajiliwa chini ya mamlaka hii zinafata taratibu ilizoweka.

 

Mhe. Spika, kabla ya taarifa hizi za vyombo vya habari (The Citizen), Waziri wa Uchukuzi wa SMT Mhe. Harisson Mwakyembe) alipokuwa akijibu suala Bungeni hivi juzi hakuonyesha kurishika kwake katika usajili wa meli (Open Registry) inayofanywa naZanzibarna kuahidi kufanya ziara ya kujaZanzibarkuonana na Waziri anaehusika kuzungumzia suala hili.  Taarifa za “The Citizen” zaweza kuwa ni muendelezo wa Mhe. Mwakyembe kutoridhika kwake katika usajili unaofanywa na Serikali kupitia uwakala wake hukoDubai.

 

Mhe. Spika,Zanzibarhaifungiki kusajili meli za nchi yeyote.

Hili ni suala la kibiashara na kwamba kwa Serikali yetu ni njia moja ya kuongeza mapato yanayoendesha Serikali, alimradi tu usajili huo hauvunji sheria za Kimataifa.

 

 

Mhe. Spika,

 

Zanzibarina uhusiano mkubwa na wa muda mrefu na nchi nyingi ikiwemoIRANna hivi karibuniZanzibarilipata ugeni (Makamo wa Rais waIran) na viongozi wetu walifanya mazungumzo ya namna ganiIRANitaendelea kusaidiaZanzibarkatika miradi ya Maendeleo. Zanzibarhaingependa kuingizwa kwa visingizio vyovyote na kwa njama zozote katika migogoro isiyowahusu.

 

Hivyo, kwa taarifa hii, Serikali inakanusha rasmi uvumi wa vyombo vya habari kuhusiana na suala hilikamataarifa hii ilivyofafanua hapo juu.

 

Mhe. Spika, naomba kuwasilisha.

 

 

 

 

Hamad Masoud Hamad

WAZIRI WA MIUNDOMBINU NA MAWASILIANO

SMZ YASHAURIWA KUANGALIA MAISHA YA KIFAHARI YA MAALIM SEIF

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetakiwa kuangalia matumizi makubwa ya kodi ya nyumba anayoishi makamo wa kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad inayofikia shilingi milioni 10 kwa mwezi.

        Akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya nchi ofisi ya makamu wa kwanza wa rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013 mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu amesema fedha hizo ni nyingi ikilingnishwa na uchumi wa Zanzibar.

        Aidha Jussa amesema makamo huyo pia anatumia fedha fedha nyingi za serikali yeye na ujumbe wake anapolala hoteli wakati akiwa katika ziara zake mjini Dar es Salaam.

        Hivyo mwakilishi huyo ameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kujenga nyumba za viongozi mjini humo ili kuepusha matumizi makubwa ya fedha za serikali kwa kulala mahotelini

DR. SHEIN AWATUNISHIA MISULI MASHEHA NA MADIWANI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa ni jambo la aibu na kusikitisha kuona ukuaji wa majaa na utupaji ovyo wa taka unaendelea katika Shehia hasa Wilaya ya Mjini na Wilaya ya Magharibi wakati Madiwani na Masheha hawachukui hatua zinazopaswa
 
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati alipofungua semina ya uongozi ya viongozi wa Serikali za Mitaa ambayo iliwahusisha Masheha, Madiwani na viongozi wa Halmashauri.
 
Aliendelea kusisitiza kuwa mifugo bado inaachiwa ovyo mijini na pia masikitiko ya wakulima kuharibiwa mazao yao na wafugaji wasojali sheria wala kanuni ziliopo.
 
Dk. Shein alisema kuwa jukumu la viongozi hao pia, ni kuchangia katika kuendeleza utalii nchini ambao unazidi kuwa ni tegemeo kubwa la uchumi lakini Mtalii hatopendelea kurudi katika mji au nchi isiyo safi na isiyojali mazingira yake.
 
Alisema kuwa uchimbaji wa mchanga unaendelea kwa kasi kubwa katika shehia za Wilaya ya Magharibi na Wilaya ya Kati ambapo pia, fukwe za pwani zimekuwa zikiharibiwa kutokana na uchafuzi na ukataji wa mikoko na kusisitiza kuwa hayo yote yanaathiri uchumi, utalii na maendeleo ya Zanzibar.
 
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa utekelezaji wa mipango ya maendeleo unaofanywa na Serikali kupitia Idara na Wizara zake huwa unatekelezwa katika shehia, kwemo upelekaji huduma za afya, elimu, maji na mengineyo na kueleza kuwa Masheha na Madiwani kupitia katika Kamati za Maendeleo za maeneo yao wanahusika na mipango hiyo.
 
Alisema kuwa Masheha na Madiwani pia, wanapaswa kuwa na ushiruki na uhusiano mkubwa katika kutunza amani na usalama ndani ya Shehia zao huku akisisitiza kuwa ulinzi unaotolewa na vyombo vya dola au Polisi Jamii ambao unawpa usala wananchi utafanikiwa tu kwa mashirikiano ya pamoja na jamii.
 
Dk. Shein alisema kuwa semina hiyo imelenga katika kutoa maelekezo ya nyanja mbali mbali za uongozi na kiutendaji lakini italitilia mkazozaidi katika masuala ya ardhi na migogoro yake, utawala bora, mazingira, maadili, uchumi na utalii kwa wote na pa, usimamizi wa fedha na manunuzi yake.
 
Kwa upande wa Utawala Bora, Dk Shein alisema kuwa Masheha na Madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba misingi ya utawala bora  imetekelezwa “Nyie hapa ndio mliopo mashinani na mti wenye shina bovu hauwezi kusimama kwa kuzingatia hayo tumeamua kuendesha semina hii kwenu ili kukupeni maelekezo”,alisema Dk. Shein.
 
Akieleza kuhusu ardhi, Dk. Shein alisema kuwa ardhi imekuwa jambo lenye kuleta utata na migogoro katika jamii ambapo ni bahati mbaya kwamba mara nyingi Masheha na viongozi wa Serikali za Mitaa huhusika na migogoro hiyo.
 
Dk. Shein alisema kuwa migogoro hiyo ya ardhi inaathiri  maendeleo ya kilimo, utalii na makaazi ya watu sanjari na kuvuruga ustawi wa uchumi nchini.
 
Alisema kuwa mara nyingi mizozo ya ardhi hutokana na ukosefu wa maadili na kwa kutokuzingatia sheria zilizopo kwa baadhi ya watendaji na matokeo yake ni kuwanyima hali zao wananchi wanaostahiki. Alisema pia viongozi kama hao wa kisiwa cha Pemba watafanyiwa semna kama hiyo mara baada ya mfunguo wa mwezi wa Ramadhani.
 
Mapema Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisema kuwa semina hiyo ni mfululizo wa semina za viongozi na watendaji wakuu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
 
Aliseama kuwa tayari semina kama hizo zimeshafanywa kwa viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu, wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu, Watendaji Wakuu wengine wa Serikali pamoja na Maafisa Tawala wa Mikoa na Wilaya.
 
Mada mbali mbali zinatarajiwa kuwasilishwa katika semina hiyo ya siku mbili ambapo katika mada ya mwanzo iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bi Amina Khamis Shaaban ilieleza juu ya ‘Hali ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo’.
 
Katika mada haiyo, Bi Amina Khamis Shaaban,alisema kuwa Mwenendo wa kushuka na kupanda kwa kasi ya mfumko wa bei kunatokana na kupanda na kushuka kwa bei za vyakula na mafuta ya petroli, hivyo bila ya kuwa na uzalishaji wa ndani unaojitosheleza, soko la nje litaendelea kupandisha mfumko wa bei kwa Zanzbar.
 
Nao Masheha na Madiwani hao walitoa michango yao mbal mbali na kupongeza juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kuwaandalia semina hiyo muhimu.
 
Katika semina hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalm Seif Sharif Hamad, Dk. Shein alikuwa ndie Mwenyekiti wa semina hiyo yenye kaulimbiu’Viongozi Tubadilike

UAMSHO YAKANUSHA KUFANYA MAANDAMANO LEO

Amir mkuu wa jumuiya ya UAMSHO Sheikh Farid Hadi

Jumuiya Ya Uamsho Na Mihadhara Ya Kiislamu (JUMIKI) imepinga uvumi uliosambazwa nchini kuwa leo kutakuwa na maandamano ya Jumuiya hiyo na kudai kuwa propaganda hizo zinaendeshwa na baadhi ya watendaji katika jeshi la polisi na usalama wa taifa ambao hawaitakii mema Jumuiya yao.
 
Hayo yamesemwa na Amiri wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Ahmed wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo Zanzíbar kuhusiana na tuhuma ambazo wamezitoa kwa Jeshi la Polisi dhidi ya Jumuiya yao.
 
Amedai kuwa Jumuiya haijapanga maandamano kwani ni taasisi inayofanya kazi zake kisheria nakwamba hata ikitokezea kufanya maandamano basi watafuata taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kulitaarifu rasmi Jeshi la Polisi.
 
Aidha amedai kuwa kuna mkakati wa muda mrefu wa kutaka kuwabatiza viongozi wakuu wa jumuiya hiyo kesi za ugaidi hususan Amir Mkuu wa jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikh Farid Hadi Ahmed ili kuzima vuguvugu la kudai Zanzibar huru.
 
Shekh Faridi amedai kuwa inasemekana kuna mahusiano makubwa baina ya watendaji ndani ya Jeshi la polisi pamoja na baadhi ya wageni wanaosadikiwa kuwa ni raia wa Marekani juu ya kuutekeleza mkakati huo baada ya kuwa tayari umeshakamilika.
 
Amedai kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za kirai ambao umekuwa ukifanywa na Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kuwanyima haki ya kufanya mihadhara yao ndani ya Misikiti  ambapo Juni 17 mwaka huu wananchi mbalimbali walijeruhiwa kwa mabomu katika vijiji vya Donge,Mkwajuni na Mahonda.
 
Ameliomba Jeshi la Polisi kufanya kazi zake za kulinda usalama wa wananchi na mali zao na kuacha kufanya kinyume chake kwani huko ni kuchochea chuki kati ya Jeshi hilo na raia.
 
Amesisitiza haja ya wazanzibari kuungana na kuachana na Itikadi zao za kivyama katika kudai hadhi ya Rais na mamlaka ya Nchi ya Zanzibar ndani na nje ya Zanzibar pale tume ya mabadiliko ya Katiba itakapoanza kazi zake.
 
Kwa upande wake Naibu Naibu Amir Jumuiya Ya Uamsho Na Mihadhara Ya Kiisilam Sheikh, Azan Khalid Hamdan amewaomba wanahabari nao kuwa makini katika taaluma yao kwa kufanya usawa wa taarifa ambazo wamekuwa wakizitoa.
 
Hivi karibuni Jumuiya hiyo ilitangaza rasmi kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la kutoa maoni yao katika mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kubadili msimamo wao wa awali wa kuisusia Tume hiyo.

SMZ KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI WA BANADARI MPYA KWAMPIGADURI

Naibu waziri wa wizara ya Mawasiliano na Miundo Issa Haji Gavu

Wizara ya mawasiliano na miundo mbinu imesema inatafuta njia mbadala za kukwepa gharama kubwa za ujenzi wa bandlari mpya eneo la Mpigaduri zinazofikia dola za Marekani milioni 800.

        Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi naibu waziri wa wizara hiyo Issa Haji Gavu amesema gharama hizo zilizopenekezwa na kampni ya ujenzi ya CRB kutoka China ni kubwa, hivyo serikali inaendelea kutafuta njia za kupata unafuu zaidi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita wizara ilikisia ujenzi wa maradi huo utagharimu dola za Marekai milioni 400 ambapo kwa sasa ulihitaji ongezeko la asilimia 10 sawa na dola milioni 500.

Hata hivyo Gavu amesema wizara imeshakamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari hiyo uliofanywa na kampuni ya CRB na hatua za ujenzi zitaanza mara baada ya fedha kupatikana.

Aidha Gavu amesema fedha za ujenzi wa mradi huo zitatokana na mikopo au misaada kutoka kwa wahisani.

Ujenzi wa bandari hiyo utakaojengwa kwa awamu tofauti itakauwa na uwezo wa kufunga gati meli tano kwa wakati mmoja, lakini awamu ya kwanza utaanza na ufungaji wa meli tatu.

MAWAZIRI WALIOCHUKUA MAENEO YA ARDH ZANZIBAR KUTAJWA HADHARANI

Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani (CUF) Hijja Hassan

Mwakilishi wa jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija ameahidi kutaja majina ya baadhi ya viongozi wa serikali hadharani wakiwemo mawaziri wanaodaiwa kuchukua maeneo ya ardhi bila ya kufuata sheria katika eneo la Mwambe kisiwani Pemba.

        Akichangia hotuba ya bajeti ya ofisi ya makamo wa pili wa rais katika kikao cha baraza la wawakilishi amesema iwapo serikali itashindwa kuwajibisha viongozi hao atajitoa muhanga kutaja hadharani majina yao.

        Mwakilishi huyo amesema hawezi kuona baadhi ya viongozi wa serikali wanawapokonya wananchi maeneo ya ardhi kwa maslahi yao binafsi, hivyo kazi kutaja viongozi hao ataifanya ndani ya kipindi cha miezi miwili

        Nae mwakilishi wa viti maalum Mgeni Hassan Juma amewataka wananchi kuunga mkono muungano wa Tanganyika na Zanzibar licha kuwepo kero nyingi za muungano.

        Hata hivyo amesema serikali inaendelea kuchukua hatua za kuzipatia ufumbuzi kero hizo huku nyingine zikiwa zimepatiwa fumbuzi.

Amesema ni vyema kwa wananchi kutoa maoni yao juu ya undwaji wa katiba mpya ili kuainisha kasoro zinazolalamikiwa na kurekebishwa kwenye muungano huo