RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa ni jambo la aibu na kusikitisha kuona ukuaji wa majaa na utupaji ovyo wa taka unaendelea katika Shehia hasa Wilaya ya Mjini na Wilaya ya Magharibi wakati Madiwani na Masheha hawachukui hatua zinazopaswa
 
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati alipofungua semina ya uongozi ya viongozi wa Serikali za Mitaa ambayo iliwahusisha Masheha, Madiwani na viongozi wa Halmashauri.
 
Aliendelea kusisitiza kuwa mifugo bado inaachiwa ovyo mijini na pia masikitiko ya wakulima kuharibiwa mazao yao na wafugaji wasojali sheria wala kanuni ziliopo.
 
Dk. Shein alisema kuwa jukumu la viongozi hao pia, ni kuchangia katika kuendeleza utalii nchini ambao unazidi kuwa ni tegemeo kubwa la uchumi lakini Mtalii hatopendelea kurudi katika mji au nchi isiyo safi na isiyojali mazingira yake.
 
Alisema kuwa uchimbaji wa mchanga unaendelea kwa kasi kubwa katika shehia za Wilaya ya Magharibi na Wilaya ya Kati ambapo pia, fukwe za pwani zimekuwa zikiharibiwa kutokana na uchafuzi na ukataji wa mikoko na kusisitiza kuwa hayo yote yanaathiri uchumi, utalii na maendeleo ya Zanzibar.
 
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa utekelezaji wa mipango ya maendeleo unaofanywa na Serikali kupitia Idara na Wizara zake huwa unatekelezwa katika shehia, kwemo upelekaji huduma za afya, elimu, maji na mengineyo na kueleza kuwa Masheha na Madiwani kupitia katika Kamati za Maendeleo za maeneo yao wanahusika na mipango hiyo.
 
Alisema kuwa Masheha na Madiwani pia, wanapaswa kuwa na ushiruki na uhusiano mkubwa katika kutunza amani na usalama ndani ya Shehia zao huku akisisitiza kuwa ulinzi unaotolewa na vyombo vya dola au Polisi Jamii ambao unawpa usala wananchi utafanikiwa tu kwa mashirikiano ya pamoja na jamii.
 
Dk. Shein alisema kuwa semina hiyo imelenga katika kutoa maelekezo ya nyanja mbali mbali za uongozi na kiutendaji lakini italitilia mkazozaidi katika masuala ya ardhi na migogoro yake, utawala bora, mazingira, maadili, uchumi na utalii kwa wote na pa, usimamizi wa fedha na manunuzi yake.
 
Kwa upande wa Utawala Bora, Dk Shein alisema kuwa Masheha na Madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba misingi ya utawala bora  imetekelezwa “Nyie hapa ndio mliopo mashinani na mti wenye shina bovu hauwezi kusimama kwa kuzingatia hayo tumeamua kuendesha semina hii kwenu ili kukupeni maelekezo”,alisema Dk. Shein.
 
Akieleza kuhusu ardhi, Dk. Shein alisema kuwa ardhi imekuwa jambo lenye kuleta utata na migogoro katika jamii ambapo ni bahati mbaya kwamba mara nyingi Masheha na viongozi wa Serikali za Mitaa huhusika na migogoro hiyo.
 
Dk. Shein alisema kuwa migogoro hiyo ya ardhi inaathiri  maendeleo ya kilimo, utalii na makaazi ya watu sanjari na kuvuruga ustawi wa uchumi nchini.
 
Alisema kuwa mara nyingi mizozo ya ardhi hutokana na ukosefu wa maadili na kwa kutokuzingatia sheria zilizopo kwa baadhi ya watendaji na matokeo yake ni kuwanyima hali zao wananchi wanaostahiki. Alisema pia viongozi kama hao wa kisiwa cha Pemba watafanyiwa semna kama hiyo mara baada ya mfunguo wa mwezi wa Ramadhani.
 
Mapema Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisema kuwa semina hiyo ni mfululizo wa semina za viongozi na watendaji wakuu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
 
Aliseama kuwa tayari semina kama hizo zimeshafanywa kwa viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu, wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu, Watendaji Wakuu wengine wa Serikali pamoja na Maafisa Tawala wa Mikoa na Wilaya.
 
Mada mbali mbali zinatarajiwa kuwasilishwa katika semina hiyo ya siku mbili ambapo katika mada ya mwanzo iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bi Amina Khamis Shaaban ilieleza juu ya ‘Hali ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo’.
 
Katika mada haiyo, Bi Amina Khamis Shaaban,alisema kuwa Mwenendo wa kushuka na kupanda kwa kasi ya mfumko wa bei kunatokana na kupanda na kushuka kwa bei za vyakula na mafuta ya petroli, hivyo bila ya kuwa na uzalishaji wa ndani unaojitosheleza, soko la nje litaendelea kupandisha mfumko wa bei kwa Zanzbar.
 
Nao Masheha na Madiwani hao walitoa michango yao mbal mbali na kupongeza juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kuwaandalia semina hiyo muhimu.
 
Katika semina hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalm Seif Sharif Hamad, Dk. Shein alikuwa ndie Mwenyekiti wa semina hiyo yenye kaulimbiu’Viongozi Tubadilike

Advertisements