Waziri wa nchi ofisi ya rais Mohammed Aboud

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imezuwia maeneo yake kufanyiwa utafiti wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kufuatia utafiti kama huo kufanyika katika maeno ya Tanzania bara.

Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi waziri wa nchi ofisi ya makamu wa pili wa rais Mohammed Aboud amesema suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta litafanywa na wanzazibari wenyewe wakati utakapofika na sio kampuni za kigeni.

Amesema serikali imeshatoa raarifa hiyo kwa serikali ya muungano kutoyaruhusu maeneo yake kufanyiwa utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia

Waziri Aboud serikali inaendelea kuchukua hatua za kisheria ya kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya muungano.

Amesema katika kikao kilichofanyika hivi karibuni suala la mafuta na gesi asilia lilikuwa ni miongoni mwa agenda zilizojadiliwa na ilikubaliwa suala hilo lipatiwe ufumbuzi wa haraka .

Hata hivyo waziri Aboud amesema serikali haitambuli mikataba yoyote iliyosainiwa awali ya upande wa pili wa muungano kuyaruhusu makampuni ya kigeni kutafuta mafuta katika maeneo ya Zanzibar.

Tamko hilo la waziri Aboud katika baraza la wawakilishi kumefuatia madai yaliotolewa na mwakilishi wa jimbo la mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu aliedai kampuni ya Petro Brass imeruhusiwa kufanya utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika baadhi ya maeneo ya Zanzibar

Advertisements