Archive for July, 2012

BENK YA BIASHARA AFRIKA YAHIDI KUTOA MKOPO WA UNUNUZI WA MELI ZANZIBAR

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Afrika
{CBA} Bw. Yohane Kaduma akikabidhi mchango wa Maafa kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi kufuatia ajali ya Meli ya M.V. Skagit hivi karibuni.

Benki ya Biashara ya Afrika { CBA } inajaribu kuangalia utaratibu wa namna itakavyoweza kusaidia kutoa mkopo ili kuchangia kufanikisha azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya ununuzi wa Meli kubwa  ya kusafirishia Abiria na Mizigo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Bwana Yohane  Kanuma wakati akiwasilisha mchango wa Maafa kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Yohane alimueleza Balozi Seif kwamba Taasisi yao haina sababu ya kutochangia suala hilo ili kujaribu kusaidia nguvu za kuepuka majanga yanayoweza kukingika ndani ya Sekta ya Usafiri wa Baharini.
Alisema kitakachozingatiwa zaidi ni jinsi gani pande hizo mbili yaani Benki hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitakavyofikia makubaliano ya masharti ya mkopo utakaokubalika kutolewa na Benki hiyo.
Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa CBA alifahamisha kwamba Jamii kupitia Viongozi wa Taasisi inapaswa kuendelea kuwa makini katika kulinda roho za Raia kwa hali yoyote ile ambayo imo ndani ya uwezo wao.
“ Tunapaswa kuwa makini katika kulinda Maisha  ya Watu kwani hakuna fedha wala mali inayoweza kulipa roho za Watu”. Alisisitiza Bwana Yohane.
Alizitaka Familia zilizopatwa na misiba ya Jamaa zao katika ajali hiyo ya Meli ya M.V. Skagit kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Bima ya Afya Tanzania Bwana Peter Daniel akikabidhi mchango wa Maafa kwa Balozi Seif alisema Uongozi wa Shirika hilo umeguswa na Janga hilo lililopelekean kupotea kwa roho za Watu kadhaa hapa Nchini.
Bwana Peter alifahamisha kwamba mchango wao licha kwamba ni mdogo lakini unaweza kuwa chachu ya kuungana na familia zilizopatwa na isiba hiyo katika kupunguza machungua hayo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Jaman Investiment inayotoa huduma katika Viwanja vya ndege Bwana  Qovirvi Sadrudin akitoa mchango wa Maafa alizitaka Familia za Watu waliofiwa na wale waliopotelewa na jamaa zao kuwa wavumilivu.
Bwana Sandrudin alisema huo ni msiba mzito ambao unamgusa kila mwana jamii ndani ya Taifa hili la Tanzania.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliendelea kusisitiza kwamba Serikali imeshafanya maamuzi ya kununu Meli Mpya za Usafiri wa Abirina Mizigo kwa uhakika na salama.
Alisema hatua za makusudi zitaendelea kuchukuliwa katika suala zima la kukabiliana na Maaafa wakati yanapotokezea yale ya bahati mbaya na si uzembe.
“ Katika kukabiliana na Maafa tutajitahidi  zaidi hata kama  wenzetu wengine watatuona wabaya”. Alifafanua Balozi Seif.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali imeaanza kuonyesha njia ambayo wengine lazima waifuate kwa kuizuia Meli yake ya  Serikali ya M.V. Maendeleo kutofanya kazi mpaka ikaguliwe na Taasisi za Mamlaka ya Usafiri licha ya kurejea hivi karibuni  matengenezoni Nchini Kenya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuzipongeza Taasisi zote zinazojitolea kutoa misaada yao ambayo itasaidia hatua zote za kukabiliana na janga hilo kubwa.

SEKTA YA UVUVI NA UFUGAJI ZANZIBAR KUAJIRI VIJANA 300

Miongoni mwa athari za uvuvi haramu, unaotokana na wavuvi wa Zanzibar kukosa taaluma ya kuvua bahari kuu.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kutekeleza miradi miwili ya uvuvi wa bahari kuu na ufugaji itakayozalisha nafasi 300 za ajira kwa vijana katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013.

        Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo waziri Abdilahi Jihadi Hassan amesema miradi hiyo itatekelezwa kwa pamoja kati ya wizara ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika na wizara mifugo na uvuvi.

        Amesema miradi hiyo itaingiziwa shilingi milioni 550 kupitia program ya ajira kwa vijana ambapo shughuli za ufugaji zimetengewa shilingi milioni 150 na uvuvi wa bahari kuu zimetengewa shilingi milioni 400.

        Waziri Jihadi amesema kati ya vijana hao watakaopatiwa na fasi za hizo 160 ni ajira za ufugaji na 80 ni ajira za ufugaji  wa mbuzi wa maziwa na kienyeji.

        Aidha amesema katika ajira za uvuvi wa bahari kuu vijana 60 watapatiwa boti mbili za uvuvi wa kina kirefu cha maji.

        Wizara Mifugo na uvuvi katika bajeti hiyo imeomba kuidhinishiwa shilingi bilioni tano na milioni 292 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa matumizi ya kazi za kawaida na maendeleo.

SMZ-KUNUNUA MELI MPYA

Meli ya Mv. Mapinduzi iliyokuwa inamilikiwa na SMZ, lakini kwa sasa imeuzwa na kuzama katika kisiwa cha Madagasca

RAIS  wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, ameiagiza Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuandaa utaratibu wa kupata fedha ndani ya wiki moja kwa ajili ya kununua meli kubwa mpya ya abiria wapatao 1000 na yenye uwezo wa kuchukua mizigo ya tani 100.
 
Dk. Shein ametoa agizo hilo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na uongozi wa Shirika la Meli pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Shirika hilo ambapo pia kikao hicho kilihudhuriwa na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na  Wizara ya Nchi Afisi ya Rais  Fedha, Uchumi na  Mipango ya Maendeleo.
 
Katika kikao hicho maalum Dk. Shein ameiagiza Wizara hiyo kutafuta  fedha hizo kutokana na vianzio vya ndani au nje ya nchi ama kutokana na  taasisi zinazohusiana na mambo ya fedha.
 
Alieleza kuwa katika kipindi  kisichozidi miezi miwili ujumbe maalum uende kwa  Kampuni zinazotengeneza meli nchini Korea Kusini, China au Japan kwa ajili ya kuwasilisha fedha za utangulizi kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo.
 
Mapema uongozi wa Shirika la Meli, ulimueleza Dk. Shein  kuwa kwa kawaida ujenzi wa meli yenye ukubwa huo, huchukua mwaka  mmoja kukamilika.
 
Kikao hicho ambacho kilikuwa na lengo la kuangalia mwelekeo na Mipango ya Shirika la Meli pia, kilijadili hali halisi ya meli za Shirika la Meli na  baadae kujadili  masuala ya ununuzi wa meli mpya itokayowaondoshea usumbufu wa usafiri wa baharini wananchi wanaosafiri kati ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara.

TAARIFA YA KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI JUU YA KUZAMA KWA MELI YA MV. SKAGIT

 

Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma

 

TAARIFA YA KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA JUU YA  TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA SKAGIT  ILIYOTOKEA TAREHE 18.07.2012 KATIKA ENEO LA KISIWA CHA CHUMBE NJE KIDOGO YA ZANZIBAR.

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana tena mbele ya Baraza lako tukufu tukiwa wazima wa afya ili kujadili mambo mbali mbali yanayohusu mstakbali mzima wa maendeleo ya nchi yetu. Aidha tuishukuru neema hii aliyotupa M/Mungu ya kuendelea kutupa neema ya pumzi zake ili kuweza kutekeleza majukumu yetu ambayo tulikula kiapo kwa kukamata Msahafu kuwatumikia wananchi wetu kwa ukweli, uwazi na uadilifu mkubwa na tunamuomba tene atuzidishie uzima na afya njema ili tuiokoe nchi yetu kutokana na janga la umasiskini na nnaamini kwa ukweli na uadilifu tunaoendelea nao hivi sasa basi naamini si muda mrefu nchi yetu itapiga hatua kubwa za maendeleo .

Mheshimiwa Spika, Aidha kwa niaba ya kamati nakushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama mbele ya Baraza lako tukufu ili niwasilishe taarifa ya kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa juu ya tukio hilo la maafa. Pia naomba  nawashukuru wananchi wangu wa jimbo la K/pura walionileta hapa kuja kuwawakilisha na nnaomba waendelee kuniamini na nnawaahidi kuwatumikia na nitajitahidi kuhakikisha kuwa nitawatumikia kwa uadilifu mkubwa na nitaishauri Serikali yetu kila ambalo nitahisi linaweza kuisaidia Serikali yetu, na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya kamati, nachukua fursa hii kumuomba Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi wale wote waliofariki kutokana na ajali hiyo, na pia kuwataka kuwa na subra wale wote waliopoteza  ndugu na jamaa  zao. Pia na wale walionusurika katika ajali hiyo tunawatakia afya njema na inshallah Mwenyezi Mungu atawape afueni ili tuweze kujumuika nao na  kuweza kuendelea na majukumu ya kujenga Taifa letu.

Mheshimiwa Spika,Sisi Wajumbe wako wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wewe mwenyewe binafsi tulipata mshituko mkubwa baada ya kupata tarifa ya kuzama kwa meli  mchana wa siku ya jumatano ya tarehe 18.07.2012 kwa masikitiko makubwa iliyokua ikitoka Dar-es-Salaam kuja Zanzibar,kwani ilitukumbusha machungu tuliyoyapata takriban ni Mwaka ukizingatia ni karibu Mwaka mmoja tu  uliyopita hapa nchini kwetu tuliweza kupata msiba mkubwa unaolingana na huu.

Mheshimiwa Spika,kamati yangu inasikitika sana kwa kuona kuwa visiwa vyetu vya Unguja na Pemba vimekumbwa na msukosuko mkubwa katika usafiri wa baharini ukiacha suala la kuzama kwa meli hii kwani kwa mtu yeyote aliyekuwa makini hakupigwa na mshangao kwa kutokea ajali hii kwani kulikuwa kuna kila dalili ya kutokea ajali baharini kwani kumekuwa na mfululizo wa matukio mbali mbali yakuashiria kutokea ajali baharini kwa baadhi ya meli kuzimika injini ovyo mara kwa mara huko Baharini zikiwa katika safari zake za kila siku zikiwa na abiria wengi ndani yake.

Mheshimiwa Spika,tukio la kuzama kwa meli limetupa funzo kubwa, kwani tatizo kubwa tulilokuwa nalo hapa ZNZ ni kutokuwa waaminifu na waadilifu kwa kusimamia majukumu tunayopewa au dhamana tunayopewa na wananchi wetu aidha kwa uzembe au tamaa binafsi inayopekea kutokuwajibika ipasavyo kwa umma, kwani kuna mamlaka iliyopewa jukumu la kusimamia kuhakikisha usalama wa vyombo vya baharini laikini inaonesha kuwa mamlaka hiyo imeshindwa kazi na ndio maana uzembe mkubwa unaendelea kufanyika ikiwemo kutokukagua vizuri injini za boti hizo,upakiaji abiria kiholela na ukataji wa tiketi ovyo bila kutumia vitambulisho pamoja na uuzwaji ovyo wa tiket vichochoroni bila ya kutumia Ofisi zinazotambulikana kitu ambacho kinachopelekea kupakia abiria wengi kuliko uwezo wake. Ndio maana hata takwimu zinayotolewa wakati chombo kinapopata ajali inakuwa ni tofauti na hali halisi ya idadi ya watu wanaokuwemo. Kwa hiyo, tunaitaka Serikali kuhakikisha kwamba inasimamia watendaji wake kutekeleza yale majukumu waliyopewa ili kuepusha ajali kama hizo zisitokezee tena.

Mhe Spika, jengine tunalojifunza nia kwamba Serikali yetu kutozifanyia kazi kwa haraka ripoti mbalimbali za aidha za kamati inazoziunda wao wenyewe au zile za Baraza lako tukufu au hata za taasisi mbali mbali Srikali inazopelekea kwani ukiangalia mambo mengi yanayoshauriwa basi yanakuwa ni kwa faida ya nchi yetu na pale zinapodhararauliwa basi matokeo yake wakati mwengine yakuwa na athari kubwa kwa jamii kwa ujumla.

Mhe Spika , kwa funzo hilo Serikali yetu ililolipata kama kawaida yetu tunaishauri sasa wakati umefika kuzifanyia kazi ripoti zote ilizopelekewa ukiacha zile za Baraza bali ni kwa ripoti zote zilizopelekwa Serikalini.

Mheshimiwa Spika,jambo jengine inaonesha kuna udhaifu mkubwa katika ukaguzi na usajili wa meli kutokuangalia historia ya meli hiyo kuanzia mwaka iliyotengenezwa,kazi inazoweza kuzifanya,muda wa uhai wa kutumika kwa chombo hicho,lakini pia na udhaifu wa (modification) zinazofanywa ili kuongeza nafasi za kupakilia abiria bila ya kuzingatia uwezo wa injini ya chombo hicho kwa lengo la kutengeneza faida kubwa bila kujali maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika,imekuwa ni jambo la kawaida kwa hivi sasa mtu akitaka kusafiri kwa boti au kwa meli anawaza mara tatu tatu kwani hana uhakika wa kufika salama safari yake, hii inaonesha kuwa hakuna uhakika wa salama wa maisha yake, leo hii  imekuwa hata wanafamilia wanaposafirisha jama zao huwa presa juu juu mpaka wafike safari na kuwajuilisha kuwa wamefika salama, kwa hiyo hivi sasa Serikali imeweka rehani maisha ya wanachi wake kwani hakuonekani juhudi zozote za waliokabidhiwa majukumu ya kuwasimamia usalama wa abiria wetu kama wako makini kiasi hicho, hii ni kusema kwamba wameshindwa kazi.

Lakini kwa kuwa kwa mara ya kwanza Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa imesikia kilio cha Wawakilishi na wananchi wa Zanzibar kwa kumtaka Waziri ajiuzulu ambapo suala hili tulilipendekeza tokea ilipozama meli ya Spice Islander tulimtaka ajiuzulu ili kuonesha uwajibikaji wa kisiasa, lakini kwa bahati mbaya hakufanya hivyo lakini tunamshukuru kwa hivi sasa kwa kuwa ameamua kuwajibika ili kuonesha kuwa na yeyé ameguswa katika tukio hili kubwa la kitaifa. Na hili wala asione taabu wala aibu kwani kwa mfumo huu tuliokuwa nao hivi sasa wa Serikali ya umoja wa kitaifa wa demokrasia ya ukweli na uwazi ni jambo la kawaida sana tu na tunawaomba wengine wanaposhindwa kusimamia majukumu yao basi waamue mapema kuliko kusubiri kung’olewa kwa nguvu.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha sana kwa wananchi wetu, kwani hata kuna baadhi ya wahangana waliopata ajali katika meli ya MV SPICE ISLANDER hawajapata ubani wao uliotengwa na Serikali, lakini leo hii tayari kuna msiba mwengine mkubwa ulioikumba nchi yetu, inawezekana pia miongoni mwa familia waliopata maafa hayo na katika maafa haya ikawa yamewakuta tena kama wapo watu hawa basi tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subra kwani ni mtihani mkubwa kwao na inabidi washukuru kwani kila mtihani anaokupa Mwenyezi Mungu basi ukiwa na subra kuna kheri pia inakuja baadae nawaomba Wajumbe wenzangu wa Baraza hili pamoja na Watanzania wote kwa ujumla tuwaombee kila la kheri katika kukabiliana na mitihani hii pia tumuombe Mwenyezi Mungu awaepushe na mitihani mengine.

Mheshimiwa Spika,kwa tukio hili kuna baadhi ya maneno yanayozungumzwa na baadhi ya wanasiasa kuwa kuna kundi ndani baraza lako tukufu kwamba lina chuki za ubaguzi wa kisiasa kwa baadhi ya mawaziri tunataka kuwahakikishia wananchi wote wa Zanzibar kuwa sisi sote ni kitu kimoja na tunafanya kazi kwa pamoja kuwatumikia wananchi wetu bila ya chuki wala upendeleo wowote, bali ni kwa maslahi ya umma tu. Kwani kwa hivi sasa tumeamua kuweka kando itikadi zetu za kisiasa na kuamua kujenga nchi yetu kwa pamoja kwa maslahi ya Taifa letu na wananchi wetu, kwa hiyo tunaomba kila mmoja atimize majukumu yake aliyotumwa na wananchi wake kwa upande wa Wawakilishi ya kuisimamia ipasavyo Seriakali na kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kwa mujibu wa Katiba na Sheria zote , za hapa ZNZ na Tanzania nzima. Vile vile kusimamia uwajibikaji wa watumishi wote wa umma katika majukumu waliokabidhiwa na Serikali, lakini pia na mawaziri kwa upande wao kuhakikisha wanawasimamia walio chini yao ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar.

Mhe Spika,  kamati yangu inaishauri Serikali kuendelea kulitumia eneo la kama kuwa ni eneo la kudumu kwa ajili kuzikia kwani eneo hilo inaonyesha eneo hilo lilitelekezwa baada kuzikwa watu waliofariki katia ajali ilyopita, lakini pia ukizingatia kuwa hivi sasa eneo la makaburi ya mwanakwerekwe limeshajaa kwa muda mrefu lakini bado linaendelea kuzikiwa maiti hadi vivi sasa jambo ambalo halipendezi hata kidogo.

Mhe Spika. Kamati yangu kutokana na funzo la ajali hii ya tatu mfululizo ndani ya miaka mitano tumeona iko haja ya kuwashauri wananchi wetu kujikatia bima za maisha ili yanapotokea majanga kama haya waweze kulipwa Bima ya maisha au ya afya kwa wale waliojeruhiwa au kupoteza uwezo wa kufanya kazi tene katika maisha yao kuliko kutegemea ubani utakaotolewa na Serikali kama utakuwepo.

Mhe Spika,  ripoti ya Serikali imeelezea kuwa wamewasaidia jamaa wa marehemu gharama za mazishi, usafirishaji wa maiti ,sanda na ubao lakini kamati yangu inaiomba Serikali pia kuwasaidia na gharama za Tahtimu kwani hali za familia zetu tunazijua kuwa nyingi zinaishi katika hali duni ya maisha na pengine hao waliofariki wengine ndio tegemeo lao katika familia, kwa hiyo kwao wao msiba unakuwa ni mara mbili. Kwa hiyo tunaamini jambo hilo litawapunguzia machungu wakati wa kuomboleza msiba.

Mhe Spika, katika ripoti ya ya Mhe Waziri ametueleza kuwa kuna baadhi ya wasamaria wema wanaendelea kufika ofisi ya Makamo wa pili wa Rais kutoa ubani wa mkono wa pole, na kwa upande fedha taslim wameziweka katika Account maalum iliyofunguliwa wakati wa ajali ya MV SPICE ISLANDER’S , lakini hadi leo Serikali yetu bado haijaanzisha mfuko wa maafa ambao utaweza kutumika au kusaidia wakati wowote maafa yatakapotokea aidha kwa upande wa Baharini ,au nchi kavu kwani ajali ziko za aina nyingi tu, kwani kuna Mafuriko, Moto, ajali za Ndege, Meli, Upepo mkali, n.k. kwa hiyo kamati yangu inaishauri Serikli kuanzisha mfuko wa maafa kwani si busara kuendelea kutumia pesa kutoka mfuko Mkuu wa Serikali, kama ilvyo hivi sasa kwani inasababisha kuwazuia wafanya biashara, Mashirika ,Makampuni au taasisi au mtu yeyote anayehitaji kuchangia mfuko huo kushindwa kufanya hivyo, lakini pia tunata kujua kuwa katia account hiyo maakum je kutakuwa na utaratibu mpya wa utoaji ubani kwa kiasi kili kile kilichotolewa katika ajali ya mwanzo?

Mhe Spika, Lakini pia tunaiuliza Serikali kupitia ahadi zilizotolewa na baadhi ya taasisi za fedha waliahidi kuwasomesha baadhi ya mayatima waliochwa na waliopoteza maisha katika ajali ya MV SPICE ISLANDER, je Serikali kupitia Ofisi yako imelifuatilia kwa kiasi gani? Na kama limetekelezwa je ni mayatima wangapi hadi sasa wanasomeshwa na taasisi hizo?.

Mhe Spika, kamati yangu inaiomba Serikali kuimarisha kikosi chetu cha KMKM pamoja na kikosi cha Zimamoto na uokozi ili kuweza kukabiliana na maafa ya ajali yoyote inayowezac kutokea aidha kwa Baharini au nchi kavu, kuwa na zana za kisasa ikwemo kuwa na Helikopta ya uokozi ambayo itakuwa na huduma za matibabu ya dharura inapokuwa angani ili kuweza kuokoa maisha ya wa wananchi wetu popote majanga yatakapokuja kutokea, vile vile tunaiomba Serikali yetu kuandaa utaratibu mzuri wa uokozi kwani tumeona udhaifu mkubwa wakati wa harakati za uokoaji pale Bandarini hapakuwa na utaratibu mzuri wa nani aliekuwa na amri ya mwisho katika kuongoza zoezi zima la uokozi, kwani tumeshuhudia hata vyombo vilivyokuwa vikitumika vilikuwa ni vikubwa kitu ambacho kilihitajika kutumika pia vyombo vidogovidogo ambavyo vingeliweza kusaidia zaidi huduma za uokozi.

Mhe Spika, katika hali iliyokuwa si ya kawaida au fadhaa tulishangaa kuona baada ya kutokea ajali chombo cha mwanzo kwenda kwenye tukio kiliwaacha wazamiaji ambao waneliweza kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi badala yake chombo hicho walipanda viongozi wakiwemo mawaziri utadhani wanakwenda kuangalia snema huko baharini wakati wao wenyewe hawajui hata kuogelea seuze kuokoa watu waliopata ajali , hili pia ni funzo kubwa tunatakiwa tujipange vizuri, vile vile kitu chengine cha kushangaa ni kule kuona hata kuna baadhi ya boti ambazo zilikwenda kuokoa watu waliozama kusikia nazo zilizimalizika mafuta huko baharini kitu ambacho ni kibaya sana kwani kinaweza kusababisha ajali nyingine huko baharini kwa hiyo inaonyesha kuwa bado hatujakuwa na mipango mizuri ya uokozi pale majanga yanapotokea,

Mhe Spika, Kamati yangu inaiomba Serikali kufanya ukaguzi wa kina kwa vyombo vyote vya Baharini, ikiwemo Engine pamoja na uwezo wa Manahodha na Mabaharia wanofanyakazi katika vyombo hivyo na wakigundulika wasiokuwa na uwezo kuachishwa kazi na ni bora kuwa na vyombo vichache vyenye uhakika kuliko kuwa na vyombo vingi visivyokuwa na ubaora au kiwango, .

Mhe Spika, kamati yangu bado inaiomba Serikali yetu kufanya kila linalowezekana kununua Meli ya kubebea abiria na mizigo kwani ni aibu kuwa sisi tunachaguliwa na wananchi hao hao na tunalipwa mishahara kupitia kodi zao lakini tunashindwa kuwahakikishia usalama wa maisha yao.

Mhe Spika, Lakini pamoja na Serikali kununua Meli hizo kwa kuwa mzingira ya nchi yetu ni ya visiwa sio kama watu wote wataweza kusafiri kwa siku moja na kupanda Meli hizo la Serikali kwa hiyo bado ni lazima kutakuwa ulazima wa kuwa na vyombo binafsi , ndio maana tukasema kuwa suala kubwa hapa na la ulazima ni kuhakikisha ukaguzi wa kina wa usalama wa vyombo hivyo kwani hata hizo Meli za Serikali pia nazo zitahitajika kukaguliwa kila wakati kwani sio kama hizo Meli za Serikali hazitaweza kupata ajali zikiwa nazo hazitakuwa na ubora .

Mhe Spika, kwa kumalizia tunaishauri Serikali yetu kuwa sasa wakati umefika wa kuyatekeleza maoni na ushauri wa kakati zote aidha ilizoziunda wenyewe Serikali ,ripoti za washauri mbali mbali wa nje na ndani na zile za Baraza la wawakilishi kwani zina faida kubwa kwa nchi yetu kaka zitatekelezwa kwa vitendo na muda muafaka, vinginevyo hata hizo idara zilizoundwa kila wizara Idara za utafiti zitakuwa hazina maana yeyote kwani nao baada ya kufanya utafiti baadae pia hutoa ripoti kwa hiyo ripoti hizo kama hazikufanyiwa kazi yatakaua ndio hayo hayo (BUSINESS AS USSUAL)

Mhe Spika kwa mara nyingine tena naomba niwashukuru  wajumbe wa kakati yangu kwa kuwa wastahamilivu na kunipa mashirikiano makubwa kuandaa ripoti hii kwani tuliweza kuaa hadi saa sita za usiku na kuweza kuikamilisha asubuhi hii na kuiwakilisha hapa Barazani,

Mwaisho kabia naomba kuwashukuru wananchi wote wa ZNZ pamoja na wananchi wangu wa jimbo la Kwamtipura walionileta hapa ili ukwatumika nnawaahidi kuendelea kuwatumikia kwa uadilifu na moyo wangu wote.

Mhe Spika mwisho kabisa naomba kumkaribisha Mhe Hamad Masoud Hamad katika nyumba yetu ya Back Bancher ili kushirikiana nasi kuwatumikia wananchi wetu wa ZNZ kuwaletea maendeleo, tunakuombea kila la kheri katika kazi yako hii mpya ambayo kwa miaka mingi uliitumikia kwa uadilifu mkubwa, na tunamuomba M/Mungu akuepushe na shari nyengine naomba kuwasilisha .

Mhe Spika naomba kuwasislisha.

Ahsante sana.

Ahsante

 

…………………

MHE: HAMZA HASSAN JUMA

KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIOGOZI WAKUU WA KITAIFA

BARAZA LA WAWAKILISHI

ZANZIBAR.

 

            

KAULI YA SERIKALI KUHUSU TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA MV. SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18.07.2012 KATIKA ENEO LA BAHARI YA CHUMBE

Mohammed Aboud Mohammed

KAULI YA SERIKALI KUHUSU TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA MV. SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18.07.2012 KATIKA ENEO LA BAHARI YA CHUMBE

=======================================

 

Mheshimiwa Spika;

Kwa heshima naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa leo tukiwa wazima na wenye afya njema. Pili, naomba nichukue nafasi hii adhimu kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kutupatia fursa hii adhimu ili kuwasilisha mbele ya Baraza lako Tukufu taarifa ya maafa ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit iliyotokea katika bahari ya Chumbe tarehe 18.07.2012.

 

1.0 Utangulizi

 

Mheshimiwa Spika,

Meli ya MV. Skagit ilitengenezwa nchini Marekani mwaka 1989 na imesajiliwa Zanzibar tarehe 25/10/2011, na kupewa nambari ya usajili 100144. Meli hiyo ina uzito wa GRT96 ambayo inamilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Limited ya Zanzibar.

 

Mheshimiwa Spika,

Mnamo tarehe 18.07.2012 majira ya saa saba na nusu za mchana ilipatikana taarifa ya ajali ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit katika bahari ya chumbe nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Meli hiyo ilikuwa katika safari zake za kawaida ya kutoka Dar-es-Salaam kuja Zanzibar.

 

Kwa mujibu wa manifest ya abiria iliyowasilishwa na wamiliki wa meli kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority-TPA) na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na Nchi Kavu Tanzania (Surface and Marine Transport Authority-SUMATRA), meli hiyo ilikuwa imechukua jumla ya watu 290 wakiwemo abiria watu wazima 250, watoto 31 na mabaharia 9.

 

Mheshimiwa Spika

Taarifa hii inaelezea kwa kina juu ya hali halisi ya tukio pamoja na hatua zote zilizochukuliwa kuanzia tarehe 18/07/2012 hadi hivi sasa.

 

Mheshimiwa Spika

Mara baada ya tukio hili, Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Taifa ilikutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya hatua za kuchukua pamoja na kuandaa taarifa rasmi ya Serikali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. Aidha, Baraza la Mapinduzi lilikaa usiku wa tarehe 18.07.2012, na kutoa maagizo juu ya hatua za kuchukua ikiwemo kuwepo kwa matayarisho katika hospitali ya mnazi Mmoja ya kupokea majeruhi, kutayarisha eneo la Maisara kwa ajili ya mapokezi na utambuzi wa maiti; kutayarisha eneo la kuzika miili ya marehemu huko Kama; kuweka takwimu sahihi za majeruhi na waliofariki katika ajali hiyo; pamoja na kutolewa kwa taarifa rasmi ya hali ya uokozi iliyokuwa inaendelea.

 

2.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA

 

Mheshimiwa Spika

Kufuatia maagizo hayo ya Serikali, hatua zifuatazo zilichukuliwa: –

 

 • Vituo cha mapokezi ya wahanga wa ajali hiyo vilifunguliwa katika maeneo ya Bandari ya Malindi, Hospitali ya Mnazi Mmoja na uwanja wa Maisara.
 • Vikosi vya Ulinzi na Usalama vilipelekwa katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha huduma za ulinzi na uokozi wa haraka.
 • Kazi ya uchimbaji wa makaburi katika eneo la Kama ilifanyika kwa mashirikiano makubwa ya viongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi. Jumla ya makaburi 80 yalichimbwa.
 • Sala na dua maalum ya kuwaombea marehemu wote ilifanyika baada ya sala ya Adhuhuri jana tarehe  22.07.2012 katika misikiti yote ya Unguja na Pemba na Kitaifa ilifanyika katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Zanzibar.
 • Kuorodhesha majina ya wale wote ambao wanasadikiwa walikuwemo ndani ya chombo kilichopata ajali na hadi sasa hawajulikani walipo. Taarifa hizi zinakusanywa kupitia ngazi ya Shehia na Wilaya kwa Unguja na Pemba na kwa Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa Tanzania Bara.
 • Kutoa huduma ya kuwasafirisha majeruhi baada ya kupata matibabu kurudi makwao.
 • Kutoa huduma za usafiri kwa walioshiriki katika shughuli zote za operesheni.

 

 

3.0 MATOKEO YA OPERESHENI

 

3.1 Shughuli za uokozi

 

Mheshimiwa Spika;

Kutokana na operesheni iliyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa mashirikiano makubwa ya wananchi yamepelekea hadi kufika tarehe 22.07.2012 kuwa na idadi ya watu waliookolewa wakiwa hai kufikia 146 na miili ya waliofariki dunia iliyopatikana kufikia 73. Kati ya maiti hizo 68 zilipokelewa kituo cha Maisara na 5 zilipelekwa moja kwa katika eneo la makaburi la Kama kwa vile maiti hizo zilikuwa zimeshaharibika.

 

Kwa waliookolewa wakiwa hai waliweza kufikishwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa uchunguzi na matibabu. Hadi hii leo, majeruhi wote walishatibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani mwao.

 

Mheshimiwa Spika;

Katika kituo cha Maisara maiti zilipangwa ili kuwawezesha ndugu na jamaa kutambua maiti zao na kwa kurahisisha kazi hiyo, Shirika la Utangazaji kupitia kituo chake cha Televisheni kilichukua picha za sura za marehemu na kuzionyesha zikiwa tayari zimewekewa namba ili kurahisisha utambuzi na uchukuaji wa maiti hizo. Kupitia utaratibu huu, jumla ya maiti 50 zilitambuliwa na kukabidhiwa jamaa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi. Idadi ya maiti ambao hawakutambuliwa ni 23 na mazishi yao yalisimamiwa na Serikali katika eneo la Kama. Aidha, maiti mmoja aliyetambuliwa alilazimika kuzikwa Kama kwa vile mwili wake ulikuwa umeharibika sana sambamba na ndugu wa marehemu huyo kutochukuliwa na jamaa na ndugu zake. Kila maiti alizikwa katika kaburi lake chini ya usimamizi wa mashekhe kutoka Ofisi ya Mufti na Wakfu na Mali ya Amana.

 

Aidha, katika kituo cha Maisara huduma za uoshaji na sala ya maiti zilitolewa na pia wale wote waliochukua maiti wao walipatiwa usafiri, sanda na ubao kwa ajili ya kuzikia.

 

3.2 Juhudi za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana

 

Mheshimiwa Spika,

Katika jitihada za Serikali za kuhakikisha miili zaidi ya marehemu iliyotokana na ajali ya meli inapatikana, Serikali ilivitaka vikosi vyake ulinzi na usalama vikiongozwa na KMKM kuendesha zoezi la kuitafuta meli na miili iliyosalia. Kazi ya kuendesha operesheni ya kuitafuta meli pamoja na abiria ilianza mara tu baada ya kusikia kutokea kwa ajali hiyo. Jumla ya watu waliohai 146 waliokolewa siku hiyo na maiti 31 zilipatikana.

 

Asubuhi ya tarehe 19.07.2012, wazamiaji kutoka KMKM, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na makampuni binafsi walifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuanza kazi rasmi. Wazamiaji hao walifanikiwa kupata maiti 37 na hawakupata abiria aliye hai. Hata hivyo, wazamiaji hao hawakuweza kuiona meli.

 

Mheshimiwa Spika

Vikosi hivyo viliendelea na jitihada za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana kwa kujigawa katika makundi matatu. Makundi mawili yalihusika na kazi ya utafutaji wa watu katika maeneo ya ukanda wa eneo la tukio. Kundi jengine lilijihusisha na kazi ya uzamiaji (diving) kwa ajili ya kuitafuta meli chini ya bahari.

 

3.3 Kukusanya taarifa za watu waliokuwa hawajaonekana kupitia Ofisi za Masheha na Wilaya:

 

Mheshimiwa Spika,

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliziagiza ofisi zote za Wilaya na Shehia kuorodhesha majina ya watu waliokuwa hawajaoneka na waliofariki na kuziwasilisha orodha hizo kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ili kufanyiwa uhakiki na kupata orodha sahihi kwa ajili ya matumizi na kumbukumbu za baadae. Hadi kufikia tarehe 22.07.2012 zaidi ya watu 100 wameripotiwa hawakuonekana ama wakiwa hai au maiti. Hata hivyo, kwa uhakiki wa awali imebainika kwamba baadhi ya watu wameorodheshwa zaidi ya mara moja katika maeneo tofauti.

 

3.4 Viongozi Wakuu wa Kitaifa kutoa mkono wa pole

 

Mheshimiwa Spika

Viongozi Wakuu wa Kitaifa pamoja na viongozi wengine wanatarajiwa kufanya ziara za kutoa pole na kuzifariji familia zilizofiliwa na zilizopotelewa na ndugu zao kwa maeneo yote yalizoathirika Unguja na Pemba. Kazi hiyo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

 

3.5 Kuratibu upokeaji wa misaada

 

Mheshimiwa Spika

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa iliendelea kupokea misaada ya kifedha na vifaa kutoka kwa watu binafsi, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika ya Umma, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

 

Hadi kufikia tarehe 22.07.2012 jumla ya Shilingi320,000,000/-zimepokelewa na kuingizwa katika akaunti ya Mfuko wa Maafa Zanzibar (Zanzibar Disaster Funds) ilioko Benki ya Watu wa Zanzibar, ambayo imefunguliwa maalum kwa ajili ya michango ya aina hiyo. Aidha, vifaa na bidhaa mbalimbali zimepokelewa  kwa ajili ya kusaidia shughuli za operesheni ya uokozi.

 

 

4.0 GHARAMA ZA OPERESHENI

 

Mheshimiwa Spika

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliipatia Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa jumla ya shilingi milioni ishirini (20,000,000/-) kwa ajili ya kugharamia shughuli za operesheni ambapo hadi kufikia tarehe 22.07.2012 fedha zote zilikwisha tumika.

 

5.0 TULICHOJIFUNZA KUTOKANA NA TUKIO HILI (LESSONS LEARNED)

 

Mheshimiwa Spika

Kutokana na tukio hili la kuzama kwa meli ya MV. Skagit tumeweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo ni changamoto kwetu katika kuimarisha kazi na huduma za kukabiliana na maafa nchini. Miongoni mwa mambo hayo ni haya yafuatayo: –

 

 • Umakini na maamuzi sahihi na ya haraka yaliyochukuliwa na viongozi wetu yameweza kuleta ufanisi mkubwa katika operesheni ya uokozi na hivyo kupelekea kuokoa maisha ya wananchi wetu wengi.
 • Muitikio wa haraka wa taasisi mbalimbali za kukabiliana na maafa, zikiwemo taasisi za Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, Sekta Binafsi na Jumuiya za Kiraia umepelekea watu wengi kuweza kuokolewa wakiwa hai pamoja na kupatikana kwa maiti hali ambayo imewezesha maiti wengi kuzikwa na familia zao.
 • Kutokana na wananchi wengi kutumia mtandao wa mawasiliano wa Zantel, kulisababisha ugumu wa mawasiliano kutokana na minara ya kampuni hiyo kuzidiwa na matumizi.
 • Udogo wa sehemu ya kuhifadhia maiti (motuary) ulipelekea maiti wasiotambuliwa na jamaa zao kuzikwa haraka na Serikali.
 • Uhaba wa vifaa vya kisasa vya uokozi pamoja na wataalamu wa uzamiaji (divers) umepelekea zoezi la uokozi kuwa gumu na kuchukua muda.
 • Kukosekana kwa taarifa za uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na maafa ikiwemo uwezo wa vifaa na wataalamu ni changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi.

 

 

6.0 SHUKRANI

 

Mheshimiwa Spika

Kwa mara nyengine tena kwa niaba ya Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa naomba nimshukuru Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake kubwa alizochukua ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanaokolewa. Tunamshukuru kwa maelekezo yake na miongozo aliyotupatia ambayo kwa kiasi kikubwa ilitusaidia kufanikisha kazi za uokozi. Pia, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo yao na msaada mkubwa walioutoa katika kukabiliana na maafa hayo. Aidha, tunamshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda kwa msaada mkubwa aliotupatia kupitia Ofisi yake.

 

Tunawashukuru pia Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kutupatia miongozo ya mara kwa mara katika jitihada za kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza athari za maafa yaliyotokea.

 

Vile vile tunatoa shukrani za dhati kwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Usalama la Taifa kwa maelekezo yao juu ya hatua za kuchukuliwa katika kukabiliana na janga hili na majanga yanayoweza kutokea baadae. Shukrani za dhati pia zinatolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zao za haraka zilizosaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi. Pia tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa karibu nasi na kwa michango yao ya hali na mali katika kukabiliana na tukio hili la kusikitisha.

 

Mheshimiwa Spika

Shukrani pia zinatolewa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, angani na nchi kavu kwa jinsi walivyoshirikiana na Serikali katika kulikabili tukio hili. Wananchi wa maeneo ya jirani hasa wavuvi na wamiliki wa hoteli na kampuni za kitalii wanapewa shukrani za pekee kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu tokea hatua za awali baada ya kupatikana taarifa za kuzama kwa meli ya Skagit. Tunashukuru washirika wa maendeleo na wawakilishi wa nchi marafiki kwa jinsi walivyolichukulia suala hili na kutuunga mkono katika msiba huu wa kitaifa. Vilevile tunazishukuru taasisi za kidini hasa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na Ofisi ya Mufti kwa kusaidia maandalizi ya mazishi ya marehemu waliotokana na ajali hiyo.

 

Tunawashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa namna walivyoshirikiana na Kamati. Tunawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa na wafanyakazi wa Idara ya Kukabiliana na Maafa kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kipindi chote toka kutokea kwa janga hili. Tunawashukuru wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa kupokea tokeo hili kwa masikitiko makubwa katika kukabiliana na janga hili. Aidha, tunawashukuru wale wote walioweza kuchangia kwa hali na mali katika msiba huu.

 

 

 

 

 

7.0 HITIMISHO

 

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo nawaomba wajumbe wa Baraza lako tukufu waipokee taarifa hii na kutupatia ushauri ili uweze kutusaidia katika harakati za kukabiliana na maafa hapa nchini.

 

Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba kuwasilisha.

 

Ahsanteni sana

 

 

………………………………

MOHAMED ABOUD MOHAMED [MBM]

WAZIRI WA NCHI

OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS

ZANZIBAR

 

WAZIRI WA MIUNDO MBINU ZANZIBAR HAMAD MASOUD AJIUZULU

Waziri wa zamani Hamad Masoud

Waziri mpya Rashid Seif Suleiman

Waziri wa Mawasiliano na miundo mbinu, Zanzibar Hamad Masoud Hamad amejiuzulu kufuatia kuzama kwa meli ya Mv. Skygit iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 100.

Kwa mujibu wa taarifa ya katibu wa baraza la mapinduzi na katibu mkuu kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ilisema rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amekubali ombi la waziri Hamad kujiuzulu.

Tarifa hiyo imesema tarehe 20 julai, 2012 Hamad alimuandikia barua rais Shein ya kumuomba ajiuzulu kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya mv. Skagit iliyotokea julai 18 mwaka huu.

Kufuatia kujiuzulu kwa waziri huyo, Dk Shein amemteua mwakilishi wa jimbo la Ziwani kutoka chama cha wananchi CUF Rashid Seif Suleiman kuwa waziri wa miundombinu na mawasiliano.

Wakati huo huo, rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein ameunda tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya mv. Skagit.

Tume hiyo ni ile iliyoundwa kufuatia kuzama kwa meli ya Mv. Spece Islander Septemba mwaka jana.

Mwenyekiti wa tume hiyo ni jaji Abdulhakim Ameir Issa, wajumbe ni Meja Jenerali Said Omar, Comdr. Hassan Mussa Mzee, Kapteni Abdulla Yussuf Jumbe, Kaptein Abdulla Juma Abdulla, mwanasheria Salum Taoufiq.

Wengine ni Kaptein Hatibu Katandula, Bi. Mkali Fauster Ngowo, Ali Omar Chengo na Shaaban Ramadhan Abdalla katibu wa tume hiyo.

Akizungumza na zenji Fm radio mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF taifa Profisa Ibrahim Harouna Lipumba amesema hatua hiyo inaonesha uwajibikaji wa kisiasa kwa viongozi wa chama hicho serikalini.

Amesema mfano wa kiongozi huyo kujiuzulu unafaa kuigwa na wakuu wa taasisi za ukozi ambazo zimeonekana kudhorota katika shughuli za ukozi wakati meli hiyo ilipozama)

Kujiuzulu kwa Hamad kunafuatia shindikizo la baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na wananchi wakimtaka waziri huyo kujiuzulu kufuatia matukio mawili ya kuzama meli yaliopishana kwa miezi tisa na kusababisha maafa makubwa.

Waziri mpya Rashid Seif Suleima

KODI YA MISHAHARA YA WATUMISHI WA MUUNGANO KUBAKI ZANZIBAR

Omar Yussuf Mzee

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imo katika hatua za mwisho za kujua idadi ya wafanyakazi wa taasisi za muungano wanaofanya kazi Zanzibar ili kuwatoza kodi kwenye mishahara yao.

Waziri anaeshughulikia masuala ya fedha na uchumi Omar Yussuf Mzee amesema kodi hizo zitasaidia kuimarishaji utoaji wa huduma za kijamii kama vile, maji, afya na elimu.

Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi amesema mpango huo utasaidia kupatikana kwa zaidi ya shilingi bilioni 21 katika mwaka huu wa fedha 2012/2013.

Amesema katika kikao cha kujadili kero za muungano hivi karibuni kiliagiza kurekebisha sheria ya kodi ya mapato ili kuruhusu kodi za ajira kuhamishiwa sehemu anayofanyia kazi muhusika